Jibu la Swali
Swali:
Mkutano wa kwanza wa kilele kati ya Rais wa Marekani Biden na Rais wa Urusi Putin ulifanyika mjini Geneva mnamo Jumatano, 2021/6/16. Je, nini maana ya mkutano huu? Na nini lengo lake? Je, kuna matokeo chanya yaliyofikiwa katika mkutano wa marais hao wawili mjini Geneva, kwa maana ya kwamba, je, uhusiano kati ya Marekani na Urusi unaelekea kuimarika baada ya miaka ambayo ilielezewa kuwa mbaya zaidi katika historia ya nchi hizo mbili?
Jibu:
Haiwezekani kuelewa vipimo vya mkutano wa kilele kati ya Marekani na Urusi isipokuwa kwa kuelewa mazingira yaliyopelekea kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika miaka ya hivi karibuni:
1- Vyombo vingi vya habari na baadhi ya wanasiasa wanarudia kutoa maelezo ya nchi hizi mbili, Marekani na Urusi, kama "majitu mawili" (giants), ikiwa ni mwendelezo wa ukweli uliokita akilini kwamba Marekani na "Umoja wa Kisovieti" ndizo nchi zenye nguvu na kubwa zaidi duniani na kila moja ina kambi yake. Ukweli ni kwamba udhaifu mkubwa ulioikumba nchi ya Urusi baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti uliishusha daraja kubwa kutoka kwenye kiwango cha ushindani wa kimataifa na Marekani. Kwa sababu hiyo yote, mkutano wa kilele uliofanyika kati ya marais wa nchi hizo mbili una umuhimu mdogo sana kuliko mikutano ya kilele kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti ambayo ilikuwa na matokeo mengi, kwani hakuna kilichobaki katika misingi ya ukuu wa Urusi isipokuwa nguvu ya kijeshi, hasa ya kinyuklia, makombora na uwezo wake wa anga za juu. Ama kinyume na hivyo, hakuna ukuu wowote nchini Urusi!
2- Uhusiano wa Urusi na Marekani ulianza kuelekea kwenye kuzorota mwishoni mwa utawala wa Obama, ambapo kulikuwa na vikwazo kutokana na Urusi kuikalia kwa mabavu rasi ya Crimea mnamo mwaka 2014 na kufukuzwa kwake kutoka katika kundi la mataifa manane makubwa (G8), kisha vikwazo kutokana na kuingilia uchaguzi wa Marekani mnamo mwaka 2016, na utawala wa Obama kuwafukuza wanadiplomasia 35 wa Urusi na kuweka vikwazo dhidi ya vyombo vya ujasusi vya Urusi mwishoni mwa Desemba 2016, yaani baada ya Trump kushinda uchaguzi wa Marekani na kabla ya kuchukua majukumu ya ofisi yake (Deutsche Welle, 2021/1/14)... Na licha ya maneno yote matamu aliyokuwa akiyatoa Trump kuelekea Putin, Marekani iliendelea kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Urusi, na kusukuma uhusiano kati yao kuelekea kwenye mvutano. Ilifunga ofisi za ubalozi wa Urusi katika miji mingi ya Marekani, na kubana idhaa za habari za Urusi nchini Marekani. Vikwazo vya Marekani viliwekwa dhidi ya Urusi kwa sababu za msingi na zisizo na msingi; viliwekwa kwa sababu ya kukamatwa kwa mpinzani wa Urusi Navalny, na viliwekwa kwa shutuma za kumtia sumu mpinzani wa Urusi Skripal nchini Uingereza mnamo mwaka 2018, na viliwekwa dhidi ya kampuni za teknolojia za Urusi kwa tuhuma za mashambulizi ya kimtandao kama ilivyokuwa mwishoni mwa utawala wa Trump. Na utawala wa Biden ulipokuja, ulizidisha mgogoro wa uhusiano huo, ambapo Rais wa Marekani Biden alimuelezea Rais wa Urusi Putin kama "muuaji" na kwamba atalipa gharama ya kuingilia kwake katika uchaguzi wa Marekani (Sky News Arabic, 2021/3/17). Balozi wa Urusi aliondoka Washington kufuatia hali hiyo mnamo Machi 2021, kisha balozi wa Marekani akaondoka Moscow mwezi uliofuata... Na Marekani ilitishia kuitenga Urusi na mfumo wa kifedha wa kimataifa.
3- Utawala wa Kidemokrasia wa Biden una chuki zaidi dhidi ya Urusi na rais wake Putin na unamtuhumu kuwa ndiye sababu ya Hillary Clinton kushindwa katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016. Wanademokrasia walipokuwa upinzani walikuwa wakimtaka Rais wa zamani Trump kuiadhibu Urusi na kumtuhumu kwa kuifanyia upole, na walikuwa wakimfanya ajihisi vibaya katika hilo na kuitishia Urusi ikiwa watashinda uchaguzi wa 2020. Rais wa Kidemokrasia Biden aliposhinda katika uchaguzi huo, jambo hilo lilienda sambamba na mashambulizi makali sana ya kimtandao dhidi ya mifumo ya kampuni ya SolarWinds inayotumiwa na mashirika nyeti ya serikali ya Marekani, na ujasusi wa Marekani ukaishutumu Urusi kwa mashambulizi haya ya kimtandao... Na Marekani ikaanza kuiita Urusi kama "adui"... Hata siku mbili kabla ya mkutano wa kilele, Biden alitishia kuingiza Ukraine katika muungano wa NATO! Hivyo basi, mkutano huu ulikuwa hauendani na mvutano kati ya nchi hizo mbili, bali una sura nyingine. Na kwa kutafakari mazingira yake na mwendo wake, inabainika kuwa:
أ- Mkutano kati ya marais hao wawili ulimalizika baada ya saa mbili na nusu badala ya saa nne zilizopangwa, na hakuna mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari uliofanywa kati ya marais hao. Kila mmoja wao alifanya mkutano wake wa waandishi wa habari peke yake, na mikutano yote miwili ilipeperushwa na Al-Jazeera mnamo 2021/6/16 na vyombo vingine vya habari moja kwa moja. Taarifa ya pamoja ilijikita katika makubaliano ya pande zote mbili kwamba hakuna mshindi katika vita vya kinyuklia, ingawa hakuna dalili yoyote ya vita hivyo kati yao. Rais wa Marekani Biden aliahidi kuendeleza ahadi ya Washington katika mkataba wa START 3 wa kupunguza silaha za kimkakati baada ya kamati zilizokubaliwa kuundwa kukamilisha yanayohitajika katika upande huu. Masuala mengi ya migogoro kati ya nchi hizo mbili yalijadiliwa, na Rais wa Urusi alimuuliza mwenzake wa Marekani kuhusu kumwita "muuaji". Biden alizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu athari mbaya za uwezekano wa kifo cha mpinzani wa Urusi Navalny gerezani, lakini aliuelezea mkutano huo kuwa wa manufaa na chanya na alikubali kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba mkutano huo ulijumuisha kuitishia Urusi ikiwa itaingilia uchaguzi wa Marekani tena au kufanya mashambulizi ya kimtandao tena. Rais wa Urusi katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema kuwa ni vigumu kusema kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaimarika, lakini alizungumza juu ya mwangaza wa tumaini kwa hilo, na aliishambulia Marekani katika masuala ya haki za binadamu akizikumbusha magereza ya ujasusi ya Marekani huko Guantanamo na nchi nyingine na vitendo vya kinyama vya Marekani dhidi ya watu weusi na dhidi ya mataifa mengine, ikiwa ni jibu kwa ukosoaji mkali wa Marekani kuhusu haki za binadamu ndani ya Urusi. Biden alizungumza juu ya umuhimu wa kufanya mkutano wa moja kwa moja kati yake na Putin ili kuepuka kutoelewana kokote katika uhusiano kati yao, na akaashiria kuwa mustakabali wa uhusiano huo unategemea hatua kutoka Urusi.
