Swali:
Hivi karibuni mgogoro wa kisiasa na kiuchumi umezidi kati ya Trump na Ulaya, hasa Ujerumani... Ingawa ilitegemewa kuwa kashikashi hizi zilizofanywa na Trump zingekoma baada ya kipindi cha kampeni za uchaguzi, kama ilivyo ada ya wagombea huko Magharibi... Lakini zimeendelea kuongezeka baada ya yeye kuchukua mamlaka. Ni nini sababu za hali hii? Kisha, kwa nini mgogoro huu ni mkubwa zaidi na Ujerumani? Na ni matokeo gani yanayotarajiwa kufuatia migogoro hii inayozidi kati ya Marekani na Ulaya, hasa Ujerumani? Jazakumullah Khayran.
Jibu:
Kwanza: Kuhusu sababu za kuongezeka kwa mgogoro huo wa kisiasa na kiuchumi, ni kutokana na kile alichokifanya Trump wakati wa kampeni za uchaguzi na baada yake, kupitia tabia za kiburi na uchochezi dhidi ya washirika wake, achilia mbali vibaraka:
1- Rais wa Marekani amesisitiza, kulingana na imani yake aliyoiorodhesha wakati wa kampeni za uchaguzi za 2016, kwamba nchi za NATO zina deni kwa Marekani kutokana na mchango mkubwa wa Marekani katika bajeti ya muungano huo, na kwamba nchi hizo lazima ziilipe Marekani kwa ajili ya ulinzi iliozipa katika miongo iliyopita! Baada ya kuchukua madaraka tarehe 20/01/2017, Rais wa Marekani alianza kujaribu kutekeleza imani yake hiyo na kuifanya kuwa misimamo rasmi ya dola huko Marekani. Alianza kuwataka Wazungu, hasa Wajerumani, kuchangia zaidi katika bajeti ya NATO, muungano ambao Trump alionyesha mashaka makubwa juu yake. Vilevile, alianza kulalamika mbele ya Wajerumani kuhusu nakisi ya mizania ya kibiashara ya nchi yake na Ujerumani. Katika mkutano wake wa kwanza na Kansela wa Ujerumani mjini Washington (Rais wa Marekani Donald Trump alimpokea Kansela wa Ujerumani Angela Merkel siku ya Ijumaa katika Ikulu ya White House, lakini mvutano ulikuwa dhahiri na hitilafu zilikuwa wazi, hasa kuhusu faili za biashara huria na uhamiaji...) (France24, 17/03/2017). Kabla ya mkutano wake naye (Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa Ujerumani ina deni kwa NATO la "kiwango kikubwa cha fedha" na kwamba Berlin lazima iilipe Marekani zaidi kwa ulinzi imara na ghali sana inaoutoa kwa Ujerumani. Alisema hayo siku moja baada ya kukutana na Kansela Angela Merkel, na Trump aliandika kwenye Twitter: "Ujerumani inadaiwa kiasi kikubwa cha fedha na NATO na inategemewa Marekani ipokee kiasi kikubwa zaidi kwa ajili ya ulinzi imara na ghali sana inaoutoa kwa Ujerumani"...) (Youm7, 18/03/2017). Ujerumani imekataa kuchukuliwa na Marekani kwa akili ya bosi wa mafia anayedai kodi za ulinzi (Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani siku ya Jumapili alikataa shutuma za Rais wa Marekani Donald Trump kwamba nchi yake inadaiwa na NATO kiasi kikubwa cha fedha, na Marekani kwa gharama za kijeshi. Ursula von der Leyen, aliye karibu na Kansela Angela Merkel, alisema katika taarifa yake: "Hakuna akaunti ambapo madeni yamesajiliwa kwa NATO," akiongeza kuwa gharama ndani ya NATO zisichukuliwe kama kipimo pekee cha juhudi za kijeshi za Ujerumani...) (France24, 19/03/2017).
2- Katika mkutano wa kilele wa NATO tarehe 25/05/2017, Rais wa Marekani aliongeza sauti ya hotuba yake dhidi ya nchi za Ulaya kuhusu mchango wao wa kifedha katika muungano huo (Rais wa Marekani Donald Trump aliwahutubia viongozi wa nchi za NATO kwa maneno yaliyowachanganya wahudhuriaji, ambao walionyesha ishara za mshangao kutokana na hotuba hiyo ya Trump, katika matamshi ya kushtua kuhusu uungaji mkono wa Marekani kwa NATO. Trump alionekana katika video akiwakemea viongozi wa NATO na kuwapa darsa, na maoni yao yalionyesha mshangao wao, hususan Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais mpya wa Ufaransa Emmanuel Macron. Trump alisema katika video hiyo, kulingana na tafsiri ya "Arabi21", kwa viongozi wa NATO: "Wanachama wa NATO lazima wachangie sehemu yao ya haki, na kutimiza ahadi zao za kifedha." Alisema akiwakemea: "Nchi 23 kati ya nchi 28 wanachama bado hazijalipa ahadi zao za kifedha kwa muungano," akiongeza kuwa jambo hili "si la haki kwa watu wa Marekani na walipa kodi nchini Marekani." Alisema kuwa "nchi nyingi kati ya hizi zimejilimbikizia kiasi kikubwa cha fedha katika miaka iliyopita kwa NATO, na bado hawajalipa." Alizidisha kukemea viongozi hao akisema kuwa "katika miaka minane iliyopita Marekani imetumia msaada mkubwa kwa muungano wa NATO kuliko nchi zote za NATO zilizounganishwa." Ilikuwa wazi kwa viongozi wa NATO kushtushwa na kauli za Trump, na walianza kutazamana, huku kukiwa na dalili za mvutano kutokana na mazungumzo yake yasiyo na kifani na yasiyotarajiwa. Trump aliwakebehi viongozi hao akisema: "Sijawauliza hata mara moja gharama ya makao makuu mapya ya NATO! Nakataa kufanya hivyo"...) (Arabi21, 27/05/2017).
- Matamshi na misimamo haya yote ya Trump yamesababisha kuundwa na kuongezeka kwa migogoro hiyo na Ulaya.
Pili: Kuhusu kwa nini mgogoro umeongezeka zaidi na Ujerumani kuliko nchi nyingine za Ulaya, hii inatokana na sababu zifuatazo:
1- Ujerumani ndiyo kitovu kikubwa zaidi cha kifedha barani Ulaya, na ni uchumi wa nne duniani baada ya Marekani, China na Japan. Kwa hivyo, macho ya Trump yamebaki yakielekezwa kwake katika jaribio la kuvuna fedha nyingi kutoka kwake kwa maslahi ya Marekani. Hasa kwa kuwa Marekani inaitumia Ujerumani kama kisingizio dhidi ya hatari ya Urusi ili kuishinikiza Ujerumani kuchangia zaidi ndani ya NATO. Hiki ni kisingizio ambacho Marekani inakitumia dhidi ya nchi zote za Ulaya, hasa za Mashariki, ili kuzidi kuzifunga kijeshi na Marekani.
2- Pia, kutokana na upande wa matumizi madogo ya Ujerumani katika muungano, kwani Berlin inatumia 1.2% ya mapato yake ya kitaifa kwa masuala ya kijeshi (dola bilioni 42). Kwa hivyo, inatumia kidogo kuliko Ufaransa ambayo matumizi yake ya kijeshi ni 1.79% ya pato lake la kitaifa (dola bilioni 44). Nchi za NATO zilikuwa zimekubaliana kuwa kila mwanachama atumie 2% ya pato lake la kitaifa, jambo ambalo Uingereza pekee ndiyo inalitekeleza pamoja na nchi nyingine chache na ndogo barani Ulaya, wakati nchi kuu za bara hilo hazitekelezi. Ikumbukwe kuwa Marekani inatumia 3.61% ya mapato yake ya kitaifa kwa masuala ya kijeshi (dola bilioni 664), na hivyo yenyewe pekee inabeba zaidi ya theluthi mbili ya matumizi ya kijeshi ndani ya mfumo wa NATO (takwimu za matumizi ya kijeshi zilizotajwa hapo juu ni kama zilivyochapishwa na tovuti ya Al-Araby Al-Jadeed 27/05/2017 kwa ajili ya matumizi ya mwaka 2016).
