(Silsila ya majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fiqhi")
Kwa Abu Husam
Swali:
Assalamu Alaikum wa Rahmatullahi wa Barakatuh... Naomba ufafanuzi kuhusu suala la Mtume (saw) kuwavua washirikina wa Kiarabu (kuwatenga) na wale aliowakubalia katika makafiri wa Yemen kubaki katika dini yao. Je, tunachukulia uvuaji huu (exception) kwa haki ya washirikina wa Kiarabu kama kizuizi cha ujumla (qayid lil-umum) uliokuja katika kitabu cha Ad-Dawlah al-Islamiyyah chapa ya 7 ukurasa wa 144: "Na makundi mawili ya mwisho wanaachiwa na yale wanayoamini na wanayoyaabudu..." na makundi hayo mawili ni: Ahlul Kitab na washirikina? Na kadhalika, je, ni kizuizi kwa yale yaliyokuja katika mradi wa Katiba Ibara ya 27 aya ya (b)? Au uvuaji huu ni maalum kwa kizazi kile pekee? Na nataka kuongeza swali jingine kuhusiana na yaliyokuja katika kitabu cha Ad-Dawlah al-Islamiyyah chapa ya 7 ukurasa wa 144: "Dola inawawekea jaji miongoni mwao atakayeangalia migogoro yao katika mahakama za Dola", na pia katika kitabu hicho hicho ukurasa wa 146 aya ya (d): "...kutoka kwa majaji miongoni mwao katika mahakama za Dola na si katika mahakama maalum". Tunaomba ufafanuzi wa namna ya kazi ya majaji hawa na hali yao? Ikijulikana kuwa nimefanya utafiti kuhusu hilo katika Utangulizi wa Katiba kabla ya kuwapandishia swali langu lakini sikupata jibu. (Yaani, je inajuzu kwa mahakama ya Dola kutoa hukumu mbili? Hukumu kwa Uislamu na hukumu nyingine kwa yasiyokuwa Uislamu?) Na kwenu kuna shukrani za dhati. Ndugu yenu Abu Bilal.
Jibu:
Wa Alaikum Salaam wa Rahmatullahi wa Barakatuh,
Maswali yako mawili yanahusu nukuu ifuatayo kutoka katika kitabu cha Ad-Dawlah al-Islamiyyah ukurasa wa 146:
(...Hii ni kwa upande wa Waislamu. Ama wasio Waislamu ambao wanafuata itikadi isiyokuwa itikadi ya Kiislamu, wao ni:
4- Washirikina nao ni waabudu masanamu, Masabai, Majusi, Wahindu na wote ambao si miongoni mwa Ahlul Kitab.
Na makundi mawili ya mwisho wanaachiwa na yale wanayoamini na wanayoyaabudu, na wanaenenda katika masuala ya ndoa na talaka kulingana na dini zao, na Dola inawawekea jaji miongoni mwao atakayeangalia migogoro yao hii katika mahakama za Dola, ama vyakula na mavazi, wao hufanyiwa muamala kulingana na hukumu za dini zao ndani ya mfumo mkuu (yaani ndani ya kile kinachoruhusiwa na sheria ya Uislamu). Wasio Ahlul Kitab hufanyiwa muamala kama ule wa Ahlul Kitab, Mtume (saw) alisema kuhusu Majusi:
«سنوا بهم سنة أهل الكتاب»
"Watendeeni kama mnavyowatendea Ahlul Kitab."
Ama miamala na adhabu, hizo hutekelezwa kwa wasio Waislamu kama zinavyotekelezwa kwa Waislamu sawasawa. Adhabu husimamiwa kwa wasio Waislamu kama zinavyosimamiwa kwa Waislamu, na miamala ya wasio Waislamu hutekelezwa na kuvunjwa kama inavyotekelezwa na kuvunjwa miamala ya Waislamu sawasawa, bila ubaguzi au upendeleo kati ya mtu mmoja na mwingine...)
Na katika kitabu hicho hicho ukurasa wa 147:
(Na muhtasari wake ni kwamba Dola katika siasa yake ya ndani inatekeleza Sheria ya Kiislamu kwa wote wanaobeba uraia, wawe ni Waislamu au wasio Waislamu, na utekelezaji wake unakuwa kwa namna ifuatayo:
d - Masuala ya ndoa na talaka kati ya wasio Waislamu huamuliwa kulingana na dini zao kutoka kwa majaji miongoni mwao katika mahakama za Dola na si katika mahakama maalum, na masuala haya kati yao na Waislamu huamuliwa kulingana na hukumu za Kiislamu kutoka kwa majaji Waislamu...) Mwisho.
Vilevile yale yaliyokuja katika Ibara ya saba kifungu (b):
(Ibara ya 7 - Dola inatekeleza Sheria ya Kiislamu kwa wote wanaobeba uraia wa Kiislamu, wawe ni Waislamu au wasio Waislamu kwa namna ifuatayo: b - Wasio Waislamu wanaachiwa na yale wanayoamini na wanayoyaabudu ndani ya mfumo mkuu) Mwisho.
