Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Jilbab na Kuishusha Chini na Jinsi Inavyomtofautisha Mwanamke Muungwana na Mjakazi!

September 18, 2018
5418

(Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Kwa Mohamed Abou Youssef

Swali:

Sheikh wetu mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Mwenyezi Mungu akuhifadhi, Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh,

Imekuja katika kitabu cha Mfumo wa Kijamii ukurasa wa 49 yafuatayo: "Na inashartiwa katika Jilbab iwe imeshushwa kwenda chini mpaka ifunike miguu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema katika aya:

يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ

'Wanteremshie shuka zao (jilbab zao) juu yao.' Yaani wanashusha jilbab zao kwa sababu (من) hapa si ya تبعيض (sehemu) bali ni ya بيان (ubainifu), yaani wanashusha shuka na vazi la nje kwenda chini" mwisho wa nukuu.

Hakika aya kwa ukamilifu wake ni kama ifuatavyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاء الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ وَكَانَ اللَّهُ غَفُوراً رَّحِيماً

"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie shuka zao (jilbab zao). Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana (kuwa ni waungwana) wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." (Al-Ahzab: 59)

Ikiwa neno "Idnaa" (kuteremsha) litafasiriwa kama kuishusha (chini), kama ilivyobainishwa hapo juu, basi ukamilifu wa maana unakuwa haueleweki kwangu katika neno lake Mtukufu:

ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ

"Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe." Kwani maana hiyo haikai sawa akilini mwangu pale wanawake wanapotakiwa kushusha jilbab zao chini kwa sababu hiyo ndiyo njia ya wao kutambulika ili wasiudhiwe. Je, kuna uhusiano gani kati ya kuishusha chini na wao kutambulika na hivyo usalama wao dhidi ya kuudhiwa? Na maana zilizopo katika vitabu vya tafsiri kuhusu neno "Idnaa" ni kuhusiana na kifuniko cha kichwa, na inakuwa sababu ya hukumu (ili watambulike wasiudhiwe) kama ilivyobainishwa katika sababu za kushuka kwa aya (Asbab al-Nuzul) kuhusiana na mwanamke muungwana na mjakazi, hapo ndipo maana ya mwanzo wa aya inasandana na mwisho wake.

Tufahamisheni Mwenyezi Mungu awarehemu na niondoleeni utata huu. Wassalamu Alaikum Warahmatullahi.

Jibu:

Walaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

Hakika swali lako ni kuhusu yale yaliyokuja katika Mfumo wa Kijamii kuhusiana na Jilbab na kuishusha kwenda chini na jinsi inavyomtofautisha mwanamke muungwana na mjakazi... Na kabla sijakujibu kuhusu kauli yako katika swali "haikai sawa akilini mwangu", kabla ya hapo nakurejeshea yale yaliyomo katika Mfumo wa Kijamii kuhusu mada hii ukurasa wa 68-70:

(Ama aya ya pili nayo ni kauli yake Mtukufu:

يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ

'Wanteremshie shuka zao (jilbab zao) juu yao.' Kwani hiyo haionyeshi kufunika uso kwa hali yoyote ile, iwe kwa kutamkwa (mantuq) wala kwa kufahamika (mafhum), na hakuna ndani yake neno lolote linaloashiria hilo, si neno moja wala katika muundo wa sentensi, hata kwa kudhania usahihi wa sababu ya kushuka kwa aya. Aya inasema:

يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ

Na maana yake ni wanashusha juu yao jilbab zao, na (من) hapa si kwa ajili ya تبعيض (sehemu) bali ni kwa ajili ya بيان (ubainifu) yaani wanashusha juu yao jilbab zao. Na maana ya 'Adna al-Satr' ni kuushusha, na 'Adna al-Thawb' ni kuushusha, na maana ya 'Yudnina' ni wanashusha. Na Jilbab ni milhafah (shuka kubwa), na kila kinachotumika kusitiri kama nguo na vinginevyo. Au ni vazi linalofunika mwili mzima. Imesemwa katika Al-Qamus al-Muhit: (Jilbab mfano wa sirdab na sinmar: ni kanzu na nguo pana ya mwanamke isiyofikia milhafah, au kile anachofunika kwayo nguo zake kama milhafah). Na Al-Jawhari amesema katika Al-Sahah: (Jilbab ni milhafah na inasemekana ni mula'ah). Na imekuja katika Hadithi: Jilbab ina maana ya mula'ah (shuka) anayoitumia mwanamke kujifunika juu ya nguo zake. Kutoka kwa Um Atiyyah (ra) amesema:

