Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Uhusiano kati ya Marekani na India chini ya uongozi wa Modi na suala la Kashmir - Uhusiano wa China na Afghanistan... na Taliban

March 11, 2015
3958

Jibu la Swali:

Swali:

Swali langu lina matawi matatu, nikiomba radhi:

Kwanza: Mkutano wa hivi karibuni kati ya Obama na Modi ulipata matangazo mengi kwenye vyombo vya habari, lakini haukuzaa uamuzi wowote wa kweli. Inaonekana bado kuna matatizo kati ya Marekani, India, na chama cha Bharatiya Janata Party (BJP). Je, inawezekana kuashiria masuala hayo yanayozua mivutano kati ya pande hizo mbili?

Pili: Kwa kuzingatia kuwa chama cha BJP nchini India na chama cha Nawaz nchini Pakistan vyote ni vitiifu kwa Marekani, na kwamba suala la Kashmir linaidhoofisha India, kwa nini India inachelewesha utatuzi wa suala la Kashmir?

Tatu: China inakutana na Taliban kwa ajili ya mazungumzo ya upatanishi; je, Marekani imeruhusu jambo hilo, au linatokea bila ya ridhaa yao? Na nini lengo la China katika upatanishi huu?

Mwenyezi Mungu akulipe kheri.

Jibu:

Kwanza: Ili kuelewa mahusiano kati ya Marekani na India chini ya uongozi wa Modi, ni lazima kuzingatia mambo yafuatayo:

1- Modi alirithi mzigo mzito wa matatizo ya mahusiano kati ya chama cha Congress na Marekani wakati wa utawala wa chama hicho uliodumu kwa miaka kumi. Kabla ya hapo, wakati wa miaka ya utawala wa chama cha BJP, mahusiano kati ya New Delhi na Washington yalinawiri kwa kiwango kisichopata kushuhudiwa, lakini yote hayo yalibadilika wakati BJP iliposhindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2004 na chama cha Congress—ambacho ni kitiifu kwa Uingereza—kiliposhika madaraka. Mnamo mwaka 2010, Bunge la India lilipitisha Sheria ya "Dhamana ya Nyuklia," ambayo iliweka vizuizi vikubwa kwa wasambazaji wa vinu vya nishati ya nyuklia; lengo likiwa ni kuizuia Marekani na makampuni yake kuingia katika soko la India. Utekelezaji wa sheria hiyo ulifanya isiwezekane kukamilisha mkataba wa nyuklia wa kiraia na Marekani wa mwaka 2005. Kwa upande mwingine, New Delhi ilikataa katakata majaribio ya Marekani ya kuanzisha mazungumzo kuhusu Kashmir, na ikaitaka Washington kuchukua hatua kali dhidi ya Pakistan kufuatia mashambulizi ya Mumbai mwaka 2008. Vilevile, kulikuwa na hitilafu na Washington kutokana na hatua yake ya kuvibana nchi za BRICS (Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini), na kuhusu migogoro mingi ya kibiashara. Ilitarajiwa kuwa nchi zote mbili zingekuwa na mahusiano mengi ya kibiashara ya pamoja yaliyoanza wakati wa miaka ya utawala wa chama cha Congress, lakini Marekani ilipinga, kwa mfano, matumizi ya nembo ya "Made in India" kwa paneli za mionzi ya jua (solar panels), ikieleza kuwa huo ni ukiukaji wa sheria za Shirika la Biashara Duniani (WTO). India bado inashughulika na kujitetea dhidi ya malalamiko yaliyowasilishwa kwenye chombo cha usuluhishi wa migogoro katika WTO na Marekani mwaka 2013...

2- Wakati wa utawala wa chama cha Congress, umma wa India ulikuwa na taswira hasi kuhusu Marekani, ambayo ilizidi kuwa mbaya kutokana na jinsi Washington ilivyowatendea wanadiplomasia wa India kwa dharau. Matokeo yake, jukumu la kwanza la Modi lilikuwa ni kuboresha taswira ya Marekani miongoni mwa Wahindi, hasa miongoni mwa tabaka la kisiasa. Modi alijitahidi kung'arisha taswira ya Marekani mbele ya umma wa India kupitia ziara ya Obama nchini India akiwa mgeni rasmi wa Jamhuri ya India, sambamba na kusaini mkataba wa nyuklia...

3- Rais Obama kwa sasa, kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Marekani katika vuli ya mwaka 2016, ni kama "lame duck" (bata mlemavu), na msisitizo wake mkubwa ni ushindi wa chama cha Democratic katika uchaguzi huo. Vyovyote iwavyo, Obama analazimika kugawanya muda wake kati ya kushiriki katika kampeni za uchaguzi wa ndani na kuzingatia migogoro mingi nje ya nchi. Hivyo, haiwezekani kwa Obama kuweza kufanya makubwa ili kuvuka athari za miaka 10 ya utawala wa chama cha Congress nchini India.

Kutokana na mambo haya, ni vigumu kushuhudia maendeleo yoyote ya dhahiri kwenye matangazo yaliyotolewa katika mkutano wa kilele kati ya Obama na Modi. Kwa uchache, kutakuwa na ushirikiano wa karibu kuhusu masuala yanayounganisha maslahi ya Marekani na India katika eneo hilo, kama vile kupambana na "ugaidi" unaotokea Pakistan, na kupunguza ushawishi wa China. Hata hivyo, kuna vikwazo vingi vilivyotengeneza pengo fulani kutokana na utawala wa chama cha Congress, na itachukua muda kwa Modi na Obama kuvishinda na kuviondoa. Aliyekuwa balozi wa Marekani nchini India (Robert Blackwell) wakati akitoa hotuba kuhusu mahusiano kati ya Marekani na India chini ya zama za Modi huko New Delhi mnamo Januari 2015 alisema: "...kuhusu mkakati wa Marekani kuelekea India katika miaka miwili ijayo, kwa maoni yangu, matarajio yetu yanapaswa kuwa ya wastani, tofauti na jinsi ilivyokuwa mwanzoni mwa muongo uliopita. Hakuna Waziri Mkuu huyu wala Rais huyu atakayeweza kuleta mabadiliko ya kimkakati katika mahusiano kati ya Marekani na India. Hivyo basi, kwa maoni yangu, hakutakuwa na ushirikiano wa kimkakati wa kweli kati ya nchi hizo mbili katika miaka miwili ijayo." ["Mazingira ya Uhusiano kati ya Marekani na India, na Biashara ya Pamoja", 24 Januari 2015].

Kwa maneno mengine, Blackwell anatarajia kuwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili yatapata nguvu mpya na kurejesha uimara wake kamili wakati wa mrithi wa Obama na si kabla ya hapo.

Pili: Kuhusu suala la Kashmir, nalo pia lilikumbwa na utata mwingi wakati wa utawala wa chama cha Congress, jambo linalomfanya Modi kuhitaji muda ili kuweza kuliweka suala la Kashmir kwenye meza ya mazungumzo:

1- Tangu chama cha Congress kishike madaraka mwaka 2004, suala la Kashmir limewekwa kando, ingawa Pakistan, chini ya utawala wa Musharraf, ilitoa makubaliano mengi ili kuanzisha mchakato wa mazungumzo uliokwama kati ya nchi hizo mbili. Hata hivyo, chama cha Congress kilikataa mpango wowote uliowasilishwa na Musharraf na kusisitiza kuwa suala la Kashmir ni suala la ndani.

2- Hali iliendelea kuwa hivyo hadi mashambulizi ya Mumbai mnamo Novemba 2008. Baada ya hapo, fursa zote za kurejesha mazungumzo kuhusu suala la Kashmir ziliganda kabisa, na serikali ya India ilibadilisha lugha yake, ikishinikiza Pakistan kukubali makosa katika mashambulizi hayo, na kufanya kazi ya kudhibiti makundi yote ya wapiganaji yanayofanya kazi ndani ya Pakistan, hasa kundi la "Lashkar-e-Taiba"... Serikali ya India mnamo Oktoba 2010 iliituhumu idara ya usalama ya Pakistan (ISI) kuhusika na kupanga mashambulizi hayo, na ikasema katika taarifa yake: "Idara ya usalama ya Pakistan (ISI) ilihusika katika kupanga shambulizi la kigaidi la mwaka 2008 huko Mumbai..." ["Serikali ya India: Maajenti wa Pakistan wako nyuma ya mashambulizi ya Mumbai", Hindustan Times, 19 Oktoba 2010].

