Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Yale Ambayo Benki za Kiislamu Huita Murabahah na Hukumu ya Sharia Kuhusu Hilo!

August 31, 2020
5575

Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Yale Ambayo Benki za Kiislamu Huita Murabahah na Hukumu ya Sharia Kuhusu Hilo!

Kwa Ashraf Abdul Halim Titi

Swali:

Assalamu Alaikum. Tunajua kwamba Murabahah kama dhana inaruhusiwa kisheria, lakini naamini kuwa uhalisia wa Murabahah hivi sasa katika benki za Kiislamu unapingana na Sharia, hasa kwa watu wetu wa Palestina. Mteja huchagua bidhaa kwa mfanyabiashara na kukubaliana naye bei, kisha hufanya mkataba na benki, na benki huinunua bidhaa hiyo na kumkabidhi mteja. Benki huweka rehani bidhaa hiyo, iwe ni nyumba au gari au nyinginezo, kisha huhamisha umiliki wake baada ya kulipa kiasi kinacholingana na thamani ya bidhaa kikijumuisha kiasi cha ziada au asilimia fulani inayoamuliwa kulingana na muda wa malipo. Benki huhesabu kiasi hicho cha ziada kama gharama za usimamizi wa muamala... Je, mnaweza kufafanua hukumu ya Sharia katika miamala ya aina hii? Barakallahu fikum.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Swali lako linajumuisha mambo matatu:

Kwanza: Murabahah na hukumu yake...

Pili: Yale ambayo benki za Kiislamu huyaita kuwa ni Murabahah...

Tatu: Suala la kuweka rehani bidhaa iliyonunuliwa...

Na huu hapa ndio ufafanuzi:

  • Kuhusu uhalisia wa Murabahah na hukumu yake, tulishafafanua hilo katika jibu la swali la tarehe 19 Rajab 1434 AH - 29 Mei 2013, na miongoni mwa yaliyokuja katika jibu hilo ni haya yafuatayo:

[... Murabahah kilugha inamaanisha kupata faida (rib-h). Inasemwa: Nimeuza bidhaa kwa murabahah, au nimeinunua kwa murabahah.

Kistilah: Ni pale muuzaji anapotoa bidhaa yake ili auze kwa gharama aliyoipata yeye pamoja na faida inayojulikana. Ni miongoni mwa miamala ya uaminifu (buyu’ al-amanat) kwa sababu inategemea uaminifu wa muuzaji katika kuelezea gharama ya bidhaa kwake.

Nayo inaruhusiwa kisheria kwa sababu ni ununuzi kwa faida juu ya bei ambayo muuzaji aliinunulia. Ikiwa muuzaji atasema: "Nakuuzia bidhaa hii kwa faida kadhaa juu ya bei niliyoifanyia ununuzi," na mnunuzi akajua bei hiyo na akakubali, basi hii inajuzu kwa sababu ni uuzaji unaojulikana.] Mwisho.

  • Ama kuhusu yale yaliyokuja katika swali lako kuhusu kile kinachoitwa uuzaji wa Murabahah katika benki za Kiislamu, tulishajibu suala hili kwa kina mnamo tarehe 24 Rajab al-Fard 1434 AH - 03 Juni 2013, na nakurejeshea yaliyokuja katika jibu hilo:

[... Miamala ya benki za Kiislamu inayoitwa uuzaji wa Murabahah ni miamala inayopingana na Sharia, kutokana na vipengele kadhaa, ambavyo muhimu zaidi ni:

Kwanza: Kwamba benki hufanya mkataba wa mauzo na mnunuzi kabla ya benki yenyewe kununua gari au jokofu... Na Mtume ﷺ amekataza kuuza kile ambacho hukimiliki. Kutoka kwa Hakim bin Hizam, amesema: Nilisema: Ewe Mtume wa Allah, anakuja mtu akiniomba nimuuzie bidhaa ambayo sina, kisha naiuza kwake (naenda) sokoni, akasema:

لَا تَبِعْ مَا لَيْسَ عِنْدَكَ

"Usiuze kile ambacho hakiko kwako." (Imepokelewa na Ahmad). Huyu alimuuliza Mtume ﷺ kuhusu mnunuzi anayemjia ili kununua bidhaa ambayo haiko naye, kisha anaenda sokoni na kuinunua na kumuuzia, Mtume ﷺ akamkataza kufanya hivyo isipokuwa bidhaa iwe naye kwanza kisha amuonyeshe mnunuzi; akitaka ainunue na asipotaka asiinunue.

Ili kufafanua hili tunasema: Mtu anayeenda benki kuomba mkopo wa fedha... Benki humuuliza kwa nini unataka mkopo au pesa, mtu huyo husema ili ninunue jokofu au gari au mashine ya kufua nguo... Kisha benki hufanya makubaliano na mtu huyo kuwa itamnunulia jokofu na kumuuzia kwa awamu kwa bei kadhaa, na hayo yanakuwa makubaliano ya lazima kabla ya benki kununua jokofu hilo, kisha benki huenda na kununua jokofu kwa ajili ya mtu huyo, na mtu huyo hawezi kuacha kununua jokofu kutoka kwa benki, kwa sababu makubaliano na benki yalifanyika kabla ya jokofu kuwa milki ya benki, hivyo mkataba umekamilika kabla ya benki kumiliki jokofu.

Wala isisemwe kuwa benki inamuuzia mnunuzi baada ya benki kuwa tayari imeshainunua, isisemwe hivyo kwa sababu makubaliano ya benki na mnunuzi yameshafanyika kwa namna ya ulazima kabla ya benki kununua bidhaa, kwa ushahidi kwamba mnunuzi hawezi kukataa kuinunua baada ya benki kumnunulia, hivyo mkataba umefanyika kwa namna ya kisheria kabla ya benki kuinunua.

Na kama benki ingekuwa na ghala lenye majokofu na ikamwonyesha mtu, akitaka ananunua na asipotaka hanunui, kama muuzaji mwingine yeyote wa majokofu, hapo basi uuzaji ungeswihi kwa fedha taslimu au kwa awamu.

Pili: Haidjuzu ikiwa mnunuzi amechelewa kulipa awamu miongoni mwa awamu, deni likaongezwa kwa mnunuzi kwa sababu hii ni riba, nayo ndiyo inayoitwa riba al-nasi’ah, na ilikuwa ikifanyiwa kazi wakati wa ujahiliya. Ilikuwa ikifika muda wa kulipa deni na mdaiwa akashindwa kulipa, basi muda huongezwa na deni huongezwa. Uislamu ukaja na kuuharamisha uharamishaji wa moja kwa moja, na ukampa muda mdaiwa mwenye dhiki bila ya nyongeza katika deni:

وَإِنْ كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ وَأَنْ تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَكُمْ إِنْ كُنْتُمْ تَعْلَمُونَ

"Na ikiwa (mdaiwa) ni mwenye dhiki, basi (mpe) muda mpaka apate wepesi. Na mkisamehe, ni bora kwenu, ikiwa mnajua." (Surah Al-Baqarah [2]: 280).

Kwa hivyo, haijuzu kufanya muamala na benki kulingana na yaliyotajwa hapo juu.] Mwisho.

  • Ama suala la kuweka rehani bidhaa iliyonunuliwa mpaka kulipwa kwa awamu zote, tulishajibu hilo mnamo tarehe 06 Sha'ban 1436 AH - 24/05/2015 kwa jibu la kina ambalo ndani yake mlikuja:

[... Suala hili linajulikana katika fiqhi kwa jina la (rehn al-mabi' 'ala thamanihi), yaani bidhaa iliyouzwa kubaki kama rehani kwa muuzaji mpaka mnunuzi alipe thamani yake. Suala hili halijitokezi ikiwa muuzaji na mnunuzi ni kama alivyosema Mtume wa Allah ﷺ katika hadith aliyoitoa Bukhari kutoka kwa Jabir bin Abdullah (ra):

رَحِمَ اللَّهُ رَجُلاً سَمْحاً إِذَا بَاعَ، وَإِذَا اشْتَرَى، وَإِذَا اقْتَضَى

"Mwenyezi Mungu amrehemu mtu ambaye ni mkarimu anapouza, anaponunua, na anapodai."

Lakini wakati mwingine wanatofautiana kuhusu nani aanze kupokea bidhaa kwanza au kulipa thamani kwanza, na muuzaji anaweza kukusudia baada ya mkataba wa mauzo kuizuia bidhaa, yaani kuiweka kama rehani kwake mpaka alipwe thamani yake. Kutokana na hapo linazuka suala hili, ambalo limetofautiana miongoni mwa mafaqihi; kuna wanaoliruhusu kwa masharti, na kuna wasioliruhusu, na kuna wengine wanaoliruhusu katika hali moja na kutoiliruhusu katika hali nyingine... na kadhalika.

Na lile ninalolionelea kuwa na nguvu zaidi baada ya kusoma suala hili ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Aina ya bidhaa iliyouzwa:

1- Bidhaa iwe ya kupimwa kwa pishi au uzani au kukadiria (urefu)... n.k., kama vile uuzaji wa mchele, pamba au vitambaa... n.k.

2- Bidhaa iwe si ya kupimwa kwa pishi au uzani... n.k., kama vile uuzaji wa gari, nyumba au mnyama... n.k.

Pili: Thamani ya bidhaa:

1- Iwe ni ya hapo kwa hapo (hallan), yaani taslimu, kama vile kununua bidhaa kwa elfu kumi taslimu zinazolipwa mara moja.

2- Iwe ni ya muda mrefu (mu'ajjalan), kama vile kununua bidhaa kwa elfu kumi utakazolipa baada ya mwaka.

3- Sehemu yake iwe ya haraka na sehemu nyingine ya baadae, kama kununua bidhaa kisha unalipa malipo ya kwanza elfu tano, na unalipa elfu tano nyingine baada ya mwaka mfano, au unailipa kwa awamu za kila mwezi...

Tatu: Hukumu ya kisheria inatofautiana kulingana na mambo yaliyotajwa hapo juu:

Hali ya Kwanza: Bidhaa ambayo si ya kupimwa kwa pishi wala uzani... yaani kama uuzaji wa nyumba, gari au mnyama...:

1- Thamani iwe taslimu, yaani unanunua gari kwa elfu kumi taslimu, na hili liwe limethibitishwa katika mkataba.

Katika hali hii, inajuzu kwa muuzaji kuizuia bidhaa, yaani ibaki kama rehani kwake mpaka ilipwe thamani ya haraka kulingana na mkataba. Dalili ya hilo ni hadith tukufu aliyoitoa Tirmidhi na akasema kuihusu ni "hadith hasan" kutoka kwa Abu Umamah amesema: Nilimsikia Mtume ﷺ akisema katika hotuba ya mwaka wa Hijja ya Kuaga:

العَارِيَةُ مُؤَدَّاةٌ، وَالزَّعِيمُ غَارِمٌ، وَالدَّيْنُ مَقْضِيٌّ

"Kitu kilichoazimwa lazima kirudishwe, mdhamini anawajibika, na deni lazima lilipwe."

Al-Zaeem: mdhamini; Gharim: anayewajibika kufidia. Na namna ya kutolea ushahidi katika hadith hii ni kauli yake ﷺ "na deni lazima lilipwe," kwani mnunuzi akipokea bidhaa kabla ya kulipa thamani basi atakuwa ameinunua kwa deni, na "deni lazima lilipwe," yaani kipaumbele ni kulipa deni maadamu ununuzi ulikuwa wa taslimu, na kwa maneno mengine alipe thamani kwanza maadamu thamani katika mkataba ilikuwa taslimu ya hapo kwa hapo... Al-Kasani anasema katika Bada’i al-Sana’i akifafanua hadith hii: (Kauli yake – amani na swala zimshukie – "Deni lazima lilipwe," ameielezea – amani na swala zimshukie – deni kwa kuwa ni lenye kulipwa kwa ujumla au moja kwa moja; hivyo kama ukicheleweshwa ukabidhi wa thamani (pesa) kuliko ukabidhi wa bidhaa basi deni hili litakuwa halijalipwa, na huku ni kwenda kinyume na andiko.)

Kwa hivyo, inajuzu kwa muuzaji kuizuia bidhaa kwake mpaka mnunuzi alipe thamani, na kwa hilo hapatakuwa na deni, na hili linaendana na mkataba kwa sababu uuzaji haukuwa wa deni bali ulikuwa wa thamani taslimu.

2- Thamani iwe ya muda mrefu (deni), kama kununua gari kwa elfu kumi utakazolipa baada ya mwaka, basi katika hali hii haijuzu kuizuia bidhaa mpaka malipo ya thamani yakamilike kwa sababu thamani ni ya muda mrefu kulingana na mkataba kwa makubaliano ya muuzaji, hivyo haijuzu kwake kuizuia bidhaa ili kudhamini thamani yake maadamu yeye ameiuzia kwa thamani ya baadae, na amedondosha haki yake mwenyewe ya kuizuia bidhaa, na kwa hivyo haijuzu kwake kuizuia bidhaa bali amkabidhi mnunuzi.

3- Thamani iwe imegawanyika, ya haraka na ya baadae, kama kununua gari kwa malipo ya awali elfu tano unazolipa taslimu sasa, na elfu tano nyingine unalipa baada ya mwaka mara moja, au unalipa kwa awamu katika nyakati zijazo.

Katika hali hii, inajuzu kwa muuzaji kuizuia bidhaa mpaka yalipwe malipo ya haraka, na baada ya hapo haijuzu kwake kuizuia bidhaa ili kukamilisha malipo ya baadae (awamu), na hiyo ni kutokana na tuliyoyataja katika vipengele 1 na 2.

Kwa ufupi ni kwamba inajuzu kwa muuzaji kuweka rehani bidhaa kwa thamani yake ya haraka, yaani ikiwa mkataba wa mauzo ni kwa thamani ya haraka inayolipwa sasa, basi inajuzu kwa muuzaji kuizuia bidhaa kwake mpaka mnunuzi alipe thamani ya haraka kulingana na mkataba wa mauzo.

Vile vile inajuzu kwa muuzaji kuizuia bidhaa kwake mpaka mnunuzi alipe malipo ya awali ya haraka kulingana na mkataba wa mauzo.

Wala isisemwe hapa mnunuzi anawekaje rehani bidhaa yake kabla ya kuichukua (qabdh), yaani kabla ya kuimiliki? Hiyo ni kwa sababu rehani haijuzu isipokuwa katika kile kinachojuzu kuuzwa, na kwa kuwa bidhaa iliyonunuliwa haijuzu kuuzwa isipokuwa baada ya kuichukua kulingana na hadith ya Mtume wa Allah ﷺ.

Mtume ﷺ aliyopokea Bayhaqi, kutoka kwa Ibn Abbas amesema: Mtume wa Allah ﷺ alimwambia Attab bin Asid:

إني قد بعثتك إلى أهل الله، وأهل مكة، فانههم عن بيع ما لم يقبضوا

"Hakika mimi nimekutuma kwa watu wa Allah, na watu wa Makkah, basi wakataze kuuza kile ambacho hawajakipokea (hakiko mikononi mwao)."

Na hadith aliyoipokea Tabarani kutoka kwa Hakim bin Hizam amesema: Ewe Mtume wa Allah, mimi nauza mauzo mengi, ni yapi kati ya hayo ni halali kwangu na yapi ni haramu kwangu? Akasema:

لَا تَبِيعَنَّ مَا لَمْ تَقْبِضْ

"Usiuze kabisa kile ambacho hujakipokea."

Basi hadith hizi ziko wazi katika kukataza kuuza kile ambacho hawajakichukua, sasa itakuwaje basi aiweke rehani bidhaa kabla ya kuichukua?

