** (Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni Ata bin Khalil Abu al-Rashta, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook)**
Jibu la Swali: Majini na Maumbile ya Uhusiano Kati Yao na Mwanadamu
Kwa Salem Jaradat
Swali:
As-Salaamu Alaykum wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh, Sheikh wangu,
Inafahamika kuwa dalili katika itikadi (Aqidah) ima iwe ni ya kiakili (aqli) au ya kunukuliwa (naqli).
Na imani juu ya majini ilikuwepo kwa sababu ya kuwepo kwa dalili ya kunukuliwa pekee, kutokana na kutokuwepo kwa dalili yoyote ya kimaada inayohisika inayopelekea kuamini kuwepo kwao kiakili.
Swali ni: Je, inafungamana vipi na yaliyotangulia, pale wanachuoni wanaposema kuwepo kwa kupagawa (al-mass) au kuingiliwa na jini (al-talabbus) au muingiliano mwingine wowote wa kimaada kati ya majini na wanadamu?
Na inasihi vipi wao kusema kuwa majini wana uhusiano na husuda na yale yanayoweza kumpata mtu kama vile magonjwa au majanga (kuharibika kwa kazi na kadhalika) pia?
Mwisho, unafasiri vipi aya na hadithi zilizopokelewa kuhusiana na maneno ya "kuguswa" (al-mass) na mfano wake, ikiwa hayatofahamika kama walivyoyafahamu wanachuoni hao?
Jibu:
Wa Alaykumus Salaam wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh.
1- Hakika majini ni miongoni mwa mambo ya ghaibu kwetu, kwani sisi hatuwaoni. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لاَ تَرَوْنَهُمْ
"Hakika yeye na qabila yake wanakuoneni hali nanyi hamuwaoni." (QS al-A'raf [7]: 27)
Yaani Ibilisi na watu wake, na kwa ibara nyingine ni majini, kwani Ibilisi ni miongoni mwa majini:
إِلاَّ إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ
"...isipokuwa Ibilisi; yeye alikuwa miongoni mwa majini." (QS al-Kahf [18]: 50)
2- Hakika asili katika uhusiano wetu nao ni kwamba wao wana uwezo wa kutia wasiwasi (waswasa). Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
فَوَسْوَسَ لَهُمَا الشَّيْطَانُ
"Basi Shetani aliwawatia wasiwasi wote wawili." (QS al-A'raf [7]: 20)
Na amesema:
فَوَسْوَسَ إِلَيْهِ الشَّيْطَانُ
"Lakini Shetani alimvutia wasiwasi." (QS Ta-Ha [20]: 120)
Na shetani hapa ni Ibilisi, naye ni miongoni mwa majini.
3- Mashetani hawana mamlaka ya kulazimisha (sultan jabri) juu ya mwanadamu, isipokuwa mwanadamu amfuate shetani kwa hiari yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
وَقَالَ الشَّيْطَانُ لَمَّا قُضِيَ الأَمْرُ إِنَّ اللَّهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ الْحَقِّ وَوَعَدْتُكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيْكُمْ مِنْ سُلْطَانٍ إِلاَّ أَنْ دَعَوْتُكُمْ فَاسْتَجَبْتُمْ لِي
"Na Shetani atasema itakapokatwa hukumu: 'Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi ya kweli, nami nikakuahidini lakini nikakukhalifuni. Na sikuwa na mamlaka yoyote juu yenu isipokuwa nilikuiteni, nanyi mkanitikia...'" (QS Ibrahim [14]: 22)
Na amesema:
إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلاَّ مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ
"Hakika waja wangu, wewe huna mamlaka juu yao, isipokuwa wale waliokufuata katika wapotovu." (QS al-Hijr [15]: 42)
Na amesema:
فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآَنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ * إِنَّهُ لَيْسَ لَهُ سُلْطَانٌ عَلَى الَّذِينَ آَمَنُوا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ * إِنَّمَا سُلْطَانُهُ عَلَى الَّذِينَ يَتَوَلَّوْنَهُ وَالَّذِينَ هُمْ بِهِ مُشْرِكُونَ
"Na unaposoma Qur'ani, basi omba ulinzi kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya Shetani aliyelaaniwa. Hakika yeye hana mamlaka juu ya wale walioamini na wakamtegemea Mola wao. Mamlaka yake ni juu ya wale wanaomfanya kuwa kiongozi wao, na wale wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu." (QS an-Nahl [16]: 98-100)
4- Uhusiano wowote wa kimaada kinyume na asili hii aliyoibainisha Mwenyezi Mungu unahitaji nukuu (nass) maalum. Ikiwa itapatikana nukuu juu ya hali kama hiyo, basi tutaiamini hali hiyo kulingana na nukuu hiyo.
Kwa mfano, mamlaka ya Suleiman (as) juu ya majini na amri na makatazo yake kwao... jambo hili limekuja na nukuu ndani yake, hivyo tunaliamini. Mwenyezi Mungu anasema katika Surah an-Naml kuhusu Suleiman (as):
قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَنْ يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ * قَالَ عِفْريتٌ مِنَ الْجِنِّ أَنَا آَتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ تَقُومَ مِنْ مَقَامِكَ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ
"(Suleiman) akasema: 'Enyi wakuu! Ni nani kati yenu atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajaja kwangu hali ya kuwa ni Waislamu?' Akasema Ifriti katika majini: 'Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahali pako hapo; nami kwa hakika nina nguvu na mwaminifu juu yake.'" (QS an-Naml [27]: 38-39)
Na amesema:
وَلِسُلَيْمَانَ الرِّيحَ غُدُوُّهَا شَهْرٌ وَرَوَاحُهَا شَهْرٌ وَأَسَلْنَا لَهُ عَيْنَ الْقِطْرِ وَمِنَ الْجِنِّ مَنْ يَعْمَلُ بَيْنَ يَدَيْهِ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَمَنْ يَزِغْ مِنْهُمْ عَنْ أَمْرِنَا نُذِقْهُ مِنْ عَذَابِ السَّعِيرِ * يَعْمَلُونَ لَهُ مَا يَشَاءُ مِنْ مَحَارِيبَ وَتَمَاثِيلَ وَجِفَانٍ كَالْجَوَابِ وَقُدُورٍ رَاسِيَاتٍ اعْمَلُوا آَلَ دَاوُودَ شُكْرًا وَقَلِيلٌ مِنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ
"Na tukamtiiishia Suleiman upepo, asubuhi yake ni mwendo wa mwezi mmoja na jioni yake ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamyayushia chemchemi ya shaba. Na miongoni mwa majini walikuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake; na yeyote miongoni mwao atakayeacha amri yetu, tunamwonjesha adhabu ya Moto. Walikuwa wakimfanyia alichotaka katika majengo ya juu, na sanamu, na mabakuli makubwa kama mahauzi, na masufuria makubwa yasiyoondolewa mahali pake. 'Fanyeni enyi watu wa Daud kwa kushukuru.' Na ni wachache katika waja wangu walio wenye kushukuru." (QS Saba [34]: 12-13)
5- Mtume (saw) alikuwa akishughulikia tukio lolote la kimaada kama sehemu ya miamala ya kibinadamu, maadamu haijakuja nukuu maalum kupitia Wahyi kwamba muamala huo una uhusiano na majini. Matukio yote yako namna hii; kwa mfano, akipatikana mtu aliyeuawa, akili haielekei kuwa majini ndio waliomuua isipokuwa ipatikane nukuu juu ya hilo. Hivyo basi, katika kisa cha mtu aliyeuawa kule Khaybar, uchunguzi ulijikita kwa nani aliyemuua miongoni mwa watu, na haukuelekea kwa majini:
Muslim ametoa katika Sahih yake kuwa Abdullah bin Sahl na Muhayyisah walitoka kuelekea Khaybar kutokana na shida iliyowapata. Kisha Muhayyisah akaja na kutoa habari kuwa Abdullah bin Sahl ameuawa na kutupwa kwenye kisima au shimo. Akawaendea Mayahudi na kusema: "Wallahi ninyi ndio mliomuua." Wakasema: "Wallahi hatukumuua..." Kisha kadhia hiyo ikafika kwa Mtume (saw), na Mtume (saw) akasema: "Ima watoe fidia kwa mwenzenu au watangaze vita." Basi Mtume (saw) akawaandikia barua kuhusu hilo, nao wakaandika: "Wallahi hatukumuua..." Na kisa hicho kinafahamika. Na haikuingia katika uchunguzi wa kadhia hiyo kitendo cha majini, iwe kwa karibu au mbali.
6- Hivyo basi, maadamu hakuna nukuu inayotaja uhusiano wa kimaada wa majini katika tukio fulani, basi uhusiano unabaki kuwa ni wasiwasi pekee kati ya majini na wanadamu na hauvuki hapo.
Kwa kuwa ujumbe wa Mtume (saw) ni mwisho wa risala zote, na Wahyi ulikatika baada yake, hakuna nukuu mpya. Kwa hiyo, hakuna uhusiano wa kimaada kati yetu na majini, bali ni wasiwasi pekee. Na kama tulivyosema, waswasa wa majini hauna mamlaka juu ya mtu isipokuwa mtu huyo akubali waswasa huo kwa hiari yake.
Na hivi ndivyo mambo ya kimaada yalivyokuwa yakishughulikiwa katika zama za Makhalifa Waongofu. Akili haikuwa ikielekea katika tukio lolote la kimaada—iwe ni mauaji, wizi, unyang'anyi au utapeli—kwamba ni majini, bali ilielekea kwa binadamu, kwa sababu uhusiano wa majini ni wasiwasi tu, isipokuwa kama kuna nukuu maalum. Na kwa kuwa hakuna nukuu maalum baada ya Mtume (saw), basi matukio yote ya kimaada yanatokana na binadamu na si kutokana na majini. Ulimwengu wao ni tofauti na wetu, na uhusiano wao nasi ni wasiwasi pekee.
Kulingana na hayo, mwanadamu anapougua, majini hawana uhusiano na jambo hilo, bali ugonjwa hutibiwa kulingana na yale yaliyokuja katika Uislamu, yaani kwa kujitibu:
Iwe dawa hiyo ni ya kimaada, kama ilivyokuja katika hadithi kupitia Usamah bin Sharik aliyesema: Nilimjia Mtume (saw) na maswahaba zake wakiwa kama vile kuna ndege juu ya vichwa vyao (wametulia), nikasalimia kisha nikaketi. Wakaja mabedui kutoka huku na kule na kusema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je, tujitibu?" Akasema:
«تَدَاوَوْا فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ لَمْ يَضَعْ دَاءً إِلاَّ وَضَعَ لَهُ دَوَاءً غَيْرَ دَاءٍ وَاحِدٍ الْهَرَمُ»
"Tibiweni, kwani hakika Mwenyezi Mungu (Azze wa Jalla) hakuweka ugonjwa ila ameweka na dawa yake, isipokuwa ugonjwa mmoja tu; uzee." Yaani isipokuwa mauti. (Imetolewa na Abu Dawud).
Au iwe dawa ni kwa njia ya dua na ruqyah, kama ilivyopokelewa katika hadithi aliyoitoa Muslim kupitia kwa Aisha Mama wa Waumini (ra): "Kwamba Mtume (saw) alikuwa akifanya ruqyah kwa dua hii:
«أَذْهِبْ الْبَاسَ رَبَّ النَّاسِ بِيَدِكَ الشِّفَاءُ لاَ كَاشِفَ لَهُ إِلاَّ أَنْتَ»
'Ondoa madhara, Ewe Mola wa watu, mkononi Mwako kuna shifa (ponyo), hakuna wa kuiondoa (shida) ila Wewe.'" Au mfano wa dua hizo kutoka kwenye Qur'an au Sunnah au dua yoyote inayoafikiana nazo.
Ama kukimbilia kwa wale wanaodai kuwa wana uhusiano wa kimaada na majini kwa ajili ya kumponya mgonjwa, basi huo ni utapeli na ulaghai unaofanywa na madajali hao ambao huwanasa watu wa kawaida ili kuwadhulumu na kula mali zao kwa batili.
