Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Jinsi ya Kuepuka Ukafiri au Ushirikina na Kufa nikiwa Muislamu

April 30, 2017
8567

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni Kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Jinsi ya Kuepuka Ukafiri au Ushirikina na Kufa nikiwa Muislamu

Kwa Islam Zidan

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Nitajiepusha vipi na ukafiri au ushirikina na kufa nikiwa Muislamu? Kwa sababu sitaki kuwa miongoni mwa wale ambao vitendo vyao vimepotea... Na je, ukafiri ni kitendo tu, au kauli, au itikadi???

Tafadhali nijibu, Allah awabarikie.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Hakika swali lako limegawanyika katika sehemu mbili:

Kwanza: Ni vipi mtu anajiepusha na ushirikina na ukafiri na kufa akiwa Muislamu...

Pili: Je, ukafiri ni kitendo, kauli, au itikadi...

Tutaingia kwenye jibu la sehemu ya pili ya swali kwa sababu jibu la sehemu ya kwanza limejengeka juu yake...

  • Jibu la sehemu ya pili ya swali:

Hakika itikadi (aqidah) na imani zina maana moja, nayo ni kusadikisha kwa kukatiki (at-tasdiq al-jazim) kunakoafikiana na uhalisia kutokana na dalili. Mahali pa imani ni moyoni, na inategemea kusadikisha kwa kukatiki, na si kusadikisha tu kwa kawaida; na lazima iwe inaafikiana na uhalisia na iwe imetokana na dalili ili iweze kutulia ndani kabisa ya nyoyo, na hapo ndipo mtu anakuwa muumini... Ukafiri kadhalika mahali pake ni moyoni, kwa sababu unahusiana na kusadikisha, na mahali pa kusadikisha ni moyoni... Amesema Subhanahu:

قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا قُلْ لَمْ تُؤْمِنُوا وَلَكِنْ قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ

"Wametoa kauli Mabedui: 'Tumeamini.' Sema: 'Hamjaamini, lakini semeni: "Tumesilimu," kwani imani bado haijaingia nyoyoni mwenu...'" (QS Al-Hujurat [49]: 14), kwa sababu haikuwa imetulia nyoyoni mwao...

وَلَكِنَّ اللَّهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ أُولَئِكَ هُمُ الرَّاشِدُونَ

"Lakini Mwenyezi Mungu amekupendezeeni imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na akakuchukizisheni ukafiri, na upotovu, na uasi. Hao ndio walioongoka." (QS Al-Hujurat [49]: 7).

مَنْ كَفَرَ بِاللَّهِ مِنْ بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَكِنْ مَنْ شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِنَ اللَّهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

"Anayemkana Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake - isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetulia juu ya imani - lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao, na watapata adhabu kubwa." (QS An-Nahl [16]: 106).

Kwa hiyo, mhimili wa imani na ukafiri upo kwenye kusadikisha kwa moyo na kuitakidi kwake na si kwenye kauli na kitendo, kwa sababu kauli na kitendo ni katika vitendo vya viungo na ulimi na vyote viwili ni tofauti na kusadikisha kwa moyo... Isipokuwa ni lazima kuzingatia mambo mawili katika muktadha huu, nayo ni:

1- Hakika kauli na kitendo, ingawa si itikadi, vinaweza kuashiria itikadi na kuidhihirisha, na katika hali hii, kauli na kitendo huchukua hukumu ya itikadi na mtu anaweza kukufuru kwavyo. Muislamu hukufuru katika hali nne:

a- Kwa itikadi: Kama vile kuitakidi kitu kisichokuwa cha Kiislamu, mfano wake ni kuitakidi utume wa yeyote baada ya Muhammad (saw), kama anayeitakidi utume wa Qadiyani; huyo hukufuru kwa itikadi yake hii kwa sababu moyo wake umefungamana na kitu kisichokuwa cha Kiislamu.

b- Kwa shaka: Na hiyo ni kama vile kutilia shaka jambo la yakini katika mambo ya Kiislamu. Mwenye kutilia shaka utume wa Muhammad (saw) anakuwa kafiri kwa sababu hiyo, kwani moyo wake haujafungamana tena na kusadikisha utume wa Muhammad (saw).

c- Kwa kauli inayoashiria itikadi: Kama vile mtu kusema kuwa hakuna Muumba au kwamba Qur’ani Tukufu si maneno ya Allah. Mwenye kusema kauli kama hii anakuwa kafiri kwa kauli yake inayoashiria itikadi yake, lakini inashartiwa katika hali hii kuwa kauli hiyo isiwe na uwezekano wa kufafanuliwa kivingine (ta'wil), bali ukafiri ndani yake uwe wazi na wa kukatiki.

d- Kwa kitendo kinachoashiria itikadi: Kama vile kusujudu sanamu au kuswali swala ya Mayahudi na Manasara. Kitendo kama hiki kinaashiria itikadi ya mwenye nacho. Mwenye kusujudu sanamu au kuswali swala ya Mayahudi au swala ya Manasara, anakuwa amekufuru kwa kitendo chake hiki kutokana na kuashiria kwake itikadi inayopingana na Uislamu. Vilevile katika hali hii, kitendo hakitakiwi kuwa na uwezekano wa kufafanuliwa kivingine, bali ukafiri uwe wazi na wa kukatiki.

Hizi ndizo hali nne ambazo Muislamu hukufuru kwazo... Ama kuitakidi kitu kisichokuwa cha Kiislamu na kutilia shaka kitu cha kukatiki katika Uislamu, ni dhahiri kuwa hayo ni katika vitendo vya moyo kwa sababu itikadi na shaka zinahusiana na kusadikisha... Lakini kauli na kitendo vyenyewe si vitendo vya moyo, bali ni vitendo vya viungo na ulimi, isipokuwa vinapohusiana na kitendo cha moyo kwa kuashiria yaliyomo moyoni mwa itikadi, basi huchukuliwa kama itikadi katika mifano iliyotajwa hapo juu... Na kauli na vitendo vingine vyote visivyoashiria itikadi ya mwenye navyo vinabaki nje ya mzunguko wa ukafiri na imani, kama vile anayefanya maasi miongoni mwa maasi hali ya kuwa anakiri Uislamu na itikadi yake... Kwa hiyo, walichokuwa nacho Waislamu ni kutomkufurisha Muislamu kwa dhambi aliyoifanya isipokuwa kama ndani yake kuna kukanusha (inkar), kama asiyefunga na huku anakanusha faradhi ya saumu; huyu hukufuru kwa hilo. Ama yule asiyefunga na huku anakiri faradhi ya saumu, huyo ni fasiqi na si kafiri, kwa sababu takfiri haitokei isipokuwa kwa yakini. Takfiri ni jambo kubwa katika Uislamu na Mtume (saw) anasema:

إِذَا قَالَ الرَّجُلُ لِأَخِيهِ يَا كَافِرُ فَقَدْ بَاءَ بِهِ أَحَدُهُمَا

"Mtu akimwambia ndugu yake, 'Ewe kafiri,' basi mmoja wao ameshaingia katika ukafiri huo." (Imepokelewa na Al-Bukhari kupitia kwa Abu Hurairah). Na katika riwaya ya Ahmad kutoka kwa Ibn Umar, kutoka kwa Mtume (saw) amesema:

مَنْ كَفَّرَ أَخَاهُ فَقَدْ بَاءَ بِهَا أَحَدُهُمَا

"Mwenye kumkufurisha ndugu yake, basi mmoja wao ameshaingia katika ukafiri huo."

2- Hakika kusadikisha kwa kukatiki katika lugha kunaashiria lazima ya kuafikiana kwa ulimi na moyo. Kwa hivyo hatakiwi kukanusha kile anachokisadikisha kwa kukatiki. Hawezi mtu kusema "Mimi namuamini Allah, nakatiki kuwa Yeye ndiye Muumba wa ulimwengu huu na hana mshirika," kisha anasema kuwa "Allah anakosea" au "Ana mshirika" au "Si Muumba", au anakanusha alichokifaradhi Allah Subhanahu Muumba wa ulimwengu, ikiwa imethibiti kwa yakini kuwa Yeye Subhanahu amekifaradhi, kama kusema "Namwamini Allah" kisha anakanusha Swala au Saumu au jambo lolote linalojulikana katika dini kwa ulazima (ma'lum minad-din bid-dharurah)... Hakika huyu atakuwa kafiri kwa sababu anakanusha amri ya Allah iliyothibiti kwa kukatiki.

Kwa ajili hiyo, Ibilisi – laana za Allah ziwe juu yake – alikufuru kwa sababu alikanusha usahihi wa amri ya Allah kwake ya kumsujudia Adam, pamoja na kwamba aliamini kuwepo kwa Allah lakini alikanusha usahihi wa amri Yake Subhanahu pale aliposema Subhanahu:

قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِنْهُ خَلَقْتَنِي مِنْ نَارٍ وَخَلَقْتَهُ مِنْ طِينٍ

"Akasema (Mwenyezi Mungu): 'Nini kilichokuzuia kumsujudia nilipokuamuru?' Akasema: 'Mimi ni bora kuliko yeye; umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.'" (QS Al-A'raf [7]: 12). Hapo alitangaza kuwa Allah Subhanahu amekosea katika amri Yake ya kumsujudia... Ibilisi (laana za Allah ziwe juu yake) aliona kuwa usahihi ulikuwa Adam amsujudie yeye na si yeye amsujudie Adam, akakanusha (laana za Allah ziwe juu yake) usahihi wa amri ya Allah, na kwa hilo akawa miongoni mwa makafiri wahalifu... Hivyo ndivyo walivyokufuru wale waliokuwa na yakini juu ya ukweli wa ishara alizokuja nazo Musa (as) katika nyoyo zao, lakini wakazikanusha kwa ndimi zao na kuziita ni uchawi. Amesema Ta’ala:

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنْفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ

"Na wakazikanusha kwa dhuluma na kujitukuza, na hali nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi." (QS An-Naml [27]: 14).

Muhtasari:

Asili katika ukafiri ni kuwa ni itikadi (isiyo ya Kiislamu) na si kauli wala kitendo, isipokuwa kama kauli au kitendo kinaashiria itikadi au ndani yake kuna kukanusha jambo la kukatiki katika Uislamu. Katika hali hizi, kauli na kitendo huchukua hukumu ya itikadi na huwa ni ukafiri, na Allah atulinde na hilo.

  • Jibu la sehemu ya kwanza ya swali:

Ama jinsi ya kuepuka ukafiri na ushirikina na kufa nikiwa Muislamu, marejeo yake ni mambo mawili ya kimsingi:

1- Kufuata njia sahihi katika kuchukua itikadi kama ilivyobainishwa na Qur’ani Tukufu na Sunnah tukufu za Mtume. Tunaweza kujumuisha vipengele vyake muhimu katika nukta zifuatazo:

a- Kuchukua itikadi kwa yakini na si kwa dhana; yaani dalili zinazoashiria jambo linalohitajika ziwe ni dalili za kukatiki katika kuthibiti kwake na katika maana yake. Amesema Subhanahu:

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ لَيُسَمُّونَ الْمَلَائِكَةَ تَسْمِيَةَ الْأُنْثَى * وَمَا لَهُمْ بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِنْ يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا

"Hakika wasioamini Akhera, bila shaka huwaita Malaika kwa majina ya kike. Nao hawana ujuzi wa hayo, hawafuati ila dhana tu; na hakika dhana haitoshi kitu mbele ya haki." (QS An-Najm [53]: 27-28). Hivyo dhana haitoshi katika itikadi, bali lazima iwe yakini ya kukatiki.

b- Kutegemea katika kufahamu itikadi dalili za kiakili katika mambo yanayoingia chini ya hisia, kama vile kutafakari viumbe wa Allah, na kutegemea dalili za nakala (an-naqliyyah) zilizokuja kupitia Wahyi katika mambo ya ghaibu yasiyoingia chini ya hisia, na kusimama tu pale andiko lilipofika. Yaani kutofanya mambo ya itikadi ya Kiislamu na falsafa zake kuwa magumu, bali kuchukua kwake na kufahamu kwake kuwe kwa wepesi na usahili, na wakati huo huo kuwe kwa kina na mwangaza, kama vile walivyochukua na kufahamu maswahaba wa Mtume (saw):

  • Mtu atafakari na kuzingatia viumbe na kuviangalia, hapo atatambua kuwa vina Muumba. Amesema Ta’ala:

أَفَلَا يَنْظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ * وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ * وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ * وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ

"Je! Hawawaangalii ngamia jinsi walivyoumbwa? Na mbingu jinsi ilivyoinuliwa? Na milima jinsi ilivyowekwa? Na ardhi jinsi ilivyotandazwa?" (QS Al-Ghashiyah [88]: 17-20). Na amesema Ta’ala:

أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ * أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بَلْ لَا يُوقِنُونَ

"Je, wao wameumbwa pasina kitu chochote, au ni wao ndio waumbaji? Au wameumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini." (QS At-Tur [52]: 35-36). Na amesema Ta’ala:

وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِلْمُوقِنِينَ * وَفِي أَنْفُسِكُمْ أَفَلَا تُبْصِرُونَ

"Na katika ardhi zipo ishara kwa wenye yakini. Na katika nafsi zenu; je, hamuoni?" (QS Adh-Dhariyat [51]: 20-21).

