(Sfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashta, Ameer wa Hizb ut-Tahrir juu ya maswali ya wageni wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Kwa Nazia Rehman
Swali:
(Assalaam u alaykum Sheikh mpenzi, Mwenyezi Mungu (swt) akulinde na akukirimu. Je, unaweza kufafanua ufafanuzi wa kukanza mali (Hoarding)? Katika kuishi wakati huu wa hali isiyoeleweka chini ya mfumo wa kibeberu, ni rahisi kufikiri kwamba tunapaswa kuwa na pesa kando kwani haijulikani ni lini dharura itatokea na gharama za ghafla za huduma za afya au safari ya dharura zinaweza kuwa kubwa mno kubebeka. Pia katika baadhi ya tamaduni ni jambo la kawaida sana kuweka dhahabu ya harusi kama rasilimali kwa ajili ya watoto kwa ajili ya ndoa zao. Kwa kutumia uhalisia huu na uelewa wa wazi wa kukanza mali, tafadhali unaweza kuelezea. Je, inaruhusiwa kwetu kuwa na akiba kwa ajili ya baadaye au tunawajibika kuzungusha utajiri wote? JazakAllah hu Khairan. Waslaam u alaykum. Umm Emaan – Pakistan) mwisho.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.
Mwanzoni, nakunukulia baadhi ya yale yaliyokuja katika kitabu cha Nfumo wa Kiuchumi (Al-Nidham al-Iqtisadi) kuhusu kuzuia kukanza mali na ufafanuzi wake:
(Kuzuia Kukanza Dhahabu na Fedha
...Utajiri huu mkubwa unawaandalia wamiliki wake fursa za kuweka akiba, na unasaidia kupata mapato makubwa, hivyo utajiri mkubwa unabaki pale penye mali nyingi, kwani mali huvuta mali. Ingawa juhudi ina athari katika kupata utajiri na kuandaa fursa za kutumia mali, hakuna hatari yoyote itokanayo na hali hiyo kwa uchumi; badala yake, unakuza utajiri wa kiuchumi wa jamii kama unavyokuza utajiri wa mtu mmoja mmoja. Lakini hatari hutoka tu kwenye fedha zinazokanzwa (zinazolundikwa) na baadhi ya watu wenye utajiri mkubwa. Kwa kukanza fedha, kiwango cha mapato hushuka, ukosefu wa ajira huenea, na watu hufika katika hali ya umaskini. Kwa hivyo, ni lazima kushughulikia kukanza fedha. Fedha ndicho chombo cha kubadilishana kati ya mali na mali, kati ya mali na juhudi, na kati ya juhudi na juhudi; ni kipimo cha mabadilishano haya. Zikitoweka sokoni na zisifikiwe na mikono ya watu, mabadilishano haya hukoma na gurudumu la uchumi husimama. Kwa kadiri chombo hiki kinavyopatikana mikononi mwa watu, ndivyo kasi ya kazi inavyosukumwa mbele...
...Hata hivyo, lazima ifahamike kwamba madhara haya yanatokana na kukanza fedha, na si kutokana na kuweka akiba. Kuweka akiba hakusimamishi gurudumu la kazi, bali kinacholisimamisha ni kukanza mali. Tofauti kati ya kukanza (kanz) na kuweka akiba (iddikhar) ni kwamba kukanza ni kukusanya fedha moja juu ya nyingine bila ya hitaji, hivyo ni kuzuia fedha kuingia sokoni. Ama kuweka akiba ni kuhifadhi fedha kwa ajili ya hitaji miongoni mwa mahitaji, kama vile kukusanya fedha ili kujenga nyumba, kuoa, kununua kiwanda, kufungua biashara, au mengineyo. Aina hii ya kukusanya fedha haiathiri soko wala gurudumu la kazi; kwa sababu si kuzuia mali, bali ni kuikusanya ili kuitumia, kwani itazunguka itakapowekwa katika matumizi. Kwa hiyo, hakuna hatari katika kuweka akiba, hatari ipo tu katika kukanza fedha, yaani kukusanya baadhi yake juu ya nyingine bila ya hitaji.
Uislamu umeruhusu kuweka akiba ya dhahabu na fedha kwa sababu ni kukusanya fedha kwa ajili ya hitaji. Hivyo umeruhusu mtumwa aliyefanya mkataba wa ukombozi (mukatab) kufanya kazi na kukusanya fedha moja juu ya nyingine ili alipe kile kinachomuwajibikia kwa bwana wake ili awe huru. Umeruhusu mwanaume kukusanya fedha ili apate mahari ya mwanamke wa kumuoa. Na umeruhusu kukusanya fedha ili kutekeleza ibada ya Hijja. Na haukuweka katika mali hii iliyokusanywa ya dhahabu na fedha chochote isipokuwa Zaka ikiwa itafikia kiwango cha nisabu (nisab) na kutimia mwaka (hawl).
Dhahabu na fedha, wakati aya iliposhuka kuzuia kuzikanza, zenyewe zilikuwa ndizo chombo cha kubadilishana na kipimo cha juhudi katika kazi na manufaa ya mali, iwe zimepigwa chapa kama dirham na dinari, au hazijapigwa chapa kama miche ya dhahabu na fedha (bullion). Kwa hiyo, katazo limeelekezwa kwenye dhahabu na fedha kwa sifa yake ya kuwa chombo cha kubadilishana.
Ama kukanza dhahabu na fedha, Uislamu umeharamisha hilo kwa tamko la wazi la Qur'an. Allah (swt) amesema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ
"Na wale wanaokanza dhahabu na fedha, na hawazitoi katika njia ya Allah, basi wabashirie adhabu kali." (QS. At-Tawbah [9]: 34)
Onyo hili la adhabu kali kwa wanaokanza dhahabu na fedha ni dalili iliyo wazi kwamba Shari'ah imetaka kuacha kukanza kwa takwa la mkazo, hivyo kukanza dhahabu na fedha ni haramu...) Mwisho wa nukuu kutoka kwenye Mfumo wa Kiuchumi kuhusu kukanza mali, na ni lazima ieleweke vyema kwa sababu majibu yanategemea maelezo haya.
Hapo awali tuliulizwa swali linalofanana na swali lako, na jibu langu kwa muulizaji tarehe 13/01/2014 lilikuwa kama ifuatavyo:
(1- Kukanza mali ni kuikusanya bila ya hitaji. Ikiwa kuna hitaji la kishari'ah, kama vile unakusanya mali ili ujenge nyumba, ununue ardhi, ujenge kiwanda, unataka kuoa, au una watoto unawakusanyia ada zao za masomo shuleni, au ili ununue gari, au mfano wa hayo, basi huku ni kukusanya kwa ajili ya hitaji na si kukanza mali. Bali ni kukusanya kwa njia ya halali na hutolewa Zaka ikiwa nisabu yake itatimiza mwaka. Ama kukusanya kwa ajili ya jambo la kufikirika tu (lisilo la hakika), basi hilo ni kukanza mali na hairuhusiwi. Kwa mfano, anakusanya mali kwa uwezekano kwamba huenda kukatokea tetemeko la ardhi likabomoa nyumba yake naye anataka kujenga nyumba wakati huo, au anakusanya mali moja juu ya nyingine akisema: "Haya ni matumizi ya miaka ishirini ijayo!"
2- Kukusanya matumizi yake na wale anaowahudumia yanayomtosha kwa mwaka mmoja ni jambo linaloruhusiwa na si kukanza mali kwa sababu Mtume (saw) alikuwa akiwapa mama wa waumini matumizi ya mwaka. Muslim ametoa kutoka kwa Umar, amesema: "Mali ya Banu al-Nadir ilikuwa miongoni mwa kile ambacho Allah alimpa Mtume Wake bila ya Waislamu kupigana kwa farasi wala ngamia. Hivyo basi, ilikuwa ni mali mahususi ya Mtume (saw), naye alikuwa akitoa matumizi kwa ajili ya familia yake kwa mwaka mzima, na kilichobaki alikuwa akikiweka katika kununua farasi na silaha kama maandalizi katika njia ya Allah". Nawawi anasema katika sharh yake ya Sahih Muslim (Na kauli yake: "Anatoa matumizi kwa familia yake kwa mwaka mzima" inamaanisha anatenga kwa ajili yao matumizi ya mwaka mmoja, lakini alikuwa akiyatumia kabla ya kuisha kwa mwaka katika njia za kheri, hivyo mwaka ulikuwa hauishi akiwa nayo...). Kwa hiyo, kukusanya mali kwa ajili ya matumizi kwa muda wa mwaka mmoja si kukanza mali, na hutolewa Zaka ikiwa nisabu yake imetimiza mwaka.
3- Mwanamke anayefanya kazi, akikusanya mali ili imsaidie katika harusi yake, basi huku si kukanza mali... Hali kadhalika anapokuwa na watoto, inaruhusiwa kwake kuwakusanyia ada zao za shule, au mahitaji yao... Haya yote si kukanza mali, bali nisabu hutolewa Zaka ikiwa itatimiza mwaka.
4- Vivyo hivyo kwa mwanamume, inaruhusiwa kwake kukusanya mali ili aoe, na hilo si kukanza mali. Na anapokuwa na watoto, inaruhusiwa kwake kuwakusanyia ada zao za shule au mahitaji yao... Haya yote si kukanza mali, bali nisabu hutolewa Zaka ikiwa itatimiza mwaka.
5- Ama kukusanya mali kama tahadhari ya kukabiliana na majanga ambayo yako mbali kutokea kwa kigezo kwamba yakitokea yatabomoa nyumba... na kuharibu milki... naye anataka kukusanya mali kama tahadhari kwa hali hizo zisizo za kawaida, basi hili hairuhusiwi.
6- Na suluhisho ninaloliona kwa wale ambao Allah amewafungulia mali nyingi inayozidi matumizi yao ya mwaka mmoja na kwa wale wanaowahudumia, na kusiwe na hitaji linalokusudiwa kutumiwa mali hiyo, basi naona mmiliki wa mali anapaswa kuiekeza katika mradi wa halali wa kiviwanda, kibiashara, au kilimo, au atoe sadaka au kulea mayatima au kutoa katika milango ya kheri ya sawasawa, na asiiache mali hiyo ikikusanywa moja juu ya nyingine bila kuitumia, kwani hapo itampitikia hukumu ya kukanza mali, yaani "kuihifadhi bila hitaji linalokusudiwa kuitumia", nalo ni haramu.)
Natumai katika hili kuna kutosheka.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashta
14 Jumada al-Ula 1440 H 20/01/2019 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Ameer (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Facebook Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Ameer (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Google Plus