** (Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mkubwa Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")**
Jibu la Swali:
Kwa Abu Qusay
Swali:
As-Salaamu Alaykum ewe Sheikh, Allah arefushe umri wako mpaka uone ushindi ukipatikana kwa idhini ya Allah...
Nina swali kuhusu tofauti kati ya Kheri na Shari, na Husn (Uzuri) na Qubth (Ubaya)? Hii ni kwa sababu mada hii inapojadiliwa, majibu ya vijana huwa yanatofautiana. Tafadhali tufafanulie tofauti kati ya mada hizo mbili, na Allah akubarikie.
Jibu:
Wa Alaykumus Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
A- Husn na Qubth (Uzuri na Ubaya), na Kheri na Shari ni istilahi (maneno ya kitaalamu) kwa wanachuoni wa Misingi ya Fiqhi (Usul al-Fiqh), hivyo maana zake zinaeleweka kama walivyoweza kuziweka na kuzitumia, na si kama maana zake zinavyokuja kilugha. Hii ina maana kwamba, ili ujue maana zake na tofauti iliyopo kati yake, ni lazima uzichukue kutoka kwa wanachuoni wa Usul na si kutoka kwa wanachuoni wa lugha. Kwa hiyo, usifungue kamusi na kutafuta maana ya Husn (uzuri), Qabih (ubaya), Khayr (kheri) na Sharr (shari) kisha ukasema "hizi hapa", bali unatafuta kwa wanachuoni wa Usul ni maana gani waliyoipangia, kisha unachukua maana hiyo.
B- Wanachuoni wa Usul wamemjadili (Al-Hakim) yaani yule anayetoa hukumu juu ya vitendo; ikiwa ni faradhi, mandub (inayopendekezwa), mubah (inayoruhusiwa), makruhu au haramu, na juu ya vitu ikiwa ni halali au haramu? Hii inamaanisha kwa upande wa amri na makatazo yanayofungamana navyo, yaani kwa upande wa sifa (kusifiwa) na lawama (kulaumiwa) kwa ajili ya vitendo hivyo. Kisha, nini kinachotokana na hilo katika suala la thawabu (malipo) au adhabu.
Utafiti huu kutoka upande huu ndio unaoamua kwao Husn na Qabih. Kwa hiyo, kile kilichokuwa kinalingana na amri za Sharia, chenye kusifiwa na kuamriwa, kikawa ni Husn (uzuri) na kina thawabu. Na kile kilichokuwa kinyume na hukumu za Sharia, chenye kulaumiwa na kukatazwa, kikawa ni Qabih (ubaya) na kina adhabu. Kwa sababu hiyo, Husn na Qubth hutumika wakati wa kutoa hukumu juu ya vitendo na vitu kwa upande wa hukumu ya Sharia ni nini, na kwa upande wa kile kinachotokana na hilo katika sifa au lawama, yaani thawabu na adhabu.
Hivyo basi, tunapojadili wizi kwa mfano, kwa upande wa kutoa hukumu juu yake kwamba ni haramu, na kwa upande wa sifa na lawama na kile kinachotokana nalo (thawabu au adhabu) yaani kwamba unahusisha kukatwa mkono au moto wa Jahannam, hapa tunasema wizi ni Qabih (mbaya).
C- Vilevile wanachuoni wa Usul walijadili kipimo ambacho mtu hukipimia madhara ya kitendo hiki kwake au manufaa yake kwake, na kisha mtu kuamua kukifanya kitendo hicho au kuacha kukifanya. Ikiwa watawasilisha kitendo fulani kwenye kipimo cha Uislamu walichokiridhia, na matokeo ya kipimo yakawa ni "manufaa" kulingana na kipimo cha Uislamu, basi hukipenda kitendo hicho na kukifanya na kukiita "Kheri". Na ikiwa matokeo ya kipimo yakawa ni "madhara", hukichukia kitendo hicho na kuacha kukifanya na kukiita "Shari".
Kwa hiyo, wakati wa kufanya utafiti kuhusu wizi kwa mfano, kwa upande wa kipimo cha Uislamu ambacho unakipimia manufaa au madhara yake kwako ili ufanye au uache, basi kinachotumika hapa ni Kheri na Shari.
Hivyo unasema wizi ni Shari kwa sababu katika kipimo cha Uislamu ni madhara, na kwa sababu hiyo huufanyi.
D- Kwa namna hii, unauita wizi kuwa ni Qabih (ubaya) ikiwa mada ya utafiti ni kuhusu kutoa hukumu juu yake yaani uharamu wake, na kwa upande wa thawabu na adhabu yaani kukatwa mkono duniani au moto Akhera.
Na unauita wizi kuwa ni Shari ikiwa mada ya utafiti wako ni kipimo ambacho unakipimia manufaa na madhara, ambapo unaupima kwa mizani ya Uislamu, na si kwa maslahi yako au matamanio yako; hivyo unaukuta ni wenye madhara, unauchukia na kuacha kuufanya, na unauita Shari.
E- Muhtasari:
Ikiwa mada ya utafiti ni kutoa hukumu juu ya kitendo na kitu, na kisha kile kinachotokana nalo katika thawabu au adhabu, basi sifa za Husn na Qubth (Uzuri na Ubaya) ndizo zinazotumika hapa.
Na ikiwa mada ya utafiti ni kipimo unachopimia manufaa na madhara ya kitendo, na kisha kukipenda kwako na kukifanya, au kukichukia kwako na kukiacha, basi sifa za Kheri na Shari ndizo zinazotumika hapa.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir: facebook
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir: Googleplus
Link ya jibu kutoka kwenye ukurasa wa Twitter wa Amir: Twitter
Link ya jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir