Swali:
Imenukuliwa katika kitabu cha Al-Siyasah al-Iqtisadiyyah al-Muthla ukurasa wa (105) mstari wa tano, usemi usemao: "Ama kuhusiana na Dar al-Harb, kila ambaye hana uraia wa Kiislamu anachukuliwa kuwa ni mgeni, awe Muislamu au si Muislamu, na huchukuliwa kama Harbi (mtu wa nchi ya vita) kisheria, isipokuwa kwamba Muislamu haruhusiwi kumwaga damu yake wala kuchukua mali yake. Ama hukumu zinazohusiana na mali na hukumu nyinginezo, anachukuliwa kama asiye Muislamu sawia; hastahiki kupewa matumizi (nafaqa), harithi yeyote katika raia wa Dola, wala harithiwi."
Swali ni: Je, nchi (Dar) ni miongoni mwa vizuizi vya mirathi kama vile mauaji, utumwa, na tofauti ya dini? Ikiwa tutachukulia kuwa mtu Muislamu anaishi katika nchi ya kikafiri na ana baba Muislamu katika nchi ya Kiislamu (Dar al-Islam), na baba yake akafariki, ni ipi dalili ya kutomrithisha? Na je, anastahiki mali hiyo au haistahiki kwa mujibu wa kauli ya Mtume (saw):
إِنَّ اللَّهَ أَعْطَى كُلَّ ذِي حَقٍّ حَقَّهُ
"Hakika Mwenyezi Mungu amempa kila mwenye haki haki yake."
Jibu:
Kizuizi (Al-mani’): Ni kile ambacho kuwepo kwake kunapelekea kutokuwepo (kwa hukumu)...
Vizuizi vya mirathi vilivyokubaliwa na Maimamu wanne ni vitatu: Utumwa, mauaji, na tofauti ya dini. Na walitofautiana katika mambo mengine ikiwemo kuritadi (kurudi nyuma kutoka katika Uislamu), na tofauti ya nchi mbili (ikhtilaf al-darayni)... na yote haya yana maelezo yake ya kina...
Sisi tunachukua tofauti ya nchi (ikhtilaf al-dar) kama kizuizi cha mirathi, yaani anayeishi katika nchi ya kikafiri (Dar al-Kufr) harithiani na anayeishi katika nchi ya Kiislamu (Dar al-Islam). Hapa tunamaanisha mkaazi wa kudumu, yaani kile wanachokiita sasa "raia", na si yule aliyekwenda kwa ajili ya haja fulani kisha akarejea... wala haihusu tofauti ya nchi mbili zilizopo katika nchi za Waislamu leo ambapo hakuna Dar al-Islam kama vile Iraq na Syria... kwa sababu asili katika nchi za Waislamu ni kuwa nchi moja. Katika hali hizi, tofauti ya nchi haizuii kurithiana.
