Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kwa Abu Al-Asim Al-Shami
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh, Amir wetu mpendwa, amani ya Allah na rehema zake ziwe juu yako. Swali hili limekuwa likinizunguka akilini tangu muda mrefu, kwa hivyo naomba ufafanuzi kutoka kwako, nikimuomba Allah akujalie afya na uzima na akufungulie kwa ufunguzi Wake mkuu.
Kwa nini tunategemea mahesabu ya falaki katika kuainisha nyakati za swala tano mwaka mzima, lakini hatutegemei mahesabu hayo katika kuainisha kuanza kwa saumu na Eid?
Jibu:
Tayari tulishatoa jibu kuhusu swali kama hili mnamo tarehe 25/11/2003, ambamo ilielezwa:
[... - Allah (swt) ametaka tufunge na tufungue kwa kuuona mwezi mwandamo, na akajaalia (Subhaanahu) kuonekana kwa mwezi kuwa ndio sababu (sabab) ya saumu na kufungua:
صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ
"Fungeni kwa kuuona (mwezi) na fungueni kwa kuuona."
Tukiiona hilali (mwezi mwandamo) ya Ramadhani tunafunga, na tukiiona hilali ya Shawwal tunafungua.
- Anayefuatilia maandiko (nusoos) yaliyokuja kuhusu saumu atayakuta yanatofautiana na maandiko yaliyokuja kuhusu swala. Saumu na kufungua vimefungamanishwa na kuonekana kwa mwezi (ru'yah):
صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ
"Fungeni kwa kuuona (mwezi) na fungueni kwa kuuona."
فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ
"Basi atakayekuwa miongoni mwenu katika mwezi huo na aufunge." (QS. Al-Baqarah [2]: 185)
Kwa hivyo, kuonekana kwa mwezi ndiyo hukumu. Lakini maandiko kuhusu swala yamefungamanishwa na wakati:
أَقِمِ الصَّلاَةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ
"Shika Sala jua linapopinduka." (QS. Al-Isra [17]: 78)
إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلَّوْا
"Jua likipinduka basi swalini."
Hivyo swala inategemea wakati; kwa njia yoyote ile utakaohakikisha wakati umefika basi unaswali. Ukiangalia jua ili uone wakati wa kupinduka kwake (zawal), au ukiangalia kivuli ili uone kivuli cha kila kitu kimekuwa mfano wake au mara mbili yake kama ilivyokuja katika hadithi za nyakati za swala, ukifanya hivyo na ukahakikisha, swala ni sahihi. Na kama hukufanya hivyo, bali ukahesabu kwa falaki na ukajua kuwa wakati wa zawal ni saa fulani, kisha ukaangalia saa yako bila ya kutoka nje kuona jua au kivuli, swala itakuwa ni sahihi. Yaani, unahakikisha wakati kwa njia yoyote ile. Kwa nini? Kwa sababu Allah (swt) amekutaka uswali kwa kuingia kwa wakati, na amekuachia uhuru wa kuhakikisha kuingia kwake bila kuainisha namna ya kuhakikisha.
Ama kuhusu saumu, amekutaka ufunge kwa kuuona mwezi, hivyo akakuainishia sababu (sabab). Bali zaidi ya hapo, amekuambia ikiwa mawingu yatazuia kuonekana kwake na usiuone, basi usifunge hata kama mwezi upo nyuma ya mawingu na una uhakika wa kuwepo kwake kwa mahesabu ya falaki.
حَدَّثَنَا آدَمُ حَدَّثَنَا شُعْبَةُ حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ زِيَادٍ قَالَ سَمِعْتُ أَبَا هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ يَقُولُ: قَالَ النَّبِيُّ ﷺ أَوْ قَالَ قَالَ أَبُو الْقَاسِمِ ﷺ صُومُوا لِرُؤْيَتِهِ وَأَفْطِرُوا لِرُؤْيَتِهِ فَإِنْ غُبِّيَ عَلَيْكُمْ فَأَكْمِلُوا عِدَّةَ شَعْبَانَ ثَلَاثِينَ
"Adam ametuhadithia, Shu'bah ametuhadithia, Muhammad bin Ziyad ametuhadithia akisema: Nilimsikia Abu Hurairah (ra) akisema: Nabii ﷺ alisema, au alisema Abu Al-Qasim ﷺ: 'Fungeni kwa kuuona (mwezi) na fungueni kwa kuuona, na mkifichwa na mawingu basi kamilisheni idadi ya Shaabani kuwa siku thelathini.'" (Imepokelewa na Bukhari).
Yaani, msipouona basi kamilisheni idadi ya Shaabani kuwa siku thelathini.
- Hakika Allah (swt) ndiye muumba wa ulimwengu, na Yeye (Subhaanahu) ndiye aliyemfundisha mwanadamu asichokijua. Hivyo elimu ya mwendo wa sayari na mambo yake ya ndani ni katika fadhila za Allah kwa watu. Lakini Allah (swt) hakututaka tutegemee mahesabu kwa ajili ya saumu, bali alitutaka tuuone mwezi. Hivyo tunamwabudu Yeye (Subhaanahu) kama alivyotaka, na hatumwabudu kwa kile asichokitaka.
Hivyo basi, kuonekana kwa mwezi pekee ndiyo hukumu katika kufunga na kufungua, na si mahesabu ya falaki. Na kwa msingi huo, tunasema kutofaa kutumia mahesabu ya falaki katika saumu na kufungua, bali ni kuonekana kwa mwezi pekee kwa sababu ndivyo ilivyokuja katika maandiko.]
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
22 Sha'ban 1443 H 25/03/2022 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir (Allah amhifadhi) Web