Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Swapo na Utumaji wa Fedha

January 20, 2016
7227

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali: Swapo na Utumaji wa Fedha

Kwa Muhammad Al-Zaru

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Ninaomba kwa Mwenyezi Mungu uwe katika hali nzuri ya afya na heri, na ninaomba kuwa bishara ya Mtume ﷺ imekaribia. Swali langu: Je, inajuzu kubadilisha sarafu moja kwa sarafu nyingine bila mimi kuipokea na kisha itumwe sehemu nyingine? Kwa mfano: Ninataka kununua dinari 1,000 kutoka kwa mfanyabiashara wa kubadilisha fedha (sarraf) na tukakubaliana kila kitu, kisha nikamlipa kiasi tulichokubaliana katika kikao hicho hicho na nikamwambia aitume hiyo pesa sehemu fulani bila mimi kuipokea hiyo dinari 1,000. Je, hili linajuzu au ni sharti kuwepo na upokeaji (taqabudh)? Baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako, akusaidie, akuthibitishe na kukunusuru kwa ushindi.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Hakika muamala huu hauishii tu kwenye utumaji fedha (hawala), bali unaambatana na muamala wa kubadilisha fedha (sarf), kwani wewe unanunua dinari kwa sarafu nyingine. Kwa mfano, unampa riyal 3,000 mkabala wa dinari 1,000 kisha yeye anazituma kwenye upande unaoutaka. Hii ina maana kwamba kwanza ni kubadilisha fedha (sarf) na baada ya hapo ni utumaji (hawala):

  • Kuhusu kubadilisha fedha (sarf) kati ya sarafu mbili tofauti, ni lazima iwe mkono kwa mkono, yaani upokeaji uwe wa papo hapo, vinginevyo itakuwa haramu:

Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Sulayman bin Abi Muslim, amesema: Nilimuuliza Aba Al-Minhal kuhusu kubadilisha fedha (sarf) mkono kwa mkono, akasema: Mimi na mshirika wangu tulinunua kitu fulani mkono kwa mkono na kingine kwa mkopo (nasi’ah). Kisha akatujia Al-Bara bin Azib, tukamuuliza, naye akasema: Mimi na mshirika wangu Zaid bin Arqam tulifanya hivyo na tukamuuliza Mtume ﷺ kuhusu hilo, akasema:

مَا كَانَ يَدًا بِيَدٍ، فَخُذُوهُ وَمَا كَانَ نَسِيئَةً فَذَرُوهُ

"Kile kilicho mkono kwa mkono, kichukueni; na kile kilicho cha mkopo, kiacheni." (HR Bukhari)

Na Muslim amepokea kutoka kwa Malik bin Aws bin Al-Hadathan, kwamba amesema: Nilitoka huku nikisema nani anabadilishana dharaham? Talha bin Ubaydullah akasema – naye alikuwa kwa Umar bin Al-Khattab: Tuonyeshe dhahabu yako, kisha uje kwetu mtumishi wetu atakapokuja tukupe fedha yako (wariq). Umar bin Al-Khattab akasema: Hasha, walahi! Aidha umpe fedha yake sasa hivi, au umrudishie dhahabu yake, kwani Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

الْوَرِقُ بِالذَّهَبِ رِبًا، إِلَّا هَاءَ وَهَاءَ، وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ رِبًا، إِلَّا هَاءَ وَهَاءَ، وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ رِبًا، إِلَّا هَاءَ وَهَاءَ، وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ رِبًا، إِلَّا هَاءَ وَهَاءَ

"Fedha kwa dhahabu ni riba isipokuwa (ikiwa ni) chukua na chukua (papo hapo), na ngano kwa ngano ni riba isipokuwa chukua na chukua, na shayiri kwa shayiri ni riba isipokuwa chukua na chukua, na tende kwa tende ni riba isipokuwa chukua na chukua." (HR Muslim)

Pia Muslim amepokea kutoka kwa Ubadah bin Al-Samit, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ، وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ، وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ، وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ، وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ، وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ، مِثْلًا بِمِثْلٍ، سَوَاءً بِسَوَاءٍ، يَدًا بِيَدٍ، فَإِذَا اخْتَلَفَتْ هَذِهِ الْأَصْنَافُ، فَبِيعُوا كَيْفَ شِئْتُمْ، إِذَا كَانَ يَدًا بِيَدٍ

"Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, shayiri kwa shayiri, tende kwa tende, na chumvi kwa chumvi, kiasi sawa kwa kiasi sawa, mkono kwa mkono. Na vikihitilafiana aina hizi, basi uzeni mnavyotaka ikiwa ni mkono kwa mkono." (HR Muslim)

Na maana ya "mkono kwa mkono" (yadan bi yadin) ni upokeaji wa papo hapo (taqabudh), huyu anachukua riyal na mwingine anachukua dinari, na hayo yote yanafanyika kwa wakati mmoja...

  • Baada ya wewe kuzipokea, unazituma kwenye upande ule, iwe kupitia kwa huyu mfanyabiashara wa fedha au mwingine.

  • Mtu anaweza kusema, kuna haja gani ya kupokea pesa ikiwa pesa hizo hizo zitatumwa? Jibu ni kwamba haja hiyo inatokana na hadithi za Mtume ﷺ, kwani ndani yake mna dalili wazi, yenye kutilia mkazo, isiyo na utata wala utatanishi. Zimekuja kwa maneno ya wazi na yenye kukata (qath'i ad-dalalah) yanayoonyesha ulazima wa upokeaji wa papo hapo: "ha'a bi ha'a" (chukua na chukua), "yadan bi yadin" (mkono kwa mkono). Maneno haya ni miongoni mwa dalili zilizo wazi kabisa kuhusu upokeaji wa papo hapo, hivyo hayakubali maelezo mengine (ta'lil) wala tafsiri nyingine (ta'wil). Hivi ndivyo ninavyofahamu kutokana na hayo, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Facebook wa Amir: https://web.facebook.com/AmeerhtAtabinKhalil/photos/a.122855544578192.1073741828.122848424578904/436013699929040/?type=3&permPage=1

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Google Plus wa Amir: https://plus.google.com/u/0/b/100431756357007517653/100431756357007517653/posts/iFhJXgLhnG5

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Twitter wa Amir: https://twitter.com/ataabualrashtah/status/689513371595579392

Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir: http://archive.hizb-ut-tahrir.info/arabic/index.php/HTAmeer/QAsingle/3676/

Share Article

Share this article with your network