3- Kufuatia mashambulizi ya Mumbai, mahusiano kati ya Islamabad na New Delhi yalizidi kuwa ya wasiwasi, na jaribio lolote kutoka upande wa Pakistan au Marekani la kushinikiza kurejeshwa kwa mazungumzo kuhusu Kashmir lilikataliwa na India.

4- Wakati huo, Marekani ilikuwa ikiishinikiza India kupunguza mvutano katika mpaka na Pakistan, hasa kwenye mstari wa udhibiti (Line of Control), ili Pakistan iweze kuhamisha vikosi vyake kwenye mpaka na Afghanistan ili kuisaidia Marekani kupambana na upinzani nchini Afghanistan. Lakini India haikubadilisha msimamo wake kuhusu Kashmir, na Pakistan na Marekani zililazimika kukubali ukweli huo mpya.

5- Wakati wa utawala wa chama cha Congress nchini India, maoni ya umma yaliganda dhidi ya makubaliano yoyote kuhusu suala la Kashmir kwa Pakistan. Hivyo basi, Modi alipoingia ofisi ya Waziri Mkuu mnamo Mei 26, 2014, alikuwa akikabiliana na miaka 10 ya msimamo mkali wa chama cha Congress wa kutokubali kujadiliana kuhusu Kashmir.

6- Marekani imejaribu kuandaa mazingira ya kukaribiana kati ya India na Pakistan kama hatua ya mazungumzo kwa ajili ya kupata suluhu ya Kashmir. Kutokana na hilo, Nawaz alikaidi hisia za Waislamu na kuitembelea India kumpongeza Modi na kuhudhuria sherehe za kutawazwa kwake, hali ya kuwa anajulikana kwa uadui wake dhidi ya Waislamu... hatua hiyo iliongeza utengano badala ya kukaribiana...

7- Kisha kuna jambo jingine nalo ni kwamba vyama vyote vya India vinashikilia Kashmir kama sehemu yake, na kwa hivyo hata kama vyama vya Janata na Nawaz ni vitiifu kwa Marekani, si rahisi kutatua suala la Kashmir kwa njia ya mazungumzo. Bali suluhu sahihi na ya uadilifu ni kukomeshwa kwa uvamizi wa Wahindu kwa nguvu, na hilo ni jambo rahisi kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ikiwa nchini Pakistan kungekuwa na dola yenye ikhlasi kwa Mwenyezi Mungu (swt) na Mtume Wake (saw), na tunatumai itakuwa hivi karibuni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Pamoja na haya yote, si jambo lisilowezekana kwa Marekani kuzikutanisha pande mbili hizo, lakini jambo hili linaweza kuchukua muda.

Tatu: Uhusiano wa China na Afghanistan... na Taliban:

1- China imevutiwa sana na kuendeleza mahusiano ya kibiashara na Afghanistan, na kampuni ya Metallurgical Group Corporation inayomilikiwa na serikali ilitumia dola bilioni 3 kwenye mgodi wa shaba huko Mes Aynak "takriban kilomita 50 kusini mwa Kabul". Kampuni ya Taifa ya Petroli ya China (CNPC) "kampuni kubwa zaidi ya mafuta nchini humo," ilikubaliana mnamo mwaka 2011 kuendeleza bonde la "Amu Darya" nchini Afghanistan, mradi ambao utazalisha dola bilioni 7 za faida. Kampuni ya CNPC imesaidia kuanzisha kituo cha kwanza cha uzalishaji mafuta nchini Afghanistan, kikiwa na uwezo wa kila mwaka wa mapipa milioni 1.5 ["China na Uwepo wake nchini Afghanistan", gazeti la The National, 1 Novemba 2014]. Zaidi ya hayo, hivi karibuni China imetangaza mradi wa "New Silk Road" (Barabara Mpya ya Hariri) wenye gharama ya mabilioni ya dola. Mradi huo una sehemu tatu: sehemu ya kwanza inaanzia Xi'an nchini China, inapita Pakistan na kuishia Uturuki. Sehemu ya pili inaanzia Bangladesh hadi Myanmar, huku ya tatu ikiunganisha pwani ya Fujian ya China na dunia nzima. Kufufua Ukanda wa Kiuchumi wa Barabara ya Hariri ilikuwa ni wazo la Rais Xi Jinping, na limekuwa likifanyiwa kazi, kuendelezwa na kuharakishwa utekelezaji wake tangu robo ya mwisho ya mwaka 2013. Hivyo, Afghanistan ni kipande muhimu katika mradi huu mkubwa. Pia, hamu kubwa ya China ya maliasili itaongezeka nchini Afghanistan, kukiwa na zaidi ya dola trilioni 1 katika uwezekano wa utajiri wa madini.

