Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

JIBU LA SWALI: Jibu la Kutosha kwa Wale Wanaosema Kwamba Hatulazimiki Kufuata Njia ya Mtume (saw) katika Kufikia Utawala na Kujenga Dola

January 30, 2017
6875

**Bismillahir Rahmanir Rahim**

**Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"**

**Jibu la Swali**

**Kwa Ahmed Abu Eid**

Swali:

Assalam Alaikum... Sheikh wetu.. Je, inawezekana kunipa jibu la kutosha kwa wale wanaosema kwamba hatulazimiki kufuata njia ya Mtume (saw) katika kufikia utawala na kujenga dola...?

Jibu:

Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,

Kwa ufupi, jibu la kutosha ni hili:

1- Mwulize yule anayesema kwamba hatulazimiki kufuata njia ya Mtume (saw) katika kufikia utawala:

Mwambie, ikiwa unataka kutawadha, unatafuta dalili gani ili kujua wudhu? Je, hutafuti dalili za wudhu? Au unatafuta dalili za Hajj kwa mfano? Bila shaka atajibu kuwa anatafuta dalili za wudhu...

Kisha mwulize, na ikiwa unataka kujua hukmu za saumu, je, hutafuti dalili za saumu? Au unatafuta dalili za jihadi ili ujue jinsi ya kufunga? Atajibu kuwa anatafuta dalili za saumu ili ajue hukmu za saumu.

Kisha mwulize, ikiwa unataka kujua hukmu za swala, je, hutafuti dalili za swala? Au unatafuta dalili za zaka? Atajibu kuwa anatafuta dalili za swala.

Na hivi ndivyo ilivyo kwa suala lolote ambalo anataka kujua hukmu zake, atatafuta dalili zake katika sheria.

Sasa, mwulize kuhusu kujua jinsi ya kusimamisha Dola, je, hatafuti dalili za kisheria zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) kuhusu jinsi ya kusimamisha Dola? Hatatafuta dalili za jihadi kwa mfano, au swala, au zaka... bali atatafuta dalili za kusimamisha Dola. Na Mtume (saw) alisimamisha Dola mara moja kwa njia ya kutafuta nusra (Talab an-Nusrah) katika marhala ya maingiliano (marhalat at-tafa’ul). Kwa hivyo, njia ya kusimamisha Dola ni kutafuta nusra.

Na swali sasa ni: je, kutafuta nusra ni fardhi, au ni jambo lililopendekezwa (mandub), au ni halali (mubah)...? Ikiwa kutafuta nusra ni fardhi, basi tutakuwa tumelazimika kufuata njia hii katika kusimamisha Dola. Na kwa kulifanyia utafiti suala hili, tunapata yafuatayo:

Kutafuta nusra ni fardhi, na dalili ya hilo ni kwamba Mtume (saw) hakubadilisha njia hii licha ya mashaka aliyoyapata katika kuitafuta. Aliitafuta kutoka kwa kabila la Thaqif lakini wakamrudisha kwa ubaya na kuyajeruhi miguu yake (saw)... na Mtume wa Allah (saw) hakubadilisha njia hiyo na kufuata njia nyingine, bali aliendelea (saw) kutafuta nusra kutoka kwa makabila mengine; aliitafuta kutoka kwa Bani Shayban, na kutoka kwa Bani Amir... n.k. Aliitafuta zaidi ya mara kumi na kadhaa, na hawakumuitikia, na pamoja na hayo Mtume (saw) hakubadilisha njia hiyo na kufuata njia nyingine licha ya mashaka yaliyokuwemo. Na katika misingi ya kifiqhi (Usul), kukaririwa kwa hitaji pamoja na kuwepo kwa mashaka ni kielelezo (qarinah) kwamba hitaji hilo ni fardhi.

Yaani kutafuta nusra ni fardhi... na kwamba ndiyo njia pekee aliyoifuata Mtume (saw) katika kusimamisha Dola, na akaendelea nayo mpaka Allah alipomkirimu kwa Maansari (wasaidizi), wakampa baia ya pili ya Aqaba, kisha akahajiri kwenda Madina na akasimamisha Dola.

Huu ni ufupisho kwa mwenye moyo au anayegaa sikio naye anashuhudia. Ama wakaidi, hoja yao ni dhaifu kwa sababu kila mmoja wao anakubali kutafuta dalili za wudhu ili atawadhe, na anakubali kutafuta dalili za saumu ili afunge, na anakubali kutafuta dalili za swala ili aswali... na hatafuti dalili za kitendo kingine tofauti na kile anachotaka kukifanya. Wajibu kwake ikiwa ana akili ni kukubali kutafuta dalili za kusimamisha Dola ikiwa anataka kusimamisha Dola. Na hakuna dalili alizozibainisha Mtume (saw) kwa kitendo chake na kauli yake isipokuwa kutafuta nusra (Talab an-Nusrah) ambayo Mtume (saw) aliifanya katika mwisho wa marhala ya maingiliano... na njia hii ni fardhi. Huu kwa ufupi ndio jibu la kutosha na lenye kukidhi juu ya wajibu wa njia tunayofuata katika kusimamisha Dola.

Mwishoni, ninakusalimia, na ninaomba Allah Subhanahu wa Ta'ala akufungulie milango ya kheri kupitia mikono yako.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

02 Jumada al-Ula 1438 Hijria Inayoambatana na 30/01/2017 Miladi

Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka kwa ukurasa wa Amir kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka kwa tovuti ya Amir

Share Article

Share this article with your network