Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Mali Iliyoporwa (Mali ya Ghasbu)

March 09, 2018
5933

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah, Ameer wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Mali Iliyoporwa (Mali ya Ghasbu)

Kwa Fuad Hus

Swali:

Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Sheikh wetu mtukufu:

Kama inavyojulikana, ardhi yote ya Palestina imeporwa na kijidola cha Kiyahudi, na kuna majengo na ardhi nyingi zilizoporwa ambazo wamiliki wake halisi hawajulikani. Baadhi ya ardhi hizi zinamilikishwa na dola ya Kiyahudi kwa watu binafsi au kampuni ili wawekeze katika miradi yao binafsi. Mimi naishi Palestina na nimepewa ofa ya kukodisha jengo (duka) katika jengo linalomilikiwa na Myahudi kwenye ardhi iliyoporwa katika moja ya vijiji vya Palestina, na wamiliki wa ardhi hii hawajulikani, ima ni (wakimbizi au waliofukuzwa makwao).

Je, inajuzu kukodisha jengo hili? Na ikiwa wamiliki halisi wa ardhi hawajulikani, je, hukumu inabadilika? Au inachukuliwa kama ardhi ya ghasbu (iliyoporwa) na haijuzu kuifanyia miamala ya kuuziana, kununua, wala kukodisha?

Barakallahu fikum Sheikh wetu mtukufu, na Mwenyezi Mungu akuzidishie nguvu mwilini na upana katika elimu, na afungue kheri kupitia mikono yako.

Jibu:

Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,

Ewe ndugu yangu, hakika mali iliyoporwa (ghasbu) inabaki kuwa ni mali ya mmiliki wake, hivyo haijuzu kununua wala kukodisha kutoka kwa mporaji. Maelezo yake ni kama ifuatavyo:

Mali iliyoibiwa au iliyoporwa ni ya mmiliki wake popote inapopatikana. Ahmad ametoa hadithi kutoka kwa Samurah, amesema: Mtume wa Allah ﷺ amesema:

إِذَا سُرِقَ مِنَ الرَّجُلِ مَتَاعٌ، أَوْ ضَاعَ لَهُ مَتَاعٌ، فَوَجَدَهُ بِيَدِ رَجُلٍ بِعَيْنِهِ، فَهُوَ أَحَقُّ بِهِ، وَيَرْجِعُ الْمُشْتَرِي عَلَى الْبَائِعِ بِالثَّمَنِ

"Ikiwa mtu ataibiwa bidhaa, au akapotelewa na bidhaa, kisha akaipata mkononi mwa mtu fulani, basi yeye ndiye mwenye haki zaidi nayo, na mnunuzi atarudi kwa muuzaji kudai thamani yake (fedha zake)."

Nass (andiko) hii inaonesha kuwa mali iliyoibiwa ni ya mmiliki wake. Vilevile, Mtume ﷺ anasema:

عَلَى اليَدِ مَا أَخَذَتْ حَتَّى تُؤَدِّيَ

"Mkono unawajibika kwa ulichokichukua mpaka utakapokirudisha." (Imetolewa na At-Tirmidhi na akasema: Hii ni hadithi Hasan). Hii inahusu mali iliyoporwa (ghasbu).

Hivyo basi, yule aliyepora ardhi amefanya jambo la haramu na amefanya dhambi kubwa kwa mujibu wa kauli yake ﷺ:

من ظلم قِيدَ شبرٍ من الأرض طوّقه من سبع أرضين

"Atakayedhulumu (kuchukua kwa dhulma) kiasi cha shibri moja ya ardhi, atavikwa (shingo yake) kutoka ardhi saba." (Imetolewa na Muslim kutoka hadithi ya Aisha r.a).

Maana yake ni kwamba yeyote anayepora kitu chochote katika ardhi, kiwe kidogo au kikubwa, amefanya dhambi ambayo ataadhibiwa kwayo Akhera. Na hapa duniani anastahiki adhabu ya Ta’zir (adhabu ya kisheria inayowekwa na hakimu) na analazimika kurudisha kile alichokipora kwa mmiliki wake, katika hali ile ile aliyoipora kwayo, kwa kauli yake ﷺ:

عَلَى اليَدِ مَا أَخَذَتْ حَتَّى تُؤَدِّيَ

"Mkono unawajibika kwa ulichokichukua mpaka utakapokirudisha." (Imetolewa na At-Tirmidhi).

Ikiwa mali iliyoporwa itaharibika mikononi mwa mporaji, au akabadilisha hali yake—kama vile kushona kitambaa alichokipora, au kuyeyusha madini aliyoyapora, au kuchinja mnyama aliyempora—basi analazimika kumlipa mmiliki wake thamani ya mali hiyo.

Kwa hiyo, ikiwa unajua kuwa kitu fulani kimeibiwa au kimeporwa, basi usikinunue wala usikikodishe. Na ikiwa una shaka pia usikinunue, kwani Mtume ﷺ anasema:

دَعْ مَا يَرِيبُكَ إِلَى مَا لَا يَرِيبُكَ

"Acha kile kinachokutia shaka na ufuate kile kisichokutia shaka." (Imetolewa na At-Tirmidhi kutoka kwa Al-Hasan bin Ali r.a, na At-Tirmidhi akasema: "Hii ni hadithi Hasan Sahih").

Kwa ajili hiyo, madamu una yakini kuwa ardhi hiyo imeporwa—iwe unamjua mmiliki wake au humjui—muhimu ni kuwa una uhakika imeporwa, basi haijuzu kwako kuikodisha kwa sababu mporaji haimiliki ardhi hiyo, na kwa hivyo hawezi kufanya mkataba wowote na wewe.

Hivyo basi, Allah Akutosheleze na kukuepusha na ukodishaji huo, na tafuta jengo lingine la kukodisha, Allah Atakubarikia ndani yake na itakuwa kheri kwako katika dini na dunia. Na hata liweje jengo hilo lililoporwa, usilisikitikie, na Allah yuko pamoja nawe.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu al-Rashtah

20 Jumada al-Akhirah 1439 Hijria Sawa na 08/03/2018 Miladi

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Ameer (Allah amuhifadhi) kwenye Facebook

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Ameer (Allah amuhifadhi) kwenye Google Plus

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Ameer (Allah amuhifadhi) kwenye Twitter

Kiungo cha jibu kutoka ukurasa wa Ameer (Allah amuhifadhi) Web

Share Article

Share this article with your network