Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Baraza la Uasisi la Kampuni za Hisa

January 26, 2023
1990

Mfululizo wa majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizbut Tahrir

kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi"

Jibu la Swali

Baraza la Uasisi la Kampuni za Hisa

Kwa Hamzeh Shihadeh

Swali:

Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Natumai kuwa mko katika afya njema na heri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nina swali kuhusu kampuni za hisa (Joint Stock Companies):

Swali: Kwa nini hatuchukulii baraza la uasisi la kampuni za hisa kuwa ni kama ijab (utoaji ofa) na qabul (ukubali)?

Jibu:

Walaikum Assalam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh.

Hakika kampuni za hisa ni kampuni za mali (sharikat amwal), yaani zinawakilisha mali za washiriki na si nafsi zao. Baraza la uasisi vivyo hivyo linawakilisha mali na si watu; mwenye hisa mbili ana kura mbili, na mwenye hisa kumi ana kura kumi, na kadhalika. Hivyo, kampuni ya hisa ni kampuni ya mali, na aina hii haifungiki katika Uislamu. Kuwepo kwa mshirika wa mwili (sharik al-badan) ni nguzo ya msingi katika kampuni kwa mujibu wa mikataba ya makampuni katika Uislamu, na mali pekee haianzishi mkataba. Kulingana na hili, baraza la uasisi katika kampuni za hisa linawakilisha mali, yaani ni upande mmoja tu, hivyo halianzishi mkataba, na kufuatia hilo hakuna ijab na qabul...

Imeelezwa katika kitabu cha Mfumo wa Kiuchumi (An-Nidham al-Iqtisadi) uk. 162-168 kuhusu kampuni za hisa kwa kina, nitakutajia baadhi ya vipengele:

[Hii ndiyo kampuni ya hisa, na ni miongoni mwa kampuni batili kisheria, na miongoni mwa miamala ambayo haijuzu kwa Mwislamu kuifanya. Ama upande wa ubatili wake na uharamu wa kushiriki ndani yake, unabainika kupitia yafuatayo:

  • Hakika ufafanuzi wa kampuni katika Uislamu ni: mkataba kati ya wawili au zaidi, ambao wanakubaliana kufanya kazi ya kimali kwa lengo la kupata faida. Hivyo ni mkataba kati ya wawili au zaidi, kwa hiyo haisihi kuwepo kwa ridhaa kutoka upande mmoja tu, bali ni lazima ridhaa ipatikane kutoka pande mbili au zaidi...

  • Kisha huweka hati ambayo ni mfumo (sheria) wa kampuni, kisha baada ya hapo inafuatiwa na kutia saini kwenye hati hiyo kwa kila anayetaka kushiriki. Kutia saini kwake pekee kunachukuliwa kuwa ni ukubali (qabul). Wakati huo anachukuliwa kuwa ni muasisi na mshirika. Yaani ushirika wake unakamilika pale anapotia saini, au pale muda wa ununuzi wa hisa (subscription) unapoisha. Hapa ni wazi kwamba hakukujitokeza pande mbili zilizofanya mkataba kwa pamoja, wala hakuna ijab na qabul, bali ni upande mmoja tu unaokubali masharti na kisha kwa ridhaa hiyo anakuwa mshirika. Hivyo kampuni ya hisa si makubaliano kati ya wawili, bali ni ridhaa ya mtu mmoja juu ya masharti. Kwa sababu hiyo, wanauchumi wa mfumo wa kirasilimali na wanasheria wa Magharibi walisema kuwa uwajibikaji ndani yake ni aina fulani ya utendaji wa hiari ya upande mmoja (unilateral will)...

  • Kwa msingi huu, mkataba wa kampuni ya hisa kupitia hiari ya upande mmoja unakuwa ni mkataba batili kisheria; kwa sababu mkataba kisheria ni kufungamana kwa ijab inayotoka kwa mmoja wa wafanya mkataba na qabul ya mwingine, kwa namna ambayo athari yake inaonekana katika kile kinachofanyiwa mkataba. Na mkataba wa kampuni ya hisa haukufikiwa hivyo...

  • Zaidi ya hayo, kampuni katika Uislamu inashartiwa kuwepo kwa mwili (badan), yaani kuwepo kwa mtu mwenye uwezo wa kutenda (at-tasarruf), kwa sababu kinachokusudiwa kwa mwili katika kampuni, uuzaji, upangishaji, na mikataba mingine yote, ni yule mtu anayetenda, na si mwili wa nyama au juhudi za kimwili. Hivyo, kuwepo kwa mwili ni kipengele cha msingi katika kufungika kwa kampuni. Ikiwa mwili upo, kampuni inafungika, na ikiwa mwili haupo katika kampuni, basi kampuni haifungiki na haipo tangu msingi wake. Na kampuni ya hisa haina mwili kabisa, bali inakusudia kuondoa kipengele cha kiutu katika kampuni na haikipi uzito wowote. Kwani mkataba wa kampuni ya hisa ni mkataba kati ya mali pekee, na hakuna kuwepo kwa kipengele cha kiutu ndani yake; mali ndizo zilizoshirikiana zenyewe kwa zenyewe na si wamiliki wake. Mali hizi zimeshirikiana bila kuwepo kwa mshirika wa mwili pamoja nazo. Kukosekana kwa mwili kunaifanya kampuni kutofungika, hivyo ni batili kisheria, kwa sababu mwili ndio unaotenda katika mali, na kwake yeye pekee ndiko kunakoegemezwa utendaji wa mali. Ikiwa mwili haupo, utendaji haupo.

  • Ama kuhusu kuwa watu wamiliki wa mali ndio wanaotekeleza ridhaa ya kuchangia mali, na kuwa wao ndio wanaochagua baraza la usimamizi (board of directors), ambalo linatekeleza kazi katika kampuni, hilo halionyeshi kuwa kuna mwili katika kampuni. Kwani ridhaa yao ilikuwa ni kuifanya mali iwe mshirika, na si wao kuwa washirika. Hivyo mali ndiyo mshirika, na si mmiliki wake. Na ama kuhusu wao kuwa ndio wanaochagua baraza la usimamizi, haina maana kuwa wamewakilisha (kutoa wakala) kwa ajili yao, bali mali zao ndizo zilizowakilishwa na wao, na uwakilishi haukuwa kwa ajili yao binafsi. Ushahidi wa hilo ni kwamba mwanahisa ana kura kulingana na kiasi anachomiliki; anayemiliki hisa moja ana kura moja, yaani uwakilishi (wakala) mmoja, na mwenye hisa elfu moja ana kura elfu moja, yaani mawakala elfu moja. Hivyo uwakilishi unakuwa kwa ajili ya mali na si kwa ajili ya mtu. Hii inaonyesha kuwa kipengele cha mwili kimepotea, na kampuni imeundwa na kipengele cha mali pekee...

  • Kwa hili, mkataba wa kampuni ya hisa kutoka upande huu unakuwa ni batili kisheria, hivyo kampuni ya hisa ni batili, kwa sababu haikufungika kama kampuni, na hailingani na ufafanuzi wa kampuni katika Uislamu.] Unaweza kukamilisha mada hii katika kitabu cha Mfumo wa Kiuchumi, mlango wa Kampuni za Hisa.

Natumai kuwa katika hili kuna ukamilifu wa kubainisha ubatili wa kampuni za hisa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye Hekima zaidi.

Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah

03 Rajab Al-Haram 1444 H Inayoambatana na 25/01/2023 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mwenyezi Mungu amlinde) kwenye Facebook: https://www.facebook.com/HT.AtaabuAlrashtah/posts/731997021821003

Share Article

Share this article with your network