Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kufunga Siku Kumi za Kwanza za Dhul-Hijjah

July 28, 2019
3774

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir

kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Kwa Rashid Al-Radhi

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil, Allah akulinde na kukuifadhi,

Nina swali linalohusiana na kufunga siku kumi za kwanza za Dhul-Hijjah; je, ni jambo linalopendekezwa (mustahabb) na kuchukuliwa kuwa miongoni mwa vitendo vyema, au ni uzushi (bid’ah) na halikupokelewa kutoka kwa Mtume (saw)? Kwani nimesoma baadhi ya hadithi zilizopokelewa katika uwanja huu ambazo zinaonekana kana kwamba zinapingana. Je, inawezekana kuunganisha hadithi hizi? Tufahamishe, Allah akubariki.

Jibu:

Walaikum Assalam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Zimepokelewa hadithi kuhusu kufunga siku tisa za Dhul-Hijjah na hususan siku ya tisa ambayo ni siku ya Arafa... Kadhalika, zimepokelewa hadithi kuhusu fadhila za vitendo vyema katika siku kumi za kwanza za Dhul-Hijjah. Pia imepokelewa kutoka kwa Mama wa Waumini Aisha (ra) kwamba yeye hakumuona Mtume (saw) akifunga katika siku kumi hizo... Tutataja baadhi ya hadithi hizi, na baada ya hapo tutataja namna ya kuziunganisha pamoja, In Shaa Allah:

Kwanza: Mapitio ya baadhi ya hadithi kuhusu maudhui ya kufunga siku tisa za Dhul-Hijjah:

1- Kufunga siku tisa za Dhul-Hijjah ikiwemo siku ya Arafa

  • Muslim ametoa katika Sahih yake kutoka kwa Abu Qatada amesema: Mtume wa Allah (saw) amesema:

ثَلَاثٌ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ وَرَمَضَانُ إِلَى رَمَضَانَ فَهَذَا صِيَامُ الدَّهْرِ كُلِّهِ، صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ، وَصِيَامُ يَوْمِ عَاشُورَاءَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ

"Siku tatu katika kila mwezi, na Ramadhani hadi Ramadhani, huu ndio funga ya mwaka mzima. Funga ya siku ya Arafa, nataraji kwa Allah kuwa itafuta (madhambi ya) mwaka uliopita na mwaka unaokuja, na funga ya siku ya Ashura, nataraji kwa Allah kuwa itafuta (madhambi ya) mwaka uliopita." (Sahih Muslim)

  • Na Muslim ametoa katika Sahih yake kutoka kwa Abu Qatada al-Ansari (ra) amesema: Mtume wa Allah (saw) aliulizwa kuhusu funga ya siku ya Arafa akasema:

يُكَفِّرُ السَّنَةَ الْمَاضِيَةَ وَالْبَاقِيَةَ

"Inafuta (madhambi ya) mwaka uliopita na uliobakia." (Sahih Muslim)

  • Ahmad ametoa katika Musnad yake kutoka kwa Hunaidah bin Khalid kutoka kwa mkewe, kutoka kwa baadhi ya wake wa Mtume (saw) amesema:

كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَصُومُ تِسْعَ ذِي الْحِجَّةِ

"Mtume wa Allah (saw) alikuwa akifunga siku tisa za Dhul-Hijjah." (Imetolewa pia na Al-Bayhaqi katika Shu'ab al-Iman, na Abu Dawood katika Sunan yake).

2- Vitendo vyema katika kumi la Dhul-Hijjah

  • Al-Bukhari ametoa katika Sahih yake kutoka kwa Said bin Jubayr kutoka kwa Ibn Abbas, kutoka kwa Mtume (saw) kwamba amesema:

مَا العَمَلُ فِي أَيَّامٍ أَفْضَلَ مِنْهَا فِي هَذِهِ، قَالُوا: وَلاَ الجِهَادُ؟ قَالَ: وَلاَ الجِهَادُ، إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ يُخَاطِرُ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ، فَلَمْ يَرْجِعْ بِشَيْءٍ

"Hakuna vitendo katika siku yoyote vilivyo bora zaidi kuliko katika siku hizi (kumi za Dhul-Hijjah). Wakasema: Je, hata Jihad? Akasema: Hata Jihad isipokuwa mtu aliyetoka akahatatarisha nafsi yake na mali yake na asirudi na chochote." (Sahih Al-Bukhari)

  • Al-Bayhaqi ametoa katika Sunan al-Kubra kutoka kwa Said bin Jubayr kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume (saw) amesema:

مَا الْعَمَلُ فِي أَيَّامٍ أَفْضَلَ مِنْهُ فِي عَشْرِ ذِي الْحِجَّةِ. قَالُوا: يَا رَسُولَ اللهِ، وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللهِ؟ قَالَ: وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فِي سَبِيلِ اللهِ ثُمَّ لَا يَرْجِعُ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْءٍ

"Hakuna vitendo katika siku yoyote vilivyo bora zaidi kuliko katika kumi la Dhul-Hijjah. Wakasema: Ewe Mtume wa Allah, je, hata Jihad katika njia ya Allah? Akasema: Hata Jihad katika njia ya Allah isipokuwa mtu aliyetoka na nafsi yake na mali yake katika njia ya Allah kisha asirudi na chochote katika hivyo." (Imetolewa pia na Ibn Hibban katika Sahih yake).

3- Hadithi ya Mama wa Waumini Aisha (ra)

Muslim ametoa katika Sahih yake: Ametuhadithia Abu Bakr bin Abi Shaybah, na Abu Kuraib na Is-haq - Is-haq amesema: Ametuhadithia, na wengine wawili wamesema: - Ametuhadithia Abu Muawiyah, kutoka kwa Al-A'mash, kutoka kwa Ibrahim, kutoka kwa Al-Aswad, kutoka kwa Aisha (ra), amesema:

مَا رَأَيْتُ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم صَائِماً فِي الْعَشْرِ قَطُّ

"Sijawahi kumuona Mtume wa Allah (saw) akifunga katika kumi (la Dhul-Hijjah) kabisa." (Sahih Muslim)

Pili: Kuunganisha baina ya dalili:

Hakika hadithi za kwanza zinabainisha kuwa Mtume (saw) alikuwa akifunga siku tisa za kwanza za Dhul-Hijjah na hususan siku ya Arafa...

Na hadithi za pili zinabainisha fadhila ya vitendo vyema katika siku kumi za kwanza za Dhul-Hijjah...

Na hadithi ya Aisha (ra) inasema kuwa yeye hakumuona Mtume (saw) akifunga katika siku kumi za kwanza za Dhul-Hijjah...

Na kama ilivyo katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah, Juzu ya Tatu, mlango wa "Al-Ta’adul wa Al-Tarajih" – kipengele cha saba:

(Saba: Dalili inayothibitisha (al-muthbit) hupewa kipaumbele kuliko dalili inayokanusha (an-nafi). Ikiwa kuna dalili mbili, moja ikithibitisha na nyingine ikikanusha, basi ile inayothibitisha hupewa kipaumbele kwa sababu inajumuisha ziada ya elimu. Hiyo ni kama habari ya Bilal kwamba Mtume (saw) aliingia ndani ya Al-Ka'bah na kuswali, na habari ya Usama kwamba aliingia na hakuswali; basi hadithi ya Bilal hupewa kipaumbele.)

Kwa hivyo, inayothibitisha hupewa kipaumbele kuliko inayokanusha. Yaani, zile hadithi zinazofahamisha kufunga kwa Mtume (saw) katika siku ya Arafa na siku nyingine tisa za kwanza za Dhul-Hijjah ndizo zinazopewa kipaumbele dhidi ya hadithi ya Mama wa Waumini Aisha (ra). Hii inamaanisha kuwa kufunga siku tisa za Dhul-Hijjah, na hususan siku ya tisa ya Arafa, si uzushi (bid’ah) bali ndani yake kuna ujira mkubwa sana. Na Allah ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Natumai jibu hili linatosheleza.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah

25 Dhul-Qa'dah 1440 AH 28/07/2019 CE

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Allah amuhifadhi) kwenye Facebook

Share Article

Share this article with your network