ب- Kwa uchunguzi, tunakuta kuwa Marekani ndiyo iliyokuwa ikichukua hatua ya kuishinikiza Urusi, na kwamba Marekani ndiyo iliyozidisha mgogoro wa uhusiano kati yao hadi kufikia kiwango ambacho Rais wa Urusi Putin alikielezea hapo awali kama "chenye uharibifu mkubwa". Ni yeye, yaani Marekani, aliyechukua hatua ya kufanya mkutano wa kilele kati ya viongozi hao wawili bila ya kuwa na makubaliano juu ya pointi za migogoro kati yao. Urusi iliona heri na kushangilia kwamba Biden ndiye rais wa kwanza wa Marekani kuamua kukutana na rais wake katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi kama uthibitisho wa Kirusi juu ya umuhimu ambao Washington inaipa Moscow. Rais wa Marekani Biden akaizidi kete kwa kuitembelea Uingereza na kukutana na Waziri Mkuu wake Johnson, na akafanya mkutano wa kilele wa nchi saba kubwa (G7) nchini Uingereza kuwa wa mahudhurio ya ana kwa ana baada ya kutarajiwa kuwa wa kidijitali kupitia mtandao. Biden akazidisha kwa mkutano wa mahudhurio ya ana kwa ana wa NATO huko Brussels na akafanya mikutano kadhaa wakati huo, ikiwa ni pamoja na Rais wa Uturuki Erdogan. Pia mjini Brussels, Biden alifanya mkutano wa nadra wa aina yake na marais wa Baraza la Ulaya Charles Michel na Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, na hivyo mkutano wa Biden-Putin ukawa ni mmoja tu wa mikutano mingi ambayo Rais wa Marekani alifanya ana kwa ana katika ziara yake ya Ulaya, yaani kudunisha matumaini ya Urusi katika mkutano maalum kwa ajili yake pekee!
ج- Kwa hayo yote, inaweza kusemwa kuwa matokeo chanya ya mkutano wa kilele kati ya viongozi hao wawili yalikuwa madogo sana na yalikomea kwenye kurejeshwa kwa mabalozi wa nchi hizo mbili katika miji mikuu ya kila mmoja, na ahadi kuhusu mkataba wa kimkakati wa START 3, na kwamba kuimarika kwa uhusiano kati yao kunategemea hatua zijazo za Urusi, yaani makubaliano yake na makosa yake kama lile kosa la kimkakati la Urusi lililojitokeza katika kuisaidia Marekani nchini Syria. Kwa kutangaza kwa rais wake Putin kuingilia kwake kijeshi nchini Syria baada ya mkutano wake na Rais wa Marekani Obama mjini New York mnamo Septemba 28, 2015, Urusi ilikuwa imetoa huduma zake za kijeshi kwa ajili ya maslahi ya Marekani. Labda Urusi ilikuwa ikisukumwa na chuki yake dhidi ya Uislamu na Waislamu kupigana nchini Syria, na labda ilisukumwa pia kuvunja kutengwa kwake kimataifa baada ya kuikalia kwa mabavu rasi ya Crimea mwaka 2014 na vikwazo vya Magharibi vilivyofuata. Lakini muhimu zaidi ni kwamba Marekani imeonja huduma za kijeshi za Urusi na kuona umuhimu wake wa kuhudumia ushawishi wake nchini Syria na kwamba sasa inatamani sana kuhamishia jukumu hili kwenye eneo linaloizunguka China. Hivyo kuingilia kwa Urusi nchini Syria huku ikijua ubeberu wa Bashar kwa Marekani lilikuwa kosa kubwa la kimkakati ambalo haliwezi kufanywa na uongozi wenye akili wa nchi yoyote huru.
د- Ama malengo ya Marekani yasiyotangazwa kutokana na shinikizo lake kwa Urusi ni kuifanya Urusi kuwa chombo cha kimataifa katika mkakati wa Marekani dhidi ya China. Ikiwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger ndiye aliyesanifu ushirikishwaji wa Urusi katika kuishinikiza China na kuilazimisha kuishi kwa amani na Marekani wakati wa vita vya Vietnam katikati ya miaka ya sitini ya karne iliyopita, basi huyu mzee wa Marekani ameendelea kutazamwa na duru za kisiasa za Marekani kama mfikiriaji wa kimkakati wa kisiasa na mwenye mtazamo wa kina katika siasa za kimataifa. Kwa hiyo, duru hizo zilimpangia mnamo mwaka 2016 mikutano miwili muhimu na ya pekee akiwa na umri wa miaka tisini na wagombea wa urais wa Marekani Hillary Clinton na Donald Trump, na mapendekezo yake kwao yalikuwa ni umuhimu na ulazima wa kuishirikisha Urusi na kuisukuma pamoja na Marekani dhidi ya China.
