Jibu la Swali
Jibu:
Maelezo uliyoyataja kutoka katika kitabu Al-Khilafah pia yanapatikana katika kitabu Nidhamu ya Utawala ukurasa wa 60 (toleo la Kiarabu). Yanafafanua hukumu ya kisheria pindi Khilafah inaposimama katika nchi inayotimiza masharti manne, na nchi hiyo ikampa bay’ah Khalifa, basi Khilafah hiyo inakuwa imesimama na kuanza kufanya kazi hata kama nchi hiyo haiwakilishi (wengi wa Ahlul Halli wal ‘Aqdi katika nchi nyingi za Kiislamu). Kwa hivyo, ikiwa bay’ah ya Khilafah itatolewa katika nchi yenu, basi Khilafah inakuwa imesimama hata kama nchi yenu haiwakilishi sehemu kubwa ya Ummah au wengi wa Ahlul Halli wal ‘Aqdi ndani yake. Hii ni kwa sababu kusimamisha Khilafah ni fardh al-kifayah (faradhi ya kutosheleza), na yule anayetekeleza faradhi hiyo kwa namna yake sahihi anakuwa ametekeleza jambo lililoamrishwa, na wengine wanakuwa wamefungika nalo kisheria.
Ama matini nyingine katika Nidhamu ya Utawala ukurasa wa 85 (toleo la Kiarabu) inayosema: "Inaruhusiwa kwa wale waliochukua mamlaka kumpendekeza mtu miongoni mwa Waislamu wenye sifa za kushika utawala na mamlaka na wanaotimiza masharti ya kusimama kwa Khilafah, na kuwakusanya Ahlul Halli wal 'Aqdi katika nchi hiyo au wengi wao, na kuwaomba wampe bay'ah mtu huyo waliyempendekeza ili awe Khalifa. Hivyo basi, Ahlul Halli wal 'Aqdi hutoa bay'ah kwa ridhaa na hiyari juu ya Kitabu cha Allah na Sunnah za Mtume Wake, na hapo Khilafah inasimama kupitia bay'ah hiyo."
Hili linahusiana na namna ya kusimama kwake katika nchi hiyo.
Hivyo basi, maudhui ya kwanza ni tofauti na maudhui ya pili.
Ya Kwanza: Ni jibu kwa swali linalouliza: Je, ni lazima kuwepo kwa bay’ah ya wengi wa Ahlul Halli wal ‘Aqdi katika sehemu kubwa ya Ummah wa Kiislamu ili Khilafah isimame? Yaani, ikiwa itasimama katika nchi yenu, je, ni lazima kuwe na bay’ah ya nchi nyingi za Kiarabu na nchi nyingine za Kiislamu ili Khilafah isimame katika nchi yenu? Ikiwa Misri, kwa mfano, haitatoa bay’ah, je, Khilafah katika nchi yenu itakuwa haijasimama?
Jibu: Hapana, bali kusimama kwake katika nchi yoyote inayotimiza masharti, na bay’ah ya nchi hii kwa mtu anayetimiza masharti, kunaifanya kuwa Khilafah sahihi na iliyosimama kisheria, na ni wajibu kwa Waislamu waliosalia kutoa bay’ah ya utiifu na kuingia katika dola hii.
Ya Pili: Ni jibu kwa swali linalouliza: Ni vipi Khilafah inasimama katika nchi yenu ikiwa tayari tumejua kutokana na jibu la kwanza kwamba Khilafah inasimama humo (katika nchi yenu) hata kama Waislamu waliosalia hawajatoa bay’ah?
Jibu: Ni kwamba Waislamu au wenye nguvu na ushawishi (ashabu al-quwwah wal-man'ah) miongoni mwao wachukue mamlaka katika nchi hiyo na kumuondooa mtawala anayetawala kwa mifumo ya kikafiri, kwa lengo la kusimamisha utawala wa Kiislamu, kisha wampendekeze Muislamu anayetimiza masharti na kuwaomba Ahlul Halli wal ‘Aqdi katika nchi hiyo au wengi wao wampe bay’ah Khalifa juu ya Kitabu cha Allah na Sunnah za Mtume Wake, na hapo Khilafah inakuwa imesimama kwake.
Kwa hivyo, maudhui haya mawili yanakamilishana na hayakinzani.
25/02/2004 BK