Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Baba Kukataa Kazi Aliyopewa Binti Yake

December 23, 2013
4288

** (Sfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)**

Kwa Z.G

Swali:

As-salamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

Ningependa kukuuliza kuhusu jambo linalohusiana na kazi niliyopewa, lakini babangu amekataa kwa mtazamo wake kwamba jamii hii ni yenye uharibifu, na kwamba wajibu wake kama baba ni kumlinda binti yake na kuwa mwangalifu naye dhidi ya mambo maovu yanayoenezwa na baadhi ya watu katika jamii.

Kuhusu muktadha wa kazi hiyo, ni kama mwongozaji na mtoa huduma ya kwanza kwa watoto wa umri wa miaka tisa. Na mwongozo utahusu Al-Quds; kuta zake, misikiti yake na kila kitu kinachohusiana nayo, na nitafanya kazi na mfanyakazi mwenzangu wa kike. Lakini babangu aliniambia kuwa jambo hilo haliishii tu kwenye kufanya kazi na msichana huyu, bali aliniambia kuwa mambo yataendelea na kuleta matawi mengine ambayo hatuyahitaji. Na kulingana na ujuzi wangu na kile nilichopewa, maingiliano yangu yatakuwa na huyu mfanyakazi mwenzangu pekee. Lakini baba yangu anasisitiza kukataa kazi hii kwa kiwango kile kile cha msisitizo nilionao ndani yangu wa kutaka kupata uzoefu huu. Pia aliniambia kuwa kazi yoyote ya namna hii haikubaliki kabla ya kusimama kwa Dola ya Khilafah na kuwepo kwa mchunga anayewalinda raia wake, nini maoni yako??

Jibu:

Wa Alaykum As-salamu Warahmatullahi Wabarakatuh

Hakika jambo la kwanza ni kumtii baba yako, kwani yeye anakutakia usafi na utakaso...

Hakika kazi yako kama mwongozaji wa watoto kuhusu Al-Quds ni mubah ikiwa itaishia kwenye jambo hili pekee. Lakini taasisi utakayofanya kazi ndani yake huenda kazi yake isiishie tu kwa watoto, bali inawezekana ikahitaji shughuli nyingine za baadaye zenye mchanganyiko wa jinsia (ikhtilat) au mfano wake, na inaonekana kuwa baba yako anahofia hilo. Kwa vyovyote vile, bila shaka unajua kwamba Maswahaba (ra), wanaume kwa wanawake, walikuwa wakiepuka baadhi ya aina za mubah ambazo ziko karibu na vumbi la haramu ili wasitumbukie katika haramu.

Na kwa ufupisho: Elewana na baba yako; akikinai kwamba kazi hii haijachanganyika na vumbi la haramu na moyo wake ukatulia kwamba taasisi hiyo utakayofanya kazi nayo itajitolea kuwa kazi hiyo isiwe na mchanganyiko wa jinsia (ikhtilat), bali iishie tu kwenye kuwaongoza watoto, akitulia kwa hilo basi ni kheri. Lakini ikiwa hatakubali, basi mtii hata kama kazi hiyo ni mubah tupu na hataki utoke kwenda kufanya kazi hiyo, basi mtii na utapata malipo na thawabu. Kwani Allah Subhanahu amefungamanisha ibada Yake na kuwafanyia wema wazazi wawili, na miongoni mwa kuwafanyia wema ni kuwatii katika lile ambalo ni kheri. Allah Subhanahu amesema:

وَقَضَى رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِنْدَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُلْ لَهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُلْ لَهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا

"Na Mola wako Mlezi amehukumu kuwa msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, au wote wawili, basi usiwaambie hata 'Ah!' (usiwakaripie), wala usiwakemee, na useme nao maneno ya heshima." (Al-Isra [17]: 23)

Na Ahmad ametoa katika Musnad yake kutoka kwa Abdullah bin Amr amesema: Hakika baba yangu alinishitaki kwa Mtume (saw), akasema:

أَطِعْ أَبَاكَ مَا دَامَ حَيًّا، وَلَا تَعْصِهِ

"Mtii baba yako maadamu yuko hai, na usimuasi."

Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network