ه- Na licha ya kuwa malengo haya ya Marekani hayajatangazwa, Marekani inayafikisha kwa Urusi kwa njia moja au nyingine na kwamba Urusi inaelewa vizuri. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Lavrov alithibitisha (kuwa Marekani haitaweza kuigeuza Urusi kuwa chombo cha kuhudumia maslahi yake, na kukabiliana na China... wanajadili sasa na kwa uzito, jinsi ya kuitumia Urusi dhidi ya China kwa maslahi yao... wakitaka kutufanya kuwa chombo cha kuhudumia maslahi ya Marekani." Aliongeza: "Lakini bila shaka jambo hili halitafanikiwa kwetu".) RT 2018/12/24.
و- Na hiki ndicho hasa ambacho Marekani inakitaka kutoka kwa Urusi, ndiyo maana inaishinikiza na kuleta mvutano wa hali ya hewa nayo ikiitumia nadharia ya Henry Kissinger ya kuidhibiti China kwa kuishirikisha Urusi. Vinginevyo, Urusi haishindani na Marekani katika uchumi wala katika siasa za kimataifa na hakuna sifa za mataifa makubwa ndani yake isipokuwa zana za kijeshi. Mikataba ya Marekani na Umoja wa Kisovieti kisha ya Urusi imeweka zana za kijeshi za Urusi katika mfumo wa nidhamu mbali na kuitishia Marekani. Hata Marekani imejiondoa katika mikataba mingi kama vile mkataba wa makombora ya kuzuia makombora uliotiwa saini tangu mwaka 1972 na ikajenga ngao yake ya makombora. Urusi haina uchumi wenye nguvu unaoiwezesha kuendeleza zaidi uwezo wake wa kijeshi sawa na uwezo ulio nao Marekani... Hivyo basi, uwezo wa kinyuklia na wa kimkakati wa Urusi haukuwa sababu na chocheo la Marekani kuleta mvutano katika uhusiano nayo, bali mvutano huu katika uhusiano na Urusi ulikuwa unakusudiwa kuishinikiza ili ijitenge na China ambayo imekuwa kitovu cha tahadhari kubwa kwa Marekani. Waziri wake wa zamani wa ulinzi Patrick Shanahan aliwataka viongozi wa jeshi lake kuzingatia China akisema "China, kisha China, kisha China" (Al-Jazeera Net, 2019/1/3).
ز- Pamoja na hayo, Marekani kwa kuleta mvutano katika uhusiano na Urusi imeshindwa hadi sasa kuisukuma Urusi dhidi ya China, hasa kwa kuwa shinikizo la Marekani kwa Urusi lilienda sambamba na shinikizo lake kwa China kupitia vita vya kibiashara, na jambo hili limeunda ukaribu wa Urusi na China... Yaani shinikizo la Marekani kwa Urusi ili kuilazimisha kwenda nayo dhidi ya China limeanza kutoa matokeo kinyume na yale ambayo Marekani inataka, na bila shaka inatambua hatari ya mwelekeo wa Urusi wa kukaribiana na China... Kwa hiyo, utawala wa Biden uliamua kuweka kando mbinu ya "shinikizo" dhidi ya Urusi, na badala yake kutoa "mwangaza wa tumaini" kupitia mkutano wa kilele, na kisha kuweka mbali ukaribu wa Urusi na China kadiri inavyowezekana... na kufungua mazungumzo makubwa nayo kupitia kamati zilizoundwa katika mkutano wa viongozi hao wawili.