Jibu la swali lako la kwanza:
Hakukusudiwi hapa kwa washirikina wale washirikina wa Kiarabu, bali inakusudiwa waabudu masanamu wasio Waarabu kama baadhi ya makabila ya Kiafrika. Na hawa hawalazimishwi kuacha dini zao, na Dola inawafanyia muamala kama wa Ahlul Kitab isipokuwa tu hailiwi vichinjwa vyao wala hawaolewi wanawake wao... Ama washirikina wa Kiarabu waabudu masanamu, hukumu ya kisheria kwao ilikuwa ni hiari kati ya Uislamu au kuuawa, na hawa hajapaki hata mmoja wao katika zama zetu hizi, bali walimalizika katika zama za Maswahaba (ra). Yule ambaye hakusilimu miongoni mwao wakati huo, Waislamu walimpiga vita. Na tumebainisha hukumu zao katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Pili kama ifuatavyo:
"Ama washirikina wa Kiarabu, haikubaliwi kutoka kwao suluhu wala dhima (ulinzi), lakini wanalinganiwa kwenye Uislamu; wakisilimu wanaachiwa, na wasiposilitu wanapiganwa. Allah (swt) amesema:
سَتُدْعَوْنَ إِلَى قَوْمٍ أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ تُقَاتِلُونَهُمْ أَوْ يُسْلِمُونَ
"Mtaitwa kwa watu wenye nguvu nyingi; mtapigana nao au wasilimu." (QS. Al-Fath [48]: 16)
Maana yake ni mpaka wasilimu. Na aya hii inahusu wale ambao Mtume wa Allah (saw) alikuwa akiwapiga vita nao ni waabudu masanamu miongoni mwa Waarabu. Hii inaonesha kuwa wanapiganwa ikiwa hawajasilimu. Na imepokelewa pia kupitia njia ya Al-Hasan akisema: "Mtume wa Allah (saw) aliamrisha Waarabu wapiganwe juu ya Uislamu, na kisikubaliwe kwao kingine chochote, na akaamrisha wapiganwe Ahlul Kitab mpaka watoe Jizya kwa mikono yao huku wakiwa wadogo." Abu Ubayd amesema: Na tunaona kuwa Al-Hasan alikusudia kwa Waarabu hapa ni waabudu masanamu miongoni mwao ambao si Ahlul Kitab. Ama wale waliokuwa miongoni mwa Ahlul Kitab, Mtume wa Allah (saw) aliikubali (Jizya) kutoka kwao na hilo liko wazi katika hadith. Na haijathibiti kuwa Mtume (saw) alichukua Jizya kutoka kwa yeyote katika waabudu masanamu miongoni mwa Waarabu, na hakukubali kutoka kwao baada ya kushuka aya ya Ushindi (Fath) na Surat At-Tawbah isipokuwa Uislamu au vita. Na yale yaliyopokelewa kuwa alichukua Jizya kutoka kwa Waarabu kama watu wa Yemen na watu wa Najran, hakika aliichukua kutoka kwa Ahlul Kitab; Wakristo na Mayahudi, na hakuichukua kutoka kwa waabudu masanamu miongoni mwa Waarabu." Mwisho.
Jibu la swali lako la pili:
Ama yale yaliyokuja katika nukuu iliyotajwa kusema: "...na Dola inawawekea jaji miongoni mwao atakayeangalia migogoro yao hii katika mahakama za Dola...", na kusema kwake: "Masuala ya ndoa na talaka kati ya wasio Waislamu huamuliwa kulingana na dini zao kutoka kwa majaji miongoni mwao katika mahakama za Dola na si katika mahakama maalum...", haimaanishi kuwa majaji Waislamu ndio wanaohukumu kati yao kulingana na sheria zao. Bali maana yake ni kwamba hukumu kati yao inakuwa kutoka kwa majaji miongoni mwao, yaani kutoka kwa wasio Waislamu. Lakini majaji hawa hawatengewi mahakama maalum (za kando), bali wanakuwa na vyumba vya kutoa hukumu ndani ya majengo ya mahakama za Dola na wanakuwa ni wenye kufuata mahakama za Dola upande wa kiidara. Na suala la kuteua majaji haliachiwi kwao, bali linakuwa kwa utaratibu wa Dola. Dola ndiyo inayowateulia majaji miongoni mwao wanaohukumu kati yao katika masuala ya ndoa, talaka na yanayoambatana nayo. Na hii haimaanishi kuwa mahakama za Dola zinahukumu kwa hukumu mbili: hukumu ya Kiislamu na hukumu isiyo ya Kiislamu, bali mahakama za Dola zinahukumu kwa Uislamu pekee. Lakini ndani yake huwekwa vyumba vinavyofuata mahakama hizo kiidara ambavyo ndani yake wanahukumu majaji wasio Waislamu katika migogoro inayozuka kati ya wasio Waislamu katika masuala ya ndoa, talaka na viambatanisho vyake, kulingana na dini zao na sheria zao, kama ilivyothibitishwa na Sheria (Sharia).
Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Google Plus wa Amir