Swali:
Tunajua kwamba ni haramu kwa mtawala kupanga bei ya bidhaa za watu kwa sababu Mtume (saw) anasema:
إِنَّ اللَّهَ هُوَ الْخَالِقُ الْقَابِضُ، الْبَاسِطُ الرَّازِقُ، الْمُسَعِّرُ، وَإِنِّي لَأَرْجُو أَنْ أَلْقَى اللَّهَ وَلَا يَطْلُبُنِي أَحَدٌ بِمَظْلَمَةٍ ظَلَمْتُهَا إِيَّاهُ فِي دَمٍ وَلَا مَالٍ
"Hakika Allah Ndiye Muumba, Mwenye kuzuia, Mwenye kukunjua (riziki), Mpaji, na Mpangaji bei. Na mimi natarajia kukutana na Allah hali ya kuwa hakuna yeyote kati yenu anayedai dhulma kwangu katika damu wala mali." (Imepokelewa na Ahmad).
Na pia Mtume (saw) anasema:
مَنْ دَخَلَ فِي شَيْءٍ مِنْ أَسْعَارِ الْمُسْلِمِينَ لِيُغْلِيَهُ عَلَيْهِمْ، فَإِنَّ حَقًّا عَلَى اللَّهِ أَنْ يُقْعِدَهُ بِعُظْمٍ مِنَ النَّارِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ
"Yeyote atakayeingilia chochote katika bei za Waislamu ili awaghalishie (awapandishie bei), basi ni haki ya Allah kumketisha kwenye sehemu kubwa ya Moto Siku ya Kiyama." (Imepokelewa na Ahmad).
Swali ni: Ikiwa baadhi ya wafanyabiashara katika eneo fulani wataamua kupanga bei ya bidhaa fulani, kwa mfano mkutano wa wafanyabiashara wa mchele na makubaliano yao ya kuuza mchele kwa wafanyabiashara wengine na kwa watu kwa bei maalum; je, kupanga bei ya bidhaa hiyo kwa makubaliano kati ya wafanyabiashara kunachukuliwa kuwa ni haramu, au haramu ni ile inayopangwa na serikali pekee na si makubaliano ya wafanyabiashara?
Jibu:
Ni wazi kutokana na hadith ya pili uwepo wa 'illah (sababu ya kisheria), na ikiwa 'illah hiyo itapatikana, basi hukumu hufuata 'illah hiyo... Ikiwa makubaliano ya wafanyabiashara ni kwa ajili ya kupandisha bei, basi katazo hilo linawahusu. Na ikiwa makubaliano yao ni kwa ajili ya kuzuia ushindani usio wa haki na kupanga utaratibu wa kuuza na kununua, kiasi kwamba muuzaji asiweze kuficha bidhaa (kuhodhi) kwa mfano ili aiuze kwa bei ya juu zaidi, na kuwaacha wafanyabiashara wengine wakiuza bila yeye kutoa bidhaa yake, yaani kuifanyia ukiritimba (ihtikar) kisha kuja kuiuza inapokuwa adimu, na kadhalika... basi katika hali hii, hakuna kosa kwa wafanyabiashara kupanga utaratibu wa mchakato wa kuuza na kununua.
Hata hivyo, kukutana kwa wafanyabiashara na kuridhiana kwao juu ya bei fulani ni jambo lenye uwezekano mkubwa (mazhannah) wa kupandisha bei, hususan ikiwa wao ndio wamiliki wa bidhaa hiyo na hakuna mwingine anayeiuza. Hivyo makubaliano yao katika hali hii, hata kama hayakutamka wazi kupandisha bei, mara nyingi hupelekea hilo. Kwa hiyo, huangukia chini ya kaida ya kisheria: "Al-wasila ila al-haram haram" (Njia inayopelekea kwenye haramu ni haramu). Kushiriki kwao katika kuamua bei ya bidhaa hupelekea kughali kwake, ikiwa si kwa yakini basi ni kwa dhana yenye nguvu (ghalabatu dhan), na dhana yenye nguvu inatosha hapa.
Kwa sababu hiyo, kauli yenye nguvu zaidi kwangu ni kwamba makubaliano ya wafanyabiashara kupanga bei ya bidhaa hayaruhusiwi. Badala yake, jambo hilo liachwe kwenye bei ya soko inayotokana na kila mfanyabiashara kupanga bei zake kulingana na hali yake. Katika hili kuna wasaa kwa watu, na kuepukana na kupandisha bei...
Nimependezwa katika mlango huu na kile kilichoelezwa katika kitabu At-Turuq al-Hukmiyyah cha Ibn al-Qayyim al-Jawziyyah, chini ya mlango: "Faslu inayohusu wagawaji wanaogawanya ardhi na nyumba na vitu vingine kwa ujira," ambapo ilielezwa:
"Kutokana na hapa: Wanazuoni zaidi ya mmoja – kama Abu Hanifah na wenzake – wamewakataza wagawaji wanaogawanya ardhi na nyumba na vinginevyo kwa ujira: wasishirikiane (kufanya umoja wa bei), kwani wakishirikiana – na watu wanawahitaji – watawapandishia ujira (gharama)."
Ninasema: "Hali kadhalika inapaswa kwa kiongozi wa Hisbah (idara inayofuatilia masuala ya soko na maadili): kuwakataza waoshaji wa maiti na wabebaji wa majeneza kushirikiana (kwa kuweka bei moja), kwa sababu ya kile kilichomo ndani yake cha kuwapandishia watu ujira, na hali kadhalika ushirikiano wa kila kundi ambalo watu wanahitaji manufaa yao..." Mwisho wa nukuu.