Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kushuka kwa Surah Muhammad (saw)

February 22, 2004
1824

Jibu la Swali

Kushuka kwa Surah Muhammad (saw)

Ndugu mpendwa, Baada ya salamu,

Unasema katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah Juzuu ya Pili, katika mada ya mateka, kwamba Surah Muhammad (saw) ilishuka kabla ya Vita vya Badr, pamoja na kwamba kuna riwaya zinazosema tofauti na hivyo. Je, ni upi ushahidi wa kushuka kwake kabla ya Badr?

Ni kweli kuna riwaya zinazoeleza kuwa Surah Muhammad haikushuka kabla ya Badr.

Lakini kuna mambo yanayopewa uzito (tarjihi) kuliko riwaya hizo:

أ- Mtume (saw) alitoa hukmu kuhusu mateka siku ya Badr, na hii ina maana kwamba hukmu ya mateka ilikuwa tayari imeshateremka, kwa sababu Mtume (saw) hatoi hukmu bila ya wahyi.

ب- Hakuna katika Qur'ani Tukufu hukmu ya mateka isipokuwa katika Surah Muhammad (saw):

فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً

"Basi baada ya hayo ni aidha kuwafanyia ihsani (kuwaachia huru bila fidia) au kuwataka wajifidie." (QS. Muhammad [47]: 4)

ج- Aya isemayo:

فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنْتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً

"Basi mnapokutana (katika mapigano) na wale waliokufuru, wapigeni shingoni mwao mpaka mkiwashinda kabisa (kuwadhoofisha), basi wafungeni pingu kwa nguvu, kisha baada ya hapo ni aidha kuwafanyia ihsani au kuwataka wajifidie." (QS. Muhammad [47]: 4)

Aya hii imeanza kwa neno (فإذا - na pindi/basi mnapo...) ikiwa na maana kwamba hukmu iliyoko katika aya ilishuka kabla ya kutokea mapigano. Aya inabainisha hukmu ya mateka pindi mapigano yanapotokea, na hayakutokea mapigano yaliyokuwa na mateka yaliyohitaji hukmu isipokuwa Vita vya Badr.

Pia, kauli yake Subhanahu: {حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنْتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ} ni bayana ya hukmu ya wakati ambao kutekwa (kuchukuliwa mateka) kunafanyika katika uwanja wa vita, nayo ni baada ya kuwadhoofisha (kuwashinda kabisa). Hivyo, itakuwa ilishuka kabla ya Vita vya Badr, kwa sababu suala la kuwadhoofisha maadui (al-ithkhan), mara ya kwanza kutokea, lilitokea katika Vita vya Badr. Hivyo, kubainisha kwamba kuteka mateka kunafanyika tu baada ya kuwadhoofisha adui ni bayana ya hukmu mpya ambayo ilikuwa bado haijatokea.

Kwa ajili hiyo, maana ya dhahiri ya aya (mantūq) inaonesha kuwa ilishuka kabla ya kutokea mapigano, na ilishuka kubainisha hukmu ya mateka kabla ya kutokea mapigano na kabla ya kutokea kwa kuwadhoofisha maadui {فإذا لقيتم}, {حتى إذا أثخنتموهم}. Na aya hupewa uzito (tarjihi) kuliko hadith maadamu haiwezekani kuzioanisha, kwani kama ingewezekana, basi kuoanisha (jam’u) ingekuwa bora zaidi. Na kwa kuwa haiwezekani kuzioanisha kwa sababu riwaya zinasema kuwa hukmu ya mateka ilikuja baada ya Badr, wakati aya inaonesha kuwa hukmu ya mateka ilikuja kabla ya Badr, basi hapo inafanyiwa kazi kanuni ya at-tarjihi (kutoa uzito). Hivyo aya inapewa uzito dhidi ya hadith zinazoipinga.

Jambo hili linasisitizwa na kuimarishwa na ukweli kwamba hakuna hukmu ya mateka isipokuwa katika Surah Muhammad, na hapakuwa na mapigano yaliyohitaji hukmu ya mateka isipokuwa Badr, na kwamba Mtume alitoa hukmu kwa mateka wa Badr, naye (saw) hatoi hukmu isipokuwa kwa wahyi.

2 Muharram 1425 H 22/02/2004 M

Share Article

Share this article with your network