Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Kulipa Siku za Ramadhani Zilizompite Mtu

February 04, 2025
1707

Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizbut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jawabu la Swali

Kulipa Siku za Ramadhani Zilizompite Mtu

Kwa Eenas Mohammed

Swali:

Assalamu Alaikum, ningependa kuuliza kuhusu kulipa siku za saumu...

Katika hali ambayo sikumbuki vizuri kulipa kwangu siku zilizopita kwa miaka mingi, yaani nilikuwa nikilipa lakini zinabaki siku nyingine ambazo sikukamilisha kuzilipa. Baadhi ya wanafamilia yangu wanasema nilikuwa nikilipa nao, na wengine wanasema hawakumbuki kama nilikuwa nikizilipa zote... Katika hali kama hii, nifanye nini? Nimeuliza sana, na majibu yalikuwa ni kutoa kafara ya mali, na baadhi yao walisema ni lazima kutoa mali na kufunga. Na ikiwa ni lazima nifunge, sikumbuki ni siku ngapi ninazopaswa kulipa. Kwa hiyo, nifanye nini?

Jawabu:

Waalaykum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Tumeshawahi kujibu swali kama hili mnamo tarehe 13/05/2019 tukisema:

[Sisi hatufanyi tabanni (kuchagua rai moja ya kisheria kuwa ya chama) katika masuala ya ibada, bali tunamwachia Mwislamu kufuata madhehebu yoyote katika saumu au swala... n.k. Hapa nitakutajia baadhi ya maoni ya kifikihi kuhusu kulipa saumu, na lile ambalo kifua chako litatulia nalo na moyo wako kukinai nalo, unaweza kulifuata:

1- Imekuja katika kitabu "Nihayat al-Matlub fi Dirayat al-Madhhab" cha mwandishi wake Abdul Malik al-Juwayni, maarufu kama Imam al-Haramayn (alifariki: 478 H) ambacho ni katika fikihi ya Shafi'i:

(Yule aliyepitwa na saumu ya siku za Ramadhani, na akaweza kuzilipa, haijuzu kwake kuchelewesha kulipa kwake mpaka mwezi wa Ramadhani wa mwaka unaofuata, na kile tunachotaja si jambo la kupendeza tu (mustahabb), bali ni lazima, pamoja na uwezo na kuondoka kwa udhuru. Na ikiwa itachukuliwa kuwa kulipa kumecheleweshwa mpaka mwaka unaofuata bila udhuru, basi ni lazima pamoja na kulipa, kutoa muddi moja ya chakula kwa kila siku. Na ikiwa atachelewesha kulipa kwa miaka miwili au zaidi, basi kuhusu kuongezeka kwa fidia kuna maoni mawili: Moja - kwamba haiongezeki, na halazimiki kwa kuchelewesha kwa miaka mingi isipokuwa kile kinacholazimika katika mwaka mmoja... Na kauli sahihi zaidi ni kuongezeka kwa fidia na kufanyika upya, hivyo ni lazima kwa mkabala wa kuchelewesha kila mwaka muddi moja. Ikiwa atachelewesha miaka miwili, italazimika pamoja na kulipa kila siku, muddi mbili. Na hivyo hivyo kwa ziada na kuendelea; basi huu ndio msimamo katika fidia...)

Hii inamaanisha kuwa kulipa saumu ya Ramadhani kwa yule asiyefunga, analipa kabla ya Ramadhani ijayo, na akichelewa baada ya kuingia Ramadhani, basi anapaswa kulipa na kutoa fidia... Na ana maoni mengine kuwa ikiwa atachelewesha kulipa kwa miaka miwili kwa mfano, basi ni lazima fidia mbili pamoja na kulipa, na kadhalika.

2- Imekuja katika kitabu "Kashshaf al-Qina' 'an Matn al-Iqna'" cha mwandishi wake Mansur bin Yunus al-Bahuti al-Hanbali (alifariki: 1051 H):

(Mwenye kupitwa na saumu ya Ramadhani yote ikiwa imekamilika au imepungua... hulipa idadi ya siku zake... na inajuzu kuchelewesha kulipa kwake mradi wakati wake haujapita, nao ni mpaka kuandama kwa Ramadhani nyingine... hivyo haijuzu kuichelewesha mpaka Ramadhani nyingine bila udhuru... Na ikiwa atachelewesha mpaka Ramadhani nyingine au mpaka Ramadhani kadhaa, basi anapaswa kulipa na kulisha masikini kwa kila siku kile kinachotosheleza katika kafara, na fidia hairudufiki kwa kukaririwa kwa Ramadhani; kwa sababu wingi wa kuchelewesha hauzidishi wajibu kama vile lau angechelewesha Hijja ya wajibu kwa miaka mingi, asingelazimika kufanya zaidi ya kuitekeleza.)...

Hii inamaanisha kuwa yule aliyepitwa na saumu ya Ramadhani na asilipe kabla ya kuingia Ramadhani ijayo, basi anapaswa kulipa na kutoa fidia.

3- Ama katika madhehebu ya Abu Hanifa, hata kama kulipa kutachelewa kiasi gani, halazimiki isipokuwa kulipa tu. Hivyo ikiwa Ramadhani nyingine itakuja... basi hulipa kile kilichompita, na hana fidia yoyote kwa kuchelewa:

  • Imekuja katika kitabu "Al-Mabsut" cha Al-Sarakhsi aliyefariki 483 H (Fikihi ya Hanafi):

Alisema: (Mtu ambaye ana deni la kulipa siku za mwezi wa Ramadhani na asizilipe mpaka Ramadhani ya mwaka unaofuata ikaingia... anapaswa kulipa Ramadhani iliyopita na hana fidia kwetu, na kwa upande wa Al-Shafi’i, Mwenyezi Mungu Mtukufu amrehemu, inamlazimu pamoja na kulipa, kulisha masikini kwa kila siku... Na sisi tuna dhahiri ya kauli yake Aliyetukuka:

فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

"basi (atapaswa kufunga) idadi (ya siku hizo) katika siku nyingine." (QS. Al-Baqarah [2]: 184)

Na hakuna ndani yake uwekaji wa wakati maalum, na kuweka wakati kati ya Ramadhani mbili itakuwa ni ziada. Kisha hii ni ibada iliyowekewa wakati, ambapo kulipa kwake hakuwekewi wakati...)

  • Na imekuja katika kitabu "Badai' al-Sanai' fi Tartib al-Sharai'" cha mwandishi wake Ala al-Din al-Kasani al-Hanafi (alifariki: 587 H):

(...Madhehebu kwa wenzetu (wanavyuoni wa Hanafi) ni kwamba uwajibu wa kulipa hauwekewi wakati kwa sababu tulizotaja kuwa amri ya kulipa imekuja kwa ujumla bila kuainisha baadhi ya nyakati bila nyingine, hivyo huenda kwa mujibu wa ujumla wake. Na juu ya hili, wenzetu walisema: Kwamba ikiwa atachelewesha kulipa Ramadhani mpaka ikaingia Ramadhani nyingine, basi hana fidia yoyote...).

Hii inamaanisha kuwa katika madhehebu ya Abu Hanifa, wajibu ni kulipa bila fidia, yaani analipa tu miezi ambayo hakufunga.

Na kama nilivyokutajia mwanzoni, sisi hatufanyi tabanni katika ibada, bali nimekutajia baadhi ya maoni ya madhehebu ya Abu Hanifa, Al-Shafi'i na mwanachuoni wa Hanbali, na kile ambacho kifua chako kinaridhika nacho, kifanye... Mwenyezi Mungu akufanikishe katika yale anayoyapenda na kuyaridhia.

Natumai kuwa katika haya kuna utoshelevu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi. 08 Ramadhani 1440 H - 13/05/2019 M] Mwisho wa nukuu kutoka kwa jawabu letu lililopita.

Muhtasari:

1- Ukadirie siku ambazo hukufunga kulingana na kile kinachozidi katika dhana yako (ghalabat al-zhann).

2- Baada ya hapo, somea yaliyotajwa hapo juu na uchukue rai ya madhehebu ambayo moyo wako umetulia nayo. Baadhi yao kama unavyoona wanasema kulipa saumu pamoja na fidia... na wengine wanasema kulipa bila fidia.

Ama kiasi cha fidia moja kilichotajwa hapo juu, yaani (muddi), uzito wa (muddi) katika gramu ni gramu 544 za ngano... Hiyo ni kama ilivyokuja katika kitabu "Al-Amwal":

[Muddi = 1 1/3 ratili ya Baghdad. Na ratili moja = gramu 408. Muddi = 1 1/3 ratili × gramu 408 uzito wa ratili = gramu 544 uzito wa muddi ya ngano.]

Na kuna wale wanaoihesabu kwa zaidi kidogo au mfano wa huo...

Na namuomba Mwenyezi Mungu Subhaanahu aifanye saumu na kisimamo kuwa vyenye kukubaliwa.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah

05 Sha’ban 1446 H Sawiya na 04/02/2025 M

Link ya jawabu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook

Share Article

Share this article with your network