  • Kisha azingatie aya za Qur’ani Tukufu, nayo imefanywa nyepesi kwa yule ambaye Allah amemfanyia wepesi:

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِنْ مُدَّكِرٍ

"Na bila shaka Tumeifanya Qur’ani iwe nyepesi kufahamika; basi je, yupo anayekumbuka?" (QS Al-Qamar [54]: 17). Na aamini yale yaliyomo ndani yake ya hukumu na mambo ya ghaibu, wala asijishughulishe na mambo ya ghaibu yasiyoingia chini ya hisia zake, bali ayaamini kama Wahyi ulivyokuja nayo. Hivyo aamini majina ya Allah mazuri kama yalivyokuja, wala asijishughulishe na dhati ya Allah Subhanahu:

لَا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

"Macho hayamfikii, Naye anayafikia macho; Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari." (QS Al-An'am [6]: 103). Na aamini mambo yote ya ghaibu: Siku ya Mwisho, Pepo, Moto n.k., na aishie kwenye yale tu yaliyokuja katika Qur’ani Tukufu na Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allah (saw), bila kuzidisha wala kupunguza. Amesema Subhanahu:

تِلْكَ مِنْ أَنْبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهَا إِلَيْكَ مَا كُنْتَ تَعْلَمُهَا أَنْتَ وَلَا قَوْمُكَ مِنْ قَبْلِ هَذَا فَاصْبِرْ إِنَّ الْعَاقِبَةَ لِلْمُتَّقِينَ

"Hizo ni katika khabari za ghaibu Tunazokufunulia (ewe Muhammad); hukuwa unazijua wewe wala watu wako kabla ya haya. Basi subiri, hakika mwisho mwema ni wa wacha Mungu." (QS Hud [11]: 49). Na amesema Ta’ala:

قُلْ لَا يَعْلَمُ مَنْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّهُ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ

"Sema: Hakuna yeyote katika mbingu na ardhi anayejua ghaibu isipokuwa Mwenyezi Mungu, wala wao hawatambui ni lini watafufuliwa." (QS An-Naml [27]: 65).

2- Muislamu awe mkweli katika nia yake kwa Allah Subhanahu, mkweli kwa Mtume wake (saw), mwenye kumtegemea Allah Ta'ala, akiongozwa na uongofu Wake, akimcha Yeye, akijiepusha na dhuluma na uasi, akimuomba Allah Subhanahu amthibitishe juu ya haki na imani kama ilivyokuja katika hadith tukufu iliyopokelewa na At-Tirmidhi katika Sunan yake kutoka kwa Anas amesema: Mtume wa Allah (saw) alikuwa akikithiri kusema:

يَا مُقَلِّبَ القُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ

"Ewe Mgeuzi wa nyoyo, thibitisha moyo wangu juu ya dini Yako." Na kutokana na hilo, Allah atamthibitisha kwa idhini Yake kwa kauli thabiti:

يُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ وَيُضِلُّ اللَّهُ الظَّالِمِينَ وَيَفْعَلُ اللَّهُ مَا يَشَاءُ

"Mwenyezi Mungu huwathibitisha wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha wapotee madhalimu; na Mwenyezi Mungu hufanya Atakavyo." (QS Ibrahim [14]: 27). Na kila anapomcha Allah, akawa mkweli na mwaminifu, basi Allah atamfanyia wepesi jambo lake. Amesema Ta’ala:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَى وَاتَّقَى * وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَى * فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَى * وَأَمَّا مَنْ بَخِلَ وَاسْتَغْنَى * وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَى * فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَى * وَمَا يُغْنِي عَنْهُ مَالُهُ إِذَا تَرَدَّى * إِنَّ عَلَيْنَا لَلْهُدَى * وَإِنَّ لَنَا لَلْآخِرَةَ وَالْأُولَى

"Basi ama yule anayetoa na akamcha Mungu, na akasadikisha neno jema, Tutamfanyia wepesi njia ya kuelekea kwenye urahisi (Pepo). Na ama yule anayefanya ubakhili na akajiona kuwa amejitosheleza, na akakanusha neno jema, basi Tutamfanyia wepesi njia ya kuelekea kwenye ugumu (Moto). Na mali yake hayatamfaa chochote atakapoangamia. Hakika ni juu Yetu kutoa uongofu. Na hakika ni Yetu Sisi Akhera na ya kwanza (dunia)." (QS Al-Layl [92]: 5-13).

3- Na mwisho, namtanabahisha muulizaji kuwa Muislamu anayeamini itikadi ya Kiislamu, yaani anayeamini Allah, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake, Siku ya Mwisho, na Qadhwa na Qadar kheri yake na shari yake kama ilivyokuja katika kitabu cha Allah Subhanahu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا آَمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي أَنْزَلَ مِنْ قَبْلُ وَمَنْ يَكْفُرْ بِاللَّهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الْآَخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

"Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na Kitabu alichokiteremsha kwa Mtume Wake, na Kitabu alichokiteremsha kabla. Na anayemkataa Mwenyezi Mungu, na Malaika Wake, na Vitabu Vyake, na Mitume Wake, na Siku ya Mwisho, basi bila shaka amepotea upotovu ulio mbali." (QS An-Nisa [4]: 136).

Na kama ilivyokuja katika hadith ya Mtume (saw) iliyotolewa na Al-Bukhari kutoka kwa Abu Hurairah, na Muslim kutoka kwa Abdullah bin Umar na tamshi ni la Muslim: Abdullah bin Umar amesema, baba yangu Umar bin Al-Khattab alinihadithia: Siku moja tukiwa kwa Mtume wa Allah (saw), alitutokea mtu mwenye nguo nyeupe sana, mwenye nywele nyeusi sana, hakuonekana kuwa na alama za safari, na hakuna yeyote miongoni mwetu aliyemtambua. Alikaa mbele ya Mtume (saw), akaegemeza magoti yake kwenye magoti yake, na akaweka viganja vyake juu ya mapaja yake, akasema: "Ewe Muhammad, nieleze kuhusu Uislamu." Mtume wa Allah (saw) akasema:

«الْإِسْلَامُ أَنْ تَشْهَدَ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللهِ e، وَتُقِيمَ الصَّلَاةَ، وَتُؤْتِيَ الزَّكَاةَ، وَتَصُومَ رَمَضَانَ، وَتَحُجَّ الْبَيْتَ إِنِ اسْتَطَعْتَ إِلَيْهِ سَبِيلًا»

"Uislamu ni kushuhudia kuwa hakuna mungu isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah, kusimamisha Swala, kutoa Zaka, kufunga Ramadhani, na kuhiji Nyumba ukiwa na uwezo." Akasema: "Umesema kweli." Tukashangazwa naye, anamuuliza kisha anamsadikisha! Akasema: "Nieleze kuhusu Imani." Akasema:

«أَنْ تُؤْمِنَ بِاللهِ، وَمَلَائِكَتِهِ، وَكُتُبِهِ، وَرُسُلِهِ، وَالْيَوْمِ الْآخِرِ، وَتُؤْمِنَ بِالْقَدَرِ خَيْرِهِ وَشَرِّهِ»

"Ni kumuamini Allah, Malaika wake, Vitabu vyake, Mitume wake, Siku ya Mwisho, na kuamini Qadar kheri yake na shari yake." Akasema: "Umesema kweli." Akasema: "Nieleze kuhusu Ihsan." Akasema:

«أَنْ تَعْبُدَ اللهَ كَأَنَّكَ تَرَاهُ، فَإِنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فَإِنَّهُ يَرَاكَ»

"Ni kumuabudu Allah kama vile unamuona, na ikiwa humuoni, basi Yeye anakuona." ... Akasema: Kisha akaondoka, nikakaa kwa muda, kisha (Mtume) akaniambia: "Ewe Umar, unamjua muulizaji?" Nikasema: "Allah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi." Akasema: "Huyo ni Jibril, amewajia kuwafundisha dini yenu."

Mwisho kabisa, namuomba Allah Subhanahu amjaalie muulizaji maisha mema atakayoyatumia katika kumtii Allah Subhanahu na kumtii Mtume Wake (saw), ili afuzu katika nyumba mbili, na huko ndiko kufuzu kukubwa.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta

3 Sha'ban 1438 H Ikiwafikiana na 30/04/2017 M

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Google Plus

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri kwenye Twitter

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri Web

Share Article

Share this article with your network