Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Maswali: Kulipa Deni kwa Njia Bora

April 21, 2018
5035

(Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Ameer wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Maswali Kulipa Deni kwa Njia Bora

Kwa: Asma Jube - Om Ahmad - الواثقه بوعد الله

Swali kutoka:

1- Asma Jube

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Ikiwa mtu amekopa tani moja ya chuma kama ilivyo katika mfano, kisha akairejesha tani hiyo pamoja na ziada kwa utashi wake mwenyewe na bila shinikizo kutoka kwa mkopeshaji... Je, hiyo haihesabiki kuwa ni katika kulipa deni kwa njia bora (husnu al-qadha)? ... Tafadhali tufahamishe.

2- Om Ahmad

Kama ilivyotajwa, haijuzu kukopesha kitu ili kirudishwe kikiwa pungufu au zaidi, bali kirudishwe kama kile ulichokopesha kwa aina yake na kiasi chake, Jazakallahu khairan. Lakini nimepata mkanganyiko katika neno "kulipa deni kwa njia bora", na kwa nini haichukuliwi kuwa ni riba ikiwa ziada yoyote katika aina na kiasi kama ilivyotajwa kwenye jibu inachukuliwa kuwa ni riba? Hebu tuelezeni kwa nini tumeichukulia Hadithi ya Mtume alipokopa mwana-ngamia (bakran) na akamrudisha ngamia bora aliyekomaa (khiyaran raba’iyan) kuwa ni kulipa deni kwa njia bora, na tukachukulia anayekopa tani ya chuma na kuirudisha tani moja na nusu kuwa ni riba? Je, haikutajwa kuwa haijuzu ziada katika aina na kiasi?

3- الواثقه بوعد الله

Assalamu Alaykum Sheikh wetu mtukufu na Jazakallahu khairan... Imetajwa katika jibu... Na ni lazima deni lirudishwe kwa mwenyewe bila ziada ya "manufaa", vinginevyo itakuwa ni riba... Je, unamaanisha ziada... Yaani ziada iliyoshartiwa na mkopeshaji wakati wa kukopa... Ama bila kutaja sharti hilo haijuzu ziada?

Jibu la maswali haya matatu kwa kuwa yanahusu mada moja:

(Wa Alaykum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Kuhusu kile kilichokuja katika Hadithi ya Mtume ﷺ kuhusu kulipa deni kwa njia bora (husnu al-qadha), hiyo haimaanishi ziada katika idadi, uzito, au kipimo, bali inamaanisha idadi ile ile, uzito ule ule, na kipimo kile kile, lakini inajuzu kwa kitu bora zaidi. Mfano, ikiwa mtu amekopa ngano yenye uzito wa kilo 10, inajuzu kuirudisha kwa ngano bora zaidi lakini kwa uzito ule ule wa kilo 10. Na ikiwa amekopa pishi kumi za mchele, inajuzu kuzirudisha kwa mchele bora zaidi lakini kwa kipimo kile kile cha pishi kumi. Na ikiwa amekopa kondoo, inajuzu kurudisha kondoo bora zaidi lakini si kondoo wawili... Huku ndiko kulipa deni kwa njia bora zaidi, lakini si kwa kuongeza uzito, kipimo, au idadi.

Na kwa msingi huo, inaeleweka Hadithi ya Mtume ﷺ iliyokuja katika jibu letu lililopita, na haya ndiyo matini yake:

Kutoka kwa Abu Rafi’ amesema:

اسْتَسْلَفَ رَسُولُ اللَّهِ ﷺ بَكْرًا فَجَاءَتْهُ إِبِلٌ مِنْ الصَّدَقَةِ فَأَمَرَنِي أَنْ أَقْضِيَ الرَّجُلَ بَكْرَهُ فَقُلْتُ لَمْ أَجِدْ فِي الْإِبِلِ إِلَّا جَمَلًا خِيَارًا رَبَاعِيًا فَقَالَ النَّبِيُّ ﷺ أَعْطِهِ إِيَّاهُ فَإِنَّ خِيَارَ النَّاسِ أَحْسَنُهُمْ قَضَاءً

"Mtume ﷺ alikopa mwana-ngamia (bakran), kisha ngamia wa sadaka wakafika, akaniamuru nimlipe yule mtu mwana-ngamia wake. Nikasema: Sijapata katika wale ngamia isipokuwa ngamia bora aliyefikia umri wa miaka sita (jamalan khiyaran raba’iyan). Mtume ﷺ akasema: Mpe huyo, kwani hakika watu bora ni wale wanaolipa deni kwa njia bora." (Imepokewa na Abu Dawood na wengineo).

Yaani alimrudishia ngamia aliye bora na mzuri zaidi kuliko ngamia aliyemkopa, lakini kwa idadi ile ile, yaani alimlipa ngamia mmoja.

Na hivi ndivyo ilivyokuja katika jibu letu kuhusu kukopa tani ya chuma na kuirudisha tani moja na nusu kwa mfano; hilo haijuzu, bali ni kwa uzito ule ule.

Muhtasari ni kwamba kulipa deni kwa njia bora haimaanishi ziada katika uzito, kipimo, au idadi, bali ni kwa uzito ule ule, kipimo kile kile, na idadi ile ile, lakini inajuzu kuwa wa aina bora zaidi ikiwa mkopaji anataka kulipa kwa kilicho bora bila mkopeshaji kusharti hilo, kwa sababu Mtume ﷺ alilipa kwa kilicho bora na kizuri zaidi bila sharti la mkopeshaji.

Imekuja katika kitabu cha Nizam al-Iqtisadi (Mfumo wa Kiuchumi) katika mlango wa Riba:

(Ama mkopo (qardh), unajuzu katika aina hizi sita, na katika nyinginezo, na katika kila kitu kinachomilikiwa na kinachofaa kutolewa katika umiliki. Na riba haiingii humo isipokuwa ikivuta manufaa, kutokana na aliyoyapokea Al-Harith bin Abi Usamah kutoka katika Hadithi ya Ali (ra) kwa tamshi:

أَنَّ النَّبِيَّ ﷺ نَهَى عَنْ قَرْضٍ جَرَّ مَنْفَعَةً

"Kwamba Mtume ﷺ alikataza mkopo unaovuta manufaa." Na katika riwaya nyingine:

كُلُّ قَرْضٍ جَرَّ مَنْفَعَةً فَهُوَ رِبًا

"Kila mkopo unaovuta manufaa, basi huo ni riba." Na kinachovuliwa hapo ni kile kilicho katika mkondo wa kulipa deni kwa njia bora bila ziada [ya kiasi], kutokana na aliyoyapokea Abu Dawood kutoka kwa Abu Rafi’ amesema: "Mtume ﷺ alikopa mwana-ngamia (bakran), kisha ngamia wa sadaka wakafika, akaniamuru nimlipe yule mtu mwana-ngamia wake. Nikasema: Sijapata katika wale ngamia isipokuwa ngamia bora aliyefikia umri wa miaka sita (jamalan khiyaran raba’iyan). Akasema: Mpe huyo, kwani hakika watu bora ni wale wanaolipa deni kwa njia bora.")

Na isisemwe kuwa hiba na zawadi ni halali, hivyo ikiwa atalipa deni kwa ziada ya uzito, idadi, au kipimo kwa moyo mkunjufu bila sharti ni halali; hilo lisisemwe kwa sababu hili linajuzu ikiwa halikufungamana na suala la mkopo. Hakika ziada hapa imetokea kwa ajili ya mkopo, nayo ni manufaa yanayotokana nao, ambayo yanajumuishwa na yale aliyoyapokea Al-Harith bin Abi Usamah kutoka kwa Ali (ra) kwa tamshi: "Kwamba Mtume ﷺ alikataza mkopo unaovuta manufaa," na katika riwaya nyingine: "Kila mkopo unaovuta manufaa, basi huo ni riba."

Pia lisisemwe kuwa ubora wa aina ni manufaa; hilo lisisemwe kwa sababu Mtume ﷺ aliliruhusu hilo na akalihesabu kuwa ni katika kulipa deni kwa njia bora kama ilivyo katika Hadithi ya Abu Rafi’ iliyotajwa hapo juu.

Natumai katika hili kuna utoshelevu, Insha Allah.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta

05 Shaban 1439 H 21/04/2018 M

Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Ameer (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye: Facebook Google Plus Twitter Web

Share Article

Share this article with your network