(Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mheshimiwa Ata bin Khalil Abu al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)
Jibu la Swali
Kwa: Haitham Alamour
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Sheikh wetu mpendwa, nina swali la kimatibabu ambalo ni muhimu sana kupata jibu lake. Mimi ni daktari ninayefanya kazi katika hospitali ya akina mama na uzazi ambapo hufanyika operesheni za cesarean (upasuaji) ikiwa mwanamke anahitaji hivyo, au ikiwa maisha ya kijusi au maisha yake yako hatarini.
Kuna baadhi ya wanawake wajawazito wanaosumbuliwa na magonjwa yanayofanya kipindi chao cha ujauzito kuwa kigumu na chenye changamoto kubwa, jambo ambalo huwalazimu kutoingia uja uzito au kuachanisha vipindi vya uzazi kwa angalau miaka 3 hadi 4. Hivyo wanalazimika kutumia njia za kuzuia uzazi, lakini baadhi ya wanawake njia hizo haziwasaidii kupata nafasi inayohitajika, hivyo hupata ujauzito katika vipindi vya karibu karibu. Hali hii inatishia maisha yao kwa sababu ya kufanyiwa operesheni nyingi za cesarean zinazofuatana. Miongoni mwa wanawake hao kuna wenye matatizo ya utepe wa mgongo (disc), na wengine hupatwa na kuvuja damu kwa wingi (hemorrhage). Hapo madaktari hukimbilia kufunga mirija ya uzazi (fallopian tubes) moja kwa moja ili wasipate ujauzito tena baada ya kuzaa watoto. Hali hii imekuwa maarufu miongoni mwa wanawake ambapo baadhi huja hospitalini na kudai kutoweza kubeba ujauzito na kwamba hawawezi kutumia njia za kuzuia uzazi, hivyo wanataka kufunga mirija moja kwa moja ilhali umri wao hauzidi miaka 36, na wengine wana umri wa miaka 32. Humshinikiza daktari bingwa amfanyie upasuaji ili kufunga mirija moja kwa moja.
Swali ni: Ni ipi hukumu ya Sharia kwa daktari anayefuatilia hali ya mwanamke katika hatua za ujauzito na kuona kuwa ujauzito ni mgumu kwake na kwamba anapaswa kufanya operesheni ya kufunga mirija moja kwa moja? Na ni ipi hukumu ya daktari anayefuata tu maneno ya mwanamke bila kuhakikisha kama maneno yake ni sahihi?
Jibu:
Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Hakika kuzuia uzazi kwa muda inaruhusiwa kulingana na dalili zinazojulikana za al-azl (kutoa mbegu nje)...
Ama kuzuia uzazi kwa kudumu na kusababisha ugumba, hilo ni haramu. Hivyo, utumiaji wa dawa zinazozuia uzazi moja kwa moja na kukata kizazi, na kufanya operesheni za upasuaji zinazozuia uzazi moja kwa moja na kukata kizazi ni haramu, haijuzu kufanya hivyo. Hii ni kwa sababu hukumu hiyo inalingana na hukumu ya kuhasiwa (al-khisa’), hivyo inaingia chini yake na kuchukua hukumu yake. Kwani vitendo hivi hukata kizazi kama vile kuhasiwa kunavyokata kizazi, na kumekuja makatazo ya wazi dhidi ya kuhasiwa.
Kutoka kwa Sa’d bin Abi Waqqas amesema:
رَدَّ رسولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم على عُثمانَ بنِ مظعونَ التَّبَتُّلَ، ولو أذنَ له لاخْتَصَيْنا
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimkataza Uthman bin Maz’oon kujitenga na wanawake (tabattul), na lau angemsaidia (angemruhusu), basi tungejihasi." (Muttafaq 'alayh).
Na Uthman bin Maz’oon alikuwa amemjia Mtume (saw) akasema: "Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni mtu ambaye upweke unanawia vigumu, basi niruhusu nijihasi. Akasema:
لا، ولكنْ عَلَيكَ بالصِّيامِ
"Hapana, lakini ni juu yako kufunga."
Na katika tamko jingine amesema: "Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, unaniruhusu nijihasi? Akasema:
إن اللهَ أَبْدَلَنا بالرَّهْبانِيَّةِ الحَنيفيَّةَ السَّمْحَةَ
"Hakika Mwenyezi Mungu ametubadilishia badala ya urahibu (rahbaniyah) kwa dini ya Hanifiyyah iliyo nyepesi."
