Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wageni kwenye ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"
Jibu la Swali
Hukumu ya Kisheria Kuhusu Sherehe za Uchumba Kabla ya Akdi ya Ndoa
Kwa Manar Aljunaidi
Swali:
Assalamu Alaikum,
Swali kuhusu jambo ambalo limeenea sana kwetu, nalo ni kufanya sherehe baada ya kile kinachojulikana kama kusoma Fatiha au posa, ambapo mchumba wa kike huvaa mavazi maalum na kujipamba kama bibi harusi, huvaa pete, hucheza (dansi) na mambo mengine kabla ya kufungwa kwa akdi (ndoa). Je, jambo hili linajuzu kisheria kwa sababu ni kutangaza (ushahidi)? Ikizingatiwa kuwa hapo awali haikuwa inajuzu kuvua hijabu au kujipamba mbele ya mchumba isipokuwa baada ya kufunga akdi. Tufahamisheni, Mungu awafahamishe na akuzidishieni kheri.
Jibu:
Walaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Hairuhusiwi kwa mwanamke kufunua 'awrah yake mbele ya mwanamume mgeni (ajnabi) anayetaka kumuoa mpaka akdi ya ndoa itimie baina yao, kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu (swt):
وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ
"Wala wasionyeshe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao." (QS. An-Nur [24]: 31)
Mwanamume kabla ya akdi ya ndoa si mume (ba'l), hivyo mwanamke hafunui 'awrah yake mbele yake. Ikiwa akdi ya ndoa itakamilika kwa mujibu wa Sharia, mwanamume huyo anakuwa mume wa mwanamke huyo, na wakati huo inaruhusiwa kwake (mwanamke) kufunua 'awrah yake mbele yake kwa sababu amekuwa mke wake kupitia akdi... Ama kabla ya kukamilika kwa akdi, yeye si mume wake, na si sahihi kwake mwanamke kufunua 'awrah yake mbele yake... Kwani kuruhusiwa kwa kufunua 'awrah ni miongoni mwa hukumu zinazotokana na akdi ya ndoa... Na kusoma Fatiha au kutangaza uchumba hakuchukui nafasi ya akdi ya ndoa, na wala hakuna hukumu yoyote ya ndoa inayotokana na uchumba huo... Kwa hivyo, yale yaliyotajwa katika swali kuwa mchumba anafunua 'awrah yake kwa mchumba wake, kujipamba na kucheza (naye au mbele yake) baada ya kusoma Fatiha au posa na kabla ya akdi ya ndoa, basi kufunua 'awrah huku kwa mchumba, kujipamba na kucheza naye ni jambo la haramu...
Tumebainisha katika kitabu cha Mfumo wa Kijamii baadhi ya mambo yanayohusiana na ndoa na akdi ya ndoa, na nakunukulia baadhi ya mambo yenye uhusiano na mada hii:
[Pindi makubaliano yanapofikiwa kati ya mwanamume na mwanamke kuhusu kuoana, basi ni lazima wafanye akdi ya ndoa, kwani ndoa haitimii isipokuwa kwa akdi ya kisheria. Na ndoa hii haiwi ndoa isipokuwa kwa akdi ya kisheria iliyofanyika kulingana na hukumu za Sharia ili iwe halali kwa mmoja wao kufurahia mwenzake, na ili hukumu zinazotokana na ndoa zianze kutumika. Maadamu akdi hii haijafanyika, basi hakuna ndoa...
Ndoa hufungika kwa kutoa na kukubali (Ijab na Qabul) kisheria... Na ili ndoa ifungike (in’iqad), masharti manne yanapaswa kutimia:
Kwanza - Kukusanyika kwa pamoja katika kikao cha kutoa na kukubali (Ijab na Qabul)...
Sharti la pili - Kila mmoja kati ya wafungaji akdi asikie maneno ya mwenzake na ayaelewe...
Sharti la tatu - Kutopingana kati ya kukubali na kutoa, iwe ni katika kutoa kote au sehemu yake.
Sharti la nne - Sheria iwe imeruhusu kuoana kwa mmoja wa wafungaji akdi na mwenzake, kwa kuwa mwanamke awe Mwislamu au mwanamke wa Kitabu (Kitabiyya), na mwanamume awe Mwislamu tu.
Ikiwa akdi imekamilisha masharti haya manne, ndoa inakuwa imefungika. Ikiwa haijakamilisha hata moja kati ya hayo, ndoa haijafungika na inakuwa batili tangu msingi wake. Na ikiwa ndoa imefungika, ni lazima kwa usahihi wa ndoa hiyo kukamilisha masharti ya usahihi (sihha), ambayo ni masharti matatu:
- Mwanamke awe ni mahali halali kwa akdi ya ndoa. (Yaani, kwa mfano, asichanganye kati ya dada wawili).
- Ndoa haisihi bila ya walii, kwani mwanamke hamiliki kujiozesha mwenyewe, wala kumozesha mwingine, na pia hamiliki kumpa uwakala mtu mwingine asiyekuwa walii wake katika kumozesha. Akifanya hivyo, ndoa yake haisihi.
- Kuhudhuria kwa mashahidi wawili Waislamu, watu wazima, wenye akili, wanaosikia maneno ya wafungaji akdi na kuelewa kwamba lengo la maneno yaliyotokea katika kutoa na kukubali ni akdi ya ndoa.
Ikiwa akdi itakamilisha masharti haya, inakuwa sahihi, na ikiwa itakosa sharti moja, inakuwa ndoa batili (fasid). Hata hivyo, haishurutishwi katika akdi ya ndoa kuandikwa, au kusajiliwa katika waraka, bali kupatikana tu kwa kutoa na kukubali kati ya mwanamume na mwanamke kwa matamshi au kwa maandishi kwa kutimiza masharti yote, hufanya akdi ya ndoa kuwa sahihi iwe imeandikwa au la...] Mwisho wa nukuu.
Hivyo basi, ndoa kama ilivyobainishwa katika Mfumo wa Kijamii haiwi isipokuwa kwa kufunga akdi ya kisheria ya ndoa kwa namna iliyotajwa hapo juu. Na kutangaza uchumba hakuchukui nafasi ya akdi ya ndoa, na wala hakusababishi hukumu zinazotokana na akdi ya ndoa, ikiwemo kuruhusiwa kwa mwanamke kufunua 'awrah yake kwa yule aliyefunga naye akdi ya ndoa.
Natumai jambo hili liko wazi, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi na Mwenye Hikima zaidi.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
14 Safar 1443 H Inayoambatana na 21/09/2021 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amiri (Mungu amuhifadhi) kwenye Web