Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri"
Kwa Asad Al-Dhahiriya
Swali:
Imetajwa katika kitabu cha Al-Mafahim cha Hizb ut-Tahrir ukurasa wa 35, mstari wa 7 na 9 "Falsafa ya Kiislamu", na jambo linalofahamika kwetu ndani ya Hizb ni kwamba hakuna falsafa wala wanafalsafa katika Uislamu.
Mwenyezi Mungu awalipe kila la kheri.
Jibu:
Imekuja katika kitabu cha Al-Mafahim ukurasa wa 35 yafuatayo:
"Kwa msingi huo, tendo la mwanadamu ni mada inayofanywa na mwanadamu kimada, isipokuwa anapofanya hivyo hutambua mafungamano yake na Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa tendo hili ni halali au haramu. Hivyo basi, hufanya tendo hilo au kuliacha kwa msingi huo. Na huu utambuzi wa mwanadamu juu ya mafungamano yake na Mwenyezi Mungu ndio Ruuh. Na hiyo ndiyo inayomlazimisha mwanadamu kuijua sheria ya Mwenyezi Mungu ili kupambanua vitendo vyake; afahamu kheri kutokana na shari anapojua vitendo vinavyomridhisha Mwenyezi Mungu na vinavyomghadhibisha, na apambanue kibaya kutokana na kizuri pale sheria inapomfanyia bayana tendo zuri na tendo baya, na ili aone tunu zinazohitajika kwa maisha ya Kiislamu katika jamii ya Kiislamu kulingana na vile sheria inavyozielezea. Kwa hili, anaweza anapofanya tendo na kutambua mafungamano yake na Mwenyezi Mungu, kulitekeleza tendo hilo au kuliacha kulingana na utambuzi huo, kwa sababu anajua aina ya tendo, sifa yake na thamani yake. Na kutokana na hapa, falsafa ya Uislamu ilikuwa ni kuchanganya mada na ruuh, yaani kufanya vitendo viongozwe na amri za Mwenyezi Mungu na makatazo Yake. Na falsafa hii ni ya kudumu na ni lazima kwa kila tendo, liwe dogo au kubwa, jepesi au zito. Nayo ndiyo taswira ya maisha. Na kwa kuwa akida ya Kiislamu ndiyo msingi wa maisha, na ndiyo msingi wa falsafa, na ndiyo msingi wa mifumo, basi ustaarabu wa Kiislamu — ambao ni jumla ya dhana (mafahim) kuhusu maisha kwa mtazamo wa Kiislamu — ulijengeka juu ya msingi mmoja wa kiroho, ambao ni akida, na taswira yake kwa maisha ilikuwa ni kuchanganya mada na ruuh, na maana ya furaha kwa mtazamo wake ilikuwa ni radhi za Mwenyezi Mungu."
Naam, hii ndiyo falsafa kwa maana ya Kiislamu (kuchanganya mada na ruuh), yaani utambuzi wa mafungamano na Muumba, hivyo ni istilahi sahihi kwa maana hii...
Ama kuitumia kwa mujibu wa istilahi ya Kiyunani au mfano wake, yaani (utafiti wa yaliyo nje ya kuwepo/vitu vinavyoonekana au yaliyo nje ya mada), jambo hili Uislamu unalikataa. Imekuja katika kitabu cha At-Tafkeer (Fikra) chenyewe katika utangulizi wake ukurasa wa (4), yaani kabla ya yaliyotajwa hapo juu:
"Ubinadamu umepita umbali huu mrefu wa maisha, na umri wa zama, huku ukijishughulisha zaidi na matunda ya akili na matunda ya kufikiri bila ya kujishughulisha na uhalisia wa akili na uhalisia wa kufikiri. Ni kweli kwamba wamepatikana waliojaribu kuelewa uhalisia wa akili miongoni mwa wanachuoni wa Kiislamu na wanachuoni wasio Waislamu, huko nyuma na sasa, lakini walishindwa kuufikia uhalisia huu. Na wamepatikana waliojaribu kuchora njia ya kufikiri, lakini ingawa walifanikiwa katika nyanja fulani za matunda ya njia hii kupitia mafanikio ya kisayansi, lakini walipotoshwa na kutojua kufikiri kwenyewe kama kufikiri, na wakawapotosha wengine miongoni mwa waigaji ambao walishangazwa na mafanikio haya ya kisayansi. Na kabla ya hapo, tangu zama za Wayunani (Gereki) na waliokuja baada yao, walikurupuka katika kufikia kufikiri na wakafikia kile kinachoitwa Mantiki, na wakafanikiwa kufikia baadhi ya fikra, lakini waliharibu maarifa kama maarifa, hivyo mantiki ikawa ni balaa kwa maarifa badala ya kuwa — kama ilivyokusudiwa — njia ya kuyafikia na kipimo cha usahihi wake. Vilevile, hawa waliokurupuka katika kufikia kufikiri, walifikia pia kile kinachoitwa Falsafa, au kile kinachojulikana kama kupenda hekima, na kuzama katika yaliyo nje ya kuwepo (metaphysics), yaani yaliyo nje ya mada, wakaleta utafiti wenye ladha ya maarifa na matokeo, lakini ulikuwa mbali na uhalisia, mbali na ukweli, hivyo ukawaepusha na ukweli na ukawaepusha na uhalisia, ukawapotosha wengi, na ukachezesha kufikiri kutoka kwenye njia ya usawa."
Hivyo basi, kusoma yaliyokuja katika kitabu cha At-Tafkeer kwa utulivu na kwa mazingatio, kutabainisha — Mwenyezi Mungu akipenda — ukweli katika maudhui ya falsafa...
Nikitaraji kuwa maelezo haya yanatosheleza, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
03 Jumada al-Akhirah 1443 H Sawiya na 06/01/2022 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi) kwenye: Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir (Mwenyezi Mungu amuhifadhi): Web