Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Kusitiri Mwanamke Miguu Yake Katika Swala

March 27, 2017
7151

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir

Kuhusu maswali ya watembeleaji wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jawabu la Swali

Kwa Muhamad Awesat

Swali:

As-salamu alaykum, ...na nini hukumu yake katika swala nyumbani kwake, je ni lazima kusitiri miguu yake kwa kuwa kusitiri 'awrah ni miongoni mwa sharti za usahihi wa swala?

Jibu:

Wa alaykumus-salam wa rahmatullahi wa barakatuh,

  • Yalikuja katika jawabu la swali ambalo unalitolea maoni yafuatayo:

(- Miguu miwili ni 'awrah, hivyo ni wajibu kwa mwanamke kusitiri miguu yake, na dalili ya hilo ni:

a- Mwenyezi Mungu (swt) anasema kuhusiana na vazi la mwanamke kwa upande wa chini:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَنْ يُعْرَفْنَ

"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake wa Waumini wajiteremshie uzuri nguo zao (majilbab yao). Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana." (QS Al-Ahzab [33]: 59)

Yaani waziteremshie majilbab yao kuelekea chini, na haitimii kuteremsha huku katika neno يُدْنِينَ (yaani kuteremsha) isipokuwa kwa jilbab kufika miguuni angalau na kuifunika. Ikiwa miguu imesitiriwa kwa soksi au viatu, basi kuteremsha huku kunatimia kwa jilbab kufika miguuni. Ama ikiwa haikusitiriwa kwa soksi au viatu, basi ni wajibu kwa jilbab kufika ardhini ili isitiri miguu, na hii ina maana kuwa miguu miwili ni sehemu ya 'awrah.

b- Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar akisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلاَءَ لَمْ يَنْظُرِ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَقَالَتْ أُمُّ سَلَمَةَ فَكَيْفَ يَصْنَعْنَ النِّسَاءُ بِذُيُولِهِنَّ قَالَ يُرْخِينَ شِبْرًا فَقَالَتْ إِذًا تَنْكَشِفُ أَقْدَامُهُنَّ قَالَ فَيُرْخِينَهُ ذِرَاعًا لاَ يَزِدْنَ عَلَيْهِ

"Yule anayeburura nguo yake kwa kiburi, Mwenyezi Mungu hatamtazama Siku ya Kiyama. Ummu Salama akasema: 'Basi wafanye nini wanawake na ncha za nguo zao (mabururo)?' Akasema: 'Waziteremshe kwa shubiri moja.' Akasema: 'Hapo miguu yao itafunuka.' Akasema: 'Basi waziteremshe kwa dhiraa moja, wala wasizidishe zaidi ya hapo.'" (Imepokelewa na At-Tirmidhi na akasema hadith hii ni hasan sahih).

Hadith hii iko wazi kuwa wajibu kwa mwanamke ni kusitiri miguu yake, na Ummu Salama (ra) hakutosheka na kuteremshwa nguo ya wanawake kutoka chini (mabururo) kwa shubiri moja kwa hofu ya kufunuka miguu wakati wa kutembea, hususan ikiwa mwanamke anatembea bila viatu kama ilivyokuwa ikitokea mara nyingi zamani. Hivyo Mtume (saw) akajizia kubururwa nguo ya mwanamke kwa dhiraa moja na asizidishe, na sababu iko wazi katika hadith "...إِذًا تَنْكَشِفُ أَقْدَامُهُنَّ..." (hapo miguu yao itafunuka).

Muhtasari ni kuwa miguu miwili ni 'awrah na ni wajibu kuifunika kama sehemu nyingine yoyote ya 'awrah.

  • Na kwa ufahamu, kuna rai ya Abu Hanifa kuhusu kuruhusiwa kudhihirisha miguu kwa sababu aliona katika tafsiri ya kauli yake (swt):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

"Wala wasionyeshe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika." (QS An-Nur [24]: 31)

Aliona kuwa yale yanayodhihirika si uso na viganja pekee bali ni miguu pia. Lakini kama tulivyotaja hapo juu, rai hii ni dhaifu (marjuh) kutokana na dalili ya aya tukufu na hadith ya At-Tirmidhi. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.) Mwisho.

  • Na hili ndilo tunalolifuata (tunatabanni) katika maisha ya kijamii, hivyo hairuhusiwi kwa mwanamke kutoka huku miguu yake ikiwa wazi, bali ni kama tulivyotaja hapo juu:

(Yaani waziteremshie majilbab yao kuelekea chini, na haitimii kuteremsha huku katika neno يُدْنِينَ "yaani kuteremsha" isipokuwa kwa jilbab kufika miguuni angalau na kuifunika. Ikiwa miguu imesitiriwa kwa soksi au viatu, basi kuteremsha huku kunatimia kwa jilbab kufika miguuni. Ama ikiwa haikusitiriwa kwa soksi au viatu, basi ni wajibu kwa jilbab kufika ardhini ili isitiri miguu, na hii ina maana kuwa miguu miwili ni sehemu ya 'awrah).

  • Imebakia suala moja nalo ni kusitiri miguu wakati wa swala, kwani miongoni mwa sharti za usahihi wa swala ni kusitiri 'awrah. Na kwa ajili hiyo, rai yenye nguvu zaidi (rajih) kwetu ni kuwa miguu ni wajibu kusitiriwa wakati wa swala. Isipokuwa kwamba Abu Hanifa anaona kuwa miguu miwili si 'awrah. Imekuja katika Sharh Mukhtasar al-Tahawi cha mwandishi wake: Ahmad bin Ali Abu Bakr al-Razi al-Jassas al-Hanafi (aliyefariki: 370 H) yafuatayo:

(Suala: "'Awrah ya mwanamke katika swala" Abu Ja'far amesema: "Ama mwanamke, asitiri katika swala yake kila kitu isipokuwa uso wake, viganja vyake, na miguu yake." Abu Bakr amesema: Na hiyo ni kwa sababu mwili wake wote ni 'awrah, si halali kwa mgeni (ajnabi) kutazama isipokuwa viungo hivi. Na dalili yake ni kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

Inapokelewa kuwa hayo ni wanja na pete, hivyo ikafahamisha kuwa viganja vyake na uso wake si 'awrah. Na Mtume (saw) amesema: "Mwenyezi Mungu hakubali swala ya mwanamke aliyebalehe isipokuwa kwa khimar (hijabu)", hivyo ikafahamisha kuwa kichwa chake ni 'awrah. Na kile kilichokuwa ni 'awrah: ni wajibu kusitiriwa katika swala, na kiganja, uso, na mguu si 'awrah: hivyo si lazima kwake kusitiri katika swala.) Mwisho.

  • Rai hii ni dhaifu (marjuh) kama tulivyobainisha hapo juu... lakini sisi hatutaki kufanya tabanni (kufuata rai moja rasmi) katika suala hili kwani ni ibada. Hivyo si wajibu kwa mwanamke anayeswali kwa msingi wa madhehebu ya Hanafi kufunika miguu yake katika swala... lakini rai yenye nguvu zaidi (rajih) kwetu ni wajibu wa kusitiri miguu katika swala kwa sababu ni 'awrah.

  • Muhtasari:

1- Rai yenye nguvu zaidi (rajih) kwetu ni kwamba miguu miwili ni 'awrah, na tunafuata (tunatabanni) hilo katika maisha ya kijamii, hivyo haijuzu kwa mwanamke kutoka nyumbani kwake isipokuwa na jilbab lake linalositiri miguu yake, iwe ni kwa kufika ardhini kwa kiasi kinachotosha kusitiri miguu wakati wa kutembea kwake ikiwa anatembea bila viatu, au jilbab ifike kwenye kifundo cha mguu ikiwa amevaa soksi zinazofaa kusitiri miguu, na hilo ni ili kutimiza kuteremshwa (al-idna') ambako ni kuteremsha jilbab hadi miguuni kama tulivyofafanua kwa kina katika Nidham al-Ijtima'i (Mfumo wa Kijamii).

2- Ama kusitiri miguu katika swala, rai yenye nguvu zaidi (rajih) kwetu ni wajibu wa kuisitiri, lakini hatufanyi tabanni katika suala hili kwani ni ibada, hivyo mwanamke anayefuata madhehebu ya Abu Hanifa si wajibu kwake kusitiri miguu yake wakati wa swala.

Hili ndilo tunaloona katika suala hili, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

27 Jumada al-Thani 1438 H Inayowafikiana na 26/03/2017 M

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Facebook

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Google Plus

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Ameer kwenye Twitter

Kiungo cha jawabu kutoka Tovuti ya Ameer

Share Article

Share this article with your network