Kutokana na hayo, haikuwa ajabu kwamba mara tu Ashraf Ghani alipokuwa rais wa Afghanistan, ziara yake ya kwanza ya nje ilikuwa nchini China, ambapo alitunukiwa ahadi mpya kutoka Beijing. China iliahidi kuipa Afghanistan yuan bilioni 2 (dola milioni 327) za msaada hadi kufikia mwaka 2017, pamoja na dola milioni 250 ambazo imechangia nchini Afghanistan tangu mwaka 2001. Aidha, China iliahidi kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kitaalamu 3,000 wa Afghanistan, pamoja na kusaidia katika maendeleo ya kilimo cha Afghanistan, nishati ya maji, na miundombinu.

Kutokana na yaliyotangulia, inabainika kuwa China ina maslahi makubwa ya kibiashara katika kuendeleza mahusiano imara na Afghanistan katika siku za usoni.

2- China haiwezi kutumia mahusiano yake ya kibiashara na Afghanistan isipokuwa tu kama nchi hiyo itakuwa tulivu... na utulivu unahitaji serikali yenye nguvu nchini Afghanistan, ndiyo maana China ina shauku ya kuunga mkono serikali ya Ghani kwa kadiri inavyowezekana. Waziri wa Mambo ya Nje wa China (Wang Yi) alisema wakati wa ziara yake mjini Kabul mnamo Februari 22, 2014: "Amani na utulivu katika nchi hii vina athari kwa usalama wa magharibi mwa China, na muhimu zaidi, vinaathiri utulivu na maendeleo ya eneo zima. Tunatumai kuona maridhiano ya kisiasa yenye msingi mpana na jumuishi nchini Afghanistan haraka iwezekanavyo, na China itachukua nafasi ya ujenzi ili kurahisisha hilo... nchi iliyogawanyika haina mustakabali." [Reuters, 22 Februari 2014].

Hapa ndipo palipokuja maslahi ya China katika utulivu wa Afghanistan. Kuna jambo jingine, kwani China inahofia kitisho kinachotokana na mpaka wa Afghanistan na China, unaojulikana kama "Wakhan Corridor" (Ukanda wa Wakhan), ambao ni kipande chembamba cha ardhi kaskazini-mashariki mwa Afghanistan, kinachotoka China na Tajikistan, kikitenganisha Pakistan na jimbo la Kashmir upande wa Pakistan, na kipo kati ya Pamir kaskazini na Hindu Kush kusini, urefu wake ni karibu kilomita 350, na upana wake kati ya kilomita 13-65. Unaunda njia ya kurahisisha harakati za wapiganaji wa Kiislamu wa Uighur, ambao wanaunda suala la usalama wa ndani kwa China, kwani Taliban inawahifadhi na kuwafunza wapiganaji wa "Harakati ya Kiislamu ya Turkestan Mashariki" kutoka kwa Wauighur nchini Afghanistan na maeneo ya kikabila nchini Pakistan, na wapiganaji wa Uighur wanapigana kwa ajili ya kuanzisha nchi huru isiyo na utawala wa China. Waziri wa Mambo ya Nje wa China alieleza hilo kwa uwazi wakati wa ziara yake mjini Kabul mwaka jana, katika taarifa iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Watu wa China kuhusu lengo la ziara hiyo ambapo alisema: "...kuimarisha ushirikiano katika nyanja ya usalama, na ushirikiano katika nyanja nyingine kama vile kupambana na ugaidi, na kupambana na Harakati ya Kiislamu ya Turkestan Mashariki..." ["Wang Yi afanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan", Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China katika Jamhuri ya Czech, 23 Februari 2014].

Kutokana na mambo yaliyotajwa hapo juu, China inaunga mkono kuendelea kwa uwepo wa Marekani nchini Afghanistan baada ya Desemba 2014; ili kudumisha utulivu. Hilo liliashiriwa wazi katika himizo la China kwa Hamid Karzai kusaini mkataba wa usalama wa nchi mbili (BSA). Mnamo Septemba 2013, msemaji wa Rais Hamid Karzai "Aimal Faizi" alisema kuwa Rais wa China anatoa msaada kwa mahusiano ya nje ya Afghanistan na nchi za kikanda na kigeni, hususan na Marekani, katika jitihada za kuleta amani na utulivu katika eneo hilo, na kwamba China inaunga mkono kuhitimishwa kwa mkataba wa usalama kati ya Afghanistan na Marekani. ["China inaunga mkono mkataba wa usalama kati ya Afghanistan na Marekani", gazeti la Khaama, 28 Septemba 2013]. Gazeti hilo liliongeza kuwa China pia ilitangaza kuwa inaunga mkono mchakato wa amani unaoongozwa na Afghanistan, na kwamba iko tayari kuchukua nafasi katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan, yaani mazungumzo ya amani na Taliban... Kutokana na kauli hizi, ambazo zote ziko katika mkondo mmoja, na taarifa nyingine zinazofanana na hizo, inabainika kuwa China inaunga mkono Marekani ili kudumisha utulivu nchini Afghanistan, na pia inaunga mkono mazungumzo ya amani na Taliban kwa ufahamu kamili wa Wamarekani.

Pia, China mnamo Novemba 2014, ilianzisha "Jukwaa la Amani na Maridhiano" kama ilivyoeleza Reuters, katika jitihada za kuchukua nafasi kubwa zaidi nchini Afghanistan ili kusukuma mbele mazungumzo ya amani, [Reuters, 11 Novemba 2014], na kutafuta njia za kupatanisha makubaliano ya amani kati ya serikali ya Ghani na harakati ya Taliban. Hivyo basi, hivi karibuni, harakati ya Taliban ilitembelea Beijing, na China inaunga mkono Pakistan kutoa shinikizo kwa harakati ya Taliban ya Afghanistan ili kufikia maridhiano na serikali ya Ghani. Hili haliwezi kufasiriwa kuwa China inataka kuchukua nafasi ya Marekani nchini Afghanistan, bali kinyume chake, maslahi ya Beijing na Washington yanawiana katika suala la kufikia utulivu nchini Afghanistan. Kuhusu suala hili, ofisa wa Marekani alisema: "Marekani na China zimekubaliana kufanya kazi pamoja ili kuunga mkono serikali ya Afghanistan, umoja wa kitaifa, vikosi vya usalama, na maendeleo ya kiuchumi; ili kuhakikisha kuwa Afghanistan haitumiwi tena kama kimbilio salama la magaidi." ["China yapiga hatua kupatanisha mazungumzo ya amani yaliyokwama na harakati ya Taliban ya Afghanistan", Economic Times, 13 Februari 2015].

Yote haya yanaashiria kuwa China inajali utulivu nchini Afghanistan kutokana na kuendeleza maslahi yake mapana ya kiuchumi humo, na inakubaliana na Marekani katika suala la utulivu wa Afghanistan... Vilevile inajali maridhiano kati ya Afghanistan na Taliban ili China ifaidike na hilo kwa kubana njia ya usambazaji wa wapiganaji wa Turkestan Mashariki, na ndiyo maana kulikuwa na mawasiliano hayo kutoka China na pande zote mbili; Afghanistan na Taliban...

Tunatumai kuwa Taliban itatambua jambo hili na kurudisha hila ya China kifuani mwake, na kuendeleza udugu wa Kiislamu kati yao na wapiganaji wa Turkestan Mashariki.

Share Article

Share this article with your network