Jibu la Swali
Swali:
Kuhusu suala la rikaz, imeelezwa katika kitabu cha Al-Amwal kwamba katika rikaz kuna khums (moja ya tano). Swali hapa ni: Kuhusu maumbo na madini yenye sifa fulani au yanayoelezea mtazamo fulani wa kimaisha kama vile misalaba na sanamu zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu, je, inajuzu kumilikiwa ikiwa ni rikaz? Kwa maana ya kuziuza na kufaidika na thamani yake na kutoa khums kutokana na hizo?
Jibu:
Kuhusu rikaz, ikiwa kitu chenyewe ni haramu, basi ni haramu kukimiliki na kukifanyia biashara kwa kuuza au kununua...
Kwa hivyo, Muislamu akipata rikaz iliyozikwa ya kitu cha haramu kama "misalaba au sanamu", haijuzu kwake kuimiliki kwa sababu ya umbo lake haramu. Lakini inajuzu kwake kuivunja ili kubadilisha umbo lake haramu na kuuza vipande vyake. Khums ya thamani yake, ikiwa Khilafah imesimama, basi inatolewa kwa dola ili itumike kwa ajili ya maslahi ya Waislamu na wahitaji. Na ikiwa Khilafah haijasimama, basi khums hiyo hutolewa kwa mafukara, masikini, na kwa ajili ya maslahi ya Waislamu, na sehemu nne zilizobaki ni zake.
Hii ni ikiwa sanamu na msalaba si mzoga (maitah), kwa sababu kuivunja hakuondoi sifa ya mzoga kutoka kwayo.
Ama ikiwa imetengenezwa kutokana na mifupa au pembe za mzoga, basi kuna hitilafu miongoni mwa mafaqihi kuhusu usafi (twahara) au unajisi wake... Na maoni ninayoyapendelea ni yale yanayosema kuwa ni najisi na sifa ya mzoga inaambatana nayo, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):
قَالَ مَنْ يُحْيِ الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ
"Alisema: Ni nani atakayeifufua mifupa nayo imesaga?" (QS. Ya-Sin [36]: 78)
Hivyo, dalili ya neno "yuhyi" (itakayoifufua) inapoambatana na mifupa inaashiria kuwa mifupa ya mzoga ni mzoga pia.
Kwa mujibu wa hayo, ikiwa sanamu au msalaba umetengenezwa kutokana na sehemu yoyote ya mzoga, basi haijuzu kunufaika nao hata kama utavunjwa, kwa sababu sehemu za mzoga ni mzoga na hukumu hiyo inazihusu.