Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Kuhusu Hadithi «... وَمَنْ مَنَعَهَا فَإِنَّا آخِذُوهَا وَشَطْرَ مَالِهِ»

April 18, 2014
4562

(Sfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)

Kwa Duaa al-Furqan

Swali:

Amir wetu mtukufu, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh, Mwenyezi Mungu aujaalie ushindi kupitia mikono yako.

Imetajwa katika kitabu cha Al-Amwal (Mali) katika maudhui ya faini, ukurasa wa 123-124: (Vilevile, kuchukua kutoka kwa anayekataa kutoa Zaka nusu ya mali yake kama ziada ya Zaka ya wajibu, ikiwa ni adhabu ya kinidhamu (ta’zir) kwake. Abu Dawood na Ahmad wamevua kutoka kwa Mtume (saw): «...na yeyote atakayeizuia basi hakika sisi tutaichukua na nusu ya mali yake»).

Inaonekana kutokana na yaliyotajwa kuwa msimamo uliopitishwa ni kuruhusiwa kuchukua faini kutoka kwa anayekataa kutoa Zaka kama adhabu ya ta’zir, licha ya kuwepo kwa hitilafu nyingi miongoni mwa mafaqihi juu ya uhalali wake. Lakini kile ambacho ningependa kukitolea ufafanuzi ni:

1- Hadithi inayotumiwa kama dalili kwa ukamilifu wake upande wa sanadi na matini; nimeitafuta na sikuipata isipokuwa Hadithi: Kutoka kwa Bahz bin Hakim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, ikiwa imenyanyuliwa kwa Mtume:

فِي كُلِّ إِبِلٍ سَائِمَةٍ فِي كُلِّ أَرْبَعِينَ ابْنَةُ لَبُونٍ لَا تُفَرَّقُ إِبِلٌ عَنْ حِسَابِهَا مَنْ أَعْطَاهَا مُؤْتَجِراً فَلَهُ أَجْرُهَا وَمَنْ مَنَعَهَا فَإِنَّا آخِذُوهَا مِنْهُ وَشَطْرَ إِبِلِهِ عَزْمَةً مِنْ عَزَمَاتِ رَبِّنَا جَلَّ وَعَزَّ لَا يَحِلُّ لِآلِ مُحَمَّدٍ مِنْهَا شَيْءٌ

"Katika kila ngamia wanaochungwa, kwa kila ngamia arobaini hutolewa binti labun mmoja (ngamia jike aliyemaliza mwaka wa pili). Ngamia wasitenganishwe na hesabu yao. Yeyote anayeitoa akitarajia malipo, basi ana thawabu yake, na yeyote anayeizuia, basi hakika sisi tutaichukua kutoka kwake pamoja na nusu ya ngamia wake; hilo ni agizo miongoni mwa maagizo ya Mola wetu, Aliyetukuka na Kushinda, na haihalalishwi chochote katika hiyo kwa familia ya Muhammad." (Imevuliwa na Ahmad)

Na katika Sunan Abu Dawood: Kutoka kwa Bahz bin Hakim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwamba Rasulullah (saw) amesema:

فِي كُلِّ سَائِمَةِ إِبِلٍ فِي أَرْبَعِينَ بِنْتُ لَبُونٍ، وَلَا يُفَرَّقُ إِبِلٌ عَنْ حِسَابِهَا مَنْ أَعْطَاهَا مُؤْتَجِراً - قَالَ ابْنُ الْعَلَاءِ مُؤْتَجِراً بِهَا - فَلَهُ أَجْرُهَا، وَمَنْ مَنَعَهَا فَإِنَّا آخِذُوهَا وَشَطْرَ مَالِهِ، عَزْمَةً مِنْ عَزَمَاتِ رَبِّنَا عَزَّ وَجَلَّ، لَيْسَ لِآلِ مُحَمَّدٍ مِنْهَا شَيْءٌ

"Katika kila kundi la ngamia wanaochungwa, kwa kila arobaini hutolewa binti labun mmoja, na ngamia wasitenganishwe na hesabu yao. Yeyote anayeitoa akitarajia malipo - Ibn al-’Alaa amesema: akitarajia malipo kwayo - basi ana thawabu yake, na yeyote anayeizuia, basi hakika sisi tutaichukua pamoja na nusu ya mali yake; hilo ni agizo miongoni mwa maagizo ya Mola wetu, Mwenye Nguvu na Mtukufu, na hakuna chochote katika hiyo kwa familia ya Muhammad."

Ama kwa tamko "فأنا آخذها وشطر ماله" (basi mimi nitaichukua na nusu ya mali yake) sikuipata.

2- Ni nini kinachokusudiwa na nusu ya mali yake? Je, ni nusu ya mali yake yote? Ama ni nusu ya mali yake ambayo ameizuia Zaka yake? Ama ni nusu ya kile kilichokadiriwa kulipwa kama Zaka katika mali yake? Au ni kama ilivyopokewa na baadhi ya watu kwamba mali yake inagawanywa sehemu mbili, kisha mchukua Zaka (musa’diq) anachagua na kuchukua Zaka kutoka katika sehemu iliyo bora zaidi kama adhabu kwa kuzuia kwake Zaka? Mwenyezi Mungu akubariki na akujaze kila la kheri kwa niaba yetu.

Jawabu:

Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.

Kuhusu Hadithi uliyoitaja: «فَإِنَّا آخِذُوهَا وَشَطْرَ مَالِهِ»:

1- Abu Dawood ametoa kutoka kwa Bahz bin Hakim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, kwamba Rasulullah (saw) amesema:

فِي كُلِّ سَائِمَةِ إِبِلٍ فِي أَرْبَعِينَ بِنْتُ لَبُونٍ، وَلَا يُفَرَّقُ إِبِلٌ عَنْ حِسَابِهَا مَنْ أَعْطَاهَا مُؤْتَجِراً - قَالَ ابْنُ الْعَلَاءِ مُؤْتَجِراً بِهَا - فَلَهُ أَجْرُهَا، وَمَنْ مَنَعَهَا فَإِنَّا آخِذُوهَا وَشَطْرَ مَالِهِ، عَزْمَةً مِنْ عَزَمَاتِ رَبِّنَا عَزَّ وَجَلَّ، لَيْسَ لِآلِ مُحَمَّدٍ مِنْهَا شَيْءٌ

"Katika kila kundi la ngamia wanaochungwa, kwa kila arobaini hutolewa binti labun mmoja, na ngamia wasitenganishwe na hesabu yao. Yeyote anayeitoa akitarajia malipo - Ibn al-’Alaa amesema: akitarajia malipo kwayo - basi ana thawabu yake, na yeyote anayeizuia, basi hakika sisi tutaichukua pamoja na nusu ya mali yake; hilo ni agizo miongoni mwa maagizo ya Mola wetu, Mwenye Nguvu na Mtukufu, na hakuna chochote katika hiyo kwa familia ya Muhammad."

2- Na Ahmad na Nasai wametoa, na tamko ni la Ahmad, kutoka kwa Bahz bin Hakim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake amesema: Nilimsikia Nabii wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema:

فِي كُلِّ إِبِلٍ سَائِمَةٍ. فِي كُلِّ أَرْبَعِينَ ابْنَةُ لَبُونٍ. لَا تُفَرَّقُ إِبِلٌ عَنْ حِسَابِهَا. مَنْ أَعْطَاهَا مُؤْتَجِراً فَلَهُ أَجْرُهَا، وَمَنْ مَنَعَهَا فَإِنَّا آخِذُوهَا مِنْهُ وَشَطْرَ إِبِلِهِ عَزْمَةً مِنْ عَزَمَاتِ رَبِّنَا لَا يَحِلُّ لِآلِ مُحَمَّدٍ مِنْهَا شَيْءٌ

"Katika kila kundi la ngamia wanaochungwa, kwa kila arobaini hutolewa binti labun mmoja. Ngamia wasitenganishwe na hesabu yao. Yeyote anayeitoa akitarajia malipo, basi ana thawabu yake, na yeyote anayeizuia, basi hakika sisi tutaichukua kutoka kwake pamoja na nusu ya ngamia wake; hilo ni agizo miongoni mwa maagizo ya Mola wetu, na haihalalishwi chochote katika hiyo kwa familia ya Muhammad."

• Hadithi hii ina hitilafu katika ufahamu wake miongoni mwa mafaqihi:

Kuna baadhi yao wanaodai kuwa imefutwa (naskh), hivyo haichukuliwi chochote isipokuwa Zaka pekee. Na wengine wanasema kuwa riwaya ya 'شطر' si hivyo kwa kuitia sukuni herufi Taa (ط), bali imekuja kwa muundo wa neno lisilojulikana mtendaji wake (majhul) 'شُطِّر' yaani mali yake igawanywe vipande viwili na mfanyakazi wa Zaka achague kati ya nusu hizo mbili. Na kuna wengine wanaosema kuwa mpokeaji alifanya makosa (wahim), bali ilitakiwa iwe "فإنا آخذوها من شطر ماله" (basi tutaichukua kutoka nusu ya mali yake) au "من شطر إبله" (kutoka nusu ya ngamia wake)...

• Na msimamo wenye nguvu zaidi (ar-rajih) kwangu katika suala hili ni kama ifuatavyo:

A- Kuhusu suala la muundo wa neno lisilojulikana mtendaji wake (majhul), suala la makosa (wahim), na suala la kufutwa hukumu (naskh), mimi nazikataa zote hizo:

Muundo wa majhul haukubaliki kwa sababu neno 'شطر' katika riwaya zote za Hadithi zinazozingatiwa limetajwa bila muundo huo.

Ama kuhusu makosa (wahim), vivyo hivyo haikubaliki, kwa sababu riwaya si "فإنا آخذوها منه شطر ماله" ili isemekwe kwamba neno "منه" ni kosa la mpokeaji, pamoja na kwamba kosa hapa pia haliwezi kuwepo kwa sababu haitarajiwi kwa mpokeaji anayejua Kiarabu kusema "منه شطر ماله". Itakuwaje basi ikiwa neno "منه" limefuatiwa na herufi "Waw" (na)? Je, isemekwe alikosea katika tamko "منه وشطر" badala ya "من شطر"? Hili halikubaliki...

Hiyo ni kuhusu muundo wa majhul na makosa. Ama kuhusu kufutwa kwa hukumu (naskh), hilo pia halikubaliki kwa sababu tarehe ya kutolewa haijulikani, na kwa sababu dalili ya naskh kwao si ya wazi, na dalili za jumla za Zaka hazifuti dalili maalum ya Zaka inayohusu adhabu kwa anayeizuia.

B- Na lenye nguvu kwangu ni kwamba Hadithi ya kwanza: «فَإِنَّا آخِذُوهَا وَشَطْرَ مَالِهِ» inafahamisha kuwa anayezuia Zaka, Zaka hiyo huchukuliwa kutoka kwake kwa nguvu, na hupigwa faini ya nusu ya mali yake, na inawezekana kufahamika kutoka kwayo kuwa ni nusu ya mali yake yote, yaani ile iliyowajibikiwa Zaka na mali nyinginezo ambazo hazijafikia kiwango cha Zaka kama dhahabu, fedha, ngamia, ng'ombe, mbuzi, ngano, shayiri, tende, zabibu, na bidhaa za biashara.

C- Na Hadithi nyingine: «فَإِنَّا آخِذُوهَا مِنْهُ وَشَطْرَ إِبِلِهِ» baada ya kutaja Zaka ya ngamia «فِي كُلِّ إِبِلٍ سَائِمَةٍ...», basi hii inamaanisha kuwa nusu hiyo imeunganishwa na ngamia anaomiliki, yaani inachukuliwa Zaka ya ngamia wake, na nusu ya ngamia hao. Kwa usemi ulio wazi zaidi, ikiwa ana ngamia arobaini wanaochungwa, basi Zaka yao ni mmoja "binti labun", kisha anachukuliwa faini nyingine ambayo ni nusu ya wale arobaini.

D- Na Hadithi ya pili itakuwa ni yenye kuainisha (mukhasis) Hadithi iliyotangulia, yaani hapigwi faini ya nusu ya mali yake yote, bali nusu ya mali inayotolewa Zaka.

E- Ama maana ya 'Shatr' (شطر), je, ni nusu au ni sehemu? Imetajwa katika Al-Qamus al-Muhit: (الشَّطْرُ: نِصفُ الشيءِ وجُزْؤُهُ - Shatr: ni nusu ya kitu na sehemu yake). Kwa hiyo, jambo hili huachiwa utashi wa Khalifa kwa anayezuia Zaka: Ama achukue Zaka na nusu ya mali inayotolewa Zaka, au achukue Zaka na sehemu ya mali inayotolewa Zaka, na hiyo ikiwa ni faini kwa kuzuia kwake Zaka... Ingawa mimi naelekea zaidi kwenye maana ya nusu kwa sababu ni faini, na faini ndani yake kuna maana ya adhabu na ukali. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hikima zaidi.

Kwa ufahamu, tumetaja maudhui haya katika dalili za faini, yaani kwamba kuchukua nusu ya mali yake ni faini kama ilivyokuja katika kitabu cha Al-Amwal na kitabu cha Nidham al-Uqubat (Nidhamu ya Adhabu).

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah

Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jawabu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Kiungo cha jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network