(Silsila ya majibu ya mwanachuoni mkubwa Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Jibu la Swali
Kwa Hasan Muhammad
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh, Mwenyezi Mungu akuhifadhi Amir wetu na Sheikh wetu, na akusaidie na kukunusuru,
Sheikh wetu mpendwa, kuna swali la haraka ikiwa utaniruhusu, kwani linahitaji majibu ili tujue jinsi ya kushughulikia suala ambalo tumejulishwa kuwa litatokea...
Suala lenyewe ni kwamba kuna mradi uliopo wa kujenga seli za jua kwa ajili ya umeme juu ya nguzo, na kutokana na mgogoro wa umeme unaokabili mji wa Yatta kule Hebron wanataka kutekeleza mradi huu, lakini suala ambalo nataka kuuliza haswa ni kwamba wanataka kuweka seli hizi juu ya ardhi yenye ukubwa wa dunam 15 ya makaburi ya kale na mapya. Je, inajuzu kuweka seli hizi katika makaburi haya na kando ya makaburi na juu ya nguzo zinazoyafunika makaburi kwa juu?
Mwenyezi Mungu akulipe kheri.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Hakika Mtume ﷺ amebainisha kuwa makaburi yana heshima, hivyo haijuzu kuyafukua au kuyakalia au aina yoyote ya vitendo vinavyogusa kaburi kwa namna inayopingana na heshima ya makaburi, na miongoni mwa dalili za hilo ni:
1- Abu Dawood ametoa kupitia njia ya Aisha (ra):
أَنَّ رَسُولَ اللهِ ﷺ قَالَ: كَسْرُ عَظْمِ الْمَيِّتِ كَكَسْرِهِ حَيّاً
"Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema: Kuvunja mfupa wa maiti ni kama kuuvunja akiwa hai." (Imepokewa na Abu Dawood)
Na imekuja katika Aun al-Ma'bud Sharh Sunan Abi Dawood: Al-Suyuti amesema katika kubainisha sababu ya hadithi hii, kutoka kwa Jabir (ra) amesema: Tulitoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ katika jeneza, Mtume ﷺ akaketi ukingoni mwa kaburi na tukaketi naye, mchimba kaburi akatoa mfupa wa muundi au wa mkono na akaenda kuuvunja, Mtume ﷺ akasema:
لَا تَكْسِرْهَا فَإِنَّ كَسْرَكَ إِيَّاهُ مَيِّتاً كَكَسْرِكَ إِيَّاهُ حَيّاً وَلَكِنْ دُسَّهُ فِي جَانِبِ الْقَبْرِ
"Usivunje, kwani kuuvunja ukiwa mfu ni kama kuuvunja ukiwa hai, lakini ufiche (uzike) kando ya kaburi."
Maana yake ni kwamba mfupa ikiwa upo ni lazima uhifadhiwe na uachwe ndani ya udongo.
Kwa hiyo, kufukua makaburi ya Waislamu haijuzu isipokuwa kama mifupa itakuwa imeoza na kuwa kama mchanga, na hapo ndipo inajuzu kupanda mimea na kujenga juu yake, na vitendo vingine miongoni mwa mambo yaliyoruhusiwa (mubaha). Ama ikiwa mfupa upo, haijuzu kufukua makaburi na kujenga juu yake au vitendo vinginevyo isipokuwa katika hali maalum zinazohusiana na maiti au mfano wa hayo (kama maandiko yalivyobainisha). Ama kuhusu muda gani unahitajika ili kujua kuwa maiti ameoza au la, hilo linarejelewa kwa wataalamu (ahlul khibra) na uhakiki wa uhalisia (tahqiq al-manat).
2- Hakuna hitilafu miongoni mwa mafaqihi kwamba kukalia makaburi ikiwa ni kwa ajili ya kukidhi haja ndogo au kubwa haijuzu kwa kauli moja. Na wamehitilafiana ikiwa ni kwa ajili ya jambo lingine... Imekuja katika Al-Mawsu'ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaitiyyah:
(Wamesema Hanafi – na ndiyo madhehebu yao –, Shafi’i na Hanbali kuwa ni makruhu (haipendezi) kukalia makaburi, kutokana na alichopokea Abu Marthad al-Ghanawi: "Kwamba Mtume ﷺ amesema:
لاَ تَجْلِسُوا عَلَى الْقُبُورِ وَلاَ تُصَلُّوا إِلَيْهَا
"Msiketi juu ya makaburi na wala msiswali kuelekea kwayo." (Imepokewa na Muslim)
Na kutoka kwa Abu Hurairah (ra) amesema: Mtume ﷺ amesema:
لأَنْ يَجْلِسَ أَحَدُكُمْ عَلَى جَمْرَةٍ فَتُحْرِقَ ثِيَابَهُ فَتَخْلُصَ إِلَى جِلْدِهِ خَيْرٌ لَهُ مِنْ أَنْ يَجْلِسَ عَلَى قَبْرٍ
"Hakika mmoja wenu kukalia mkaa wa moto mpaka ukaunguza nguo zake na kufika kwenye ngozi yake ni bora kwake kuliko kukalia kaburi." (Imepokewa na Muslim)
Wamesema Hanafi na Shafi’i: Na akitaka kuketi wakati wa kuzuru makaburi, aketi mbali au karibu kulingana na hadhi yake (maiti) wakati wa uhai wake. Na ibara ya Shafi’i ni: Inampasa mgeni asogee karibu na kaburi kiasi kile ambacho angesogea karibu na mwenyewe wakati wa uhai wake ikiwa angemzuru.
Na Al-Tahawi miongoni mwa Hanafi anaona, na akasubutisha kauli hii kwa Abu Hanifa, Abu Yusuf na Muhammad, kuwa inajuzu kuketi juu ya kaburi, na hili pia ndilo walilolifuata Maliki, kutokana na ilivyopokelewa kuwa Ali (ra) alikuwa akiegemea kaburi na kuketi juu yake. Al-Tahawi amesema: Na chukizo (karaha) huondoka kabisa ikiwa kuketi huko ni kwa ajili ya kusoma.) Mwisho.
3- Hivyo basi, ikiwa inakusudiwa kuanzisha mradi wa kujenga seli za jua kwa ajili ya umeme juu ya nguzo kwenye ardhi yenye ukubwa wa dunam 15 ya makaburi ya kale na mapya... basi inatakiwa kutazamwa:
Je, inawezekana kusimamisha nguzo hizi na kutekeleza seli hizo bila kukanyaga makaburi au kuyaumiza makaburi au kuyafukua au kudhihiri mifupa yake, hususan makaburi ya kale? Mimi naona hilo ni vigumu... Ama mkisema kuwa tutahakikisha hatukanyi kaburi lolote na wala hakuna nguzo yoyote itakayowekwa juu ya kaburi lolote katika makaburi mapya, basi inawezekana kuwa na ukweli kwa kauli hii kwa upande wa makaburi mapya kwa sababu yanaonekana wazi na inawezekana kuyaepuka... lakini makaburi ya kale, ikiwa makaburi hayo hayaonekani, ni vipi itahakikishwa kutopita juu yake na mfano wa hayo?
Kwa hiyo, ili kuepuka haramu au angalau kuepuka makruhu, jiepusheni na makaburi na tafuteni sehemu nyingine... Na Mwenyezi Mungu ndiye Anayejua zaidi na Mwenye hekima zaidi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
11 Rabi’ al-Awwal 1440 H Inalingana na 19/11/2018 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amhifadhi) kwenye Google Plus
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir Web