Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JAWABU LA SWALI: KUHARAKISHA KUTOA ZAKA

September 10, 2016
5277

Kwa Hussam Abu Asab

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh. Je, hukumu ya kuingia kwa wakati inatumika katika hukumu ya Zaka? Swali ni: Nikitoa Zaka ya mali bila ya kupita mwaka mmoja (hawl), je, kile nilichokitoa kwa nia ya Zaka kinahesabiwa kuwa ni Zaka, au kinahesabiwa kuwa ni sadaka na faradhi hiyo haianguki mpaka mwaka utimie juu ya mali hiyo? Na je, hali ya Zaka ni kama hali ya swala, saumu, na Hijja ambazo zimefungamana na wakati maalumu usioruhusiwa kufanya kinyume chake? Ikiwa uwajibikaji wa Zaka umefungamana na wakati ambao ni hawl, je, ni lazima kushikamana na hawl na hairuhusiwi kwetu kutoa Zaka kabla ya hapo kutokana na kile kinachopelekea kuongezeka kwa mali? Mwenyezi Mungu akujazi heri na atunufaishe kwa elimu yako, naomba jibu kwa dharura.

Jawabu:

Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kwanza: Maudhui ya kuharakisha kutoa Zaka... Haya hapa yafuatayo:

1- Hakika kukamilika kwa mwaka (hawl) ni sharti katika sababu ya Zaka (nisabu). Ikiwa sharti limetimia, yaani mwaka umepita juu ya sababu (nisabu) bila kupungua, basi Zaka imewajibika... Lakini ikiwa Zaka itatolewa kabla ya kuwajibika kwake, basi utoaji huo unajuzu kwa dalili za kisheria zilizopokelewa, ikiwemo:

Al-Bayhaqi amepokea katika Al-Sunan Al-Kubra kutoka kwa Ali:

عَنْ عَلِيٍّ، أَنَّ الْعَبَّاسَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ سَأَلَ رَسُولَ اللهِ ﷺ فِي تَعْجِيلِ صَدَقَتِهِ قَبْلَ أَنْ تَحِلَّ فَأَذِنَ لَهُ فِي ذَلِكَ

"Kutoka kwa Ali, 'Kwamba Al-Abbas (ra) alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ kuhusu kuharakisha kutoa zaka yake kabla ya wakati wake kuingia, naye akamruhusu kufanya hivyo'."

Na Al-Daraqutni amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Hujr Al-Adawi, kutoka kwa Ali amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alimwambia Umar:

إِنَّا قَدْ أَخَذْنَا مِنَ الْعَبَّاسِ زَكَاةَ الْعَامِ عَامِ الْأَوَّلِ

"Hakika sisi tayari tulichukua kutoka kwa Al-Abbas zaka ya mwaka huu katika mwaka uliopita."

Na kwa msingi huo, kuharakisha kutoa Zaka kabla ya kuwajibika kwake ni jambo linalojuzu, na kile anachokitoa mwenye kuharakisha kinakuwa ni Zaka inayomwondolea faradhi na wala si sadaka ya sunna tu...

2- Maana ya kuharakisha Zaka ni kutoa Zaka ya mali kabla ya mwisho wa mwaka. Ikiwa mali imefikia nisabu katika mwezi wa Muharram mwaka huu, basi mwisho wa mwaka wake ni Muharram ya mwaka ujao, na hapo ndipo Zaka inapowajibika. Lakini inajuzu kuharakisha Zaka hiyo inayowajibika mwishoni mwa mwaka kwa kuilipa katika mwezi wa Ramadhani mwaka huu kwa mfano, yaani kabla ya wakati wake kwa takriban miezi minne... Na katika namna yake kuna tofauti kati ya mafakihi, nakunukulia maoni mawili miongoni mwayo:

Ibn Qudama anasema katika Al-Mughni kuhusu kujuzu kwa kuharakisha Zaka kabla ya kupita kwa mwaka juu ya nisabu, na anawajibu wale wanaosema haijuzu kwa kusema: (Tuna yale aliyopokea Al-Tirmidhi, kutoka kwa Ali, kutoka kwa Mtume ﷺ: Kwamba alimwambia Umar: Hakika sisi tayari tulichukua zaka ya Al-Abbas ya mwaka huu tangu mwaka uliopita. Na katika lafudhi nyingine alisema: Sisi tulikuwa tumeharakisha sadaka ya Al-Abbas kwa mwaka wetu huu tangu mwaka uliopita. Imepokelewa na Said kutoka kwa Ata, na Ibn Abi Mulaykah, na Al-Hassan bin Muslim, kutoka kwa Mtume ﷺ kama hadith mursal). Lakini yeye anaona kuharakisha ni kwa mali ya nisabu pekee ambapo anasema:

(Na akimiliki nisabu kisha akaharakisha kutoa zaka yake na zaka ya kile anachokichuma, na kile kinachozaliwa kutokana nayo, au faida anayoipata humo, basi inamtosheleza kwa nisabu hiyo bila nyongeza yake). Na anaongeza (Na Abu Hanifa amesema inamtosheleza; kwa sababu ni kitu kinachofuata kile anachokimiliki...). Na kama unavyoona, Mazhehebu ya Hanbali yanaona kuharakisha Zaka kwa mali aliyo nayo mkononi ikiwa ni zaidi ya nisabu na hawajuzishi kuharakisha kwa nyongeza inayotokana na mali hiyo kama vile faida kwa mfano au mfano wa hayo katika kipindi kilichobaki kufika mwisho wa mwaka... Ama Abu Hanifa anajuzisha kuharakisha Zaka kwa yote hayo.

Wala sitaki kupitisha rai (tabanni) yoyote kati ya hizo mbili, na unaweza kufuata rai yoyote unayotulia nayo kati ya rai hizi mbili. Ikiwa unamiliki nisabu kwa mfano katika Muharram mwaka huu na ukataka kuharakisha Zaka katika Ramadhani badala ya kusubiri mpaka mwisho wa mwaka katika Muharram mwaka ujao, unaweza kufanya yafuatayo:

  • Ama uharakishe Zaka ya mali uliyo nayo katika Ramadhani ikiwa ni zaidi ya nisabu, na wakati wa mwisho wa mwaka katika mwezi wa Muharram, unahesabu mali uliyo nayo iliyotokana na mali uliyoharakisha Zaka yake katika Ramadhani kama faida iliyopatikana kwayo kwa mfano, kisha unazitolea Zaka nyongeza hizo juu ya mali uliyokuwa umezitolea Zaka mwezi wa Ramadhani. Kwa mfano, ikiwa mali uliyoharakisha Zaka yake mwezi wa Ramadhani ilikuwa ni "10,000" na wakati wa mwisho wa mwaka mwezi wa Muharram kulikuwa na faida iliyotokana na mali uliyotolea Zaka ya "5,000", yaani mali uliyo nayo mwishoni mwa mwaka ni "15,000", basi utaitolea Zaka ile "5,000" ya ziada kwa sababu ulishaharakisha Zaka ya ile "10,000".

  • Ama uhesabu mali uliyo nayo katika Ramadhani na ukadirie mali itakayotokana nayo kama faida kwa mfano mpaka mwisho wa mwaka katika mwezi wa Muharram na utoe Zaka ya jumla hiyo, yaani Zaka ya kile ulicho nacho Ramadhani na kile kitakachotokana nacho kinachokadiriwa mpaka mwisho wa mwaka mwezi wa Muharram, na uharakishe Zaka ya yote hayo, tuseme iwe ni 18,000. Katika hali hii, ikiwa jumla ya mali uliyo nayo "mali ya msingi na faida yake" mwishoni mwa mwaka mwezi wa Muharram itakuwa ni zaidi ya mali uliyotolea Zaka, tuseme iwe 20,000, basi ni lazima utoe Zaka ya ziada ya 2,000.

Namuomba Mwenyezi Mungu (swt) akubali Zaka yako na iwe ni yenye heri na kukuombea shifaa siku ambayo mali wala watoto hawatofaa kitu isipokuwa yule atakayemjia Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika.

Pili: Maudhui ya wakati katika Zaka na Swala:

Hakika wakati kwa upande wa Swala ni Sabab (sababu ya kisheria), na sababu inapelekea kuwepo kwa hukumu inapokuwepo na kutokuwepo kwa hukumu inapokosekana. Kwa hiyo, hukumu huzunguka nayo katika kuwepo na kutokuwepo kwake. Hivyo basi, swala haisihi kabla ya kuingia kwa wakati wala baada ya kutoka kwake. Kwa mfano, Mtume ﷺ anasema kuhusu swala ya Adhuhuri kama alivyopokea Al-Tabarani katika Al-Kabir kutoka kwa Khabbab, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:

إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلُّوا

"Jua linapopinduka (kuelekea magharibi), basi swalini."

Na Al-Bayhaqi ametoa hadith kama hiyo pia. Na anasema ﷺ katika hadith ya nyakati za swala kuhusu swala ya Adhuhuri ambayo Muslim ameipokea kutoka kwa Abdullah bin Amr:

وَقْتُ الظُّهْرِ إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ وَكَانَ ظِلُّ الرَّجُلِ كَطُولِهِ، مَا لَمْ يَحْضُرِ الْعَصْرُ

"Wakati wa Adhuhuri ni jua linapopinduka na kivuli cha mtu kikawa na urefu sawa na urefu wake, maadamu wakati wa Alasiri haujaingia."

Hizi ni sababu (asbaab), hivyo swala haisihi bila kuwepo kwa sababu, na kama tulivyosema awali, swala ya Adhuhuri haisihi kabla ya kupinduka jua (kuelekea magharibi) wala baada ya kutoka kwa wakati...

Ama hawl (mwaka mmoja) kwa upande wa Zaka, yenyewe si sababu bali ni sharti katika sababu. Kwa hivyo, kutopatikana kwa sharti ni tofauti na kutopatikana kwa sababu, hasa kwa kuwa kuna nukuu inayojuzisha kuharakisha Zaka kabla ya mwisho wa mwaka. Ama nisabu katika Zaka ndiyo sababu (sabab), na kwa sababu hiyo, kabla ya kumiliki nisabu hakuna Zaka ya faradhi bali ni sadaka tu. Huu ndio utofauti katika maudhui ya hawl katika Zaka na maudhui ya wakati katika Swala. Na katika hili kuna utoshelevu InshaAllah.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jawabu kutoka kwenye tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network