Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Kumfuata Mujtahid Zaidi ya Mmoja katika Suala Moja

May 05, 2013
4605

Jibu la Swali

Kumfuata Mujtahid Zaidi ya Mmoja katika Suala Moja

Swali:

Je, kuna maelezo yanayotosheleza kuhusu suala ambalo hairuhusiwi kumfuata (taqlid) zaidi ya mujtahid mmoja ndani yake? Kisha nitajuaje kuwa hili ni suala moja au zaidi? Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu:

Imekuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Kwanza, katika mlango wa: Kuhama baina ya Mujtahid / ukurasa wa 234, 235 yafuatayo:

"Isipokuwa lazima iwe wazi kwamba suala ambalo anaruhusiwa kuacha hukumu aliyokuwa akiifuata na kufuata hukumu nyingine, sharti yake ni kuwa liwe suala lililojitenga na mengine na kuachwa kwake kusipelekee kuvurugika kwa hukumu nyingine za kisheria. Ama ikiwa limefungamana na jambo jingine, basi hairuhusiwi kuliacha mpaka ayaache masuala yote yaliyofungamana nalo, kwa sababu yote hayo yanachukuliwa kama suala moja. Kwa mfano ikiwa ni sharti katika hukumu nyingine au ni nguzo miongoni mwa nguzo za kitendo kizima. Na hiyo ni kama swala na udhu, na kama nguzo za swala. Hivyo basi, haisihi kwa anayemfuata Ash-Shafi’i kumfuata Abu Hanifa katika kauli yake kuwa kugusa mwanamke hakubatilishi udhu, kisha akaendelea kuswali kwa mujibu wa madhehebu ya Ash-Shafi’i. Pia haisihi kumfuata anayesema kuwa michezo mingi haibatilishi swala hata iwe mingi kiasi gani, au kwamba kutosoma Al-Fatihah si nguzo miongoni mwa nguzo za swala, huku akiendelea kuswali akimfuata anayesema kuwa kitendo kingi kinabatilisha swala au kwamba Al-Fatihah ni nguzo katika nguzo za swala. Hukumu ambayo inaruhusiwa kuiacha ni ile hukumu ambayo kuiacha kwake hakuathiri vitendo vinavyotekelezwa kwa mujibu wa hukumu nyingine za kisheria." Mwisho wa nukuu.

Ni wazi kutokana na hili kwamba ufafanuzi wa suala unategemea kujitenga kwake na masuala mengine, na kuachwa kwake kusipelekee kuvurugika kwa hukumu nyingine za kisheria; hivyo basi lisiwe nguzo au sharti la kufungika au sharti la kusihi kwa hukumu nyingine, kwani hapo litakuwa halikujitenga na mengine.

Tunaweza kufafanua hili zaidi kama ifuatavyo:

"Ufafanuzi wa Suala: Kinachokusudiwa na suala hapa ni kila kitendo au kundi la vitendo ambavyo usahihi wa vitendo vingine hautegemei juu yake.

Ama sehemu ya suala, ni kila kitendo ambacho ni lazima kiwepo ili kufikia usahihi wake, kama vile masharti na nguzo.

Mifano:

Udhu: Ni vitendo ambavyo usahihi wa vitendo vingine unategemea juu yake, kwa sababu usahihi wa swala unategemea udhu. Kwa hivyo, udhu si suala kulingana na ufafanuzi, bali unachukuliwa kuwa sehemu ya swala ambayo ni lazima iwepo ili kufikia usahihi wake.

Swala: Ni vitendo ambavyo usahihi wa vitendo vingine hautegemei juu yake. Hivyo, swala ni suala, na inachukuliwa kuwa sehemu yake ni kila kile ambacho ni lazima kiwepo ili kufikia usahihi wake, kama vile nguzo na masharti ya kusihi kama tohara na kuelekea kibla.

Nia katika Saumu: Ni kitendo ambacho usahihi wa kitendo kingine unategemea juu yake, kwani usahihi wa saumu unategemea nia. Kwa hiyo, nia si suala, bali ni sehemu ya suala jingine.

Saumu: Ni kitendo ambacho usahihi wa kitendo kingine hautegemei juu yake. Hivyo, saumu ni suala, na inachukuliwa kuwa sehemu yake ni kila kile ambacho ni lazima kiwepo ili kufikia usahihi wake, kama nia na kujizuia na vile vinavyofungulisha.

Kulingana na hili, ikiwa mtu atamfuata mujtahid katika swala, ni lazima amfuate katika sehemu zake zote kama vile udhu, kuoga janaba, tayamamu, kuelekea kibla, na nguzo za swala. Na ikiwa amemfuata mujtahid katika saumu, ni lazima amfuate katika sehemu zake zote kama vile nia na ulazima wa kuitia nia kila siku au mwezi mzima, na kama inasihi mchana au ni lazima iwe usiku, na mambo yanayofungulisha na ruhusa za kufungua.

Lakini anaruhusiwa kumfuata mujtahid mwingine katika suala jingine lililojitenga.

Haya yote ni maadamu mtu huyo ni mfuasi (muqallid). Ama ikiwa atakuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi (muhakama) wa dalili na kuzilinganisha (tarjih), basi inaruhusiwa kwake kumuacha mujtahid aliyekuwa akimfuata na kufuata dalili yenye nguvu zaidi.

Natumai jambo hili limekuwa wazi... Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye Mmiliki wa taufiki.

Share Article

Share this article with your network