Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Uhakika wa Swala ya Istikhara

February 11, 2016
7334

P

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali:

Kwa Joud Radwan Radwan

Swali:

Assalamu Alaykum, nataka kujua uhakika wa Swala ya Istikhara, na je, mwenye kuswali Istikhara huona kitu katika ndoto yake baada ya Istikhara? Tafadhali jibu haraka iwezekanavyo na Mwenyezi Mungu akujazi kheri.

Jibu:

Wa Alaykum Salam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Hakika Mtume (saw) amebainisha Swala ya Istikhara ubainifu wa kutosha na uliowazi katika hadith iliyopokelewa na Al-Bukhari na wengineo kutoka kwa Jabir bin Abdullah (ra), amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa akitufundisha Istikhara katika mambo yote, kama alivyokuwa akitufundisha sura katika Qur'an, akisema:

إِذَا هَمَّ أَحَدُكُمْ بِالأَمْرِ، فَلْيَرْكَعْ رَكْعَتَيْنِ مِنْ غَيْرِ الفَرِيضَةِ، ثُمَّ لِيَقُلْ: اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْتَخِيرُكَ بِعِلْمِكَ وَأَسْتَقْدِرُكَ بِقُدْرَتِكَ، وَأَسْأَلُكَ مِنْ فَضْلِكَ العَظِيمِ، فَإِنَّكَ تَقْدِرُ وَلاَ أَقْدِرُ، وَتَعْلَمُ وَلاَ أَعْلَمُ، وَأَنْتَ عَلَّامُ الغُيُوبِ، اللَّهُمَّ إِنْ كُنْتَ تَعْلَمُ أَنَّ هَذَا الأَمْرَ خَيْرٌ لِي فِي دِينِي وَمَعَاشِي وَعَاقِبَةِ أَمْرِي - أَوْ قَالَ عَاجِلِ أَمْرِي وَآجِلِهِ - فَاقْدُرْهُ لِي وَيَسِّرْهُ لِي، ثُمَّ بَارِكْ لِي فِيهِ، وَإِنْ كُنْتَ تَعْلَمُ أَنَّ هَذَا الأَمْرَ شَرٌّ لِي فِي دِينِي وَمَعَاشِي وَعَاقِبَةِ أَمْرِي - أَوْ قَالَ فِي عَاجِلِ أَمْرِي وَآجِلِهِ - فَاصْرِفْهُ عَنِّي وَاصْرِفْنِي عَنْهُ، وَاقْدُرْ لِي الخَيْرَ حَيْثُ كَانَ، ثُمَّ أَرْضِنِي

"Ikiwa mmoja wenu atakusudia jambo, basi aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme: Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba uongofu kupitia ujuzi Wako, na nakuomba uwezo kupitia uwezo Wako, na nakuomba katika fadhila Zako kuu, kwani Wewe unaweza na mimi siwezi, na Wewe unajua na mimi sijui, na Wewe ni Mjuzi wa yaliyofichikana. Ewe Mwenyezi Mungu, ikiwa unajua kuwa jambo hili ni kheri kwangu katika dini yangu, maisha yangu na mwisho wa jambo langu - au akasema: katika jambo langu la sasa na la baadaye - basi nikadirie, nifanyie wepesi kisha nibarikie ndani yake. Na ikiwa unajua kuwa jambo hili ni shari kwangu katika dini yangu, maisha yangu na mwisho wa jambo langu - au akasema: katika jambo langu la sasa na la baadaye - basi liepushe nami na uniepushe nalo, na unikadirie kheri popote ilipo, kisha uniridhishe nalo." Akasema: "Na alitaje hitaji lake." (Mwisho).

Ni wazi kutokana na hadith hii namna ya Swala ya Istikhara; hivyo basi, anayetaka kufanya Istikhara aswali rakaa mbili za nafila kwa nia ya Istikhara, na baada ya kumaliza swala, aombe kwa dua ya Istikhara iliyotajwa katika hadith. Kwa kufanya hivi, anakuwa amekamilisha Swala ya Istikhara au dua ya Istikhara. Hii ndiyo namna ya Swala ya Istikhara... lakini kuna mambo mengine yanayohusiana na Swala ya Istikhara nayo ni:

1- Ikiwa mtu atakusudia jambo baada ya kuliyafanyia utafiti katika pande zake zote, na ikampendezea kulifanya na akataka kulitimiza, hapo ndipo aswali rakaa mbili na kuomba dua ya Istikhara kisha alifanye jambo hilo huku akimnyenyekea Mwenyezi Mungu (swt) Amfanyie wepesi ikiwa ni kheri au Aliepushe naye ikiwa ni shari. Yaani, asiswali Istikhara mpaka baada ya kulifanyia utafiti jambo hilo katika pande zake zote na kulipa kipaumbele la kulifanya, hapo ndipo aswali na kuomba Istikhara na kuendelea na kazi hiyo... na asiswali Istikhara isipokuwa baada ya kulifanyia utafiti jambo hilo na kuona umuhimu wa kulitekeleza. Angalia hadith: "Ikiwa mmoja wenu atakusudia jambo, basi aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme: Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba uongofu kupitia ujuzi Wako..." (Imepokelewa na Al-Bukhari).

2- Haikuthibiti kutoka kwa Mtume (saw) kwamba alihusisha Istikhara na maono yanayoonekana katika ndoto kama ninavyojua, pamoja na kukithiri kwa muongozo wake (saw) kwa watu kufanya Istikhara. Hivyo, hakuunganisha matokeo yake na ndoto. Katika hadith ya Jabir, maneno yake: "basi nikadirie na nifanyie wepesi, kisha nibarikie ndani yake" na maneno yake: "basi liepushe nami na uniepushe nalo, na unikadirie kheri popote ilipo, kisha uniridhishe nalo" yanaonesha kuwa yeye (saw) hakuunganisha Istikhara na ndoto inayoonekana wakati wa kulala. Bali alijaalia jambo hilo kuhusishwa na wepesi na kadari ya Mwenyezi Mungu; yaani kwamba mtu anajitahidi kufanya jambo alilofanyia Istikhara, ikiwa ni kheri Mwenyezi Mungu atamkadira na kumfanyia wepesi, vinginevyo atamuepusha nalo. Kwa hivyo, Istikhara ni kuweka jambo na chaguo mikononi mwa Mwenyezi Mungu (swt) ili Yeye amchagulie mwenye kufanya Istikhara na Amfanyie wepesi jambo analomridhia. Ikiwa Halimridhii, basi Yeye (swt) Atamuepusha nalo.

3- Hakika maneno ya Mtume (saw) katika hadith ya Jabir: "basi liepushe nami na uniepushe nalo, na unikadirie kheri popote ilipo, kisha uniridhishe nalo" baadhi ya watu wanaelewa kuwa kukunjuka kwa kifua (kuhisi furaha/wepesi) ndiyo alama ya chaguo la Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwamba ikiwa kifua kimejawa na wepesi basi mtu aendelee na jambo hilo, na ikiwa amebanika na kutoridhika nalo basi aliache, kwani kumuepusha mwenye kufanya Istikhara nalo ni kwa kupitia kutoridhika kwa moyo na kubanika kwake... Al-Shawkani amenukuu katika Nayl al-Awtar kutoka kwa Al-Nawawi akisema: "Inapasa baada ya Istikhara afanye lile linalomkunjua kifua chake, wala asitegemee kukunjuka kwa kifua ambako alikuwa na matamanio nako kabla ya Istikhara. Bali inapasa kwa mwenye kufanya Istikhara kuacha chaguo lake kabisa, vinginevyo hatakuwa anafanya Istikhara kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bali atakuwa anafanya Istikhara kwa ajili ya matamanio yake, na huenda akawa si mkweli katika kutafuta kheri na katika kujiweka mbali na elimu na uwezo na kuvithibitisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ikiwa atakuwa mkweli katika hilo, atajivua na nguvu na uwezo (wake mwenyewe) na chaguo lake kwa ajili yake mwenyewe." (Mwisho). Lakini ninachopendelea (kuchagua) ni kwamba alama hii si sahihi kwa sababu hapakuhusishwa nukuu (nass) juu yake. Hadith wanayoitegemea baadhi yao katika hilo ni hadith ambayo sanadi yake ni dhaifu sana kama walivyotaja wahakiki, na hadith hiyo ni:

Ibn al-Sunni ametoa katika 'Amal al-Yawm wal-Laylah: Ametuambia Abu al-Abbas bin Qutaybah al-Asqalani, ametuambia Ubaydullah bin al-Himyari, ametuambia Ibrahim bin al-Ala bin al-Nadhr bin Anas bin Malik, ametuambia baba yangu, kutoka kwa babu yake, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: "Ewe Anas, ukihemia (ukikusudia) jambo, basi muombe Mola wako kheri (fanya Istikhara) ndani yake mara saba, kisha tazama lile linalokuja kwanza moyoni mwako, kwani hakika kheri imo ndani yake." Ibn Hajar amesema katika Fath al-Bari: "...Na Al-Nawawi amesema katika Al-Adhkar: afanye baada ya Istikhara lile linalomkunjua kifua chake, na anatoa ushahidi kwa hadith ya Anas kwa Ibn al-Sunni: 'Ikiwa utahemia jambo basi fanya Istikhara kwa Mola wako mara saba kisha tazama lile linalokuja kwanza moyoni mwako kwani kheri imo ndani yake', na hii lau kama ingethibiti ingekuwa ndiyo tegemeo, lakini sanadi yake ni dhaifu sana..."

Na kwa ajili hiyo, hakuna kilichobaki isipokuwa kile tulichokitaja katika nukta ya kwanza, kwamba hadith inasema kuwa Istikhara inakuwa baada ya kukusudia jambo, yaani baada ya kuchukua uamuzi wa kufanya kazi hiyo kulingana na utafiti wa kutosha na kupendelea pande za kulitekeleza... Na inashuhudia usahihi wa ufahamu huu hadith iliyopokelewa na Al-Hakim katika Mustadrak yake kutoka kwa Abu Ayyub al-Ansari kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: "Ficha posa kisha tawadha na ufanye vizuri udhu wako, kisha swali kile alichokuandikia Mwenyezi Mungu Mtukufu, kisha mhidi Mola wako na mtukuze, kisha sema: Ewe Mwenyezi Mungu, hakika Wewe unaweza na mimi siwezi, na Wewe unajua na mimi sijui, na Wewe ni Mjuzi wa yaliyofichikana. Ikiwa unajiona kwangu katika Fulani - amtaje kwa jina lake - ni kheri kwangu katika dini yangu, dunia yangu na akhera yangu, basi nikadirie, na ikiwa mwengine ni kheri kwangu katika dini yangu, dunia yangu na akhera yangu, basi nikadirie." Na ni wazi kutokana na hadith hii kwamba mwenye kufanya Istikhara aliazimia kuposa mwanamke fulani lakini hakuonesha jambo hilo bali alilificha, kisha akamuomba Mwenyezi Mungu kheri ndani yake na kuliweka jambo hilo mikononi mwa Mwenyezi Mungu (swt) ili Amkadirie ikiwa kuna kheri ndani yake au Amkadirie mwanamke mwengine ikiwa kheri iko kwa mwingine, wala hakuunganisha hilo na kile anachoona katika ndoto au kukunjuka kwa kifua...

Na muhtasari ni kwamba kile ninachokipendelea katika maudhui ya Istikhara ni:

Ikiwa mtu atakusudia jambo baada ya kuliyafanyia utafiti katika pande zake zote, na ikampendezea kulifanya na akataka kulitimiza, hapo aswali rakaa mbili na kuomba dua ya Istikhara na kuliendea jambo hilo, huku akimnyenyekea Mwenyezi Mungu (swt) Amfanyie wepesi ikiwa ni kheri au Aliepushe naye ikiwa ni shari.

Yaani, asiswali Istikhara mpaka baada ya kulifanyia utafiti jambo hilo katika pande zake zote na kulipa kipaumbele la kulifanya, hapo ndipo aswali na kuomba Istikhara na kuanza kazi... Angalia hadith: "Ikiwa mmoja wenu atakusudia jambo, basi aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme: Ewe Mwenyezi Mungu, hakika mimi nakuomba uongofu kupitia ujuzi Wako..." (Imepokelewa na Al-Bukhari).

Hili ndilo ninalolipendelea kutokana na hadith, na si kuswali Istikhara na kusubiri kuona katika ndoto, au kusubiri kuona mwelekeo wake katika moja ya mambo mawili, kwa sababu hadith inasema "Ikiwa mmoja wenu atakusudia jambo...". Na kama nilivyotaja hapo awali, hili ndilo ninalolipendelea juu ya baadhi ya kauli nyinginezo, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa ukweli.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir wa Facebook:

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir wa Google Plus:

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir wa Twitter:

Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network