Bismillahi Ar-Rahmani Ar-Rahim
(Sfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")
Kwenda kwa: Samia Alshami
Swali:
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Nilitaka kuuliza kuhusu uhalali wa kufunua nyayo za miguu kwa mwanamke katika maisha ya hadhara, na je, uharamu wa kufunua nyayo ni kama uharamu wa kufunua awrah nyingine yoyote ya mwanamke? Na ni ipi mipaka ya maisha ya faragha; je, ni ndani ya nyumba pekee au maeneo ya jirani na nyumba kwa nje yanachukuliwa kuwa ni maisha ya faragha? Na katika aya ya Jilbab, je, neno idnaa (kushusha) linajumuisha kufika kwa jilbab hadi kwenye nyayo? Je, kuna maelezo ya kina kuhusu sifa za mavazi ya miguu? Jazakallahu Khairan Sheikh wetu.
Jibu:
Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.
1- Mipaka ya maisha ya faragha ni mipaka ya nyumba ambapo mwanamke anaweza kufunua awrah yake na asionekane na mwanamume ajnabiy (asiye mahram wake). Hii ina maana kuwa nje ya mipaka ya nyumba si sehemu ya maisha ya faragha. Hivyo, akitoka kwenda kununua bidhaa kwenye duka la mtaani ambapo nyumba ipo, ni lazima awe amesitiri awrah yake na kuvaa vazi la kisheria. Hii ni kwa sababu maisha ya faragha, kama tulivyosema hapo awali, ni mahali ambapo inaruhusiwa kwa mwanamke kufunua awrah yake bila kuonekana na mwanamume ajnabiy, yaani ndani ya mipaka ya nyumba.
2- Nyayo za miguu ni awrah, hivyo mwanamke ni lazima asitiri miguu yake, na dalili ya hilo ni:
a- Mwenyezi Mungu (swt) anasema kuhusu vazi la mwanamke kwa upande wa chini:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ
"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake wa Waumini wajiteremshie (wajivute chini) jilbab zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana." (QS. Al-Ahzab [33]: 59)
Yaani wazishushe jilbab zao kuelekea chini. Na kitendo cha kushusha (al-irkhau) katika neno yudnina (yaani wazishushe) hakiwezi kutimia isipokuwa kwa jilbab kufika kwenye nyayo za miguu angalau na kuzifunika. Ikiwa nyayo hizo zimesitiriwa kwa soksi au viatu, basi kushusha huko kunatimia kwa jilbab kufika kwenye nyayo. Lakini ikiwa hazikusitiriwa kwa soksi au viatu, basi ni lazima jilbab ifike hadi ardhini ili kufunika nyayo hizo. Hii ina maana kuwa nyayo ni sehemu ya awrah.
b- Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar kwamba amesema: Mtume (saw) amesema:
مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلاَءَ لَمْ يَنْظُرِ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَقَالَتْ أُمُّ سَلَمَةَ فَكَيْفَ يَصْنَعْنَ النِّسَاءُ بِذُيُولِهِنَّ قَالَ يُرْخِينَ شِبْرًا فَقَالَتْ إِذًا تَنْكَشِفُ أَقْدَامُهُنَّ قَالَ فَيُرْخِينَهُ ذِرَاعًا لاَ يَزِدْنَ عَلَيْهِ
"Yeyote atakayevuta nguo yake kwa kiburi, Mwenyezi Mungu hatamtazama Siku ya Kiyama. Umm Salama akasema: 'Basi wafanye nini wanawake na upindo wa nguo zao?' Akasema: 'Wazishushe kwa shibiri moja.' Akasema: 'Basi nyayo zao zitafichuka.' Akasema: 'Basi wazishushe kwa dhiraa moja na wasizidishe zaidi ya hapo.'" (Imetolewa na At-Tirmidhi na akasema hadith hii ni Hasan Sahih).
Hadith hii iko wazi kuwa wajibu kwa mwanamke ni kusitiri nyayo zake. Umm Salama (ra) hakutosheka na kushushwa kwa nguo za wanawake kutoka chini (upindo) kwa kiasi cha shibiri moja kwa hofu ya kufichuka kwa nyayo wakati wa kutembea, hasa mwanamke anapotembea peku kama ilivyokuwa ikitokea mara nyingi huko nyuma. Hivyo, Mtume (saw) aliruhusu kuvutwa kwa nguo ya mwanamke kwa kiasi cha dhiraa moja na asizidishe. Sababu (illah) iko wazi katika hadith: «...basi nyayo zao zitafichuka...».
Muhtasari ni kwamba nyayo za miguu ni awrah na ni lazima kuzifunika kama sehemu nyingine yoyote ya awrah.
3- Kwa taarifa, kuna maoni ya Abu Hanifa yanayoruhusu kudhihirisha nyayo kwa sababu aliona katika tafsiri ya kauli yake Subhaanahu:
وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا
"Wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika (kawaida)." (QS. An-Nur [24]: 31)
Aliona kuwa kile kinachodhihirika si uso na vitanga vya mikono pekee, bali pia na nyayo za miguu. Lakini kama tulivyotaja hapo juu, maoni haya ni dhaifu zaidi (marjuh) kutokana na ushahidi wa aya tukufu na hadith ya At-Tirmidhi. Na Allah ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.
Wassalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir