Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Ukaguzi wa Hadithi "Watakuja watu Siku ya Kiyama ambao imani yao itakuwa ya ajabu..."

October 17, 2022
3556

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa, Sheikh Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni kwenye Ukurasa Wake wa Facebook wa "Fiqhi"

Jibu la Swali

Ukaguzi wa Hadithi "Watakuja watu Siku ya Kiyama ambao imani yao itakuwa ya ajabu..."

Kwa: Azzam Abu Fara

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.

Allah akabalie ibada zenu na kila mwaka muwe na heri Sheikh wetu,

Nilikuwa nikitafuta chimbuko (takhrij) la hadithi hii lakini sijaipata kwa tamshi hili... Naomba msaada.

(Watakuja watu Siku ya Kiyama ambao imani yao itakuwa ya ajabu, nuru yao itakimbia mbele yao na kuume kwao, kisha kusemwa: heri yenu leo na amani iwe juu yenu, mmekuwa wema basi iingieni mkikaa humo milele. Malaika na manabii watawaonea wivu kwa mapenzi ya Allah kwao. Maswahaba wakasema: Ni nani hao ewe Mjumbe wa Allah? Akasema: Si miongoni mwetu wala miongoni mwenu, kwani nyinyi ni maswahaba wangu na wao ni wapenzi wangu. Hawa watakuja baada yenu na watakuta kitabu ambacho watu wamekiacha na sunnah waliyoifisha. Hivyo wataelekea kwenye kitabu na sunnah, wataifufua, wataisoma na kuifundisha watu. Watakutana katika njia hiyo na adhabu kali na yenye nguvu kuliko mliyokutana nayo. Hakika imani ya mmoja wao ni sawa na imani ya watu arobaini miongoni mwenu, na shahidi mmoja miongoni mwao ni sawa na mashahidi arobaini miongoni mwa mashahidi wenu. Kwani nyinyi mnapata wasaidizi kwenye haki na wao hawapata wasaidizi kwenye haki, watakuwa wamezungukwa na madhalimu kila mahali, nao watakuwa Baitul Maqdis na pembezoni mwake. Wakati huu nusura ya Allah itawafikia na utukufu wa Waislamu utakuwa mikononi mwao. Akasema: Ewe Allah wanusuru na uwajalie wawe marafiki zangu kwenye Hodhi (Haudh)).

Barakallahu fikum.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

1- Kuhusu maandishi (hadithi) unayoulizia, hatujaipata kwa tamshi hili katika kitabu chochote cha hadithi. Inaonekana baadhi ya matamshi yake yamechukuliwa kutoka hadithi mbalimbali zilizounganishwa pamoja na kufanywa na aliyeziunganisha kana kwamba ni hadithi moja:

أ- Pamoja na kwamba hadithi zilizoashiriwa ni hadithi za milango tofauti, na si riwaya mbalimbali za hadithi moja...

ب- Pia, baadhi ya hadithi zina matamshi yanayokaribiana na yale yaliyotajwa kwenye maandishi uliyoyauliza, lakini si matamshi yaleyale...

ج- Katika maandishi hayo pia kuna baadhi ya maana zilizopokewa kwenye baadhi ya hadithi ingawa matamshi ni tofauti...

د- Kisha, hadithi ambazo baadhi ya miundo na matamshi yake yamechukuliwa kwenye maandishi hayo, baadhi yake ni hadithi zinazokubalika (maqbul) zinazoweza kutolewa hoja, na nyingine ni hadithi zisizo sahihi na zisizoweza kutolewa hoja...

2- Nitakutajia baadhi ya hadithi hizo zinazokubalika ambazo hutolewa hoja:

  • Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Abu Malik al-Ash'ari kwamba Mjumbe wa Allah ﷺ alipomaliza swala yake, aliwageukia watu kwa uso wake na kusema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اسْمَعُوا وَاعْقِلُوا وَاعْلَمُوا أَنَّ لِلَّهِ عَزَّ وَجَلَّ عِبَاداً لَيْسُوا بِأَنْبِيَاءَ وَلَا شُهَدَاءَ يَغْبِطُهُمْ الْأَنْبِيَاءُ وَالشُّهَدَاءُ عَلَى مَجَالِسِهِمْ وَقُرْبِهِمْ مِنْ اللَّهِ

"Enyi watu, sikilizeni na mwelewe na mjueni kwamba Allah (swt) ana waja ambao si manabii wala si mashahidi, (lakini) manabii na mashahidi wanawaonea wivu kwa sababu ya vyeo vyao na ukaribu wao na Allah."

Kisha akaja mtu mmoja kutoka vijijini mwa mbali (A'rabi), akanyosha mkono wake kwa Nabii wa Allah ﷺ akisema: Ewe Nabii wa Allah, watu miongoni mwa watu si manabii wala si mashahidi lakini manabii na mashahidi wanawaonea wivu kwa vyeo vyao na ukaribu wao kwa Allah, tuelezee sifa zao. Uso wa Mjumbe wa Allah ﷺ ukawa na furaha kwa swali la yule mgeni, na Mjumbe wa Allah ﷺ akasema:

هُمْ نَاسٌ مِنْ أَفْنَاءِ النَّاسِ وَنَوَازِعِ الْقَبَائِلِ لَمْ تَصِلْ بَيْنَهُمْ أَرْحَامٌ مُتَقَارِبَةٌ تَحَابُّوا فِي اللَّهِ وَتَصَافَوْا يَضَعُ اللَّهُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَنَابِرَ مِنْ نُورٍ فَيُجْلِسُهُمْ عَلَيْهَا فَيَجْعَلُ وُجُوهَهُمْ نُوراً وَثِيَابَهُمْ نُوراً يَفْزَعُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يَفْزَعُونَ وَهُمْ أَوْلِيَاءُ اللَّهِ الَّذِينَ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ

"Ni watu kutoka makundi mbalimbali ya watu na matawi ya makabila ambao hawana uhusiano wa karibu wa kidamu, walipendana kwa ajili ya Allah na kuwa na usafi wa moyo. Allah atawawekea mimbari za nuru Siku ya Kiyama na kuwaketisha juu yake, atafanya nyuso zao kuwa nuru na nguo zao kuwa nuru. Watu watafadhaika Siku ya Kiyama lakini wao hawatofadhaika, nao ni marafiki (awliya) wa Allah ambao hawana khofu juu yao wala hawatahuzunika."

  • Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mjumbe wa Allah ﷺ alifika makaburini na kusema:

السَّلَامُ عَلَيْكُمْ دَارَ قَوْمٍ مُؤْمِنِينَ وَإِنَّا إِنْ شَاءَ اللَّهُ بِكُمْ لَاحِقُونَ وَدِدْتُ أَنَّا قَدْ رَأَيْنَا إِخْوَانَنَا

"Amani iwe juu yenu, makazi ya watu waumini, na sisi tukipenda Allah tutajiunga nanyi. Natamani laiti tungewaona ndugu zetu."

Wakasema: Je, sisi si ndugu zako ewe Mjumbe wa Allah? Akasema:

أَنْتُمْ أَصْحَابِي وَإِإِخْوَانُنَا الَّذِينَ لَمْ يَأْتُوا بَعْدُ

"Nyinyi ni maswahaba wangu, na ndugu zetu ni wale ambao bado hawajaja."

Wakasema: Utamjuaje yule ambaye bado hajaja katika Ummah wako ewe Mjumbe wa Allah? Akasema:

أَرَأَيْتَ لَوْ أَنَّ رَجُلاً لَهُ خَيْلٌ غُرٌّ مُحَجَّلَةٌ بَيْنَ ظَهْرَيْ خَيْلٍ دُهْمٍ بُهْمٍ أَلَا يَعْرِفُ خَيْلَهُ؟

"Je, unaonaje kama mtu ana farasi wenye weupe kwenye paji la uso na miguuni kati ya farasi weusi tii, je, hatamjua farasi wake?"

Wakasema: Ndiyo, ewe Mjumbe wa Allah. Akasema:

فَإِنَّهُمْ يَأْتُونَ غُرّاً مُحَجَّلِينَ مِنَ الْوُضُوءِ وَأَنَا فَرَطُهُمْ عَلَى الْحَوْضِ أَلَا لَيُذَادَنَّ رِجَالٌ عَنْ حَوْضِي كَمَا يُذَادُ الْبَعِيرُ الضَّالُّ أُنَادِيهِمْ أَلَا هَلُمَّ فَيُقَالُ إِنَّهُمْ قَدْ بَدَّلُوا بَعْدَكَ فَأَقُولُ سُحْقاً سُحْقاً

"Basi wao watakuja wakiwa na weupe kwenye nyuso na miguu kutokana na udhu, nami nitakuwa mtangulizi wao kwenye Hodhi (Haudh). Jueni kuwa kuna watu watafukuzwa kwenye Hodhi yangu kama anavyofukuzwa ngamia aliyepotea, nitawaita: 'Njooni hapa!' Kisha itasemwa: 'Hakika wao walibadilisha (dini) baada yako.' Basi nitasema: 'Potelea mbali, potelea mbali!'"

  • Muslim amepokea katika Sahih yake kutoka kwa Uqbah akisema: Nilimsikia Mjumbe wa Allah ﷺ akisema:

لَا تَزَالُ عِصَابَةٌ مِنْ أُمَّتِي يُقَاتِلُونَ عَلَى أَمْرِ اللَّهِ قَاهِرِينَ لِعَدُوِّهِمْ لَا يَضُرُّهُمْ مَنْ خَالَفَهُمْ حَتَّى تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ وَهُمْ عَلَى ذَلِكَ

"Halitaacha kundi miongoni mwa Ummah wangu kupigana juu ya amri ya Allah, wakiwashinda maadui zao, hawadhuriwi na wanaowapinga mpaka Kiyama kiwafikie wakiwa katika hali hiyo."

  • Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Al-Bara bin Azib kwamba Mtume ﷺ alimpiga mawe Myahudi na akasema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أُشْهِدُكَ أَنِّي أَوَّلُ مَنْ أَحْيَا سُنَّةً قَدْ أَمَاتُوهَا

"Ewe Allah, hakika mimi nakushuhudiza kuwa mimi ni wa kwanza kuhuisha sunnah ambayo wameifisha."

  • Ahmad amepokea katika Musnad yake kutoka kwa Abu Umamah akisema: Mjumbe wa Allah ﷺ amesema:

لَا تَزَالُ طَائِفَةٌ مِنْ أُمَّتِي عَلَى الْحَقِّ ظَاهِرِينَ لَعَدُوِّهِمْ قَاهِرِينَ لَا يَضُرُّهُمْ مَنْ خَالَفَهُمْ إِلَّا مَا أَصَابَهُمْ مِنْ لَأْوَاءَ حَتَّى يَأْتِيَهُمْ أَمْرُ اللَّهِ وَهُمْ كَذَلِكَ قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَأَيْنَ هُمْ؟ قَالَ: بِبَيْتِ الْمَقْدِسِ وَأَكْنَافِ بَيْتِ الْمَقْدِسِ

"Halitaacha kundi miongoni mwa Ummah wangu kuwa juu ya haki likiwashinda maadui zao, hawadhuriwi na wanaowapinga isipokuwa dhiki itakayowapata, mpaka amri ya Allah iwafikie wakiwa katika hali hiyo. Wakasema: Ewe Mjumbe wa Allah, wako wapi? Akasema: Baitul Maqdis na pembezoni mwa Baitul Maqdis."

  • At-Tirmidhi amepokea katika Sunan yake kutoka kwa Abu Umayyah al-Sha'bani akisema: Nilimwendea Abu Tha'labah al-Khushani nikamwambia: Unafanyaje na aya hii? Akasema: Aya gani? Nikasema: Kauli yake Allah (swt):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنْفُسَكُمْ لَا يَضُرُّكُمْ مَنْ ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

"Enyi mlioamini! Ni juu yenu (kujilinda) nafsi zenu. Hawatowadhuru walio potea mkiwapo nyinyi mmeongoka." (QS. Al-Ma'idah [5]: 105)

Akasema: Wallahi, umeuliza kwa mjuzi wake. Nilimuuliza Mjumbe wa Allah ﷺ kuhusu hilo naye akasema:

بَلِ ائْتَمِرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَتَنَاهَوْا عَنِ الْمُنْكَرِ حَتَّى إِذَا رَأَيْتَ شُحّاً مُطَاعاً وَهَوًى مُتَّبَعاً وَدُنْيَا مُؤْثَرَةً وَإِعْجَابَ كُلِّ ذِي رَأْيٍ بِرَأْيِهِ فَعَلَيْكَ بِخَاصَّةِ نَفْسِكَ وَدَعِ الْعَوَامَّ فَإِنَّ مِنْ وَرَائِكُمْ أَيَّاماً الصَّبْرُ فِيهِنَّ مِثْلُ الْقَبْضِ عَلَى الْجَمْرِ لِلْعَامِلِ فِيهِنَّ مِثْلُ أَجْرِ خَمْسِينَ رَجُلاً يَعْمَلُونَ مِثْلَ عَمَلِكُمْ

"Bali amrisheni mema na kutaneni na maovu, mpaka utapoona uchoyo unaotiiwa, na matamanio yanayofuatwa, na dunia iliyopendelewa, na kila mwenye maoni akijivunia maoni yake, basi jishughulishe na nafsi yako na uwaache watu wa kawaida. Kwani mbele yenu kuna siku ambazo kusubiri ndani yake ni kama kushika kigingi cha moto, mfanyaji kazi ndani yake ana ujira wa watu hamsini wanaofanya kazi kama yenu."

Abdullah bin Mubarak akasema: Na mwengine asiyekuwa Utbah aliniongezea: Ilisemwa: Ewe Mjumbe wa Allah, ujira wa hamsini miongoni mwetu au miongoni mwao? Akasema:

بَلْ أَجْرُ خَمْسِينَ مِنْكُمْ

"Bali ni ujira wa hamsini miongoni mwenu."

Abu Isa (At-Tirmidhi) akasema: Hii ni hadithi hasan gharib.

3- Hadithi zilizotajwa hapo juu ni hadithi zinazokubalika ambazo hutolewa hoja. Lakini pia kuna hadithi ambazo zina upungufu (maqal) na zina maneno na miundo inayofanana na baadhi ya yaliyokuja kwenye maandishi uliyoyauliza. Nitataja baadhi yake ili kubainisha kuwa maandishi hayo yameundwa kutokana na hadithi mbalimbali sahihi na zisizo sahihi:

  • Imekuja katika Al-Ibanah al-Kubra cha Ibn Battah, Mtume ﷺ amesema:

رحمة الله على خلفائي

"Rehema ya Allah iwe juu ya makhalifa wangu."

Wakasema: Ni nani makhalifa wako? Akasema:

الذين يحيون سنتي، ويعلمونها عباد الله

"Wale wanaohuisha sunnah yangu na kuifundisha kwa waja wa Allah."

Na imekuja katika Musnad al-Shihab al-Quda'i kutoka kwa Kathir bin Abdullah al-Mazni, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake, akasema: Mjumbe wa Allah ﷺ amesema:

إن الدين بدأ غريبا، وسيعود كما بدأ غريبا، فطوبى للغرباء

"Hakika dini ilianza ikiwa ngeni, na itarudi kuwa ngeni kama ilivyoanza, basi heri ni ya wageni (ghurabaa)."

Ikulilizwa: Ewe Mjumbe wa Allah, ni nani hao wageni? Akasema:

الذين يحيون سنتي ويعلمونها عباد الله

"Wale wanaohuisha sunnah yangu na kuifundisha kwa waja wa Allah."

Na imekuja katika Jami' al-Ahadith: [... Ewe Allah warehemu makhalifa wangu watakaokuja baada yangu, wakisimulia hadithi zangu na sunnah yangu na kuwafundisha watu (At-Tabarani katika Al-Awsat, Ar-Ramahurmuzi katika Al-Muhaddith al-Fasil, Al-Khatib katika Sharaf Ashab al-Hadith, na Ibn al-Najjar kutoka kwa Ibn Abbas kutoka kwa Ali). At-Tabarani amesema: Ahmad bin Isa Abu Tahir al-Alawi pekee ndiye aliyeipokea. Imesemwa katika Al-Mizan: Ad-Daraqutni amesema: Ni muongo, na hadithi hiyo ni batili...].

  • Imekuja katika Kanz al-Ummal kutoka kwa Anas akisema: Mjumbe wa Allah ﷺ amesema:

متى ألقى أصحابي؟ متى ألقى أحبابي؟

"Lini nitakutana na maswahaba wangu? Lini nitakutana na wapenzi wangu?"

Baadhi ya maswahaba wakasema: Je, sisi si wapenzi wako? Akasema:

أنتم أصحابي، ولكن أحبابي قوم لم يروني وآمنوا بي أنا إليهم بالأشواق

"Nyinyi ni maswahaba wangu, lakini wapenzi wangu ni watu ambao hawajaniona na wakaniamini, mimi nina hamu kubwa nao."

Hadithi hii ina wapokezi waliokosolewa, na baadhi ya watafiti wamesema kuwa ni hadithi munkar na ya uongo... yaani hadithi hii si miongoni mwa hadithi zinazokubalika ambazo hutolewa hoja.

4- Hivyo inabainika kuwa maandishi uliyoyauliza si hadithi ya Mtume ﷺ, bali ni maandishi yaliyoundwa, inaonekana yameandaliwa na mtu asiyejulikana ambaye amekusanya ndani yake maneno na miundo iliyokuja katika hadithi tofauti, baadhi yake ni sahihi na nyingine si sahihi. Kwa hivyo, haifai kupokelewa maandishi haya uliyoyauliza kwa kuyasifu kuwa ni hadithi kutoka kwa Mjumbe wa Allah ﷺ.

Na Allah ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

20 Rabi' al-Awwal 1444 AH 16/10/2022 BK

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir (Allah amuhifadhi) kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir (Allah amuhifadhi) Wavuti

Share Article

Share this article with your network