(Silsila ya Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wafuasi wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")
Jibu la Swali kwa: Nadir al-Za'tari
Swali:
Assalamu Alaikum ewe mwanachuoni mtukufu, ningependa kukuuliza swali linalohusu milki ya umma; je, inawezekana kubadilika kutoka milki ya kibinafsi kwenda milki ya umma ndani ya hukumu za kisheria, kama vile kubadilisha vyanzo vya maji kutoka milki ya kibinafsi kwenda milki ya umma ikiwa maslahi ya jamii yatahitajika kwa ajili hiyo? Na ikiwa dharura hiyo itaondoka, je, inarudi katika hali yake ya awali kama milki ya kibinafsi? Na mfano wake ni visima vya mafuta, ikiwa vitakauka, je, inajuzu kuwa milki ya kibinafsi?
Pamoja na shukrani nyingi, na Mwenyezi Mungu akusaidie, akuimarishe na akuongoze hatua zako. Wassalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,
Ikiwa aina yoyote ya milki ya umma imeelezewa kwa sababu (illat), basi hukumu hiyo huzunguka pamoja na sababu hiyo katika kuwepo kwake na kutokuwepo kwake... Ikiwa sababu hiyo ipo, basi aina hiyo ya milki itaendelea kuwa milki ya umma, na ikiwa sababu hiyo itatoweka, inajuzu kumiliki aina hiyo kama milki ya kibinafsi. Lakini kwa sharti kwamba sababu hiyo iwe ya kisheria iliyokuja katika nukuu za kisheria (Nass Shar’i)...
- Kwa mfano, vitu ambavyo ni katika huduma za jamii (marafiqu-l-jama'ah), huhesabiwa kuwa ni milki ya umma. Mtume (saw) amebainisha katika Hadith sifa zake, si idadi yake. Kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume (saw) amesema:
الْمُسْلِمُونَ شُرَكَاءُ فِي ثَلَاثٍ فِي الْمَاءِ وَالْكَلَإِ وَالنَّارِ
"Waislamu ni washirika katika vitu vitatu: maji, malisho, na moto." (Imepokelewa na Abu Dawood, na imepokelewa na Anas kutoka kwa Hadith ya Ibn Abbas na akaongeza ndani yake: "na thamani yake ni haramu"). Na Ibn Majah amepokea kutoka kwa Abu Hurairah kwamba Mtume (saw) amesema: "Vitu vitatu havizuiliwi: maji, malisho, na moto."
Huu ni ushahidi kwamba watu ni washirika katika maji, malisho, na moto, na kwamba mtu binafsi anazuiwa kuvimiliki. Lakini Mtume (saw) aliruhusu maji kule Taif na Khaybar kumilikiwa na watu binafsi, na kwa hakika waliyamiliki kwa ajili ya kumwagilia mimea na bustani zao. Vilevile, baadhi ya Waislamu walimiliki visima kule Madina; Al-Bukhari amepokea kutoka kwa Abdullah (ra), kutoka kwa Mtume (saw) amesema:
مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ يَقْتَطِعُ بِهَا مَالَ امْرِئٍ مُسْلِمٍ، هُوَ عَلَيْهَا فَاجِرٌ، لَقِيَ اللَّهَ وَهُوَ عَلَيْهِ غَضْبَانُ
"Yeyote atakayeapa kiapo ambacho kupitia hicho atajichukulia mali ya mtu Muislamu, naye ni muongo katika kiapo hicho, atakutana na Mwenyezi Mungu huku akiwa amemkasirikia."
Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha:
إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا
"Hakika wale wanaonunua kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao thamani ndogo..." (Surat Al Imran [3]: 77).
Aya hiyo mpaka mwisho. Akaja Al-Ash’ath akasema: "Abu Abdurrahman (Ibn Mas’ud) amewahadithia nini? Kuhusu mimi iliteremshwa Aya hii; nilikuwa na kisima katika ardhi ya binamu yangu, naye Mtume (saw) akaniambia: 'Leta mashahidi wako', nikasema: 'Sina mashahidi', akasema: 'Basi (chukua) kiapo chake', nikasema: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi ataapa', ndipo Mtume (saw) akataja Hadith hii, na Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo kusadikisha hilo." Mwisho.
Hivyo basi, ikiwa ushirika wa maji ungekuwa ni kwa sababu ya maji yenyewe (asili yake), na si kwa sababu ya sifa ya kuhitajiwa kwake, basi asingewaruhusu watu binafsi kuyamiliki. Kutokana na kauli ya Mtume: "Waislamu ni washirika katika vitu vitatu: maji...", na kutokana na yeye (saw) kuwaruhusu watu binafsi kumiliki maji, inatolewa sababu (illat) ya ushirika katika maji, malisho, na moto, nayo ni: kuwa kwake miongoni mwa huduma za jamii (marafiqu-l-jama'ah) ambazo jamii haiwezi kuzikosa. Hivyo Hadith imetaja vitu hivyo vitatu, lakini vimeelezwa kwa sababu; kwa kuwa ni huduma za jamii.
Kutokana na hilo, sababu hii huzunguka pamoja na kile kilichosababishwa nacho katika kuwepo na kutokuwepo kwake. Kila kitu ambacho kimetimia ndani yake kuwa ni miongoni mwa huduma za jamii kinachukuliwa kuwa ni milki ya umma, na kikitopoteza sifa ya kuwa huduma ya jamii, hata kama kilitajwa katika Hadith kama maji, basi hakiwi milki ya umma, bali kinakuwa miongoni mwa vitu vinavyomilikiwa kama milki ya kibinafsi. Kipimo cha kile kinachochukuliwa kuwa huduma ya jamii ni: kila kitu ambacho kisipopatikana kwa jamii—iwe ni kundi la hema, kijiji, mji, au dola—watatawanyika kukitafuta, hicho huhesabiwa kuwa huduma ya jamii, kama vile vyanzo vya maji, misitu ya kuni, malisho ya wanyama, na mfano wa hivyo.
- Kwa mfano madini, huwa ni milki ya umma ikiwa yanapatikana kwa kiasi kisicho na mwisho, kama migodi na mfano wake. Madini haya yanakuwa ni milki ya umma, na haijuzu kumilikiwa kibinafsi kwa sababu At-Tirmidhi amepokea kutoka kwa Abyadh bin Hammal: "Kwamba alikuja kwa Mtume (saw) na akamuomba amgaie chumvi (mgodi), naye akamgaia. Alipoondoka, mtu mmoja katika kikao akasema: 'Je, unajua ulichomgaia? Hakika umemgaia maji ya idd (maji yasiyokatika).' Akasema: 'Basi akamnyang'anya (akauondoa kwake).'" Na maji ya idd ni yale yasiyokatika. Alifananisha chumvi na maji ya idd kwa sababu ya kutokatika kwake. Hadith hii inaonyesha kuwa Mtume (saw) alimgaia chumvi ya mlimani Abyadh bin Hammal, lakini Mtume (saw) alipojua kuwa ni madini ya kudumu yasiyokatika, alirudi nyuma kutoka katika ule ugawaji wake na akachukua, na akazuia milki ya mtu binafsi juu yake, yaani akaufanya kuwa milki ya umma. Na hapa haikusudiwi chumvi pekee, bali kinachokusudiwa ni madini. Kutokana na Hadith hii, inabainika kuwa sababu ya kuzuia kutoa mgodi wa chumvi ni kuwa kwake "idd", yaani haukatiki.
Hukumu hii—ambayo ni kuwa madini yasiyokatika ni milki ya umma—inajumuisha madini yote, yawe madini ya dhahiri (yaliyo juu) yanayofikiwa bila gharama kubwa na watu wanayatumia, kama chumvi, wanja (kohl), yakuti, na mfano wake, au yawe ni madini ya ndani (yaliyo chini) ambayo hayafikiwi isipokuwa kwa kazi na gharama, kama madini ya dhahabu, fedha, chuma, shaba, risasi, na mengineyo. Na iwe ni madini magumu kama fuwele au majimaji kama mafuta (petroli), yote hayo ni madini yanayoingia chini ya Hadith hii. Kwa kuwa madini yasiyokatika ni milki ya umma kwa raia wote, basi haijuzu kwa dola kuwamilikisha watu binafsi au makampuni, wala kuwaruhusu watu binafsi au makampuni kuyachimba kwa ajili yao wenyewe, bali ni lazima dola yenyewe isimamie uchimbaji wa madini haya kwa niaba ya Waislamu na kwa ajili ya kusimamia mambo yao, na kila kinachochimbwa kinakuwa ni milki ya umma kwa raia wote.
Kwa hiyo, vitu vilivyotajwa katika swali vitakuwa milki ya umma ikiwa ni miongoni mwa huduma za jamii. Kwa mfano, kisima cha maji katika kijiji ambacho hakina chanzo kingine cha maji isipokuwa hicho, basi kisima hicho kinakuwa milki ya umma na haijuzu kumilikiwa kibinafsi... Ikiwa maji yatapatikana kwa watu kwa njia nyingine mbali na kisima hicho kwa kiasi cha kutosha, basi inajuzu kwa mtu yeyote kuchimba kisima katika ardhi yake na kukimiliki kwa sababu hakingekuwa miongoni mwa huduma za jamii katika hali hiyo, yaani sababu ya kuwa kwake milki ya umma imetoweka... Lakini kisima ambacho kilikuwa milki ya umma hakiwi milki ya kibinafsi (kiasili), bali kinabaki kuwa milki ya umma na inajuzu kukiuzia watu binafsi ikiwa maji yamepatikana kwa kiasi cha kutosha kwa watu, na hapo thamani yake (fedha za mauzo) huwekwa katika mlango wa milki ya umma.
Hali kadhalika chanzo cha maji (spring), ni milki ya umma ikiwa jamii haiwezi kukikosa. Ikiwa kitakauka au jamii itaanza kutokitegemea (kukikosa), yaani sababu ya kuwa huduma ya jamii imetoweka kama vile maji kupatikana kwa watu kwa kiasi cha kutosha, basi hapo inajuzu kuuza chanzo hicho kwa watu binafsi na kuweka thamani yake katika mlango wa milki ya umma.
Na kwa mfano visima vya mafuta, ni milki ya umma madamu ni "idd" isiyokatika. Ikiwa vitakauka, yaani sababu ya kuwa milki ya umma imetoweka, basi inajuzu kuuza kisima hiki kwa watu binafsi na hapo thamani yake huwekwa katika mlango wa milki ya umma.
Ndugu yenu, Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir:
![]()
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir:
![]()
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Twitter wa Amir:
![]()
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir