Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jawabu la Swali: Al-Hawl

March 10, 2017
4547

Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jawabu la Swali

Al-Hawl (Mwaka)

Kwa Kareim Siam

Swali:

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Al-Hawl sio Sanah wala Aam (mwaka), kwani inatofautiana nao na muda wake ni miezi 10 na nusu. Huu ndio Hawl kwa mujibu wa kauli yake Ta’ala:

وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا

"Na kubeba mimba kwake na kumwachisha ziwa ni miezi thlathini." (QS. Al-Ahqaf [46]: 15)

Tukiondoa miezi 9 ya ujauzito, inabaki miezi 21, kumaanisha kwamba kila Hawl moja ni miezi 10 na nusu. Kadhalika kauli yake Ta’ala:

يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ

"Mama wawanyonyeshe watoto wao kwa miaka miwili kamili." (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Yaani miezi 21 baada ya kuzaliwa... Hivyo basi, Zaka inatolewa kila baada ya miezi 10 na nusu, na hii inamaanisha kila miaka 7 tunatoa Zaka mara 8.

Jawabu:

Wa Alaykum Salam Warahmatullahi Wabarakatuh...

Inaonekana hukuwa na muda wa kutosha kuanza swali lako kwa salamu ya Kiislamu! Vyovyote iwavyo, haina neno, tumeanza sisi kwa niaba yako katika swali na pia katika jawabu! Je, si bora zaidi kutofanya ubakhili katika salamu ewe Kareim?!

Ilinipitikia mawazoni mwangu nisikujibu kwa sababu mbili: Kwanza, kwamba Al-Hawl kwa maana ya mwaka ni jambo lililothibiti katika lugha na katika Sharia. Pili, wewe huulizi ili ujue jawabu bali unatoa uamuzi wa jawabu kuwa Hawl ni miezi kumi na nusu kisha unajengea juu yake ibada ambayo ni Zaka kama ilivyokuja katika swali!

Lakini baada ya kulitafakari jambo hilo, nimeona nijibu ili swali lako lisisababishe aina fulani ya mkanganyiko kwa baadhi ya watu, hivyo nasema na kwa Mwenyezi Mungu ndio mafanikio:

Kwanza: Al-Hawl katika lugha inamaanisha mwaka (Sanah au Aam). Na kwa sababu ya umaarufu wa maana hii, baadhi ya kamusi huitumia kwa maana ya mwaka bila kuifafanua, kana kwamba ni jambo lililokubalika kuwa na maana ya mwaka! Nakunukulia yaliyokuja katika idadi ya kamusi za lugha zilizotaja maana yake:

  • Lisan al-Arab: (Al-Aam: Ni Al-Hawl, unajumuisha msimu wa baridi na msimu wa joto, na wingi wake ni A’waam).

  • Al-Sahhah Taj al-Lugha wa Sahhah al-Arabiyyah: (Wal-Hawl: Ni mwaka...).

  • Al-Qamus al-Muhit: (Al-Hawl: Ni mwaka, wingi wake ni: Ahwal na Hu’ul na Huwul).

  • Taj al-Arus: (Hawl: Ni mwaka kutokana na kugeuka kwake na mzunguko wa jua katika mawio na machweo yake).

  • Al-Qamus al-Fiqhi: (Al-Hawl: Ni mwaka).

Pili: Na kwa kuwa Qur'ani ni maneno ya Kiarabu yaliyo wazi, basi inafasiriwa kwa lugha ya Kiarabu, na ndiyo maana ilikuja katika tafsiri:

  • Tafsir al-Tabari = Jami' al-Bayan chapa ya Shakir (5/31) Abu Ja'far amesema: Kuhusu kauli yake:

حَوْلَيْنِ

"miaka miwili" (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Inamaanisha miaka miwili (Sanatayn): Muhammad bin Amr aliniambia, akasema Abu Asim alituambia, akasema Isa alituambia, kutoka kwa Ibn Abi Najih, kutoka kwa Mujahid:

وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ

"Na mama wawanyonyeshe watoto wao kwa miaka miwili kamili." (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Yaani miaka miwili.

  • Ma'ani al-Qur'an wa I'rabuhu cha Al-Zajjaj (1/312) Na maana ya:

حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ

"miaka miwili kamili" (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Ni miezi ishirini na minne, kuanzia siku anayozaliwa mpaka siku anayoachishwa ziwa...

  • Tafsir al-Baghawi - Tayyiba (1/277) Kauli yake Ta'ala:

حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ

"miaka miwili kamili" (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Yaani miaka miwili, na akataja neno 'kamili' kwa ajili ya mkazo (ta'kid)...

Tatu: Ama kuhusu uliyoyataja kuhusu aya:

وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا

"Na kubeba mimba kwake na kumwachisha ziwa ni miezi thlathini." (QS. Al-Ahqaf [46]: 15)

Kisha ukasema kwamba ujauzito ni miezi (9) na hivyo basi kumwachisha ziwa ni miezi (21), na ukaichukulia hii miezi (21) kuwa ni miaka miwili (Hawlayn) kama ilivyo katika aya tukufu:

وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ لِمَنْ أَرَادَ أَنْ يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ

"Na mama wawanyonyeshe watoto wao kwa miaka miwili kamili kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha." (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Basi umekosea katika ufahamu na makadirio! Wewe umekisia kuwa muda wa ujauzito ni thabiti miezi tisa na hili ni kosa, kwani muda wa ujauzito unaweza kuwa 9, 8, 7, 6... Ama kilicho thabiti ni Hawl (mwaka mmoja) kuwa ni miezi 12, na kwa sababu hiyo tafsiri ya aya hizi mbili inakuwa hivi:

وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ

"Na mama wawanyonyeshe watoto wao kwa miaka miwili kamili." (QS. Al-Baqarah [2]: 233)

Yaani akina mama wanyonyeshe kwa miaka miwili kamili (miezi 24)... Na aya:

وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا

"Na kubeba mimba kwake na kumwachisha ziwa ni miezi thlathini." (QS. Al-Ahqaf [46]: 15)

Na hii inamaanisha kuwa kiwango cha chini cha ujauzito ni miezi sita kwa sababu ukamilifu wa kunyonyesha yaani utimilifu wake ni (miezi 24), hivyo inabaki kwa kiwango cha chini cha ujauzito (30-24=6 miezi sita)... Na hili ni jambo maarufu kwa mafaqihi hawataofautiana katika hilo.

Nne: Hivyo basi, hukufanya vyema katika ufahamu na makadirio, ukaifanya ile iliyo thabiti (ambayo ni Hawl) kuwa inayobadilika, na ukaifanya inayobadilika (ambayo ni ujauzito) kuwa thabiti! Hivyo ukageuza maana ya aya, na ukaishia kusema kuwa Hawl ni miezi kumi na nusu, nayo ni kauli ambayo si kosa tu, bali ni "uongo/ghalati".

Natumai mada imekuwa wazi... Mwenyezi Mungu akuongoe katika jambo lako lililo bora zaidi.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashta

10 Jumada al-Thani 1438 H Inayosadifiana na 09/03/2017 M

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jawabu kutoka kwa ukurasa wa Amir Web

Share Article

Share this article with your network