أَمَرَنَا رَسُولُ اللَّهِ ﷺ أَنْ نُخْرِجَهُنَّ فِي الْفِطْرِ وَالأَضْحَى الْعَوَاتِقَ وَالْحُيَّضَ وَذَوَاتِ الْخُدُورِ فَأَمَّا الْحُيَّضُ فَيَعْتَزِلْنَ الصَّلاةَ وَيَشْهَدْنَ الْخَيْرَ وَدَعْوَةَ الْمُسْلِمِينَ قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ إِحْدَانَا لا يَكُونُ لَهَا جِلْبَابٌ قَالَ لِتُلْبِسْهَا أُخْتُهَا مِنْ جِلْبَابِهَا

"Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alituamuru tuwatoe katika (sikukuu ya) Fitr na Adha; wasichana waliovunja ungo, wenye hedhi, na wanawake waliomo ndani ya mapazia. Ama wenye hedhi wajitenge na swala lakini washuhudie kheri na da’wah ya Waislamu. Nikasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, mmoja wetu hana jilbab. Akasema: 'Mwenzake amvike jilbab yake (ya ziada)'." (Imepokelewa na Muslim).

Maana yake ni kuwa hana nguo anayoivaa juu ya nguo zake ili atoke kwayo, akaamuru mwenzake amwazime nguo yake miongoni mwa nguo anazovaa juu ya nguo zake. Hivyo basi maana ya aya ni: Hakika Mwenyezi Mungu alimtaka Mtume awaambie wake zake, binti zake na wanawake wa waumini washushe juu yao nguo zao wanazovaa juu ya nguo nyingine kuelekea chini, kwa dalili ya yale yaliyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba amesema: Jilbab ni ridaa inayofunika kuanzia juu mpaka chini. Basi aya inaashiria kuishusha jilbab - nayo ni nguo pana - kwenda chini, na haionyeshi kingine zaidi ya hapo... Na imekuja maana hii katika kuishusha nguo kwenda chini katika Hadithi tukufu, kutoka kwa Ibn Umar amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema:

مَنْ جَرَّ ثَوْبَهُ خُيَلَاءَ لَمْ يَنْظُرِ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَقَالَتْ أُمُّ سَلَمَةَ فَكَيْفَ يَصْنَعْنَ النِّسَاءُ بِذُيُولِهِنَّ قَالَ يُرْخِينَ شِبْرًا فَقَالَتْ إِذًا تَنْكَشِفُ أَقْدَامُهُنَّ قَالَ فَيُرْخِينَهُ ذِرَاعًا لاَ يَزِدْنَ عَلَيْهِ

"Yeyote anayeburuza nguo yake kwa kibri, Mwenyezi Mungu hatamfanyia muonekano wa rehema Siku ya Kiyama. Ummu Salama akasema: Sasa wanawake wafanyeje na ncha za nguo zao? Akasema: 'Wazishushe kwa shibri moja'. Akasema (Ummu Salama): Basi miguu yao itafunuka. Akasema (Mtume): 'Basi wazishushe kwa dhiraa moja na wasizidishe zaidi ya hapo'." (Imepokelewa na Tirmidhi na akasema hadithi hii ni Hassan Sahih). Mwisho wa nukuu.

Basi Jilbab ni nguo pana kuanzia juu mpaka chini, na hakika "Idnaa" yake ni kuishusha kwenda chini.