Na kutoka kwa Anas amesema:
كانَ النبيُّ صلى الله عليه وسلم يَأْمُرنا بالباءَةِ، ويَنْهى عنِ التَّبَتُّلِ نَهْيَاً شديداً، ويقولُ: تَزَوَّجوا الوَدودَ الوَلودَ فإني مُكاثِرٌ بِكُمُ الأُمَمَ يومَ القيامَةِ
"Mtume (saw) alikuwa akituamrisha kuoa, na akitukataza vikali kujitenga na wanawake (tabattul), na akisema: 'Ooeni wanawake wenye mapenzi na wanaozaa sana, kwani hakika mimi nitajifakhari kwa wingi wenu mbele ya umma (nyingine) Siku ya Kiyama.'" (Imevuliwa na Ahmad).
Vilevile, kukata kizazi moja kwa moja kunapingana na kile alichoweka Msharia (Ash-Shari’) kwamba kizazi na uzazi ndio asili ya ndoa. Kwa ajili hiyo, Mwenyezi Mungu (swt) amesema katika kuelezea neema kwa watu:
وَاللَّهُ جَعَلَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُمْ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ بَنِينَ وَحَفَدَةً
"Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na amekupatieni kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu." (QS. An-Nahl [16]: 72).
Na kwa hivyo, operesheni za kuleta ugumba wa kudumu ni haramu kwa mwanamume na mwanamke.
Ama ikiwa mwanamke amebeba ujauzito na madaktari bingwa waaminifu wakaamua kuwa kubaki kwa kijusi tumboni mwa mama kunatishia maisha ya mama kwa kifo, na kifo cha kijusi pamoja naye, basi katika hali hii inaruhusiwa kutoa mimba na kuokoa maisha ya mama. Na kuokoa maisha ni jambo ambalo Uislamu ulihimiza...
Ama maneno ya mwanamke kwamba yeye ni mgonjwa na anahofia maisha yake kutokana na ujauzito, hayo ni maneno yaliyo mbali na ukweli. Ni wanawake wangapi waliobeba ujauzito wakiwa wagonjwa na wakaendelea kuwa wajawazito, na wakazaa mtoto mwenye umbo kamili na mwili wenye afya... na Mwenyezi Mungu akawajalia afya na uzima... Pamoja na hayo, kama tulivyosema hapo awali, ikiwa amebeba ujauzito na kuendelea kwa ujauzito kunatishia maisha ya mama kwa kifo na kifo cha kijusi pamoja naye kwa mujibu wa ripoti ya madaktari bingwa waaminifu, basi inaruhusiwa kutoa mimba.
Kwa hiyo, ugumba ni haramu, na kutibu mwanamke wakati wa ujauzito ni jambo linalohitajika, na kulinda maisha yake wakati wa ujauzito ni jambo linalohitajika pia. Hata ikiwa ujauzito huu unatishia maisha yake kwa kifo na kifo cha kijusi pamoja naye kwa mujibu wa ripoti ya madaktari bingwa waaminifu, basi kutoa mimba inajuzu. Ama kutibiwa ili kuzuia uzazi moja kwa moja kulingana na ombi la mwanamke, basi hilo ni haramu.
Na ni juu ya madaktari kutolifanyia wepesi jambo hili; wajitahidi katika kuchunguza ujauzito na ugonjwa... kwani hiyo ni amana, na daktari anapaswa kuwajibika na hilo, na asiuze Akhera yake kwa mafanikio ya dunia hata yawe kiasi gani.
فَمَا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا قَلِيلٌ
"Basi starehe ya maisha ya dunia kwa kulinganisha na ya Akhera ni kidogo tu." (QS. At-Tawbah [9]: 38).
Mwisho, ninawahusia waume na wake kuongeza kizazi, na kuwalea kwa malezi mema, kwani Mtume (saw) atajifakhari kwao Siku ya Kiyama. Al-Bayhaqi ametoa katika Sunan al-Kubra kutoka kwa Abu Umamah (ra) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
تَزَوَّجُوا فَإِنِّي مُكَاثِرٌ بِكُمُ الْأُمَمَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ...
"Oeni, kwani hakika mimi nitajifakhari kwa wingi wenu mbele ya umma (nyingine) Siku ya Kiyama..."
Na ametoa mfano wake Al-Hakim katika Al-Mustadrak 'ala al-Sahihayn kutoka kwa Ma'qil bin Yasar (ra), na Al-Bazzar katika Musnad yake kutoka kwa Anas (ra), na wengineo.
Na Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Ta'ala huwalinda waja wema wanaume na wanawake.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashta
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus