** (Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)**
Jibu la Swali
Kuhusu Nisab ya Zaka katika Bidhaa za Biashara
Kwa Lut Abu Sunaina
Swali:
Sheikh wetu mtukufu, salamu za heri kutoka kwa Allah na baraka.
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Swali langu linahusu Nisab ya Zaka katika bidhaa za biashara: Imetajwa katika kitabu cha Al-Amwal ukurasa wa 195 kwamba Nisab ya Zaka ni Dirhamu 200 za fedha, yaani gramu 595 za fedha, au Dinari 20 za dhahabu, yaani gramu 85 za dhahabu. Leo hii, ni Nisab ipi tuitegemee katika hesabu yetu ya bidhaa za biashara, kwa kuzingatia kuwa kuna tofauti kubwa kati ya bei ya dhahabu na fedha? Kwani Dinari moja ya dhahabu inalingana takriban na mamia ya Dirhamu za fedha. Ikiwa tutapiga hesabu ya Dinari tano za dhahabu, thamani yake itavuka Nisab ya fedha. Kwa hivyo, ni Nisab ipi tuitegemee leo? Allah akubariki na atunufaishe kwa elimu yako.
Jibu:
Waalaykum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh.
Kwanza: Kwa watu wa dhahabu, Nisab ni "gramu 85 za dhahabu", na kwa watu wa fedha (silver), ni "Dirhamu 200 za fedha". Ama kwa upande wa pesa za karatasi zinazowakilisha (dhahabu au fedha), hutegemea kile kilichoandikwa juu yake ambacho inakiwakilisha; "ikiwa inayowakilishwa ni dhahabu, basi huzingatiwa Nisab ya dhahabu, na ikiwa inayowakilishwa ni fedha, basi huzingatiwa Nisab ya fedha."
Ama karatasi (fedha za sasa) ambazo hupata thamani yake kwa nguvu ya sheria na si karatasi zinazowakilisha dhahabu wala fedha – kama ilivyo sarafu ya sasa – mimi napendelea (arrajihu) kuwa ikadiriwe kwa kiwango cha chini kati ya Nisab mbili, yaani kwa fedha (silver). Hivyo, ikiwa thamani ya pesa ya karatasi itafikia Dirhamu 200 za fedha, yaani thamani ya gramu 595 za fedha, ambayo ni takriban aunsi 20 za fedha – na nadhani aunsi moja ya fedha ni takriban dola 30. Hii inamaanisha kuwa ikiwa kile alicho nacho Mwislamu kitafikia takriban dola 600 (huhesabiwa kwa usahihi), na hakuwa na deni... basi yeye ni miongoni mwa watu wa Zaka (Ahluz Zakah). Ikiwa mwaka mmoja (Hawl) utapita juu ya Nisab hiyo bila kupungua, basi anapaswa kutoa Zaka.
Ninasema kwa kiwango cha chini kati ya Nisab mbili kwa sababu kikifikia kiwango cha chini cha Nisab, mtu huyo tayari ameshakuwa miongoni mwa wanaowajibika kutoa Zaka (Ahluz Zakah), hivyo haijuzu kukivuka huku akingojea kiwango cha juu cha Nisab. Badala yake, anapaswa kuandika tarehe hii ambayo amekuwa miongoni mwa wanaowajibika kutoa Zaka, kisha baada ya kupita mwaka mmoja (Hawl), atatoa Zaka ikiwa Nisab hiyo haijapungua. Hili ndilo ninalolipendelea, na Allah ndiye Mjuzi zaidi na Hakimu zaidi.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir: https://web.facebook.com/AmeerhtAtabinKhalil/photos/a.122855544578192.1073741828.122848424578904/462064227323987/?type=3&theater
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir: http://archive.hizb-ut-tahrir.info/arabic/index.php/HTAmeer/QAsingle/3515/
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir: https://plus.google.com/u/0/b/100431756357007517653/100431756357007517653/posts/iV9Qz2DApG6?sfc=false