Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Nisab ya Zaka

May 30, 2014
5523

Jibu la Swali

Nisab ya Zaka

Swali:

Imekuja katika kitabu cha Al-Amwal ukurasa wa 158 yafuatayo:

"Ama ikiwa nisabu ya dhahabu, au fedha, imetimia tangu mwanzo wa mwaka (hawl), na kukapatikana ongezeko la mali katikati ya mwaka; ikiwa ongezeko hilo limetokana na biashara, basi huunganishwa na ile mali ya asili, na mwaka wa ongezeko hilo huchukuliwa kuwa ni uleule mwaka wa mali ya asili, kwa sababu ongezeko hilo limetokana na kukua kwa mali na ni jinsi ile ile ya mali hiyo, hivyo inafuata hukumu yake.

Ama ikiwa ongezeko hilo ni la jinsi ile ile ya nisabu, lakini halikutokana na njia ya kukua kwa mali (biashara), kama vile kupatikana kupitia mirathi au zawadi, basi ongezeko hili ni lazima lipitiwe na mwaka mzima, na haliunganishwi na mali ya asili, wala halichukui hukumu ya mwaka wake..." mwisho wa nukuu.

Kuhusu aya ya kwanza inaeleweka... lakini kuhusu aya ya pili, je, inamaanisha ikiwa nina nisabu katika mwezi wa Muharram mwaka huu, na baada ya miezi minne katika mwezi wa Jumada al-Ula nikapata dinari elfu moja kutokana na mirathi, je, nitakuwa na miaka miwili ya mali, kwa maana ya kwamba nisabu ya asili naitolea zaka katika mwezi wa Muharram ujao, lakini mirathi naitolea zaka katika mwezi wa Jumada al-Ula ujao? Yaani, kuna nyakati mbili za kutoa zaka katika kila mwaka? Au inanijuzia kutoa zaka ya mirathi mwishoni mwa mwaka wa nisabu ya asili, yaani nitoe zaka ya zote kwa pamoja katika mwezi wa Muharram wa mwaka ujao?

Jibu:

Hakika mali ambayo haikutokana na ile nisabu ya asili uliyonayo, zaka yake inawajibika wakati wa kutimia kwa mwaka wake (hawl) na si wakati wa mwaka wa nisabu ya asili. Kwa mfano, una nisabu (gramu 85 za dhahabu au dirham 200 za fedha) katika mwezi wa Muharram mwaka huu, basi zaka ya nisabu hii inawajibika baada ya kupita mwaka mmoja ikiwa haijapungua.

Ikiwa utapata dinari elfu moja kutokana na biashara ya nisabu hiyo katika mwezi wa Jumada al-Ula, basi huongezwa kwenye kile ulichonacho na zaka ya zote hutolewa katika mwezi wa Muharram wa mwaka ujao. Lakini ikiwa imekujia kupitia mirathi, yaani si kwa sababu ya nisabu uliyonayo, basi mirathi hii inawajibika kutolewa zaka baada ya kupita mwaka mmoja tangu kuipata, na si baada ya kupita mwaka wa ile nisabu. Hii inamaanisha kama ilivyoelezwa katika swali kuwa utatolea zaka nisabu katika mwezi wa Muharram wa mwaka ujao ikiwa nisabu haitakuwa imepungua wakati huo, na utatolea zaka mirathi katika mwezi wa Jumada al-Ula wa mwaka ujao; hivyo nisabu ina mwaka wake, na mirathi ina mwaka wake, hii ni kwa upande wa uwajibikaji (wujub).

Lakini unaruhusiwa kutoa zaka ya mirathi mwishoni mwa mwaka wa nisabu ya asili, yaani katika mwezi wa Muharram, na si lazima usubiri mpaka mwisho wa mwaka wa mirathi katika mwezi wa Jumada al-Ula. Kwa maneno mengine, unatoa zaka ya mali yako yote kwa mara moja baada ya kupita mwaka mmoja tangu kumiliki kwako nisabu, yaani katika mwezi wa Muharram, na hiyo ni kwa sababu inajuzu kuharakisha utoaji wa zaka (ta’jil al-zakah), yaani kuitoa kabla ya mwaka wake kutimia. Hivyo inakujuzia kutoa zaka ya mirathi kabla ya kutimia mwaka wake, ukaitoa wakati wa kutimia mwaka wa nisabu ya asili, kwa sababu Sheria imeruhusu kuharakisha zaka baada ya kufikia nisabu na kabla ya kupita mwaka mmoja. Ama wajibu ni baada ya kupita mwaka (hawl). Miongoni mwa dalili za kuharakisha utoaji wa zaka kabla ya kupita mwaka juu ya nisabu ni pamoja na:

  • Al-Bayhaqi amepokea katika Al-Sunan al-Kubra kutoka kwa Ali:

عَنْ عَلِيٍّ، "أَنَّ الْعَبَّاسَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ سَأَلَ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي تَعْجِيلِ صَدَقَتِهِ قَبْلَ أَنْ تَحِلَّ فَأَذِنَ لَهُ فِي ذَلِكَ"

"Kutoka kwa Ali, 'Kwamba Al-Abbas (ra) alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kuhusu kuharakisha zaka yake kabla ya wakati wake (wa kuwajibika) kufika, naye akamruhusu katika hilo.'"

  • Al-Darqutni amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Hujr al-Adawi, kutoka kwa Ali amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alimwambia Umar:

إِنَّا قَدْ أَخَذْنَا مِنَ الْعَبَّاسِ زَكَاةَ الْعَامِ عَامِ الْأَوَّلِ

"Hakika sisi tayari tumechukua kutoka kwa Al-Abbas zaka ya mwaka huu tangu mwaka uliopita."

  • Al-Darqutni amepokea kutoka kwa Musa bin Talha, kutoka kwa Talha kwamba Mtume (saw) amesema:

يَا عُمَرُ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّ عَمَّ الرَّجُلِ صِنْوُ أَبِيهِ؟ إِنَّا كُنَّا احْتَجْنَا إِلَى مَالٍ فَتَعَجَّلْنَا مِنَ الْعَبَّاسِ صَدَقَةَ مَالِهِ لِسَنَتَيْنِ

"Ewe Umar, je, hufahamu kwamba ami wa mtu ni kama baba yake? Hakika tulihitaji mali, hivyo tukachukua zaka ya mali ya Al-Abbas mapema kwa ajili ya miaka miwili." Wametofautiana kuhusu Al-Hakam katika isnadi yake, na usahihi ni kutoka kwa Al-Hasan bin Muslim ni mursal.

Muhtasari ni kwamba mirathi iliyokufikia baada ya kumiliki nisabu kwa miezi kadhaa, zaka yake ni wajibu baada ya kutimia mwaka wake mmoja, na si baada ya kutimia mwaka wa nisabu. Lakini inajuzu kuitolea zaka pamoja na kutimia kwa mwaka wa nisabu, yaani kabla ya kutimia mwaka wa mirathi uliyopata, na hiyo ni kutokana na kujuzu kwa kuharakisha zaka kwa mujibu wa dalili za kisheria katika mlango huu.

Share Article

Share this article with your network