Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: WAJIBU WA KUFUATANA KATIKA FUNGA YA KAFFARA

June 30, 2022
3322

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mwenye Kuheshimika Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Wajibu wa Kufuatana katika Funga ya Kaffara

Kwa: Abu Hanifa al-Shami

Swali:

Mwenyezi Mungu akubariki Amir wetu mtukufu,

Nini kitatokea ikiwa mtu ataanza kufunga miezi miwili katika mwezi wa Dhu al-Qi'dah kwa mfano, je inafaa kwake kufunga siku ya Adha, au inafaa kwake kukata mfululizo (wa kufuatana) kwa kula siku hiyo na kisha kuilipa baadaye?

Naomba ufafanuzi, na Mwenyezi Mungu akubariki.

Jibu:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Hakika wewe unatoa maoni yako katika ufafanuzi huu kwenye jibu la swali tulilolitoa mnamo tarehe 15 Sha'ban 1443 Hijria sawia na 18/03/2022 Miladi kuhusu kaffara ya kuua bila kukusudia, na je, inafaa mwezi wa Ramadhani uwe miongoni mwa miezi miwili ya kaffara ambayo Sharia imewajibisha kuifunga kwa yule asiyepata mtumwa...

Nawe unauliza kuhusu kufuatana (mfululizo) katika miezi miwili na je, ikiwa ataanza funga yake katika mwezi wa Dhu al-Qi'dah, je, inafaa kwake kufunga siku ya Adha? Na je, inafaa kwake kukata mfululizo huo kwa kula siku ya Adha?

Jibu la hilo ni kama ifuatavyo:

1- Hakika hukumu ya kaffara ya kuua bila kukusudia imekuja katika kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَنْ يَقْتُلَ مُؤْمِناً إِلَّا خَطَأً وَمَنْ قَتَلَ مُؤْمِناً خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُسَلَّمَةٌ إِلَى أَهْلِهِ إِلَّا أَنْ يَصَّدَّقُوا فَإِنْ كَانَ مِنْ قَوْمٍ عَدُوٍّ لَكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ وَإِنْ كَانَ مِنْ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ مِيثَاقٌ فَدِيَةٌ مُسَلَّمَةٌ إِلَى أَهْلِهِ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ فَمَنْ لَمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِنَ اللَّهِ وَكَانَ اللَّهُ عَلِيماً حَكِيماً

"Na haiwi kwa Muumini kumuua Muumini (mwenziwe) isipokuwa kwa makosa. Na mwenye kumuua Muumini kwa makosa, basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya (fidia) ya kukabidhiwa watu wake (aliyeuawa), isipokuwa kama watafanya sadaka (watasamehe). Na ikiwa (aliyeuawa) ni katika watu walio maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi amkomboe mtumwa aliye Muumini. Na ikiwa ni katika watu ambao pana mkataba baina yenu na wao, basi diya ikabidhiwe kwa watu wake na amkomboe mtumwa Muumini. Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo kuwa ni toba itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima." (QS An-Nisa [4]: 92)

Kulingana na aya hii tukufu, kinachotakiwa katika hali ya kutopatikana mtumwa ni kufunga miezi miwili mfululizo. Hii inamaanisha kuwa yule aliyewajibikiwa na kaffara ya funga anapaswa kufunga katika wakati ambao anaweza kutimiza takwa la aya hiyo la kufuatana (mfululizo) katika kufunga miezi miwili. Na jambo hili haliwezekani katika miezi ya Dhu al-Qi'dah na Dhu al-Hijjah kwa sababu funga hukatika ndani yake kwa kuwepo kwa siku ya Adha na siku za Tashreeq (tarehe 11, 12 na 13 Dhu al-Hijjah).

Kwa hivyo, ni wajibu kwa yule aliyewajibikiwa na kaffara ya kuua bila kukusudia kulingana na aya hii kutafuta uwezekano wa kufunga miezi miwili mfululizo bila kukatika ndani yake ambako anaweza kuepukana nako, kama tulivyobainisha katika jibu la swali letu lililopita.

