Home About Articles Ask the Sheikh
Miunganiko

Hotuba ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa mnasaba wa kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani 1425 H.

October 14, 2004
1628

Sifa njema ni za Allah, na swala na salamu zimwendee Mtume wa Allah, na jamaa zake, maswahaba zake na wanaomfuata, na baada ya hayo,

Anasema Subhanahu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

"Enyi mlioamini! Mmeandikiwa saumu kama walivyandikiwa wale waliokuwa kabla yenu ili mpate kucha Mungu." (QS. Al-Baqarah [2]: 183)

Na Anasema Azz wa Jall:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

"Mwezi wa Ramadhani ambao ndani yake imeteremshwa Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi atakayekuwa mjini katika mwezi huu na afunge." (QS. Al-Baqarah [2]: 185)

Enyi ndugu watukufu,

Enyi Waislamu,

Huyu hapa Ramadhani anatufunika kwa kheri na baraka zake, kwani ni mwezi ambao Allah ameuutofautisha na miezi mingine, akamiminia ndani yake rehema na akatukuza ndani yake malipo; mwanzo wake ni rehema, katikati yake ni maghfira, na mwisho wake ni kuacha huru na moto. Allah Subhanahu amejifanya mwezi huu kuwa ni Wake maalum ambapo humlipa amtakaye bila hesabu:

كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ

"Kila amali ya mwanadamu ni yake isipokuwa saumu, kwani hiyo ni Yangu na Mimi ndiye nitakayeilipa," kama alivyosema swala na salamu za Allah zimshukie katika hadith yake ya Qudsi.

Hakika mwezi wa Ramadhani ni mwezi ulioshuhudiwa katika historia ya Uislamu; ndani yake iliteremshwa Qur'ani Tukufu, na ndani yake kulikuwa na ushindi na ufunguzi ulio wazi (al-fath al-mubin). Ni mwezi wa kazi, juhudi na bidii, na ni mwezi wa ibada, subira na Jihadi. Ndani yake Waislamu walikuwa wakishindana katika kheri ambapo malipo na thawabu huongezwa maradufu. Na Khalifa wao na magavana wao walikuwa wakilinda usalama wa nchi na raia, na kubeba Uislamu kwenda kwa ulimwengu kupitia Da’wah na Jihadi. Hivyo, mwezi huu mtukufu ulikuwa ni mwezi wa utukufu kwa Waislamu, na mwezi wa unyonge kwa makafiri.

Hivi ndivyo Ramadhani ilivyokuwa ikija na siku zenye nuru kwa Uislamu na Waislamu. Ulikuwa ni mnara wa kheri, elimu ya uwongofu, na bendera ya Jihadi. Khalifa wa Waislamu ndiye Imamu wao, anawahukumu kwa sheria ya Allah, na anapigana Jihadi pamoja nao katika njia ya Allah; majeshi yao yakikatiza jangwa na majangwa, na majahazi yao yakipasua mawimbi ya bahari ili kulitukuza neno la Allah na kueneza uadilifu katika pembe za dunia.

Majeshi yao yalikuwa yakihutubia maji ya bahari: "Lau kama tungelijua nchi nyuma yako, basi tungeingia ndani yako ili kunyanyasa bendera ya Uislamu." Na Khalifa wao anayaita mawingu: "Nyesha maji yako popote upendapo, kwani kwa idhini ya Allah yatamwagilia ardhi ya Waislamu." Na Waislamu wako nyuma ya Khalifa wao, wakimtia nguvu mikono yake akifanya vizuri na kumuhasibu akifanya vibaya, na yeye pamoja nao wako sawa mbele ya sheria ya Allah.

Na Umma, dola, na jamii vinaendeshwa na Uislamu na vinaharakishwa nao. Wanaupokea mwezi wa Ramadhani kwa nyuso zenye furaha, kicheko na bashasha, na kuuaga wakiwa na huzuni kwa kuuacha, wakitamani kukutana nao tena ili washuhudie kheri kupitia mwezi huo na kwayo, wapate kufaulu katika nyumba mbili (dunia na akhera), na huko ndiko kufaulu kukubwa.

Hivyo ndivyo Ramadhani ilivyokuwa ikija, lakini inakuja vipi leo?

Inakuja leo ikiwa Khilafah imekwishavunjwa tangu miaka themanini na mitatu iliyopita na Waislamu hawajairejesha bado, wakati ambapo Waislamu wanapata dhambi baada ya kupita siku tatu bila nchi kuwa na Khalifa, isipokuwa yule anayejishughulisha na kazi ya kuisimamisha kwa juhudi na ukweli.

Inakuja leo huku nchi muhimu zaidi za Waislamu zikiwa zimekaliwa kwa mabavu: Palestina, Iraq, Afghanistan, Chechnya, Kashmir, Cyprus na Kusini mwa Sudan. Waislamu ni wengi lakini hawana uzito wala hisabu kutokana na kukosekana kwa Khalifa anayechunga mambo yao, anayelinda heshima yao, ambaye hutumiwa kama ngao na hupigwa vita nyuma yake.

Inakuja leo huku Waislamu, isipokuwa wale ambao Mola wangu amewahurumia, wameghalibiwa na tabia ambazo Allah hakuzishushia mamlaka yoyote. Badala ya Ramadhani kwao kuwa mwezi wa ibada na Jihadi, umekuwa mwezi wa uvivu na usingizi mrefu. Na badala ya kuwa mwezi wa ushujaa na kuthubutu, umekuwa mwezi wa kushindwa na kurudi nyuma. Na badala ya Waislamu kushindana ndani yake kwa mema na kheri, wanashindana kwa aina mbalimbali za vyakula.

Ama watawala wa Waislamu, wameuza nchi na raia, wakawatayarishia makafiri njia ya kukalia kwa mabavu nchi za Waislamu, wakatembea kwa unyonge katika msafara wa Magharibi, hususan Amerika, na wakamsaliti Allah na Mtume Wake na waumini. Ama kuhusu Ramadhani, wameitupa nyuma ya migongo yao, wameiondolea roho yake na kuifanya kuwa ni mila tu; wanaifungua kwa mchanganyiko wa maneno ya upuuzi huku wanafiki wakiwapigia makofi, kisha baraza la mazungumzo linavunjika. Na mbora wa watawala hawa ni yule anayetangaza kufunga mlango mkuu wa sehemu za anasa, maovu, migahawa na baa wakati wa nyakati za Ramadhani, kisha anaashiria kwa mshale mlango wa nyuma kwa ajili ya kuingia katika sehemu hizo zilizofungwa!

Ama redio na televisheni zao, Ramadhani kwao ni mwezi wa mikesha ya Ramadhani, tafrija za nyimbo, filamu chafu na tamthilia duni, na pamoja na hayo, vyombo hivyo vinasisitiza kuwa vinahuisha nyakati za Ramadhani!

Enyi Waislamu,

Hakika Ramadhani haina budi kurejea kwa idhini ya Allah ikimulika usiku wa Waislamu, na kujikinga chini ya bendera ya Khalifa wa Waislamu, kwani kheri katika Umma huu inaendelea, haikatiki mpaka Siku ya Kiyama. Na hakika Umma huu, katika historia yake yote, umezalisha wanaume wenye nguvu na ucha Mungu, waliofanya kazi ya kurejesha utukufu wa Umma na hadhi yake ya juu. Siku za kushindwa kwa wanajeshi wa msalaba na Watatariya kisha kufukuzwa kwao vibaya sana ni ushahidi mkubwa juu ya hilo. Na leo Umma unajivunia kuwa una vijana walioamini Mola wao na Allah akawazidishia uwongofu kutokana na fadhila Zake; wameazimia kuunganisha usiku wao na mchana wao katika kazi ya kudumu, ya ikhlasi kwa Allah Subhanahu na ya kweli kwa Mtume wa Allah (saw), ili kurejesha utukufu wa Umma kwa kusimamisha Khilafah ya Rashidah, bila kuogopa lawama za mwenye kulaumu katika njia ya Allah, mpaka wasimamishe yale waliyoazimia au wafe katika njia hiyo.

Hakika Hizb ut-Tahrir na Waislamu nyuma yake wanatambua kuwa utukufu wa Umma huu hautarejea isipokuwa kwa Khilafah. Vilevile wanatambua kuwa Mtume wa Allah (saw) amebashiri kurejea kwake ikiwa ya Rashidah kama ilivyoanza kuwa ya Rashidah. Na hakika wao wanaona kuwa siku zake zimekaribia, na kwamba wao, akipenda Allah, ndio wapanda farasi wake:

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ

"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao." (QS. An-Nur [24]: 55)

Enyi Waislamu,

Ikiwa Allah Subhanahu hakupenda mwaka huu uambatane na kusimamishwa kwa Khilafah ya Rashidah na Khalifa mwenyewe kutangaza kuanza kwa mwezi mtukufu, basi tunanyenyekea Kwake Subhanahu iwe hii ndiyo Ramadhani ya mwisho kupita kwa Waislamu bila Khilafah na Khalifa, na bila ufunguzi na ushindi, na bila nguvu na utukufu kwa Waislamu. Na hapo ndipo Ramadhani itakapopata kivuli cha Khilafah, nuru yake na ukali wake utarejea, itarejea kuwa mwezi wa ibada na Jihadi, na takbir zake mbili zitarejea:

Takbir ya muadhini ikitangaza kwa aliyefunga kufuturu kwake, na takbir ya Mujahid akitangaza kwayo ushindi wake.

إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ ۚ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا

"Hakika Mwenyezi Mungu hulifikisha jambo Lake. Hakika Mwenyezi Mungu amekujaalia kila kitu kipimo chake." (QS. At-Talaq [65]: 3)

Allah apokee kutoka kwa Waislamu wote saumu na visimamo vyao na awajalie kuwa miongoni mwa wale wanaosikiliza kauli na kufuata lile lililo bora zaidi.

1 Ramadhani 1425 H 14/10/2004 M

Amir wa Hizb ut-Tahrir Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

Share Article

Share this article with your network