3- Mizania ya kibiashara kati ya Marekani na Ujerumani inaelemea upande wa Ujerumani kwa kiasi kikubwa, takriban Euro bilioni sitini. Ukubwa wa biashara kati ya Marekani na Ujerumani ulifikia Euro bilioni 165 mwaka 2016, ambapo Euro bilioni 107 ni ukubwa wa uingizaji bidhaa wa Marekani kutoka Ujerumani, kama ilivyoelezwa katika tovuti ya Arabi21, 24/02/2017... Hii inamaanisha kuwa ukubwa wa uingizaji bidhaa wa Ujerumani kutoka Marekani ni Euro bilioni 58 pekee! Hivyo, Trump alipoteza uvumilivu na kuongeza matamshi yake dhidi ya Ujerumani: (Rais wa Marekani Donald Trump, wakati wa mkutano wake na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, alilalamikia sera ya kibiashara ya Ujerumani, kwa mujibu wa jarida la "Der Spiegel" likiwakariri washiriki wa mkutano huo. Chanzo kimoja kiliambia jarida hilo kuwa Trump alisema: "Wajerumani ni wabaya, wabaya sana. Tazama mamilioni ya magari wanayouza Marekani. Inatisha. Sisi tutazuia hilo"...) (Russia Today, 26/05/2017). Pia (Rais wa Marekani Donald Trump alisema kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa "tuna nakisi kubwa ya kibiashara na Ujerumani, mbali na kwamba wanalipa kidogo sana kuliko wanavyopaswa kwa NATO na jeshi." Aliongeza: "Hii ni mbaya sana kwa Marekani. Na hii itabadilika"...) (DW, 30/05/2017).
4- Mkutano wa NATO ulipoisha, na mkutano wa G7 nchini Italia kushindwa kuhusu masuala ya hali ya hewa, Ujerumani iliharakisha kuilinda Ulaya na kuongoza msimamo wa Ulaya. Kwa mujibu wa kile kilichoripotiwa na Al Jazeera Net 29/05/2017, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, alitoa ukosoaji mkali kwa Rais wa Marekani na kuielezea sera yake kama "ya kutoona mbali" na kwamba Marekani chini ya uongozi wa Trump haina tena nafasi ya uongozi katika jamii ya kimataifa ya Magharibi. Tovuti ya Youm7 29/05/2017 pia ilimkariri waziri huyo wa Ujerumani akisema: ("Hatua za Rais wa Marekani Donald Trump zimedhoofisha Magharibi." Aliongeza kuwa "mtu yeyote anayefanya kazi kuharakisha mabadiliko ya hali ya hewa kupitia kudhoofisha ulinzi wa mazingira, na kuuza silaha zaidi katika maeneo ya migogoro na hataki kutatua migogoro ya kidini kisiasa, anaweka amani barani Ulaya hatarini," akisisitiza kuwa sera za Washington "za kutoona mbali zinaumiza maslahi ya Umoja wa Ulaya.") Matamshi haya ya waziri wa Ujerumani yalikuja siku moja baada ya matamshi mengine ya kushtua ya Kansela wa Ujerumani Merkel (Angela Merkel alitangaza kuwa ameshawishika hatimaye kuwa Ulaya haiwezi tena kuwategemea wengine, akimaanisha Washington ambayo imekuwa ikifanya shinikizo kubwa katika siku za hivi karibuni ili kupata faida kutoka kwa washirika wake. Gazeti la "Bild" la Ujerumani lilimkariri Merkel akisema: "Wakati ule ambao tulikuwa tunawategemea wengine kikamilifu umekwisha. Hilo ndilo nililoligundua katika siku zilizopita... Sisi Wazungu lazima tuchukue mambo yetu mikononi mwetu wenyewe"...) (Russia Today, 28/05/2017).
5- Marekani imeanza kuona "kama uasi" wa Ujerumani dhidi ya Marekani na kwamba Ujerumani inajaribu kuongoza Ulaya katika kuikabili Marekani, hasa kwa kuwa Ujerumani inaongoza misimamo mingi ya Ulaya na inatafuta kujipatia nguvu kama dola ya kimataifa, hata bila kumiliki silaha za nyuklia. Ilikuwa inasubiri fursa ya kuwepo kwa mazingira ya kimataifa yanayoiruhusu kujitokeza. Leo Ujerumani inaona kuwa mazingira ya Ulaya na ulimwengu yanamsaidia kurejesha utukufu wake kwa haraka. Kwa hivyo, unaiona haijali kuongoza nchi za Ulaya katika kukabili sera za Marekani na kukabiliana na Urusi. Ukweli wa mazingira haya mapya na matayarisho ya haraka mbele ya Ujerumani ni kama ifuatavyo:
a- Kuanza kwa mchakato wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit), Ujerumani imejikomboa kutoka katika vile vikwazo vilivyokuwa vimewekwa na ushirika wa Uingereza na Ufaransa juu ya harakati zake za kimataifa kupitia Umoja wa Ulaya. Ilikuwa imenaswa na makubaliano ya Ulaya ambayo mara nyingi yalikuwa yakizitumikia Uingereza na Ufaransa kimataifa...
b- Kuonekana kwa udhaifu katika sera za Marekani, kulikojitokeza wazi kupitia Rais mpya Trump kufuata sera ya "America First" (Marekani Kwanza). Imekuwa rahisi kwa Ujerumani kujikomboa kutoka kwa vikwazo vya Marekani, kwani Ujerumani ilikuwa inafuata Marekani kutokana na maslahi ya pamoja ya Magharibi. Lakini leo, Marekani imeanza kutafuta maslahi yake waziwazi bila kuzingatia maslahi ya pamoja ya washirika wake. Hivyo, Ujerumani imepata visingizio vya kutosha kuunda sera yake yenyewe bila kujali sera ya Marekani. Sera hii ya Trump inatengeneza mazingira kwa nguvu kwa ajili ya kuibuka kwa Ujerumani upya. Ikiwa Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya zilishuhudia jinsi utawala wa Obama ulivyoziondoa kwenye mgogoro wa Syria na kuleta Urusi kutoka mbali kwa ajili hiyo, utawala ule haukujivua kubeba majukumu ya uongozi wake kwa ulimwengu wa Magharibi. Lakini utawala wa Trump leo unajivua waziwazi, na kwa kukosa busara, kutoka kwa washirika wake wa Ulaya, huku jicho lake likiwa limefunguliwa kwenye upande mmoja wa utukufu wake nao ni uchumi wa Marekani na mizigo ya kifedha inayobeba Marekani kwa ajili ya uongozi wake kwa dunia. Huku ni kutoona mbali ambako Marekani imeanza kuteseka nako na kutaacha athari.
c- Mabadiliko ya msingi nchini Ufaransa. Uchaguzi wa hivi karibuni nchini Ufaransa umebaini mabadiliko ya msingi katika maisha ya kisiasa ya Ufaransa. Ushawishi wa vyama vikuu vya mrengo wa kulia na vya kisoshalisti vilivyotawala Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia umedhoofika. Uchaguzi wa hivi karibuni wa 2017 uliwaangusha alama zote za vyama hivyo kikamilifu, na kumleta Rais kijana ambaye hatoki katika chama chochote kikongwe kisiasa... Hii inaishinikiza Ujerumani kuchuana na Ufaransa kwa nguvu katika uongozi wa kisiasa wa Ulaya.
Kwa sababu hiyo, miitikio ya Ujerumani dhidi ya sera za Trump imekuwa ndiyo inayojitokeza zaidi Ulaya, na imekuwa haina hila za uchaguzi. Washindani wa Kansela Merkel katika uchaguzi ujao wamesimama upande wake dhidi ya sera za Marekani (Martin Schulz, kiongozi wa chama cha Social Democratic na mshindani wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, aliwasilisha mpango wa pointi tano kwa ajili ya Ulaya imara katika kukabiliana na Rais wa Marekani Donald Trump. Schulz alisema wakati wa mapokezi yaliyoandaliwa na kundi la wabunge wa chama chake kwa wanauchumi siku ya Jumatano mjini Berlin kuwa: "Ulaya imara ni jambo muhimu kwa amani yetu, ustawi wetu na usalama wetu"...) (Rai Al-Youm, 31/05/2017). Pia (Martin Schulz, mpinzani wa Kansela Angela Merkel, alizitaka demokrasia zote barani Ulaya "kumfahamisha Rais wa Marekani Donald Trump mipaka yake." Schulz alisema Jumatatu usiku mjini Berlin: "Hivyo basi, wajibu wa sasa ni kusimama mbele ya mtu huyu kwa kila tunachowakilisha, na pia dhidi ya sera yake hatari ya silaha anayotaka kutulazimisha") (Arabi21, 29/05/2017).
- Ukweli huu wa Ujerumani anaouona na kuusikia Trump umemfanya aelekeze mashambulizi yake mengi kwa Ujerumani!
Tatu: Kuhusu kile kinachotarajiwa kutokana na mabadiliko haya ya kisiasa ya kimataifa, inaelekea kuwa:
Kupanuka kwa mpasuko kati ya Ulaya na Marekani kutasababisha pengo ambalo si rahisi kuzibika, isipokuwa kama Marekani itarekebisha hali hiyo kabla ya mwisho wa urais wa Trump... Kitu kinachoashiria hili na kulithibitisha ni kujiondoa kwa utawala wa Trump katika Mkataba wa Paris wa Hali ya Hewa tarehe 02/06/2017, ili kuifanya Marekani ijikute mbele ya dhoruba ya ukosoaji kutoka Ulaya iliyoelezea hatua hiyo ya Marekani kama ya makosa na hatari, ikitaka ulimwengu utegemee uongozi wa Ulaya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa (Katika taarifa ya pamoja na ya nadra iliyotolewa jana mjini Roma, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Italia Paolo Gentiloni, walielezea kusikitishwa kwao na uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika Mkataba wa Paris, wakisisitiza wakati huo huo kutowezekana kwa kujadili upya mkataba huo... Na mjini Paris, Macron aliona kuwa Rais wa Marekani amefanya kosa la kihistoria kwa kujiondoa katika mkataba huo... Mapema jana, Kamishna wa Ulaya wa masuala ya hali ya hewa Miguel Arias Cañete alisema kuwa ulimwengu "unaweza kuendelea kuitegemea Ulaya kuongoza mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani," akielezea kusikitishwa kwake kukubwa na "uamuzi wa upande mmoja wa utawala wa Trump") (Al Jazeera Net, 02/06/2017). Mpasuko huu unajumuisha nchi kuu za Ulaya, na karibu hakuna nchi iliyojitenga nao isipokuwa Uingereza ambayo inajipenyeza kama nyoka, na kama kawaida yake kutafuta kushikamana zaidi na Marekani kwa matumaini ya kuwa na nafasi muhimu zaidi duniani.
Mandhari ya Ulaya inaelekea kwenye kujitokeza zaidi kwa uongozi wa Ujerumani katika viwango vya kisiasa na kiuchumi. Kinachoashiria hili na kulithibitisha ni viongozi wa Ujerumani kuwa mstari wa mbele kujibu sera za Marekani, na kutangaza hamu ya Ujerumani ya kuhamishia mzozo na Marekani kuwa wa hadharani... Hii ikienea sana itaitingisha Ulaya kwa kiasi kikubwa, na inaweza kupelekea mwishowe Ujerumani kujiimarisha kijeshi kwa haraka na kwa silaha nzito.
- Na mambo haya mawili yanastahili kuzingatiwa kwa nguvu kwa sababu yatakayotokana nayo yataathiri kuibuka kwa hatua mpya katika siasa za kimataifa na kisha msimamo wa kimataifa.
Nne: Ni jambo la kusikitisha kwamba mabadiliko haya makubwa yanayotokea duniani, na mazingira haya mapya ya kimataifa, yote yanakuja huku kukiwa na kutokuwepo kwa dola ya Kiislamu, Dola ya Khilafah. Hivyo Waislamu hawanufaiki na mazingira haya, wala na mabadiliko hayo. Badala yake, bado kuna kikundi kidogo cha watawala vibaraka katika nchi za Waislamu wanaokesha kuzuia Uislamu usichomoze na kuathiri ulingo wa kimataifa. Zaidi ya hayo, wanakabidhi rasilimali za kiuchumi za Ummah ili kuiokoa Marekani, badala ya kuiangamiza! Lakini hawa na mabwana zao hawatadumu kwa muda mrefu dhidi ya mkondo huu, kwani mchwa wanatafuna bwana wao, na mkondo wa Ummah unaoundwa na watu wenye ikhlasi pamoja na mamilioni ya Waislamu wanaochochewa kuhukumu kwa sheria ya Mola wao na kusimamisha dini yao kupitia Khilafah kwa njia ya Utume, ni mkondo thabiti unaopanda juu na utazaa matunda yake hivi karibuni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu, Mwenye Hikma Aliyesema:
إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا
"Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza jambo Lake. Mwenyezi Mungu amekujaalia kila kitu na kipimo chake." (QS. At-Talaq [65]: 3)
12 Ramadhan 1438 H 07/06/2017 M