Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Shirikisho la Nchi Tatu Mali-Niger-Burkina Faso

July 24, 2024
2457

Swali:

Viongozi wa mabaraza ya kijeshi nchini Burkina Faso, Niger, na Mali walitangaza mnamo Jumamosi, Julai 6, 2024, katika mkutano wa kilele uliofanyika Niamey, mji mkuu wa Niger, kuhusu kutia saini makubaliano ya shirikisho (confederation). Je, kuna nguvu ya kimataifa nyuma ya tangazo hili? Na ikiwa ipo, ni nchi gani wanayoonyesha utiifu kwayo? Au je, shirikisho hili ni hatua ya hiari yao wenyewe? Ahsanteni sana.

Jibu:

Ili jibu liwe wazi, tunapitia mambo yafuatayo:

1- Nchi hizi tatu, baada ya mapinduzi yaliyotokea kati ya mwaka 2020-2023, zimekuwa zikiungana na Marekani na kufuata amri zake! Tulieleza hili katika majibu ya maswali: mnamo 2020/9/1 kuhusu mapinduzi ya Mali yaliyoongozwa na Assimi Goïta, 2023/2/7 kuhusu mapinduzi ya Burkina Faso yaliyoongozwa na Ibrahim Traoré, na 2023/8/15 kuhusu mapinduzi ya Niger yaliyoongozwa na Abdourahamane Tiani.. Na maeneo haya matatu ni nchi za Kiislamu:

a- Ama Mali: Ni nchi ya Kiislamu; Uislamu ulifika huko katika karne ya kumi na moja, na bado dini kuu nchini Mali ni Uislamu, ambapo karibu 90% ya Wamalii ni Waislamu, karibu 5% ni Wakristo, na karibu 5% ni dini nyinginezo... Na mji mkuu ni Bamako.

b- Ama Burkina Faso: Ni nchi iliyopo Afrika Magharibi, na ni nchi ya Kiislamu. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2006, zaidi ya 60.5% ya wakazi wake ni Waislamu, na karibu 23% ni Wakristo, kisha mila nyinginezo. Ina eneo la kilomita mraba 274,200, na ina idadi ya watu 21,510,181 na inategemea kilimo katika uchumi wake. Mji wa Ouagadougou ndio mji muhimu zaidi nchini humo na ndio mji mkuu.

c- Ama Niger: Iko Afrika Magharibi na ilipewa jina la Niger kutokana na Mto Niger unaopita katika ardhi yake. Inapakana na Nigeria na Benin kwa upande wa kusini, Burkina Faso na Mali kwa upande wa magharibi, Algeria na Libya kwa upande wa kaskazini, huku Chad ikiipakana kwa upande wa mashariki. Jumla ya eneo la Niger ni takriban kilomita mraba 1,270,000. Niger ni nchi ya Kiislamu, kwani Uislamu ndio dini ya idadi kubwa ya watu nchini Niger, na asilimia yao inazidi 99.3%. Uislamu ulienea katika nchi ambayo sasa ni Niger katika karne ya kumi na tano kupitia upanuzi wa Usultani wa Songhai upande wa magharibi na athari za biashara ya kupitia jangwani ikitokea Maghrib na Misri... Na mji mkuu ni Niamey.

Hivyo basi, mapinduzi yaliyotokea Mali, Niger, na Burkina Faso kati ya mwaka 2020 na 2023 yalikuwa yakiiunga mkono Marekani na yakisaidiwa nayo.

2- Mnamo Septemba 16, 2023, nchi hizi tatu zilianzisha "Muungano wa Nchi za Sahel" (Alliance of Sahel States) ili kuunda jeshi la pamoja la ulinzi dhidi ya tishio la uwezekano wa kuingiliwa kijeshi na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) nchini Niger: (Rais wa Mali, Kanali Assimi Goïta, Rais wa Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani, na Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, walikuwa wametia saini, mnamo Septemba 2023, mkataba ambao Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, alisema katika taarifa yake wakati huo: Kuwa "utakuwa ni mchanganyiko wa juhudi za kijeshi na kiuchumi kati ya nchi hizi tatu").