Kwa ajili ya ufahamu, imekuja katika Ensaiklopidia ya Fiqhi ya Kuwait (Al-Mawsu’ah al-Fiqhiyyah al-Kuwaytiyyah) kutaja maoni ya madhehebu katika suala la kukata mfululizo (kufuatana) kwa kula siku za Eid mbili na siku za Tashreeq kama ifuatavyo:

[Yatayoandama kukatika kwa mfululizo katika funga za kaffara:

Mfululizo hukatika katika funga ya kaffara kwa mambo yaliyotajwa na mafaqihi ambayo ni: ................ c- Kuingia kwa Ramadhani, Eid mbili, na siku za Tashreeq:

12- Maimamu wa Hanafi wameenda katika msimamo kuwa kuingia kwa mwezi wa Ramadhani, Idul Fitri au Idul Adha na siku za Tashreeq kunakata funga ya kaffara kwa sababu ya wajibu wa kufunga Ramadhani na uharamu wa kufunga siku zilizobaki, na kwa sababu iko ndani ya uwezo wake kupata miezi miwili ambayo haina hayo yaliyotajwa. Na hili pia ndilo waliloenda nalo Shafi’i kwa upande wa funga ya mtu asiyekuwa mfungwa. Ama mfungwa ikiwa atafunga kwa ijtihadi yake, kisha ikaingia Ramadhani au Eid kabla ya kukamilika kwa miezi miwili, basi katika suala la kukatika kwa mfululizo wake kuna khitilafu sawa na ile ya kukatika kwa sababu ya kufungua kwa mgonjwa.

Ama Maliki walitaja: Kwamba kukusudia kula siku ya Eid kunakata mfululizo wa funga ya kaffara, kama vile ikiwa atakusudia kufunga Dhu al-Qi'dah na Dhu al-Hijjah kwa kaffara ya Dhihar yake huku akijua kuingia kwa Eid katikati yake. Tofauti na ikiwa atakuwa hajui, kwani hapo haikatiki, kama vile akidhani kuwa mwezi wa Dhu al-Hijjah ni Muharram, kisha akaufunga pamoja na unaofuata akidhani kuwa ni Safar, kisha ikabainika kinyume chake...

Ama Hanbali walienda katika msimamo kuwa funga ya kaffara haikatiki kwa hilo kabisa, kwa sababu ya wajibu wa kufunga Ramadhani kwa amri ya Sharia, na kwa sababu kula Eid mbili na siku za Tashreeq ni wajibu pia kwa amri ya Sharia, yaani kwamba wakati huo Sharia imemkataza kuufunga kama ilivyo usiku.] Mwisho wa nukuu.

Hii ina maana kwamba Hanafi, Shafi'i na Maliki wanaona kuwa kula siku ya Eid kunakata mfululizo wa miezi miwili ya kaffara, yaani mwenye kaffara lazima aanze upya hesabu ya miezi miwili. Ama Hanbali, mfululizo wa miezi miwili ya kaffara haukatiki kwao kwa kula Idul Adha.

2- Ama kufunga siku ya Adha na siku za Tashreeq, hakika hilo halijuzu, na hiyo ni kwa mujibu wa hadith aliyoipokea Muslim kutoka kwa Abu Hurairah (ra) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:

نَهَى عَنْ صِيَامِ يَوْمَيْنِ يَوْمِ الْأَضْحَى وَيَوْمِ الْفِطْرِ

"Amekataza kufunga siku mbili: siku ya Adha na siku ya Fitri."

Na kwa yale aliyoyapokea Muslim kutoka kwa Nubayshah al-Hudhali amesema, amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ:

أَيَّامُ التَّشْرِيقِ أَيَّامُ أَكْلٍ وَشُرْبٍ

"Siku za Tashreeq ni siku za kula na kunywa."

Hii ina maana kwamba mwenye kaffara haijuzu kwake kufunga siku ya Adha wala siku za Tashreeq ikiwa funga ya kaffara itazijumuisha siku hizo, bali ni wajibu kwake kula katika siku hizo. Na kula kwake katika siku hizo kunamaanisha kukatika kwa mfululizo wa kufuatana katika funga ya kaffara ambayo anaanza kuifunga katika mwezi wa Dhu al-Qi'dah. Na hii inamaanisha kuwa ni wajibu kwake kuanza kufunga miezi miwili mingine mfululizo badala ya ile aliyofunga hapo awali kwa sababu ya kukatika kwa mfululizo unaotakiwa kisheria katika kufunga miezi miwili ya kaffara.

