Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Kanuni ya "Uovu Mdogo Zaidi Kati ya Miwili au Dhara Jipesi Zaidi" Kwa Walid Elmi
Swali:
Assalamu Alaikum Sheikh wetu, nina swali kuhusiana na kanuni mbili za "dhara jipesi zaidi" au "uovu mdogo zaidi" ambazo hutumiwa na kundi kubwa la walinganizi na harakati za Kiislamu kama kisingizio cha kushiriki katika chaguzi za bunge na urais. Je, hizi ni miongoni mwa kanuni za kisheria? Na je, kuna baadhi ya mafakihi waliowahi kuzizungumzia? Na ni zipi dalili zao na raddi (majibu) dhidi yake? Baraka za Allah ziwe nawe.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
Kuhusiana na kanuni hii, tulishajibu mnamo tarehe 29/08/2010, na nakunukulia yaliyokuja katika jibu letu hilo:
[Kanuni ya "Uovu Mdogo Zaidi Kati ya Miwili au Dhara Jipesi Zaidi".
Hii ni kanuni ya kisheria kwa mujibu wa idadi kadhaa ya mafakihi, na kwa wanachuoni wanaoitumia, inarejea kwenye maana moja, nayo ni: kuruhusiwa kufanya mojawapo ya vitendo viwili vilivyoharamishwa, ambacho ni kile chenye uharamu mdogo zaidi kati ya hivyo viwili, iwapo mukallaf (mwenye kuwajibika kisheria) hana njia nyingine isipokuwa kufanya mojawapo ya haramu hizo mbili, na hawezi kuziacha zote mbili kwa pamoja; kwa sababu hilo haliwezekani, yaani liko nje ya uwezo wake kwa kila hali.
لَا يُكَلِّفُ اللَّهُ نَفْساً إِلَّا وُسْعَهَا
"Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake." (QS. Al-Baqarah [2]: 286)
na Amesema Subhanahu:
فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ
"Basi mcheni Mwenyezi Mungu kadiri muwezavyo." (QS. At-Taghabun [64]: 16)
Yaani, kanuni hii kwa mujibu wa wale waliosema hivyo haitekelezwi isipokuwa ikiwa haiwezekani kujiepusha na haramu zote mbili, kiasi kwamba haiwezekani kuacha haramu hizo mbili kwa pamoja isipokuwa kwa kutokea haramu kubwa zaidi, hapo ndipo huchukuliwa dhara jipesi zaidi. Vilevile, wanachuoni hawa hawafanyi utambuzi wa dhara jipesi zaidi kufuata matamanio, bali ni kwa mujibu wa hukmu za kisheria; hivyo kuhifadhi nafsi mbili ni bora kuliko kuhifadhi nafsi moja, na tatu ni bora zaidi, na kadhalika. Na kuhifadhi nafsi kunapewa kipaumbele mbele ya kuhifadhi mali, na kuhifadhi Dar al-Islam kunaingia katika kuhifadhi dini, nako ni muhimu zaidi kuliko kuhifadhi nafsi na mali. Kadhalika Jihad na Imamah al-Udhma (Khilafah), vyote viwili vinaingia katika kuhifadhi dini tangu mwanzo na ni miongoni mwa dharura muhimu zaidi. Mwanachuoni Al-Shatibi alisema katika Al-Muwafaqat: "Nafsi zinaheshimika, zinalindwa na inatakiwa kuhuishwa kiasi kwamba ikiwa jambo litakuwa kati ya kuzihuisha na kuharibu mali kwa ajili hiyo, au kuziharibu na kuhuisha mali, basi kuzihuisha nafsi ni bora zaidi...".
Miongoni mwa mifano iliyotajwa na wanachuoni hawa katika kutekeleza kanuni hii ni:
1- Ikiwa uzazi wa mama umekuwa mgumu na ikashindikana kumuokoa mama na kijusi kwa pamoja, na jambo likahitaji uamuzi wa haraka: ima kumuokoa mama jambo ambalo linapelekea kifo cha kijusi, au kumuokoa kijusi jambo ambalo linapelekea kifo cha mama. Na ikiwa jambo litaachwa bila kufanya kazi ya kumuua mmoja wao ili kumuokoa mwenzake, au kumhuisha mmoja kwa kifo cha mwenzake, linaweza kupelekea kifo cha wote wawili. Katika hali kama hii husemwa uovu mdogo zaidi, au haramu ndogo zaidi, au mufsidah (uharibifu) jipesi zaidi, ambapo hufanyika kile kitendo kinachomuokoa yule anayetakiwa kuokolewa ambaye ni mama, hata kama kitendo hicho chenyewe kitakuwa ni kumuua mwingine.
2- Mtu anapokabiliwa na hatari ya kuangamia kwa kuzama au kuuawa na mtu mwingine, au kupata madhara makubwa mwilini na kwenye viungo vyake, au mwanamke kufanyiwa uovu wa zinaa mbele ya mtu mukallaf anayeweza kuzuia maovu hayo na wakati huo huo ana swala ya faradhi ambayo wakati wake unaweza kumpita. Hapa ima azuie haramu hiyo kisha akose kutekeleza wajibu (swala), au atekeleze wajibu katika wakati wake kisha haramu hiyo itokee, na wakati hautoshi kufanya mambo yote mawili kwa pamoja. Hapa ndipo utekelezaji wa kanuni hii unapoingia, na mizania pia inatoka kwa Sharia ambayo imefanya kuondoa haramu hizo zilizotajwa kuwa na uzito zaidi kuliko kutekeleza wajibu uliotajwa, na lau ingewezekana kufanya wajibu yote mawili kwa pamoja basi yote mawili yangekuwa lazima.
3- Na hii ni mifano mingine iliyotajwa na maimamu wawili Al-Ghazali na Izz al-Din bin Abd al-Salam (Allah awarehemu), ambapo inaonekana namna ya kutekeleza kanuni ya uovu mdogo zaidi kwao, na inaonekana pia mizania kati ya hukmu. Al-Izz alisema katika kitabu chake Qawa'id al-Ahkam fi Masalih al-Anam: "Zikikusanyika mufsidah tupu, ikiwezekana kuziepusha tutaziepusha, na ikishindikana kuziepusha zote, tutaepusha ile mufsidah mbaya zaidi na inayofuata, na ya kudhalilisha zaidi na inayofuata..." Kisha akataja mifano akasema: "Kulazimishwa (ikrah) kumuua Mwislamu kiasi kwamba asipofanya hivyo atauawa yeye, basi inamlazimu aepushe mufsidah ya kuua kwa kusubiri kuuawa yeye; kwa sababu kusubiri kwake kuuawa ni mufsidah ndogo zaidi kuliko yeye kufanya mauaji..." Huu ni mfano wa wazi kwamba ni kuchagua mufsidah jipesi zaidi au haramu ndogo zaidi kwa sababu hana namna ya kuepukana na mojawapo, na lau angeweza kuzuia mufsidah zote mbili basi ingemuwajibikia kufanya hivyo.
Alisema katika mfano mwingine: "Vilevile lau akilazimishwa kwa kuuawa ili atoe ushahidi wa uongo au ahukumu kwa batili, ikiwa yule anayelazimishiwa ushahidi au hukumu hiyo ni kumuua, au kumkata kiungo, au kuhalalisha tupu iliyoharamishwa, basi haijuzu kutoa ushahidi huo wala kuhukumu; kwa sababu kusalimu amri ili auawe ni bora zaidi kuliko kusababisha kifo cha Mwislamu bila dhambi, au kukatwa kiungo bila kosa, au kuingilia tupu iliyoharamishwa..." Yaani, ikiwa ima auawe au atoe ushahidi wa uongo dhidi ya mwingine utakaopelekea kuuawa kwake au kukatwa kiungo chake, au kuvunjiwa heshima yake, basi haijuzu kwake kutoa ushahidi bali asubiri kuuawa, kwa sababu kusalimu amri ili auawe ni bora kuliko kumuua Mwislamu mwingine...
Yaani, hali ambayo inakimbiliwa kufanya kazi kwa haramu ndogo zaidi au mufsidah jipesi zaidi ni hali ya kushindwa kuepuka haramu zote mbili au kuzizuia zote mbili.
Hii ni mifano ya utekelezaji wa kanuni ya dhara jipesi zaidi kwa mujibu wa yale yaliyotajwa na wanachuoni wanaoitumia, lakini mifano yake si ile inayopigiwa upatu na masheikh wa masultani, au wale wanaotaka Waislamu waepuke hukumu za kisheria kwa upotoshaji na uongo.
Wale wanaotumia kanuni hii kufanya haramu hii badala ya ile haramu nyingine wakitoa udhuru wa kufanya kwao hivyo kwa kuwa wanaogopa kufungwa au kufukuzwa kazi zao, basi hili halimo katika kanuni hii.
Vilevile, wale wanaosema tunashiriki katika utawala wa kikafiri pamoja na kuwa ni haramu, ili tusiwaachie watu waovu vyeo vyote vya utawala, kwa sababu kuwaachia utawala ni haramu kubwa zaidi... hili si miongoni mwa utekelezaji wa kanuni hii, bali ni kama yule anayesema tufungue baa ya kuuza pombe na tujipatie kipato kutokana nayo badala ya kafiri kuifungua na akajipatia yeye mali hiyo...
Wala si katika utekelezaji wa kanuni hii kuletewa mtu mambo mawili ya haramu akafanya jepesi zaidi kati yake ilhali ana uwezo wa kuacha yote mawili, kama kauli ya anayesema: mchagueni fulani hata kama ni msekula kafiri au mwovu, au muungeni mkono fulani na msimuunge mkono mwingine; kwa sababu wa kwanza anatusaidia na wa pili hatusaidii, au mfano wa hayo. Bali kinachosemwa hapa ni: Hakika mambo mawili yaliyowekwa mbele yetu ni haramu, hivyo haijuzu kumchagua msekula na haijuzu kumwakilisha au kumpa idhini ya kumwakilisha Mwislamu katika kutoa maoni, kwa sababu hafungamani na Uislamu, na kwa sababu anafanya vitendo vya haramu ambavyo mwakilishaji (muwakkil) haruhusiwi kuvifanya kama vile kutunga sheria na kuidhinisha miradi ya haramu, na kama vile kudai mambo ya haramu na kuyakubali na kuyaendeleza. Kwa ujumla, yeye anakataza mema na kuamrisha maovu; na kwa sababu hiyo, haijuzu kumchagua yeyote kati yao; kwa sababu kumchagua huyu au huyo ni haramu. Na kuacha kumchagua huyu au kumchagua huyo kuko ndani ya uwezo.
Wala si katika utekelezaji wa "dhara jipesi zaidi" kwa Mwislamu kukabiliwa na vitendo viwili vya haramu na ana uwezo wa kuviepuka vyote viwili, kisha akaamua kuchagua jepesi zaidi kati yake kwa kufuata matamanio yake akidai kuwa katika kuacha haramu zote mbili kuna ugumu...! Bali ni lazima kuacha haramu zote maadamu hilo linawezekana kwa mujibu wa hukmu za kisheria.
Hii ni picha fupi kuhusu "dhara jipesi zaidi" au "uovu mdogo zaidi".] Mwisho.
Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah
10 Rabi’ al-Awwal 1442 H Muwafaka wa 27/10/2020 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Facebook Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Allah amhifadhi) kwenye Tovuti