Mkataba wa pamoja uliotiwa saini na viongozi wa Mali, Burkina Faso, na Niger, mnamo Septemba 16, 2023, unaamuru kuundwa kwa "Muungano wa Nchi za Sahel". Mkataba huo wa kuanzisha muungano unajumuisha vifungu 17, cha kwanza kikieleza kuitwa "Mkataba wa Liptako-Gourma", na kwamba "pande husika zimekubaliana kuanzisha Muungano wa Nchi za Sahel, unaofupishwa kama AES", huku kifungu cha pili kikieleza kuwa lengo la mkataba huu ni "kuunda muundo wa ulinzi wa pamoja na kusaidiana kwa pande husika". Mkataba huo pia unaeleza katika kifungu chake cha 6 kuwa "shambulio lolote dhidi ya mamlaka na usalama wa ardhi ya upande mmoja, litachukuliwa kuwa ni uchokozi dhidi ya wengine, jambo linalopelekea wajibu wa kusaidiana, ikiwemo matumizi ya nguvu ya kijeshi ili kurejesha usalama". Kifungu cha 11 cha mkataba huo kinaeleza kuwa "muungano uko wazi kwa kila nchi inayoshirikiana na nchi hizi tatu katika misingi ya kijiografia, kisiasa, kijamii na kiutamaduni, na inayokubali malengo ya muungano huo". (Al Jazeera Center for Studies, 2024/06/25).

Inadhihirika kutokana na vifungu vya 6 na 11 vya muungano huu ulioundwa na nchi hizi tatu kuwa madhumuni ya kuanzishwa kwake ni kukabiliana na uingiliaji wa kijeshi wa kigeni unaowezekana, hasa wa Ufaransa, kupitia ECOWAS, na kusimama kijeshi na mmoja wao iwapo atashambuliwa kijeshi na Ufaransa. Lengo lingine ni kuunda mgawanyiko ndani ya ECOWAS, kama inavyofahamika kutokana na vifungu kumi na moja, na kuzihimiza nchi zilizo chini ya jumuiya hiyo kujiunga na muungano huu.

3- Mnamo Julai 6, 2024, Mali, Niger, na Burkina Faso zilitangaza kuanzishwa kwa shirikisho la konfedarali (confederation). Makubaliano haya yaliyotiwa saini kati ya nchi hizi tatu mnamo Julai 6, 2024, huko Niamey, mji mkuu wa Niger, ni mwendelezo wa makubaliano ya Muungano wa Nchi za Sahel yaliyotiwa saini katika mkutano wa kwanza. (Burkina Faso, Mali, na Niger zilizopo katika ukanda wa Sahel barani Afrika, zimetangaza leo Jumamosi, kuungana kwao ndani ya "shirikisho". Nchi hizo tatu, katika taarifa ya mwisho wakati wa mkutano wao wa kwanza wa kilele siku ya Jumamosi katika mji mkuu wa Niger, Niamey, zimesema kuwa maraisi wao "waliamua kuvuka hatua nyingine kuelekea ushirikiano wa ndani zaidi kati ya nchi wanachama. Kwa ajili hiyo, walipitisha mkataba unaoanzisha shirikisho kati ya Burkina Faso, Mali, na Niger chini ya jina la Shirikisho la Nchi za Sahel"... Al-Ittihad UAE, 2024/07/06).

4- Licha ya kukosekana kwa matamshi ya moja kwa moja kutoka Marekani, viashiria vyote vinaonyesha kuwa Marekani ndiyo iko nyuma ya kuanzishwa kwa nchi hizi kwa "Shirikisho la Nchi za Sahel". Kwa upande mmoja, Marekani inalitaka liwe ngome ya kuwalinda vibaraka wake katika nchi hizi dhidi ya vikwazo vya jumuiya ya ECOWAS, hasa kwa kuzingatia kuwa nchi hizo tatu hazina pwani, jambo linalokwamisha biashara zao. Kwa upande mwingine, Marekani inataka muungano huo uwe mbadala wa ECOWAS inayodhibitiwa na Ufaransa na Uingereza. Hakika, kuanzishwa kwa shirikisho hilo kumezua dhoruba ya ukosoaji dhidi yake ndani ya kundi la ECOWAS, ambalo sasa linatakiwa kufanya marekebisho, jambo lililojitokeza katika matamshi ya Rais wa Senegal; ikimaanisha kuwa kuhama kwa nchi kutoka ECOWAS kuelekea kwenye "shirikisho" hilo sasa kumewezekana.

5- Kwa hiyo, shirikisho hili si la bahati mbaya, bali lilianzishwa na Marekani kati ya nchi hizi tatu zinazoiunga mkono ili kuhifadhi makoloni yake na kuzuia uingiliaji kati wa Ulaya, hasa Ufaransa, na kurejea katika makoloni yake. Hatua zilizochukuliwa na nchi hizi kabla ya muungano huo zinathibitisha hili, zikiwemo:

a- Burkina Faso na Niger zilitangaza kujiondoa katika kikosi kazi cha nchi tano za Sahel (G5 Sahel) mnamo Novemba 2023. Pia, Mali ilijiondoa katika kikosi hicho mnamo Mei 2022. (Burkina Faso na Niger zilitangaza, Jumamosi, kujiondoa kwao kutoka kwa kundi la nchi tano za Sahel, ikiwa ni mwaka mmoja na nusu baada ya Mali kujiondoa. Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya serikali za Burkina Faso na Niger, iliyochapishwa na shirika rasmi la habari la Burkina Faso, "uamuzi huo ni wa mamlaka, na umekuja baada ya tathmini ya kina ya kundi hilo na kazi yake". Taarifa hiyo iliongeza: "Kundi la G5 Sahel haliwezi kutumikia maslahi ya kigeni kwa gharama ya maslahi ya watu wa Sahel, wala kukubali maelekezo ya nguvu yoyote ile kwa jina la ushirikiano wa kupotosha na wa kitoto unaokanusha haki ya mamlaka ya watu na nchi zetu. Hivyo basi, Burkina Faso na Niger zimebeba wajibu wa kihistoria kwa kujiondoa katika shirika hili"... Anadolu Agency, 2023/12/03). (Baraza la kijeshi nchini Mali lilitangaza katika taarifa yake siku ya Jumapili kujiondoa kwa nchi hiyo kutoka kwa kikosi cha kijeshi cha mataifa mengi katika ukanda wa Sahel barani Afrika, kilichoundwa kupigana na wanajihadi mwaka 2014. Baraza hilo lililalamikia uamuzi wa kujiondoa kwa sababu ya kutoiruhusu Mali kuongoza "Kundi la nchi tano za Sahel", ambapo Bamako ilipaswa kuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa nchi hizo (Mauritania, Chad, Burkina Faso na Niger) mnamo Februari 2022, kwa kisingizio cha ukosefu wa utulivu wa ndani nchini Mali... France24, 2022/05/16).

b- Mali, Niger, na Burkina Faso zilitangaza kujiondoa kutoka ECOWAS mnamo Januari 2024 ili kujiondoa katika ushawishi wa Ufaransa na kutoiruhusu kuingilia kijeshi kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. (Mali, Burkina Faso, na Niger ziliamua, Jumapili, kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS). Hii ilikuja katika taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi hizo tatu za Sahel, zinazoongozwa na mabaraza ya kijeshi na serikali za mpito. Taarifa hiyo ilisema kuwa nchi hizo tatu zitajiondoa kutoka ECOWAS, inayoundwa na wanachama 15, "haraka iwezekanavyo". Iliongeza kuwa ECOWAS, inayotuhumiwa kwa "kufuata ushawishi wa nguvu za kigeni" na "usaliti wa misingi yake", inajenga "tishio" kwa nchi hizo tatu... Anadolu Agency, 2024/01/28).

6- Haya yote yanaonyesha kuwa nchi hizi tatu zimejiondoa katika mashirika yote yaliyo chini ya ushawishi na maelekezo ya Ufaransa ili kuondokana na ushawishi wa Kifaransa. Ni vigumu kwa nchi hizi kujiondoa zenyewe bila uungaji mkono wa Marekani, bali ni amri ya Marekani, kama utangulizi wa kuanzisha shirikisho ambalo Marekani ililitaka ili kuisambaratisha ECOWAS au kuidhoofisha, na kisha kutikisa ushawishi wa Ufaransa au kuubadilisha katika nchi hizo tatu muhimu ambazo jumla ya idadi ya watu wake inazidi milioni 70 na zenye rasilimali zenye ushawishi za nishati na madini ambapo zilikuwa zikitumiwa na makampuni ya Kifaransa! Kisha "shirikisho" hili na msisitizo huo wa viongozi wake unahatarisha kunyakua nchi zaidi kutoka kwenye mzunguko wa ushawishi wa Ufaransa katika ukanda wa Sahel, ambazo ni serikali dhaifu sana kutokana na uporaji wa kikoloni wa Ufaransa na umaskini uliokithiri uliouacha, na kutokana na ukubwa wa ufisadi uliokithiri kati ya watawala. Mazingira haya mapya yanawashawishi wanajeshi ambao Marekani inawasiliana nao kupitia wito wa (kupambana na ugaidi), mafunzo, na msaada wa kijeshi. Kwa ujumla, inaweza kusemwa kuwa msimamo mkali wa viongozi wa nchi hizo tatu dhidi ya Ufaransa unachukuliwa kuwa tishio kubwa zaidi linalokabili ushawishi wa Ufaransa baada ya kuwa salama na thabiti kwa miongo kadhaa.

7- Hivyo basi, inabainika kuwa watawala wa nchi za Kiislamu wanahamisha utiifu wa nchi kutoka kwa mkoloni mmoja kwenda kwa mwingine. Wanaitolea kisogo Ufaransa ambayo imepora utajiri wa Waislamu na kuelekea kwa Marekani ili nayo ipore utajiri huo, huku Waislamu wakibaki katika dhiki na umaskini, kana kwamba Waislamu hawawezi kutawala nchi zao wenyewe. Ikiwa hali hii inahusu nchi zote za Waislamu, basi katika nchi za Afrika ni mbaya zaidi na yenye kina kirefu. Kila utambuzi wa Waislamu kuhusu dini yao unavyoongezeka na yakini yao kuwa kushikamana nayo ndiyo njia ya ukombozi wao duniani na akhera, ndivyo Waislamu wanavyokuwa karibu na yale yanayomridhisha Allah Ta’ala. Chuki yao itaongezeka dhidi ya kafiri mkoloni aliyestarehe na anayezidi kustarehe kwa utajiri wa nchi zao na kuwaachia wakipambana na umaskini na uhitaji. Jitihada za Waislamu na kazi yao itazidi kwa ajili ya kusimamisha dini yao na kurejesha maisha ya Kiislamu kupitia kusimamisha Dola ya Kiislamu itakayowaunganisha Waislamu, Dola ya Khilafah ya pili kwa njia ya Utume. Hilo ni baada ya utawala huu wa mabavu (Al-Mulk al-Jabri) ambao Waislamu wanaishi ndani yake. Sisi tuna utulivu, kwa idhini ya Allah, tunapoona kuwa kikombe kimefurika kwa Waislamu na kwamba wako hatua moja tu kutoka katika kujenga Dola ya Kiislamu, kuunganisha nchi za Kiislamu, na kuwafukuza makafiri wakoloni wote katika nchi zao, na hata kubeba uongofu kwenda kwa nchi hizo. Na hilo kwa Allah si jambo gumu. Anasema ﷺ katika hadith aliyoipokea Ahmad kutoka kwa Hudhayfah radhi za Allah ziwe juu yake:

ثُمَّ تَكُونُ مُلْكاً جَبْرِيَّةً فَتَكُونُ مَا شَاءَ اللهُ أَنْ تَكُونَ ثُمَّ يَرْفَعُهَا إِذَا شَاءَ أَنْ يَرْفَعَهَا ثُمَّ تَكُونُ خِلَافَةً عَلَى مِنْهَاجِ النُّبُوَّةِ ثُمَّ سَكَتَ

"…kisha utakuwepo utawala wa mabavu, na utakuwepo kadiri Allah atakavyopenda uwepo, kisha Atauondoa pindi Atakapotaka Auondoe, kisha itakuwepo Khilafah kwa njia ya Utume, kisha akanyamaza." (HR. Ahmad)

18 Muharram al-Haram 1446 H 24/07/2024 M

Share Article

Share this article with your network