** (Sfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri")**
Jibu la Swali
Athari ya Kimada ya Dua
Kwa Abu Abdullah Khalaf
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh, mpendwa Sheikh wangu. Baada ya salamu, naomba unisaidie kupata ufafanuzi katika suala la dua... Kwani imetajwa ndani ya Qur'ani Tukufu kuwa Mwenyezi Mungu humjibu mwombaji anapomwomba. Na Sunnah imetubainishia kuwa kujibiwa kwa dua kunaweza kuwa hapa duniani hivi sasa, au baadaye, au kwa kitu bora zaidi kuliko hicho duniani au Akhera. Na Hizb inabainisha katika kitabu cha Mafahimu ya Hizb ut-Tahrir kuwa dua huchuma thamani ya kiroho lakini athari na matokeo yake hayahisiki, yaani thawabu. Swali langu ni: Inawezekanaje kudhibiti athari za dua katika thawabu pekee ilhali Mwenyezi Mungu anaweza kujibu dua duniani? Na ubarikiwe.
Jibu:
(Waalaykum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh)
Inaonekana unaashiria yale yaliyokuja katika kitabu cha Mafahimu kwenye ukurasa wa 57 na 58, na kwamba mada hiyo imekutatiza. Suala liko hivi:
Yaliyoandikwa kuhusu dua katika kurasa hizo, kwamba inapata matokeo yasiyohisika "thawabu", ilikuwa katika muktadha wa hali fulani mahususi, nayo ni: pale ambapo maandiko ya kisheria yamebainisha njia (tariqah) ya kutekeleza jambo fulani, kisha tusiitumie njia hiyo na badala yake kutosheka na dua pekee. Kitabu kimepiga mfano wa Jihadi na dua kuhusiana na ufunguzi wa ngome au kupigana na adui...
Lakini katika hali nyingine isiyo hiyo, dua inaweza kuleta matokeo yanayohisika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, pamoja na kupata thawabu, kama ilivyokuja katika Hadith ya Mtume (saw) iliyotajwa kwenye swali.
Ili jambo hili liwe wazi zaidi, nitapitia yale yaliyokuja katika ukurasa wa 57 na 58 wa Mafahimu:
1- Ilikuja mwanzoni mwa ukurasa wa 57: (Na anayechunguza kwa kina matendo haya ambayo yameonyeshwa na hukumu za kisheria zinazohusiana na njia (tariqah), atakuta kuwa ni matendo ya kimada yanayopata matokeo yanayohisika na siyo matendo yanayopata matokeo yasiyohisika...) Mwisho wa nukuu.
Hii ni sahihi, kwani kwa kufuatilia dalili, inabainika kuwa matendo ya tariqah hupata matokeo yanayohisika.
2- Kisha kitabu kikafanya ulinganifu baada ya nukuu hiyo kati ya dua na Jihadi katika hali ya kufungua ngome au mji au kuua adui. Kikaona kuwa dua pekee siyo sehemu ya tariqah, na kwamba Jihadi ndiyo njia (tariqah) katika hali hii, na hiyo ni kwa mujibu wa dalili zilizokuja...
Ilikuja katika Mafahimu: (...kwa mfano, dua ni tendo linalochuma thamani ya kiroho, na Jihadi ni tendo la kimada linalochuma thamani ya kiroho, lakini dua ijapokuwa ni tendo la kimada (kwa maana ya kutamka), inapata matokeo yasiyohisika ambayo ni thawabu, hata ikiwa kusudio la anayefanya dua ni kuchuma thamani ya kiroho. Tofauti na Jihadi, kwani hiyo ni kupigana na maadui na ni tendo la kimada linalopata matokeo yanayohisika ambayo ni kufungua ngome au mji au kuua adui na mfano wa hayo, hata ikiwa kusudio la mwanajihadi ni kuchuma thamani ya kiroho...)
Hivyo ulinganifu hapa ni kati ya dua na Jihadi wakati wa kupigana na maadui au kufungua ngome...:
Ikiwa dua itafanywa peke yake, basi inapata matokeo yasiyohisika ambayo ni thawabu, na hiyo ni kwa sababu njia (tariqah) iliyokuja katika hali hii ni Jihadi na siyo dua. Hivyo mada hapa ni ulinganifu wa dua ikiwa itatumiwa peke yake katika jambo fulani bila kutumia njia (tariqah) iliyobainishwa kwa ajili ya jambo hilo.
Na haijuzu kueneza hali hii kwa kuifanya dua katika hali nyingine kuwa haina athari katika matokeo yanayohisika na kwamba inapata thawabu pekee! Kwa sababu yaliyokuja katika aya iliyotangulia yanahusiana na suala ambalo lina njia ya kivitendo katika Sharia ambayo haikuchukuliwa, bali badala yake ikachukuliwa dua pekee, hivyo dua ikawa na matokeo yasiyohisika ambayo ni thawabu.
Inaonekana utata umetokana na sentensi iliyokuja katika mfano uliopigwa, ambapo ilitajwa "lakini dua ijapokuwa ni tendo la kimada inapata matokeo yasiyohisika ambayo ni thawabu...", hivyo sentensi hiyo ikaonekana kana kwamba ni ya ujumla, yaani kwamba dua katika hali zake zote haipati ila matokeo yasiyohisika "thawabu", wakati ambapo muktadha wa mfano huo ni katika hali mahususi, nayo ni kutumia dua pekee katika kufungua ngome au kushinda adui bila kuchukua njia (tariqah) ambayo maandiko yamekuja nayo ambayo ni "Jihadi".
3- Ama dua pamoja na kuchukua sababu (al-akhdhu bil-asbab), ina athari katika matokeo, na hivi ndivyo alivyokuwa Mtume (saw) na maswahaba wake (ra). Mtume (saw) alikuwa akitayarisha jeshi kisha anaingia katika kibanda chake (Arish) akiomba, na Waislamu katika vita vya Qadisiyyah walikuwa wakitayarisha zana za kuvuka mto na Saad (ra) akimwelekea Mwenyezi Mungu na kuomba... Na hivyo ndivyo waumini wa kweli wanavyotayarisha zana na kuanza kuomba. Anayetafuta riziki anajitahidi na kutaabika huku akiomba, na mwanafunzi anasoma na kujitahidi huku akimwomba Mwenyezi Mungu (swt) mafanikio, na jambo hilo lina athari katika matokeo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Ilikuja katika Mafahimu mwishoni mwa ukurasa wa 58: (Ila ni lazima ijulikane kwamba hata kama tendo lililoonyeshwa na njia (tariqah) ni tendo la kimada lenye matokeo yanayohisika, lakini ni lazima tendo hili liongozwe na amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu, na yakusudiwe katika uendeshaji wake radhi za Mwenyezi Mungu. Vilevile ni lazima kwa Muislamu itawaliwe na utambuzi wake wa uhusiano wake na Mwenyezi Mungu Mtukufu, hivyo ajikurubishe Kwake kwa swala, dua, kusoma Qur'ani na mfano wake, na ni lazima Muislamu aamini kuwa ushindi unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa ajili hiyo, ilikuwa hapana budi kuwa na ucha Mungu uliokita vifuani kwa ajili ya kutekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu, na hapana budi kuwa na dua na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na hapana budi kuwa na kudumu na uhusiano na Mwenyezi Mungu wakati wa kufanya matendo yote.) Ni wazi kutokana na hapa umuhimu wa dua kuambatana na kuchukua sababu katika matendo yote ya muumini, na umuhimu huu umeongezeka kwa kukaririwa neno "hapana budi" ili kuashiria umuhimu mkubwa wa kuoanisha matendo yote na dua na kudumu na uhusiano na Mwenyezi Mungu...
4- Kutumia dua pamoja na kuchukua sababu ndivyo, kama tulivyosema, alivyokuwa Mtume (saw) na maswahaba wake (ra) na waumini. Na vikiambatana, vinakuwa na athari katika matokeo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kuvitumia pamoja hakupingani na njia ya Uislamu, bali kinachopingana nayo ni kutosheka na dua pekee bila kufuata njia (tariqah) ambayo maandiko yameibainisha kwa ajili ya kutekeleza fikra ya Kiislamu.
Ilikuja katika Mafahimu mwishoni mwa ukurasa wa 57 na mwanzo wa ukurasa wa 58: (Na kwa ajili hiyo, inakanushwa kwa ukali kabisa kuwa matendo yote yanayokusudiwa kutekeleza fikra ya Kiislamu yawe ni matendo yanayopata matokeo yasiyohisika, na hilo huchukuliwa kuwa ni kinyume na njia ya Uislamu...)
Yaani, kinachopingana na njia ya Uislamu ni "kuwa matendo yote yanayokusudiwa kutekeleza fikra ya Kiislamu yawe ni matendo yanayopata matokeo yasiyohisika". Ama baadhi yake kupata matokeo yasiyohisika "dua katika hali fulani" pamoja na matendo yanayopata matokeo yanayohisika "maandalizi ya kimada", basi hili ni jambo linalowezekana na ni muhimu, na halipingani na njia ya Uislamu.
5- Hivyo basi, yale yaliyokuja katika Mafahimu kuhusu dua ni katika hali mbili:
Kwanza: Ije peke yake katika kutekeleza fikra ambayo dua siyo njia ya kuitekeleza, bali maandiko yametaja njia nyingine ya kuitekeleza, kama dua pekee katika hali za kupigana na adui, kwa kusimama mbele ya ngome ili tuifungue bila kutayarisha jeshi la kupigana, bali kwa dua pekee. Katika hali hii, dua haipati chochote isipokuwa matokeo yasiyohisika ambayo ni "thawabu".
Pili: Dua kuambatana na sababu, na hili ni jambo ambalo hapana budi nalo, na katika hali hii zinashirikiana "yenyewe na kuchukua sababu" katika kuathiri matokeo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.
Na haikuja katika Mafahimu kuhusu dua chochote katika hali nyinginezo, bali hizo zinajumuishwa na Hadith ya jumla aliyoitoa Ahmad katika Musnad yake: Kutoka kwa Abi al-Mutawakkil, kutoka kwa Abi Said, kwamba Mtume (saw) amesema:
مَا مِنْ مُسْلِمٍ يَدْعُو بِدَعْوَةٍ لَيْسَ فِيهَا إِثْمٌ، وَلَا قَطِيعَةُ رَحِمٍ، إِلَّا أَعْطَاهُ اللَّهُ بِهَا إِحْدَى ثَلَاثٍ: إِمَّا أَنْ تُعَجَّلَ لَهُ دَعْوَتُهُ، وَإِمَّا أَنْ يَدَّخِرَهَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ، وَإِمَّا أَنْ يَصْرِفَ عَنْهُ مِنَ السُّوءِ مِثْلَهَا
"Hakuna Muislamu yeyote anayeomba dua ambayo haina dhambi ndani yake wala kuvunja undugu, ila Mwenyezi Mungu humpa kwayo moja ya mambo matatu: Ama amtimizie haraka dua yake, au amewekee akiba kwa ajili yake huko Akhera, au amwepushie ubaya mfano wa dua hiyo." Wakasema: "Basi tutakithirisha (kuomba)," akasema: "Mwenyezi Mungu ni mwingi zaidi (wa kutoa)."
Yaani Mwenyezi Mungu (swt) humjibu mwombaji kwa moja ya mambo matatu, na miongoni mwayo ni "ama amtimizie haraka dua yake". Na hayo ni matokeo yanayohisika.
6- Kwa mujibu wa hayo, basi kuna matokeo yanayohisika yanayowezekana kwa dua katika hali nyingine tofauti na ile iliyotajwa katika Mafahimu, kwani Hadith imetaja moja ya mambo matatu kuwa ni "amtimizie haraka dua yake" na haya ni matokeo yanayohisika... Na Mwenyezi Mungu amewafanyia hisani waja wake katika aya Zake kwamba Yeye (swt) hujibu dua ya mwenye dhiki anapomwomba, na akajaalia jibu hili kuwa ni sehemu ya ushahidi kuwa hapana mungu ila Allah. Ni wazi kutokana na yote hayo kuwa kujibu kwa mwenye dhiki hapa ni duniani, kwani neno "mwenye dhiki" ni sifa inayofahamika kwa kuomba haja ya duniani, hivyo jibu linakuwa ni lenye kuhisika kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Anasema Subhaanahu:
أَمَّنْ يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ أَإِلَهٌ مَعَ اللَّهِ قَلِيلًا مَا تَذَكَّرُونَ
"Je, nani yule anayemjibu mwenye shida anapomwomba, na akaondoa dhiki, na akakufanyeni makhalifa wa ardhi? Je, yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu? Ni machache mnayoyakumbuka." (QS. An-Naml [27]: 62)
Na Mwenyezi Mungu (swt) ametuamuru kuomba na akatuahidi jibu:
وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ
"Na Mola wenu amesema: Niombeni nitakujibuni." (QS. Ghafir [40]: 60)
Na Mtume (saw) ametafsiri kuitikiwa huku kuwa ni "moja ya mambo matatu" na miongoni mwayo ni matokeo yanayohisika. Na bila shaka, kupatikana kwa matokeo, yawe yanahisika au hayahisiki, yote hayo ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (swt).
Muhtasari:
- Yaliyoandikwa katika Mafahimu ni:
a- Njia (tariqah) ni matendo yanayopata matokeo yanayohisika.
b- Ulinganifu kati ya dua pekee na Jihadi katika suala la kufungua ngome au kupigana na adui... Dua hapa haileti matokeo yanayohisika, bali ni thawabu pekee, kwani yenyewe peke yake siyo sehemu ya tariqah ya kufungua ngome au kupigana na adui...
c- Haifai kuwa matendo yote yanayokusudiwa kutekeleza fikra ya Kiislamu yawe ni matendo yanayopata matokeo yasiyohisika, bali yanaweza kuwa ni mchanganyiko wa matendo yanayopata matokeo yanayohisika pamoja na matendo yanayopata matokeo yasiyohisika kama vile kutayarisha jeshi la kupigana pamoja na kumwomba Mwenyezi Mungu (swt) ushindi.
d- Dua ni jambo la lazima kwa Muislamu wakati wa kutekeleza matendo ya tariqah... kama alivyokuwa Mtume (saw) na maswahaba wake (ra).
- Haya ndiyo yaliyokuja katika Mafahimu kuhusu hali ya dua ambayo haiendi zaidi ya thawabu, yaani katika hali ya kutumia dua pekee kwa ajili ya suala fulani kama kufungua ngome..., na kutochukua njia (tariqah) iliyobainishwa na maandiko ya kisheria kwa ajili ya suala hilo ambayo hapa ni Jihadi.
Ama hali nyingine za dua, ziko chini ya Hadith ya jumla ya Mtume (saw): "Hakuna Muislamu yeyote anayeomba dua ambayo haina dhambi ndani yake wala kuvunja undugu, ila Mwenyezi Mungu humpa kwayo moja ya mambo matatu: Ama amtimizie haraka dua yake, au amewekee akiba kwa ajili yake huko Akhera, au amwepushie ubaya mfano wa dua hiyo." Wakasema: "Basi tutakithirisha," akasema: "Mwenyezi Mungu ni mwingi zaidi." Imepokewa na Ahmad katika Musnad yake.
Na kutokana na hayo, inabainika kuwa Mwenyezi Mungu (swt) anaweza kutimiza haja ya mwombaji hapa duniani, na hayo ni yanayohisika, au amwepushie mwombaji ubaya mfano wake duniani, na hayo ni yanayohisika, au amwekee akiba Siku ya Kiyama na hayo ni thawabu ambazo ni matokeo yasiyohisika.
Na Mwenyezi Mungu (swt) ni mwingi wa fadhila, kwani Yeye ni mwingi wa rehema na mkarimu, humkirimu mja Wake kwa thawabu za dua hata kama amemjibu dua yake duniani, basi sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir kwenye Facebook: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka tovuti ya Amir: Tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Amir kwenye Google Plus: Google Plus