Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Al-Qadha wal-Qadar

August 22, 2022
2798

Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir, kwa maswali ya wafuasi wa ukurasa wake wa Facebook "Fikri"

Jibu la Swali

Al-Qadha wal-Qadar

Kwa Mohammad Taher Hamidi

Swali:

Bismillahir Rahmanir Rahim

Kutoka Afghanistan kwenda kwa Amir wetu mfadhili!

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh

Namuomba Allah (swt) akupe afya na usalama, na tunamuomba Yeye (swt) atuharakishie ufunguzi, nusra, na kutawazwa. Amir wetu mfadhili! Katika siku hizi nilikuwa nikisoma kitabu Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah, nikakutana na maoni kuhusu suala la Al-Qadar ambayo ni tofauti na yale niliyoyakuta katika kitabu Nidhamu ya Uislamu. Nanukuu kauli hizi mbili kutoka kwenye vitabu hivi viwili, ili utufafanulie sababu ya tofauti hii, ikiwa ni tofauti kama nilivyoelewa.

Sheikh Taqiuddin an-Nabhani – Allah amrehemu – amesema katika kitabu Nidhamu ya Uislamu kwenye ukurasa wa 19, chapa ya sita, baada ya kuelezea sifa za mwanadamu: "Sifa hizi maalum ambazo Allah (swt) amezileta katika vitu, silika (ghariza), na mahitaji ya kiorganiki yaliyo ndani ya mwanadamu, ndizo zinazoitwa Al-Qadar. Kwa sababu Allah peke yake ndiye aliyeumba vitu, silika, na mahitaji ya kiorganiki, na akapima (qaddara) ndani yake sifa zake; sifa hizo hazitokani na vitu vyenyewe, na mwanadamu hana mamlaka nazo wala athari yoyote juu yake."

Kisha akaelezea Al-Qadar katika kitabu Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah, Sehemu ya Kwanza, ukurasa wa 31, chapa ya sita, ambapo amesema: "Na Al-Qadar ni sifa ambayo mwanadamu anaisababisha (yuhdithu) katika kitu, kama vile kuungua kuliko katika moto, na kukata kuliko katika kisu."

Je, hakuna tofauti katika kauli hizi mbili; kuhusu nani aliyeleta na kusababisha sifa hizo katika vitu na mwanadamu? Ni nini kinachokusudiwa na yale yaliyokuja katika kitabu Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah? Je, neno (kusababisha/kuleta – yuhdithu) linamaanisha kitu kingine mbali na kuumba na kuanzisha? Ikiwa utatutolea ufafanuzi katika kile tulichokiona kuwa ni mgongano na kupingana; utaondoa wasiwasi vifuani mwetu.

Allah akulipe kheri kwa ajili yetu na akulinde na kila shari na jambo baya.

Jibu:

Walaikum Assalam Warahmatullahi Wabarakatuh.

Kwanza: Imekuja katika Nidhamu ya Uislamu - Mlango wa Al-Qadha wal-Qadar, uk. 18-19:

[Ama Al-Qadar, ni kwamba matendo yanayotokea, iwe ni katika mzunguko unaomtawala mwanadamu, au katika mzunguko anaoutawala mwanadamu, yanatokea kutokana na vitu na juu ya vitu vinavyotokana na maada ya ulimwengu, mwanadamu na uhai. Allah ameviumbia vitu hivi sifa (khawas-iswa) maalum. Akaumba katika moto sifa ya kuunguza, na katika mbao sifa ya kuungua, na katika kisu sifa ya kukata, na akazifanya sifa hizi kuwa ni zenye kuandamana navyo (lazima) kulingana na mfumo wa kuwepo kwake na hazibadiliki. Na inapoonekana kuwa zimebadilika, basi Allah anakuwa ameziondoa sifa hizo, na hilo linakuwa ni jambo lisilo la kawaida (khariqan lil-adat), ambalo hutokea kwa Mitume na huwa ni muujiza kwao. Na kama vile alivyoumba sifa katika vitu, vivyo hivyo ameviumba silika (ghariza) na mahitaji ya kiorganiki katika mwanadamu, na akaweka ndani yake sifa maalum kama sifa za vitu. Akaumba katika silika ya aina (gharizat an-naw’) sifa ya mvuto wa kijinsia, na katika mahitaji ya kiorganiki sifa kama vile njaa na kiu na mfano wake, na akazifanya kuwa ni zenye kuandamana nayo kulingana na kanuni ya kuwepo kwake. Hivyo basi, sifa hizi maalum ambazo Allah (swt) amezileta katika vitu, silika, na mahitaji ya kiorganiki yaliyo ndani ya mwanadamu ndizo zinazoitwa Al-Qadar. Kwa sababu Allah peke yake ndiye aliyeumba vitu, silika, na mahitaji ya kiorganiki, na akapima ndani yake sifa zake; sifa hizo hazitokani na vitu vyenyewe, na mwanadamu hana mamlaka nazo wala athari yoyote juu yake. Na ni juu ya mwanadamu kuamini kuwa aliyepima sifa hizi katika vitu hivi ni Allah (swt). Na sifa hizi zina uwezo wa kumfanya mwanadamu azitumie kufanya kitendo kulingana na amri za Allah na kikawa ni kheri, au akahalifu amri za Allah na kikawa ni shari; iwe ni katika kutumia vitu kwa sifa zake, au katika kuitikia silika na mahitaji ya kiorganiki. Inakuwa kheri ikiwa ni kulingana na amri na makatazo ya Allah, na shari ikiwa inapingana na amri na makatazo ya Allah.

Kutokana na hapa, matendo yanayotokea katika mzunguko unaomtawala mwanadamu yanatoka kwa Allah, yawe ni kheri au shari. Na sifa zilizopatikana katika vitu, silika, na mahitaji ya kiorganiki zinatoka kwa Allah, ziwe zimeleta kheri au shari. Kutokana na hapa, ni lazima kwa Muislamu kuamini Al-Qadha kheri yake na shari yake inatoka kwa Allah (swt), yaani aamini kuwa matendo yaliyo nje ya uwezo wake yanatoka kwa Allah. Na aamini Al-Qadar kheri yake na shari yake inatoka kwa Allah (swt), yaani aamini kuwa sifa za vitu zilizopo katika tabia zao zinatoka kwa Allah (swt), iwe zimezalisha kheri au shari, na mwanadamu kiumbe hana athari yoyote ndani yake. Hivyo, ajali ya mwanadamu, riziki yake na nafsi yake, yote hayo yanatoka kwa Allah. Kadhalika, mvuto wa kijinsia na mvuto wa kumiliki vilivyomo katika silika za aina na kujilinda, na njaa na kiu vilivyomo katika mahitaji ya kiorganiki, vyote vinatoka kwa Allah (swt)...]

Yaani Al-Qadar katika istilahi ya (Al-Qadha wal-Qadar) ni sifa za vitu ambazo Allah ameziumba ndani yake...

Pili: Na imekuja katika kitabu Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Sehemu ya Kwanza - Mlango wa Aqida ya Kiislamu, uk. 32-33:

[.... Ama Al-Qadha wal-Qadar, dalili yake ni ya kiakili kwa sababu Al-Qadha inahusiana na mambo mawili: Kwanza, kile kinachohitajika na mfumo wa kuwepo kwa ulimwengu, na hili dalili yake ni ya kiakili kwa sababu linahusiana na Muumba. Jambo la pili ni kitendo cha mwanadamu kinachotokea kwake au juu yake kwa lazima, nalo ni jambo linalohisiwa ambalo hisi hulitambua, hivyo dalili yake ni ya kiakili. Na Al-Qadar ni sifa ambayo mwanadamu anaisababisha (yuhdithu) katika kitu, kama vile kuungua kuliko katika moto, na kukata kuliko katika kisu. Na sifa hii ni jambo linalohisiwa ambalo hisi hulitambua, hivyo basi dalili ya Al-Qadar ni ya kiakili...]

Yaani Al-Qadar katika istilahi ya (Al-Qadha wal-Qadar) ni sifa za vitu ambazo mwanadamu anazisababisha ndani yake...

Tatu: Vile vile imekuja katika kitabu hicho hicho Ash-Shakhsiyyah Sehemu ya Kwanza - Mlango wa Al-Qadha wal-Qadar, uk. 94-99:

[Na maana ya Al-Qadha wal-Qadar, au kwa maneno mengine suala la Al-Qadha wal-Qadar, ni matendo ya waja na sifa za vitu. Hiyo ni kwa sababu suala lililoelezwa ni matendo ya mja na kinachotokana na matendo haya, yaani sifa ambazo mja anazisababisha katika vitu; je, sifa hizo ni kutokana na uumbaji wa Allah, yaani Yeye ndiye aliyeziumba na kuzileta? Ama ni kutokana na mja, yaani mja ndiye aliyeziumba na kuzileta?...

Ama Al-Qadar, ni kwamba matendo yanayotokea, yawe katika mzunguko unaomtawala mwanadamu au mzunguko anaoutawala, yanatokea kutokana na vitu na juu ya vitu vya maada ya ulimwengu, mwanadamu na uhai, hivyo kitendo hiki husababisha athari, yaani kitendo hiki hupelekea kuwepo kwa jambo fulani.

Basi je, hiki anachokisababisha mwanadamu katika vitu miongoni mwa sifa, mwanadamu amekiumba ndani yake au Allah (swt) amekiumba katika vitu hivi kama alivyoviumba vitu vyenyewe?

Mchunguzi wa kina atakuta kuwa mambo haya yanayotokea katika vitu ni miongoni mwa sifa za vitu na si kutokana na kitendo cha mwanadamu. Dalili ni kwamba mwanadamu hawezi kuyaleta isipokuwa katika vitu ambavyo vina sifa hiyo miongoni mwa sifa zake. Ama vitu ambavyo havina sifa hizo, mwanadamu hawezi kuleta ndani yake kile anachotaka. Na kwa ajili hiyo, mambo haya hayakuwa miongoni mwa matendo ya mwanadamu, bali ni miongoni mwa sifa za vitu. Allah (swt) aliumba vitu na akapima ndani yake sifa zake kwa namna ambayo haiwezekani kutoa kingine isipokuwa kile alichokipima ndani yake...

Na kama alivyoviumba sifa katika vitu, vivyo hivyo ameviumba silika na mahitaji ya kiorganiki katika mwanadamu, na akaweka ndani yake sifa maalum kama sifa za vitu. Akaumba katika silika ya aina sifa ya mvuto wa kijinsia kwa mfano, na akaumba katika silika ya kujilinda sifa ya umiliki kwa mfano, na katika mahitaji ya kiorganiki sifa ya njaa kwa mfano, na akazifanya sifa hizi kuwa ni zenye kuandamana navyo kulingana na kanuni ya kuwepo kwake. Hivyo basi, sifa hizi maalum ambazo Allah (swt) amezileta katika vitu, silika, na mahitaji ya kiorganiki yaliyo ndani ya mwanadamu ndizo zinazoitwa Al-Qadar. Kwa sababu Allah peke yake ndiye aliyeumba vitu, silika, na mahitaji ya kiorganiki, na akapima ndani yake sifa zake...

Yaani aliviumba na akaumba ndani yake sifa maalum, hivyo zinatoka kwa Allah (swt), na hazitokani na mja na hana mamlaka nazo wala athari yoyote juu yake. Hivyo, huu ndio Al-Qadar. Na husemwa wakati huo kuwa Al-Qadar katika utafiti wa (Al-Qadha wal-Qadar) ni sifa za vitu ambazo mwanadamu anazisababisha ndani yake, na ni juu ya mwanadamu kuamini kuwa aliyepima sifa za vitu hivi ni Allah (swt)...]

Na kama unavyoona, imetajwa katika kitabu hicho hicho kwamba Al-Qadar katika utafiti wa (Al-Qadha wal-Qadar) ni (sifa za vitu ambazo mwanadamu anazisababisha ndani yake...) kisha akabainisha tofauti kati ya mwanadamu kuzisababisha na Allah kuziumba, akasema: (sifa ambazo mja anazisababisha katika vitu, je, sifa hizo ni kutokana na uumbaji wa Allah, yaani Yeye ndiye aliyeziumba na kuzileta? Ama ni kutokana na mja, yaani mja ndiye aliyeziumba na kuzileta?) Kisha akazidisha ufafanuzi akasema: (Yaani aliviumba na akaumba ndani yake sifa maalum, hivyo zinatoka kwa Allah (swt), na hazitokani na mja na hana mamlaka nazo wala athari yoyote juu yake. Hivyo huu ndio Al-Qadar. Na husemwa wakati huo kuwa Al-Qadar katika utafiti wa "Al-Qadha wal-Qadar" ni sifa za vitu ambazo mwanadamu anazisababisha ndani yake, na ni juu ya mwanadamu kuamini kuwa aliyepima sifa za vitu hivi ni Allah (swt)...)

Hivyo mwanadamu kwa kitendo chake katika majaribio juu ya vitu, anadhihirisha sifa na tabia za vitu ambazo Allah ameziumba ndani yake, yaani anavumbua ikiwa sifa hizo Allah ameshaziumba katika kitu hicho. Ama ikiwa sifa hiyo haikuumbwa katika kitu hicho, mwanadamu hawezi kuisababisha, kuidhihirisha wala kuivumbua. Na yale tuliyonukuu kutoka katika kitabu hapo juu yanabainisha hilo waziwazi, yaani maana ya (mwanadamu anazisababisha) ni kwamba anazivumbua au anazidhihirisha ikiwa zimeumbwa katika kitu hicho.

Natumaini hili linatosheleza, na Allah ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.

Ndugu yenu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

24 Muharram Al-Haram 1444 H Inayoambatana na 22/08/2022 M

Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa Amir (Allah amuhifadhi):

Kiungo cha jibu kutoka kwenye tovuti ya Amir (Allah amuhifadhi): Web

Share Article

Share this article with your network