** (Mfululizo wa majibu ya Mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")**
Kwa Abu Yasir
Swali:
Assalamu Alaykum, ni nani anayebeba tofauti ya thamani ya sarafu ikiwa mdaiwa atachelewa bila udhuru katika kulipa deni kwa mdai kwa miaka kumi kwa mfano, iwe deni hilo ni ujira au mkopo?
Jibu:
Wa Alaykumus Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.
Hakika ujira ulio thabiti katika dhima (liability) ni kama deni. Na yule ambaye ana deni kwa mwingine, ana haki ya kulipwa kulingana na masharti yaliyokubaliwa kati yao. Ikiwa mdaiwa atachelewa kulipa deni, basi inaangaliwa: ikiwa ana hali ngumu ya kifedha, basi mdai ampe muhula mpaka hali yake ya kifedha itakapopata nafuu na aweze kulipa deni, kwa kufuata kauli ya Mwenyezi Mungu (swt):
وَإِنْ كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ
"Na akiwa (mdaiwa) ana dhiki, basi (mpe) muhula mpaka apate wepesi." (QS. Al-Baqarah [2]: 280)
Lakini ikiwa mdaiwa ana uwezo wa kulipa na asifanye hivyo, basi analazimishwa kulipa deni, na asipofanya hivyo huadhibiwa kutokana na yale aliyoyatoa Abu Dawood na Ibn Majah kutoka kwa Amr bin Al-Sharid, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:
لَيُّ الْوَاجِدِ يُحِلُّ عِرْضَهُ وَعُقُوبَتَهُ
"Kuchelewesha (kulipa deni) kwa mwenye uwezo kunahalalisha (kuvunjiwa) heshima yake na kuadhibiwa kwake." (Imepokelewa na Abu Dawood na Ibn Majah)
Maana ya layyu al-wajid ni ucheleweshaji wa mtu tajiri (mwenye uwezo). Na maana ya yuhillu 'irdhahu ni kulalamikiwa kwake na kusemwa kwa ukali, na uqubatuhu ni kufungwa kwake gerezani.
Ama kuhusu tofauti ya thamani ya sarafu, yaani ikiwa thamani yake itashuka au kupanda ikilinganishwa na dhahabu na fedha wakati wa matumizi yake sokoni, je, mdai au mdaiwa ndiye anayebeba tofauti hiyo... suala hili lina maoni kadhaa, na lile ninaloliona kuwa na nguvu zaidi (ar-rajih) ni kwamba malipo ya deni yawe kwa sarafu ile ile na kwa idadi ile ile iliyothibiti katika dhima, ili kuepuka riba ikiwa atachukua ziada katika idadi, mradi tu sarafu hiyo bado inazunguka na inatambulika rasmi na upande ulioitoa.
Na ikiwa mdai anataka kuhifadhi mali yake dhidi ya kushuka kwa thamani, basi akopeshe kwa dhahabu au sarafu yenye nguvu ambayo huhifadhi thamani yake...
Nasi tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) aikurumu Umma huu kwa kusimamisha Khilafah Rashidah, ambapo sarafu itakuwa ni dhahabu na fedha inayobeba thamani ndani yake yenyewe, ili maisha ya kifedha yatengenee na watu wafurahie maisha yao na wawe na amani juu ya mali zao, na Mwenyezi Mungu (swt) ni Mwenye Nguvu, Mwenye Kushinda.
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Link ya jibu kutoka kwa tovuti ya Amir
Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus