(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa Wake wa Facebook)
Kwa Hamid Nasouh
Swali:
Assalamu Alaykum wa Rahmatullahi..
Imetajwa katika kitabu chenu chenye thamani (Taysir al-Wusul ila 'Ilm al-Usul) katika mjadala wa dalili ya 'illah kwamba herufi Fa katika kauli yake Swalla Allahu alayhi wa sallam: "ملكت أمرك فاختاري" inafaidisha ta'lil (utoaji sababu) kwa sababu inaenea na kuvuka (mutadiyyah)... Ama Fa katika kauli yake Allah Mtukufu "... فاجلدوا" yenyewe ni ya kimsababu (sababiyyah) yenye kikomo isiyoenea (ghairu mutadiyyah)...
Na baada ya kutafakari katika yote mawili, sijaweza kubaini tofauti hiyo..
Tafadhali naomba ufafanuzi... Allah awafanikishe katika kusimamisha dini Yake ardhini.. Wasalaam Alaykum.
Jibu:
Wa Alaykum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Kuna herufi katika lugha ambazo hufaidisha ta'lil (utoaji sababu) kupitia uwekaji wake wa kilugha (wad’i), yaani kwa tamko lake (mantuq), kama vile herufi Lam (لـ), na Kay (كي)... Ama kwa upande wa Lam, ni kama kauli yake Allah Mtukufu:
لِئَلاَّ يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ
"Ili watu wasiwe na hoja juu ya Allah baada ya (kuletewa) Mitume." (QS An-Nisa [4]: 165)
Na ama kuhusu Kay, ni kama kauli yake Allah Mtukufu:
كَيْ لا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الأَغْنِيَاءِ مِنْكُمْ
"Ili yasiwe ni mzunguko baina ya matajiri miongoni mwenu." (QS Al-Hashr [59]: 7)
Na kuna herufi ambazo hazifaidishi ta'lil kwa uwekaji wake wa kilugha, yaani kwa tamko lake, bali kwa maana yake inayofahamika (mafhum), yaani kwa lazima ya maana yake. Miongoni mwa herufi hizi ni Fa (الفاء), kwani yenyewe haifaidishi ta'lil kwa tamko lake au kwa uwekaji wake wa kilugha. Waarabu hawakuiweka kwa ajili ya ta'lil, bali inakuja kama kiunganishi cha mkusanyiko (jam’), mpangilio (tartib), upesi (fawr), au kwa ajili ya sababiyyah ya kilugha inayofaidisha ta'lil kupitia mafhum, au kwa ajili ya sababiyyah ya kilugha inayofaidisha sababu (sabab) kupitia mafhum.
Ama kuja kwake kama kiunganishi cha mkusanyiko, mpangilio, au upesi, hakuna utata katika kuifahamu. Lakini tatizo liko katika kuja kwake kwa ajili ya sababiyyah na ufuatano (ta’qib), yaani kinachokuja baada yake kinasababishwa na kilichotangulia kabla yake, au kwa maneno mengine, kinakuwa ni ufuatano wa kilichotangulia. Hapa ndipo utata hutokea katika kubainisha ikiwa imekuja kwa ajili ya sababu (sabab) au kwa ajili ya 'illah, na bila shaka hii ni kwa mujibu wa maana ya kitaalamu katika misingi ya fiqhi (Usul al-Fiqh).
Ili kupambanua kati ya vyote viwili, kuna sifa maalum za 'illah na sifa maalum za sabab. Hivyo, hutazamwa katika maana inayofahamika (mafhum) inayotokana na matumizi ya herufi Fa, yaani lazima ya maana yake; ikiwa sifa za 'illah zitaendana nayo, basi itafaidisha ta'lil, na ikiwa sifa za sabab ndizo zitaendana nayo, basi itafaidisha sababu (sabab) pekee...
Ili tusiingie ndani zaidi katika sifa za 'illah na sabab pamoja na tofauti kati yake – jambo ambalo lina matawi mengi – tutatosheka na tofauti rahisi inayoweza kuchunguzwa kwa makini ili kujua ikiwa herufi Fa imefaidisha ta'lil au sabab kupitia maana yake (mafhum). Tofauti hii ni kuambatana kwa hukumu na suala husika. Ikiwa kuna uambatanaji (musahaba) kati ya suala na hukumu, basi Fa inafaidisha 'illah. Na ikiwa suala liko kabla ya hukumu, yaani limetangulia na halijaambatana nayo, basi Fa inafaidisha sabab.
Kwa mujibu wa hayo, swali lako linaweza kuchambuliwa kuhusu utata wa tofauti kati ya: "ملكت نفسك فاختاري" (Unamiliki nafsi yako, basi chagua), na kati ya:
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ
"Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja katika wao mijeledi mia." (QS An-Nur [24]: 2)
Kabla ya kuanza, nakubainishia maana ya "ملكت نفسك فاختاري". Usemi huu unapatikana katika idadi fulani ya vitabu vya misingi (Usul) kama vile Al-Ihkam fi Usul al-Ahkam cha Al-Amidi, na Fath al-Qadir cha Kamal bin Muhammad maarufu kama Ibn al-Humam... Na hii ni kwa mujibu wa mbinu ya wanazuoni wa Usul kuashiria hadith ya Mtume (saw) alipompa hiyari Barirah ambapo alikuwa ameolewa na mtumwa, na alipoachwa huru akawa muungwana, Mtume (saw) alimpa hiyari ya kuendelea na mumewe au la, kwa sababu alishakuwa huru na hivyo anamiliki hiyari yake. Hadith hii imepokelewa na Bukhari na Muslim.
Bukhari ametoa kutoka kwa Aisha (ra), amesema: "Nilimnunua Barirah... kisha nikamwacha huru, Mtume (saw) akamwita, «فخيّرها من زوجها، فقالت: لو أعطاني كذا وكذا ما ثبتُّ عنده، فاختارت نفسها» (akampa hiyari kuhusu mumewe, akasema: Lau angenipa kadha wa kadha nisingebaki naye, basi akaichagua nafsi yake)". Na Muslim ameitoa kutoka kwa Aisha (ra) kwamba yeye alimnunua Barirah kutoka kwa watu miongoni mwa Ansar... «وخيّرها رسول الله صلى الله عليه وسلم وكان زوجها عبداً» (na Mtume wa Allah saw akampa hiyari na mumewe alikuwa mtumwa). Sasa baada ya kubainika maana ya mfano wa kwanza, na bila shaka mfano wa pili maana yake iko wazi, hebu tutazame mifano hiyo miwili:
Tazama mfano wa kwanza, umepanga hiyari (al-ikhtiyar) juu ya umiliki wa nafsi (malakiyyat an-nafs). Punde tu alipokuwa huru, alimiliki haki ya hiyari katika jambo lake, kwa hiyo inaambatana na hukumu: alikuwa huru akamiliki haki ya hiyari papo hapo. Kwa sababu hiyo, tunasema kuwa herufi Fa hapa imefaidisha ta'lil (utoaji sababu) kwa sababu ya kuambatana kwa hukumu na suala, na hiyo ni miongoni mwa sifa za 'illah.
Ama mfano wa pili, zinaa haiambatani na kupigwa mijeledi bali inatangulia. Kwa ajili hiyo, tunasema kuwa herufi Fa imefaidisha sababu (sabab) kwa sababu suala limetangulia hukumu; kwani zinaa hutangulia kupigwa mijeledi. Na hivi ndivyo ilivyo katika kila sababu. Kwa mfano, hadith iliyotolewa na Al-Bayhaqi katika As-Sunan al-Kubra kutoka kwa Khabbab bin Al-Aratt amesema: "Tulimshtakia Mtume (saw) joto kali la mchanga (wakati wa kuswali), lakini hakutusikiliza na akasema: «إِذَا زَالَتِ الشَّمْسُ فَصَلُّوا» (Jua linapopinduka – kutoka katikati ya mbingu – basi walini)".
Hapa herufi Fa inafaidisha sabab, yaani kupinduka kwa jua ni sababu ya swala, na ni wazi kuwa kupinduka kwa jua kunatangulia swala.
Kwa hiyo, ikiwa itamtatiza mtu maana ya herufi Fa, ikiwa inafaidisha 'illah au sabab kupitia maana yake (mafhum), basi atazame kuambatana kwa hukumu na suala husika. Ikiwa inaambatana nalo, basi ni 'illah, na ikiwa inachelewa baada yake, basi ni sabab. Na bila shaka, hii ni kwa upande wa uamuzi kuhusu maana ya herufi Fa na si kwa aina nyinginezo za 'illah.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu Al-Rashta
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir wa Google Plus