4- Hivyo basi, mkutano wa Biden na Putin ni kwa ajili ya kufikia lengo hili, yaani kumpa Putin mwangaza wa tumaini kwa kuondoa mvutano wa Marekani na shinikizo la vikwazo kuelekea Urusi kama njia ya kuisaidia Marekani katika msimamo wake kuelekea China au angalau kuzuia ukaribu wa Urusi na China. Ama pointi nyingine za mvutano kati ya nchi hizo mbili hazistahili umuhimu huo mkubwa; kwa mfano, mjadala kati yao kuhusu Syria na kwamba Marekani inataka kutatua mgogoro wa Syria kama inavyotaka yenyewe, jambo hili Urusi haipingi maadamu linaifanya isipoteze hadhi yake (saving face). Kadhalika nchini Afghanistan, Urusi imeshindwa kuwasha moto chini ya miguu ya Marekani nchini Afghanistan kama Marekani ilivyowasha dhidi yake wakati wa miaka ya themanini. Kisha, kuingilia kwa Urusi katika uchaguzi wa Marekani kunatokana na uwazi wa internet kama njia mpya ya ushawishi na labda Urusi haikukadiria nguvu ya majibu ya Marekani, vinginevyo ingejiepusha na uingiliaji huo. Ama mashambulizi ya kimtandao ambayo Marekani inaishutumu Urusi kuyafanya hayana athari kubwa ambayo ni vigumu kuitibu, na Biden alijibu baada ya mkutano wake na Putin kuwa Marekani ina uwezo mkubwa wa kuingilia Urusi na kufanya uharibifu wa kielektroniki ndani yake ikiwa Urusi itarudi tena kuingilia, na akatoa mfano wa uwezo wake wa kuharibu mabomba ya mafuta ya Urusi...
5- Rais wa Urusi aliondoka Geneva akijua vizuri kuwa Marekani inasubiri hatua zijazo za Urusi katika miezi ijayo na kwamba inakusudia kuchunguza na kutafakari hatua hizo kupitia kamati za pamoja zilizopitishwa kuundwa. Rais wa Urusi anajua vyema kuwa uwezo wa shinikizo la Marekani dhidi ya Urusi ni mkubwa na amejaribu baadhi yake, na anajua pia kuwa China inaweza kumwacha na kuelekea Magharibi kwa sababu maslahi yake ya kibiashara Magharibi ni makubwa zaidi kuliko maslahi yake ya kibiashara na Urusi. Kwa sababu hiyo yote, miezi ijayo huenda ikashuhudia utulivu katika uhusiano wa Marekani na Urusi, na kurejeshwa kwa mabalozi ni mwanzo. Pia inatarajiwa kuwa uhusiano wa Urusi na China utaanza kupoa; kwani kadiri uhusiano wa Urusi unavyokuwa na joto na Marekani, ndivyo unavyozidisha ubaridi katika uhusiano wake na China. Na ikiwa hilo litafanikiwa, basi hatua ya Rais wa Marekani Biden ya kufanya mkutano wa kilele na Rais wa Urusi Putin itakuwa imeweka kikomo kwa ukaribu wa Urusi na China, na kadhalika itakuwa imeiweka Urusi kwenye njia ya kuishinikiza China japo kwa kiwango kidogo kuliko matarajio ya Marekani kulingana na nadharia ya Kissinger. Na ikiwa hilo halitafanikiwa na kuendelea kwa mwelekeo wa uasi ndani ya Urusi ukiongozwa na Putin, basi inatarajiwa kuwa utawala wa Biden utaongeza shinikizo lake dhidi ya Urusi na kuitishia kwa ukanda wa moto unaoizunguka katika eneo la Caucasus ambapo kuna mzozo wa Azeri-Armenia kisha Ukraine na uungaji mkono wa Magharibi kwake ili kuunganisha tena ardhi zake...
Hivyo ndivyo mataifa haya ya kibeberu, yakiongozwa na Marekani, hayafikirii kile kinachowafaa watu, bali kile kinachoyapatia maslahi yake hata kama ni cha kuua watu.
أُوْلَـئِكَ شَرٌّ مَّكَاناً وَأَضَلُّ عَن سَءَاوِ السَّبِيلِ
"Hao wana mahali pabaya zaidi na wamepotea zaidi njia iliyo sawa." (QS. Al-Furqan [25]: 34)
Mosi wa Dhul-Qi'dah 1442 H 2021/6/20 M