Pili: Ama sababu ya kushuka kwa aya (Sabab al-Nuzul), ilikuwa ni kwa ajili ya kuwatofautisha wanawake waungwana na wajakazi. Wajakazi hawakuwa wamefaradhiwa kuvaa Jilbab, na baadhi ya wanafiki walikuwa wakiingilia wajakazi kwa maneno yasiyofaa wakiona kuwa adhabu ya kuwasumbua wajakazi ni ndogo kulinganisha na waungwana. Basi neno hilo linaposikika likielekezwa kwa mwanamke muungwana na kufikishwa mahakamani, (mnafiki) anasema "nilidhani ni mjakazi" ili apate kupunguziwa adhabu... Hivyo aya tukufu ikashuka kukata udhuru wao huu, na ikafaradhia waumini wanawake waungwana wajitofautishe na wajakazi kwa kuvaa Jilbab na kuishusha chini mpaka kwenye miguu, na hivyo wale (wanafiki) wasiweze kusema "tulidhani ni mjakazi", na hapo hawatakuwa na hoja ya kupunguziwa adhabu...

Ametoa Ibn Saad katika Al-Tabaqat kutoka kwa Abi Malik amesema: Wake za Mtume (saw) walikuwa wakitoka usiku kwa ajili ya haja zao, na baadhi ya watu miongoni mwa wanafiki walikuwa wakiingilia kati na kuwaudhi. Jambo hilo likasemwa kwa wanafiki, wakasema: Sisi tunafanya hivyo kwa wajakazi tu. Ndipo ikashuka aya hii:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُلْ لِأَزْواجِكَ وَبَناتِكَ وَنِساءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِنْ جَلابِيبِهِنَّ ذلِكَ أَدْنى أَنْ يُعْرَفْنَ فَلا يُؤْذَيْنَ

"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie shuka zao (jilbab zao). Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe."

Kutokana na hili, wapi kuna kuchanganyikiwa katika kutojua dalili ya kuishusha (Jilbab) chini ili kumtofautisha muungwana na mjakazi? Wewe unasema: (Ikiwa "Idnaa" itafasiriwa kama kuishusha chini, kama ilivyobainishwa hapo juu, basi ukamilifu wa maana unakuwa haueleweki kwangu katika neno lake Mtukufu: "Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe." Kwani maana hiyo haikai sawa akilini mwangu pale wanawake wanapotakiwa kushusha jilbab zao chini kwa sababu hiyo ndiyo njia ya wao kutambulika ili wasiudhiwe, na kuna uhusiano gani kati ya kuishusha chini na wao kutambulika na hivyo usalama wao dhidi ya kuudhiwa, na maana zilizopo katika vitabu vya tafsiri kuhusu neno "Idnaa" ni kuhusiana na kifuniko cha kichwa...)

Basi vipi maana iwe haieleweki kwako? Kwani vazi hili na kuishusha huku ni kwa ajili ya kumtofautisha muungwana na mjakazi, hivyo mnafiki hawezi kumwingilia mwanamke kisha asipewe adhabu anayostahiki kwa kusema "nilidhani ni mjakazi"! Kwa sababu kuvaa kwa mwanamke muungwana Jilbab iliyoshushwa chini kunamtofautisha na mjakazi, kwani mjakazi hakufaradhiwa kuvaa Jilbab hivyo hasitiri mwili wake wote mpaka miguu... Basi kuvaa Jilbab iliyoshushwa chini kwa upande wa mwanamke muungwana kunamtofautisha na mjakazi, na jambo hilo liko katika kiini cha maana ya aya:

ذَلِكَ أَدْنَى أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ

"Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe."

Hivyo basi, maana ya aya ni kutambulika kwa muungwana dhidi ya mjakazi, na kuishusha Jilbab ni kwa ajili ya utambulisho huu "Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe"... Yaani si kwa ajili ya kutambulika kuwa ni fulani bin fulani. Imekuja katika tafsiri ya Al-Qurtubi (14/244): (Kauli yake Mtukufu: "Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe" yaani waungwana, ili wasichanganyike na wajakazi... hivyo tamaa juu yao hukatika. Na maana yake si mwanamke atambulike mpaka ijulikane ni nani yeye).

Natumai kuwa katika haya kuna toshelezo la kufanya maana ikae sawa akilini mwako na kisha kuondoka kwa yale uliyoyataja katika barua yako: "basi haikai sawa akilini mwangu".

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

7 Muharram 1439 Hijria Sawa na 17/09/2018 Miladi

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Facebook: Facebook

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Google Plus: Google Plus

Link ya jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amhifadhi) kwenye Tovuti: Web

Share Article

Share this article with your network