Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Kwa Gadzhimurad Gamzatov
Swali:
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,
Sheikh wetu mpendwa,
Je, mtoto mdogo mchanga anayanyonya ambaye hali chakula na anakunywa maziwa ya mama pekee au maziwa ya kopo ya watoto, anahesabiwa katika kafara ya kiapo? Ikiwa kafara imeshatolewa na mtu hakuwahi kufikiria swali hili, je, arudie kutoa kafara kwa masikini?
Swali lingine linalohusiana na kafara ya kiapo: Je, inatosha kulisha masikini mara moja pekee au ni lazima mara mbili (chakula cha mchana na cha jioni)?
Swali la tatu: Mtu anayeishi Ulaya ametoa kafara ya kiapo kwa masikini nchini Ukraine na akaangalia kiasi cha kafara nchini Ukraine. Je, ilikuwa ni lazima kwake kuangalia kiasi cha kafara nchini Ulaya, au inatosha kuangalia kiasi cha fedha katika nchi anayotuma?
Jibu:
Waalaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,
1- Msingi wa kafara ya kiapo ni kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَكِنْ يُؤَاخِذُكُمْ بِمَا عَقَّدْتُمُ الْأَيْمَانَ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ فَمَنْ لَمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ذَلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ كَذَلِكَ يُبَيِّنُ اللهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
"Mwenyezi Mungu hakuwashikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini anakuwashikeni kwa mliyo yaapa kwa kusudia (kwa dhati). Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha watu wa nyumbani kwenu, au kuwavisha, au kumwachia huru mtumwa. Asiyepata hayo, basi afunge siku tatu. Hiyo ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini viapo vyenu. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyokubainishieni aya zake ili mpate kushukuru." (QS Al-Ma'idah [5]: 89)
Na kuwalisha masikini kumi ni mojawapo ya chaguzi zilizotajwa katika aya: "basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnaowalisha watu wa nyumbani kwenu."
2- Inafahamika kutokana na aya tukufu kuwa idadi ya kumi ni lazima, yaani ni lazima kuwalisha masikini kumi, hivyo haifai kumlisha masikini mmoja mara kumi kwa mfano... Na tumebainisha hayo katika jibu la swali lililopita mnamo tarehe 29/04/2022 ambapo ilisemwa:
[... Maoni ninayoyapendelea ni kwamba ikiwa andiko (nass) limekuja na idadi maalum ya masikini kama vile: "basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnaowalisha watu wa nyumbani kwenu au kuwavisha", na "asiyeweza, basi walishe masikini sitini", basi katika hali hii ni lazima kufuata idadi iliyotajwa (kumi, sitini) sawa iwe ni kutoa chakula chenyewe au thamani yake, kwa sababu idadi hiyo imekusudiwa na ni sharti la lazima. Ama ikiwa andiko limeomba kuwapa masikini bila kutaja idadi, basi inafaa kumpa masikini mmoja kwa sababu ya kukosekana kwa sharti la idadi, na inafaa kumpa zaidi ya masikini mmoja, na hiyo ni kama kauli yake Mwenyezi Mungu kuhusu Zaka: "Hakika sadaka (zaka) ni kwa ajili ya mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao na katika kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na msafiri, ni faradhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima." Hivyo, inajuzu kwa mtoaji zaka kumpa zaka yake masikini mmoja na inajuzu kuigawanya kwa masikini wengi, kwa sababu haikuja idadi maalum katika aya, bali imekuja neno "masikini" hivi hivi bila idadi... Lakini anazingatia katika hilo kuwa wanastahili zaka kwa sifa ya umasikini...].
3- Kwa mujibu wa hayo, kukamilika kwa kafara kunawajibisha kulisha masikini kumi kwa chakula cha wastani, na hii inamaanisha kuwa masikini ambaye anafaa katika kafara ni yule anayeweza kula chakula cha wastani. Ama mtoto mchanga, sipendelei kumwingiza katika dhana hii, na kwa hiyo, hahesabiwi miongoni mwa masikini wanaolishwa katika kafara ya kiapo. Ikiwa mtu atatuma chakula kwa familia masikini yenye watu kumi miongoni mwao akiwemo mtoto mchanga, basi kafara hii haijakamilika kwani ni kulisha watu tisa na si kumi, kwa sababu mchanga haingii katika dhana ya wanaolishwa. Hili ndilo ninalolipendelea na ndilo linalotuliza nafsi zaidi.. Kwa hiyo, ni lazima akamilishe kwa kumlisha masikini mwingine zaidi ya wale aliowalisha ili kafara itimie masikini kumi. Na hii ni tofauti na mtoto anayekula chakula kama vile mtoto anayejitambua (mumayyiz) na mfano wao, hawa wanafaa katika kafara, na ikiwa katika familia ya masikini kuna watoto kama hao, basi kafara inaswihi kwa kuwalisha kwa sababu wanaingia katika dhana ya wanaolishwa.
4- Mafakihi wametofautiana katika kubainisha kiasi cha chakula kwa kila masikini katika kafara ya kiapo, na katika aina ya chakula ambacho kafara hutolewa... n.k., na nitanukuu kitu kuhusu jambo hili kutoka katika Ensiklopidia ya Fiqhi ya Kuwait (Al-Mawsu’ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaitiyyah):
[... «Pili: Kwa upande wa kiasi»
- Maliki, Shafi'i na Hanbali wamekwenda kwenye msimamo kuwa ni sharti kila masikini apewe kibaba (mud) kimoja cha chakula kikuu cha nchi, na haijuzu kutoa thamani ya chakula kwa kufuata andiko la aya: "basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi". Na ni sharti asipunguze sehemu hizo, hivyo haijuzu kuwapa masikini ishirini vibaba kumi kwa kila mmoja wao nusu kibaba, isipokuwa akikamilisha kwa kumi miongoni mwao kile kilichopungua. Pia ni sharti ulishaji uwe kwa kumi, hivyo haifai kuchanganya, ikiwa atawalisha watano na kuwavisha watano haitoshi. Pia ni sharti kumpa kila mmoja katika wale kumi kibaba kwa njia ya ummiliki (tamlīk), na haifai kwa Maliki kurudia kumpa mtu mmoja, hivyo akimlisha mmoja vibaba kumi kwa siku kumi haitoshi kwake. Na Hanafi wamekwenda kwenye msimamo kuwa ni sharti kila masikini apewe vibaba viwili yaani nusu pishi (saa) ya ngano au pishi ya tende au shayiri au thamani ya hayo kwa pesa au bidhaa za biashara, kwa sababu lengo ni kuondoa haja, na hilo linaweza kutimia kwa thamani.
Ama kiasi cha chakula cha ruhusa (ibahah) kwao: ni milo miwili ya kushiba, yaani ni sharti amlishe kila masikini chakula cha mchana na cha jioni, na vivyo hivyo akiwalisha chakula cha jioni na daku, au chakula cha mchana mara mbili na mfano wa hayo, kwa sababu hiyo ni milo miwili inayokusudiwa.
Ama akimlisha mmoja chakula cha mchana, na mwingine chakula cha jioni haiswihi, kwa sababu atakuwa amegawanya chakula cha watu kumi kwa watu ishirini, na hilo haiswihi.
Pia wanaweka sharti kuwa asitoe kafara yote kwa masikini mmoja katika siku moja kwa mkupuo mmoja au kwa kutawanyika mara kumi. Lakini akimlisha masikini mmoja kwa siku kumi chakula cha mchana na jioni, au akampa masikini mmoja kwa siku kumi kila siku nusu pishi inajuzu, kwa sababu kufufuka kwa haja kila siku kunamfanya kuwa kama masikini mwingine, hivyo ni kama ametoa thamani kwa masikini kumi.
«Tatu: Kwa upande wa aina ya chakula»
- Hanafi wamekwenda kwenye msimamo kuwa kinachotosheleza katika kulisha ni ngano, au shayiri, au tende, unga wa kila kimoja ni kama asili yake kwa kipimo yaani nusu pishi katika unga wa ngano na pishi katika unga wa shayiri, na imesemwa: kinachozingatiwa katika unga ni thamani, si kipimo, na inajuzu kutoa thamani kutoka katika aina nyinginezo. Maliki wamekwenda kwenye msimamo kuwa kulisha kuwe kwa ngano ikiwa ndicho chakula chao, hivyo haitoshelezi kingine miongoni mwa shayiri au mahindi au vinginevyo, na ikiwa wanakula kingine kisichokuwa ngano basi ni kile kinacholingana nacho kwa kushibisha si kwa kipimo. Shafi'i wamekwenda kwenye msimamo kuwa kulisha kuwe kwa nafaka na matunda ambayo zaka huwajibika ndani yake, kwa sababu miili husimama kwayo, na ni sharti iwe ni chakula kikuu cha nchi. Hanbali wamekwenda kwenye msimamo wa sharti kuwa kulisha kuwe kwa ngano, shayiri na unga wake, tende na zabibu na haitoshelezi kingine hata kama ni chakula cha nchi yake isipokuwa kama vyakula hivyo vitakosekana.] Mwisho.
5- Yale ninayoyapendelea ni kwamba ikiwa ulishaji utafanyika kwa masikini kumi, uwe ni milo miwili ili kuendana na maana ya aya "basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnaowalisha watu wa nyumbani kwenu", na kulisha watu wa nyumbani huwa ni mara mbili kwa siku, ili iitwe kuwa ni kulisha, kama vile chakula cha mchana na jioni, vinginevyo atakuwa hajakamilisha kulisha watu wake. Hali kadhalika kwa masikini katika kafara ni lazima kuwalisha mara mbili kwa siku mpaka kafara ikamilike. Akitosheka na chakula cha mchana bila jioni au chakula cha jioni bila mchana haitoshelezi. Vilevile, Sharia imeweka chakula katika Ramadhani kuwa ni milo miwili: mlo wa daku na mlo wa iftari, hivyo ukamilifu wa kulisha unakuwa kwa milo hiyo miwili au mfano wake.
6- Ama kuhusu swali lako: (Mtu anayeishi Ulaya ametoa kafara ya kiapo kwa masikini nchini Ukraine na akaangalia kiasi cha kafara nchini Ukraine. Je, ilikuwa ni lazima kwake kuangalia kiasi cha kafara nchini Ulaya au inatosha kuangalia kiasi cha fedha katika nchi anayotuma?), jibu la hilo ni kwamba ninachotulizana nacho ni kuwa utoaji uwe kwa mujibu wa chakula cha wastani katika nchi ambayo mtoaji kafara yuko, kwa sababu aya tukufu inasema: "basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnaowalisha watu wa nyumbani kwenu", na hii inaashiria kuwa kulisha kunakuwa kwa mujibu wa mahali alipo mtu kwa sababu kinachotakiwa ni kulisha masikini kumi kutokana na wastani wa kile anacholisha watu wake... Ikiwa atalisha, kwa mfano, nchini Ukraine kwa dola kumi, hii inaweza kutosha kulisha masikini kumi kule, lakini haitoshi kulisha masikini kumi kwa mujibu wa hali ya Ulaya, bali inampasa kwa mfano alishe kwa dola mia moja ili awe amelisha kutokana na wastani wa kile anacholisha watu wake... Kwa hiyo, naona kuwa ni bora na ni salama zaidi kutoa kiasi kinacholingana na kulisha masikini kumi katika nchi anayoishi.
Hili ndilo ninalolipendelea na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hikima zaidi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
01 Dhul-Hijjah 1444H Sawa na 19/06/2023M
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook: Facebook