Ama tofauti ya nchi inayozuia kurithiana ni pale ambapo kuna Dar al-Islam na Dar al-Harb, na Muislamu hahajiri kutoka Dar al-Harb kwenda Dar al-Islam bali anabaki kuwa "raia" katika Dar al-Harb. Katika hali hii, tofauti ya nchi mbili inakuwa ni miongoni mwa vizuizi vya mirathi. Mwenyezi Mungu Mtukufu amekanusha uhusiano wa ulinzi na urithi (al-wilayah) baina ya yule aliyehajiri na yule ambaye hakuhajiri, pale aliposema:
وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَلَمْ يُهَاجِرُواْ مَا لَكُم مِّن وَلاَيَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّى يُهَاجِرُواْ
"Na wale walioamini lakini hawakuhama, nyinyi hamna jukumu la ulinzi (wilayah) juu yao hata kidogo mpaka wahame." (QS Al-Anfal [8]: 72)
Hivyo, ikiwa Dar al-Islam ipo na mkaazi wa Dar al-Harb hakuhajiri kwenda huko, bali akabaki na uraia wa nchi inayopigana vita na Uislamu, basi hukumu hii inamhusu. Yaani, kubaki kwake katika Dar al-Harb bila ya kufanya hijra kwenda Dar al-Islam kunakuwa ni kizuizi cha mirathi, isipokuwa ikiwa kubaki kwake katika Dar al-Harb ni kwa sababu ya kisheria kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah, Juzuu ya Pili, mlango wa "Hijra kutoka Dar al-Kufr kwenda Dar al-Islam", na hasa pale iliposemwa: "...isipokuwa yule anayeweza kudhihirisha dini yake na kutekeleza hukumu za kisheria zinazohitajika, ikiwa ana uwezo wa kuibadilisha Dar al-Kufr anayoishi kuwa Dar al-Islam, basi ni haramu kwake katika hali hii kuhajiri kutoka Dar al-Kufr kwenda Dar al-Islam. Iwe ana uwezo huo yeye mwenyewe au kwa kujiunga na kikundi cha Waislamu walioko katika nchi yake, au kwa kutafuta msaada kutoka kwa Waislamu wa nje ya nchi yake, au kwa kushirikiana na Dola ya Kiislamu, au kwa njia yoyote ile. Ni wajibu kwake kufanya kazi ya kuifanya Dar al-Kufr kuwa Dar al-Islam, na ni haramu kwake wakati huo kuhajiri kutoka hapo." Mwisho wa nukuu. Hawa na mfano wao, kubaki kwao ni jambo la kisheria... na hakuathiri kurithiana.
Kadhalika, yale yaliyokuja katika kitabu cha Muqaddimat ad-Dustur, Sehemu ya Pili, Ibara ya 189. Nakunukulia baadhi ya yaliyomo katika Muqaddimah kuhusu mlango huu:
(...Kwa mujibu wa hayo, ikiwa kuna Dar al-Islam, basi kuishi katika Dar al-Kufr kwa yule aliyewajibikiwa na hijra ni haramu. Zaidi ya hayo, kuishi katika Dar al-Kufr kunamfanya Muislamu kuwa miongoni mwa watu wa Dar al-Kufr, hivyo anatekelezewa hukumu za Dar al-Kufr kulingana na mahusiano yake na Dola ya Kiislamu na mahusiano yake na watu wengine. Had (adhabu ya kisheria) haitekelezwi juu yake "madamu anaishi katika Dar al-Kufr kwa sababu hayuko chini ya mamlaka ya Waislamu", wala hakusanywi zaka kutoka kwake, wala hamrithi mtu mwingine aliye katika Dar al-Islam, wala hawajibikiwi kupewa matumizi na yule aliye katika Dar al-Islam ambaye angewajibika kumpa kama angekuwa katika Dar al-Islam. Hii ni kwa sababu watu wa Dar al-Kufr hawatekelezwi juu yao hukumu za kisheria za serikali; hawana haki walizonazo Waislamu (raia wa Dola) wala hawawajibiki na yale yanayowawajibikia Waislamu, hivyo hukumu haziwahusu. Dalili ya hilo ni kwamba Waislamu hawaombi kwa walio katika Dar al-Kufr kuingia katika Uislamu pekee, bali pia waingie chini ya mamlaka ya Kiislamu. Sulayman bin Buraydah amepokea kutoka kwa baba yake akisema:
كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم إِذَا أَمَّرَ أَمِيرًا عَلَى جَيْشٍ أَوْ سَرِيَّةٍ أَوْصَاهُ فِي خَاصَّتِهِ بِتَقْوَى اللَّهِ وَمَنْ مَعَهُ مِنْ الْمُسْلِمِينَ خَيْراً، ثُمَّ قَالَ: اغْزُوا بِاسْمِ اللهِ فِي سَبِيلِ اللهِ، قَاتِلُوا مَنْ كَفَرَ بِاللهِ، اغْزُوا وَلاَ تَغُلُّوا وَلاَ تَغْدِرُوا وَلاَ تَمْثُلُوا وَلاَ تَقْتُلُوا وَلِيداً، وَإِذَا لَقِيتَ عَدُوَّكَ مِنْ الْمُشْرِكِينَ فَادْعُهُمْ إِلَى ثَلاَثِ خِصَالٍ أَوْ خِلالٍ، فَأَيَّتُهُنَّ مَا أَجَابُوكَ فَاقْبَلْ مِنْهُمْ وَكُفَّ عَنْهُمْ، ثُمَّ ادْعُهُمْ إِلَى الإِسْلاَمِ فَإِنْ أَجَابُوكَ فَاقْبَلْ مِنْهُمْ وَكُفَّ عَنْهُمْ، ثُمَّ ادْعُهُمْ إِلَى التَّحَوُّلِ مِنْ دَارِهِمْ إِلَى دَارِ الْمُهَاجِرِينَ وَأَخْبِرْهُمْ أَنَّهُمْ إِنْ فَعَلُوا ذَلِكَ فَلَهُمْ مَا لِلْمُهَاجِرِينَ وَعَلَيْهِمْ مَا عَلَى الْمُهَاجِرِينَ، فَإِنْ أَبَوْا أَنْ يَتَحَوَّلُوا مِنْهَا فَأَخْبِرْهُمْ أَنَّهُمْ يَكُونُونَ كَأَعْرَابِ الْمُسْلِمِينَ يَجْرِي عَلَيْهِمْ حُكْمُ اللهِ الَّذِي يَجْرِي عَلَى الْمُسْلِمِينَ وَلا يَكُونُ لَهُمْ فِي الْغَنِيمَةِ وَالْفَيْءِ شَيْءٌ إِلاَّ أَنْ يُجَاهِدُوا مَعَ الْمُسْلِمِينَ...
"Alikuwa Mjumbe wa Allah (saw) anapomweka kiongozi juu ya jeshi au kikosi cha vita, alikuwa akimuhusia kumcha Mwenyezi Mungu yeye binafsi na kuwafanyia heri Waislamu walio pamoja naye. Kisha husema: 'Piganeni kwa jina la Mwenyezi Mungu katika njia ya Mwenyezi Mungu, wapigeni waliomkufuru Mwenyezi Mungu. Piganeni lakini msifanye hiyana, msivunje ahadi, msiwakate viungo vya miili waliokufa, na msiue mtoto mchanga. Na utakapokutana na adui yako katika washirikina, basi waitie kwenye mambo matatu, lolote watakalokuitikia miongoni mwa hayo, basi likubali kwao na uwaache. Kisha waitie kwenye Uislamu, wakikuitikia, basi likubali kwao na uwaache. Kisha waitie wahame kutoka katika nchi yao kwenda kwenye nchi ya Muhajirina (Dar al-Islam), na uwajulishe kuwa wakifanya hivyo, basi watakuwa na haki zile zile walizonazo Muhajirina na watawajibika na yale yote yanayowawajibikia Muhajirina. Lakini wakikataa kuhama kutoka huko, basi uwajulishe kuwa watakuwa kama mabedui wa Kiislamu (A’rab al-Muslimin); itapitishwa juu yao hukumu ya Mwenyezi Mungu inayopitishwa juu ya Waislamu, lakini hawatakuwa na chochote katika ngawira (ghanimah) na mali ya fa-i isipokuwa wakipigana jihadi pamoja na Waislamu...'" (Imepokelewa na Muslim).
Mtume (saw) anasema: 'Kisha waitie wahame kutoka katika nchi yao kwenda kwenye nchi ya Muhajirina, na uwajulishe kuwa wakifanya hivyo, basi watakuwa na haki zile zile walizonazo Muhajirina na watawajibika na yale yote yanayowawajibikia Muhajirina.' (Imepokelewa na Muslim). Hii ni nass (maandiko) inayoshurutisha kuhama ili wapate haki tulizonazo na wawajibike na yale tuliyowajibika nayo, yaani ili hukumu ziwaenee...) mwisho wa nukuu.
Hivyo, tofauti ya nchi (ikhtilaf al-dar) kwa namna tuliyoibainisha inazuia kurithiana.