Isisemwe hivyo kwa sababu hadith hizi mbili ni kwa ajili ya bidhaa za kupimwa kwa pishi na uzani... Ama ikiwa bidhaa ni nyinginezo kama nyumba, gari na mnyama... basi inajuzu kuiuza kabla ya kuichukua kulingana na hadith ya Mtume ﷺ aliyoitoa Bukhari kutoka kwa Ibn Umar (ra), amesema: Tulikuwa na Mtume ﷺ safarini, nami nilikuwa nimepanda ngamia msumbufu wa Umar, alikuwa akinishinda na kutangulia mbele ya watu, Umar akimfokea na kumrudisha nyuma, kisha anatangulia tena na Umar anamfokea na kumrudisha nyuma, Mtume ﷺ akamwambia Umar: "Niuzie", (Umar) akasema: "Yeye ni wako ewe Mtume wa Allah", (Mtume) akasema: "Niuzie", basi akamuuzia Mtume wa Allah ﷺ, Mtume ﷺ akasema: "Yeye ni wako ewe Abdullah bin Umar, mfanyie unachotaka." Na huu ni muamala katika bidhaa kwa njia ya zawadi kabla ya kuichukua, jambo ambalo linaonyesha utimilifu wa milki ya bidhaa kabla ya kuichukua, na linaonyesha kujuzu kuiuza kwa sababu milki ya muuzaji imeshatimia.

Kwa hivyo, inajuzu kuweka rehani bidhaa kabla ya kuichukua maadamu inajuzu kuiuza kabla ya kuichukua, lakini hii ni katika hali tu ambayo bidhaa si ya kupimwa kwa pishi wala uzani... kama nyumba, gari, mnyama na mfano wa hayo, na katika hali ya kufanyika kwa mauzo kwa thamani ya haraka, au katika hali ya kuwepo kwa malipo ya awali ya haraka katika mkataba wa mauzo, basi inajuzu kuweka rehani bidhaa kabla ya kuichukua mpaka ilipwe thamani ya haraka au malipo ya awali ya haraka.

Hali ya Pili: Bidhaa ni ya kupimwa kwa pishi na uzani... kama kununua kiasi cha mchele, au pamba au kiasi cha vitambaa... basi katika hali hii haijuzu kuizuia bidhaa kwa thamani yake haijalishi uhalisia wa thamani hiyo ukoje: iwe ya haraka, au ya baadae ya mara moja au ya awamu:

Ikiwa thamani ni ya baadae, basi haijuzu kwake kuizuia bidhaa kama tulivyofafanua hapo juu.

Na ikiwa thamani ni ya haraka, pia haijuzu kwake kuizuia bidhaa, yaani kuiweka rehani, kwa sababu haijuzu kuweka rehani bidhaa ya kupimwa kwa pishi na uzani kabla ya kuichukua kulingana na hadith ya Mtume ﷺ tuliyoitaja hapo juu. Na muuzaji hapa katika hali ya uuzaji kwa thamani ya haraka yuko kati ya mambo mawili:

Ama amuuzie bidhaa kwa thamani ya haraka na kumkabidhi na amvumilie ikiwa atampa thamani sasa au baada ya muda mfupi bila ya kuizuia bidhaa kuwa rehani... Ama asiize bidhaa hiyo, yaani bila ya kuiweka rehani bidhaa hiyo kwa hali yoyote.

Kwa hivyo, ikiwa mauzo yatafanyika kwa thamani ya haraka au ya baadae katika hali ambayo bidhaa ni ya kupimwa kwa pishi au uzani, basi haijuzu kwa muuzaji kuizuia bidhaa kama rehani kwake mpaka malipo ya thamani yafanyike.

Na hili ndilo ninalolionelea kuwa na nguvu zaidi, na Allah ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.] Mwisho.

Kwa haya yote, jibu la swali lako litakuwa limekamilika, na Allah ndiye Msaidizi.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

12 Muharram Al-Haram 1442 AH Inayoafikiana na 31/08/2020

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu Amlinde) kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu Amlinde) kwenye Web

Share Article

Share this article with your network