3- Tumevutiwa wakati wa kupitia jibu la swali tulilolitoa mnamo tarehe 15 Sha'ban 1443 Hijria sawia na 18/03/2022 Miladi kwamba kuna kosa la kimaandishi lililotokea inaonekana ni kwa kuteleza, nalo ni kwamba ilikuja katika jibu lililoashiriwa:

[... kaffara ya kuua bila kukusudia ni kufunga miezi miwili mfululizo kwa yule asiyekuwa na mtumwa wa kumwacha huru au kulisha masikini sitini kama ilivyokuja katika aya tukufu: ﴿وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَنْ يَقْتُلَ مُؤْمِناً إِلَّا خَطَأً وَمَنْ قَتَلَ مُؤْمِناً خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُسَلَّمَةٌ إِلَى أَهْلِهِ إِلَّا أَنْ يَصَّدَّقُوا فَإِنْ كَانَ مِنْ قَوْمٍ عَدُوٍّ لَكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ وَإِنْ كَانَ مِنْ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ مِيثَاقٌ فَدِيَةٌ مُسَلَّمَةٌ إِلَى أَهْلِهِ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ فَمَنْ لَمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِنَ اللَّهِ وَكَانَ اللَّهُ عَلِيماً حَكِيماً﴾.].

Kauli katika jibu lililopita: (ni kufunga miezi miwili mfululizo kwa yule asiyekuwa na mtumwa wa kumwacha huru au kulisha masikini sitini), ni sahihi mpaka neno (kumwacha huru), ama sentensi (au kulisha masikini sitini) yenyewe si sahihi. Hakuna katika kaffara ya kuua bila kukusudia kulisha masikini sitini, wala aya iliyothibitishwa katika jibu haikutaja kulisha masikini sitini. Bali jibu lilikuja likisema kuwa si wajibu kwa yule asiyeweza kufunga kulisha... Kwani imekuja katika jibu lililotajwa kipengele cha 3:

(Na ninachokipendekeza zaidi ni kwamba ikiwa hataweza kufunga kwa sababu ya msingi kama tulivyotaja hapo juu, basi hana la kufanya isipokuwa amwombe Mwenyezi Mungu msamaha na ajikurubishe Kwake kwa nafila, na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na Mwenye kurehemu. Ama kwa nini hatukuipimia (qiyas) kaffara ya kuua bila kukusudia kwa kaffara ya Dhihar, ni kwa sababu hakuna qiyas katika kaffara kwani hazikupewa sababu ya kisheria (ta’lil)... n.k)

Kwa hiyo, inaonekana kuwa sentensi hii (au kulisha masikini sitini) iliwekwa kwa kuteleza katika mahali hapa kwani inapingana na mambo mengine yaliyokuja katika jibu lililoashiriwa. Na usahihi ni kusema hivi kwa kufuta sentensi isiyo sahihi:

[... kaffara ya kuua bila kukusudia ni kufunga miezi miwili mfululizo kwa yule asiyekuwa na mtumwa wa kumwacha huru kama ilivyokuja katika aya tukufu:

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَنْ يَقْتُلَ مُؤْمِناً إِلَّا خَطَأً وَمَنْ قَتَلَ مُؤْمِناً خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُسَلَّمَةٌ إِلَى أَهْلِهِ إِلَّا أَنْ يَصَّدَّقُوا فَإِنْ كَانَ مِنْ قَوْمٍ عَدُوٍّ لَكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ وَإِنْ كَانَ مِنْ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ مِيثَاقٌ فَدِيَةٌ مُسَلَّمَةٌ إِلَى أَهْلِهِ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ فَمَنْ لَمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِنَ اللَّهِ وَكَانَ اللَّهُ عَلِيماً حَكِيماً

"Na haiwi kwa Muumini kumuua Muumini (mwenziwe) isipokuwa kwa makosa... Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo kuwa ni toba itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima." (QS An-Nisa [4]: 92)

Na ni wazi kutokana na aya hiyo kwamba kinachotakiwa ni kufunga miezi hii miwili kwa kaffara, hivyo haingii ndani yake funga nyingine ya faradhi kwa ajili ya jambo lingine lisilo kaffara kama vile kufunga mwezi wa Ramadhani. Kwani nukuu ya kisheria katika funga ya Ramadhani:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَانِ فَمَنْ شَهْرَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

"Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yake Qur'ani kuwa ni uongofu kwa watu na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Basi atakayeshuhudia mwezi miongoni mwenu, na aufunge." (QS Al-Baqarah [2]: 185)

Ni tofauti na nukuu ya kisheria ya kaffara ya kuua bila kukusudia, hivyo haziingiliani pamoja.].

Natumai jibu liko wazi.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

28 Dhu al-Qi'dah 1443 Hijria Sawia na 27/06/2022 Miladi

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi): Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi): Tovuti

Share Article

Share this article with your network