7- Ama tafsiri ya aya inayotaja "kuguswa" (al-mass), inaonekana unamaanisha aya ya 275 ya Surah al-Baqarah nayo ni:
﴿الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا﴾
"Wale wanaokula riba hawasimami ila kama anavyosimama yule ambaye Shetani anamvuruga kwa kuguswa (kichaa). Hiyo ni kwa sababu walisema: 'Biashara ni kama riba tu.' Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharimisha riba." (QS al-Baqarah [2]: 275). Na hivi ndivyo inavyofasiriwa:
- Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa yule anayekula riba kama mtu anayevurugika kutokana na kifafa; anasimama na kuanguka, akihangaika katika mwendo wake, kusimama kwake na kukaa kwake, kwani kichaa kimeshamtawala kila upande. Hiyo ni kwa sababu anaichukulia riba kuwa ni kama biashara, hali ya kuwa Mwenyezi Mungu ameharimisha riba na kuhalalisha biashara.
﴿الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا﴾ Yaani wanaichukua, na inajumuisha kila aina ya kunufaika nayo. Neno ﴿يَأْكُلُونَ﴾ (wanakula) limetumika ndani ya Qur'an Tukufu kuashiria kemeo, kama ilivyo katika aya: "Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma, hakika wanakula moto matumboni mwao," na aya: "wanastarehe na wanakula kama wanavyokula wanyama, na Moto ndio makazi yao," na hapa imetumika hivyo pia.
﴿لَا يَقُومُونَ﴾ Yaani siku ya Kiyama.
﴿إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ﴾ Yaani kwamba watafufuliwa kutoka makaburini mwao wakisimama kama anavyosimama mwendawazimu aliyepata kifafa hapa duniani—yaani kichaa—na huo ni udhalilishaji kwao siku hiyo, na ni kielelezo cha katazo kali dhidi ya riba ambalo limekaririwa kusisitizwa uharamu wake katika aya hizi.
﴿مِنَ الْمَسِّ﴾ Yaani kichaa. Inasemekana: "mtu ameguswa" (mussa al-rajul) akimaanisha amepata kichaa. Na al-khabt (kuvurugwa/kupigwa) ni kupiga bila ya mpangilio kama kupiga kwa upofu.
Zimepokewa riwaya katika tafsiri ya ﴿إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ﴾ na yenye nguvu zaidi miongoni mwazo ni kwamba mwanadamu anapopatwa na kichaa, shetani anakuwa na athari kubwa zaidi juu yake kupitia wasiwasi wake, akimfanyia taswira ya mambo mengi yanayompelekea mwendawazimu huyo kuvurugika.
Ama kauli inayosema kuwa shetani ndiye anayemvunja (kumtia kifafa) au kumpelekea kwenye kichaa, basi aya haisemi hivyo. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakusema (يتخبطه الشيطان بالمس) akimaanisha shetani amemsababishia kichaa, bali aya inasema ﴿يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ﴾, yaani shetani anamvuruga kutokana na kichaa chake. Hii ina maana kuwa kichaa kilitangulia kabla ya kuvurugwa na shetani.
Hili ndilo lenye nguvu kwangu katika tafsiri ya aya hii; na inakuwa mfano wa wala riba ni kama mfano wa yule anayevurugwa na shetani kutokana na kichaa. Yaani kichaa kinamtangulia mtu kwa sababu yoyote ile, kisha shetani anamvuruga kwa wasiwasi na taswira zake.
Hivyo, shetani hakumtia mtu kifafa, yaani hakumfanya kuwa mwendawazimu, la sivyo aya ingekuwa (الذي يتخبطه الشيطان بالمس) ambapo herufi Ba ingeashiria ushikamanaji (al-ilsaq), yaani kumfanya awe na kichaa. Na mfano huu ni taswira ya hisia ya kutisha kuelezea ukubwa wa jinai ya wala riba...
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashta
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir kwenye Google Plus