Mfululizo wa majibu ya mwanachuoni mtukufu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah, Amir wa Hizb ut-Tahrir
kwa maswali ya watazamaji wa ukurasa wake wa Facebook "Fik-hi"
Kuelekea kwa Muhammad Ibrahim
Swali:
Assalamu Alaikum Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
Ndugu yetu mpendwa na mwanachuoni wetu mnyofu, naomba majibu ya swali lifuatalo:
Kauli inayosema kuwa asili katika miamala ni uhalali (al-hill) na ruhusa (al-ibahah) ni kauli yenye utata, na kuisambaza kwa jumla ya madhehebu manne kunahitaji usahihi na utafiti...
Asili hii imeenea miongoni mwa wanachuoni wa baadaye, lakini katika vitabu vya kale hatujaipata asili hii. Ibn Nujaym al-Hanafi, ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wa usuli wa Hanafi (na inasemekana kanuni hiyo imeenea kwao), alitaja kanuni mbili pekee ambazo ni:
Asili katika vitu ni uhalali (al-ibahah) madamu haijaja haramu,
Na asili katika mahusiano ya kijinsia (al-abda') ni uharamu.
Swali ni kwamba, ikiwa mahusiano ya kijinsia Sharia tukufu imechukua tahadhari na kuifanya asili yake kuwa ni uharamu ili kulinda nasaba! Je, haionekani kuwa hilo linapaswa kuenea pia katika mali na miamala ya kifedha, au angalau isisemwe kuwa asili yake ni uhalali... Kwa hiyo, ni lazima kusoma masuala ya miamala ndani ya misingi yake mikuu ili kutoa hukumu, kwani Sharia kama ilivyolinda nasaba, pia imelinda mali...
Labda ninaweza kuwa nimekosea, hasa kwa kuwa sijafuatilia kila walichosema wanachuoni na wataalamu wa usuli katika suala hilo...
Kwa sababu hatari ni kwamba kila aina ya miamala ya kisasa tunakwenda kutoa kauli ya kuhalalisha kwa kutumia (asili katika miamala ni uhalali) bila kusoma uhalisia wa suala hilo na asili ya dalili zinazolizungumzia.
Je, nini usahihi wa kanuni hii? Na je, mafaqihi waliisema?
Aliyetuma: Abu Zakaria kutoka Lebanon
Jibu:
Wa Alaikum Salaam Wa Rahmatullahi Wa Barakatuh,
Ewe ndugu yangu, hakika kuna kanuni kwa baadhi ya mujtahidina ambazo ni dhaifu (marjouh) kwetu, na miongoni mazo ni kanuni uliyoitaja (Asili katika miamala ni uhalali). Ama ile inayotegemewa kwetu na iliyopitishwa kwa nguvu ya dalili zake ni kwamba (Asili katika vitu ni uhalali madamu haijaja dalili ya uharamu) na kwamba (Asili katika vitendo ni kufungamana na hukumu ya kisheria): Tumegusia idadi ya kanuni nyinginezo na kubainisha kuwa hazina nguvu (ghayru rajihah), na huu hapa ni ufafanuzi wa hilo:
Kwanza: Imekuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiyyah al-Islamiyyah Juzuu ya Tatu, katika mlango wa (Hakuna hukumu kabla ya kuja kwa Sharia):
[Na kwa msingi huu, haisemwi kwamba asili katika vitu na vitendo ni uharamu kwa hoja kwamba ni kufanya tasarrufu katika milki ya Mwenyezi Mungu bila idhini Yake, hivyo inakuwa haramu kwa kuifanyia kiyasi na viumbe; kwa sababu aya iliyo wazi ni kwamba Mwenyezi Mungu haadhibu mpaka amlete Mtume, hivyo mtu hawi na makosa mpaka abainishiwe hukumu. Zaidi ya hapo, viumbe huumia, na Mwenyezi Mungu ametakasika na manufaa pamoja na madhara.
Vilevile haisemwi kwamba asili katika vitendo na vitu ni uhalali, kwa hoja kwamba ni manufaa yaliyo mbali na alama za uharibifu na madhara kwa mmiliki, hivyo inahalalishwa; haisemwi hivyo kwa sababu dhana ya aya ni kwamba mwanadamu amefungwa na kile alichokuja nacho Mtume; kwani huadhibiwa kwa kumuasi, hivyo asili ikawa ni kumfuata Mtume na kufungamana na hukumu za ujumbe wake, na asili siyo uhalali (ibahah) yaani kutokufungamana. Na kwa sababu ujumla wa aya za hukumu unaonyesha wajibu wa kurejea kwenye Sharia na wajibu wa kufungamana nayo, Mwenyezi Mungu (swt) amesema:
وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِنْ شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّهِ "Na jambo lolote mlilo khitalifiana, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu." (QS. Ash-Shura [42]: 10)
Na akasema:
فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ "Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume." (QS. An-Nisa [4]: 59)
Na akasema:
وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَاناً لِّكُلِّ شَيْءٍ "Na tumekuteremshia Kitabu hiki ili kubainisha kila kitu." (QS. An-Nahl [16]: 89)
Na kwa sababu Mtume (saw) anasema katika yale aliyoyapokea Ad-Daruqutni:
كُلُّ أَمْرٍ لَيْسَ عَلَيْهِ أَمْرُنَا فَهو رَدٌّ "Kila jambo ambalo haliko katika amri yetu basi hurejeshwa (hukataliwa)."
Hii inaonyesha kwamba asili ni kufuata Sharia na kufungamana nayo. Na kwa sababu manufaa yaliyo mbali na alama ya uharibifu na madhara kwa mmiliki, si hoja ya kuhalalisha...
Pia haisemwi kwamba asili katika vitu ni kusubiri (tawaqquf) na kutokuwa na hukumu; kwa sababu kusubiri kunamaanisha kusitisha utendaji kazi, au kusitisha hukumu ya kisheria, na hilo halijuzu. Na kwa sababu yaliyothibiti katika Quran na Hadith, wakati wa kukosa elimu, ni kuuliza kuhusu hukumu, na siyo kusubiri na kukosa hukumu. Mwenyezi Mungu (swt) amesema:
فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ "Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui." (QS. An-Nahl [16]: 43)
Na Mtume (saw) amesema katika hadith ya Tayammum, katika yale aliyoyapokea Abu Dawood kutoka kwa Jabir:
أَلاَ سَأَلُوا إِذْ لَمْ يَعْلَمُوا فَإِنَّمَا شِفَاءُ الْعِيِّ السُّؤَالُ "Kwanini hawakuuliza pale walipokuwa hawajui? Kwani tiba ya kutojua ni kuuliza."
Hii ilionyesha kuwa asili siyo kusubiri na kukosa hukumu.
Hivyo basi, baada ya kutumwa kwa Mtume (saw), hukumu ikawa ni ya Sharia, na ikawa hakuna hukumu kabla ya kuja Sharia; basi hukumu inategemea kuja kwa Sharia, yaani kupatikana kwa dalili ya kisheria kwa suala husika. Kwa ajili hiyo, haitolewi hukumu ila kwa dalili, kama vile isivyotolewa hukumu ila baada ya kuja kwa Sharia. Na asili ni kutafuta hukumu katika Sharia, yaani asili ni kutafuta dalili ya kisheria ya hukumu kutoka katika Sharia...
Na kwa hilo, inathibitika kanuni ya kisheria "Asili katika vitendo vya mwanadamu ni kufungamana na hukumu ya Mwenyezi Mungu". Hivyo, haijuzu kwa Muislamu kuanza tendo lolote ila baada ya kujua hukumu ya Mwenyezi Mungu katika tendo hilo kutokana na hitabu ya Sharia. Na uhalali (al-ibahah) ni hukumu miongoni mwa hukumu za kisheria, hivyo ni lazima kuwe na dalili yake kutoka katika Sharia...
Hii ni kwa upande wa vitendo. Ama kwa upande wa vitu, navyo ni vile vinavyofanyiwa vitendo, hakika asili yake ni uhalali (ibahah) madamu haijaja dalili ya uharamu. Hivyo asili ya kitu ni kuwa halali, na hakiharamishwi isipokuwa ikija dalili ya kisheria ya kukiharamisha. Hii ni kwa sababu maandiko ya kisheria yamehalalisha vitu vyote, na maandiko haya yamekuja kwa ujumla yakijumuisha kila kitu. Mwenyezi Mungu (swt) amesema:
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ "Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevitiisha kwenu vyote vilivyomo duniani?" (QS. Al-Hajj [22]: 65)
Na maana ya kuitiisha kwa Mwenyezi Mungu vitu vyote vilivyomo duniani kwa mwanadamu ni kuvihalalisha vyote vilivyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu (swt) amesema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُوا مِمَّا فِي الْأَرْضِ حَلَالاً طَيِّباً "Enyi watu! Kuleni katika vilivyomo ardhini vilivyo halali na vizuri." (QS. Al-Baqarah [2]: 168)
Na akasema:
يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا "Enyi wanaadamu! Chukueni mapambo yenu kwenye kila msikiti, na kuleni na kunyweni." (QS. Al-A'raf [7]: 31)
Na akasema:
هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولاً فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ "Yeye ndiye aliyeidhalilisha ardhi kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki yake." (QS. Al-Mulk [67]: 15)
Na hivyo ndivyo aya zote zilizokuja kuhalalisha vitu zilivyokuja kwa ujumla, hivyo ujumla wake ulionyesha kuhalalishwa kwa vitu vyote, basi uhalali wa vitu vyote unakuwa umekuja kwa hitabu ya Sharia ya ujumla. Hivyo dalili ya uhalali wake ni maandiko ya kisheria yaliyokuja kuhalalisha kila kitu. Basi ikiharamishwa kitu, ni lazima kuwe na maandiko maalum (nass mukhasis) ya ujumla huu, yanayoonyesha kuviondoa vitu hivi katika ujumla wa uhalali; na kutokana na hapa ndipo asili katika vitu ikawa ni uhalali. Kwa ajili hiyo, tunakuta Sharia, ilipoharamisha vitu, imetaja vitu hivyo vyenyewe, ikiwa ni kuviondoa katika ujumla wa maandiko, Mwenyezi Mungu (swt) akasema:
حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ "Mmeharamishiwa nyama ya mnyama aliyekufa, na damu, na nyama ya nguruwe." (QS. Al-Maidah [5]: 3)
Na Mtume (saw) amesema:
حُرِّمَتِ الْخَمْرَةُ لِعَيْنِهَا "Kileo kimeharamishwa kwa dhati yake yenyewe."
Imeelezwa na Al-Mabsut kutoka kwa Ibn Abbas, hivyo kile kilichotajwa na Sharia katika kuharamisha vitu kimeondolewa katika ujumla wa maandiko, hivyo kiko kinyume na asili...]
Na kutokana na hayo, inabainika kuwa kanuni hizo, iwe ile uliyoiashiria (Asili katika miamala ni uhalali) au nyinginezo kama tulivyoashiria hapo juu, ni kanuni dhaifu (marjouh) kwetu. Na rai sahihi ni ile inayofungamana na vitendo na vitu kwa namna tuliyoitaja, yaani (Asili katika vitendo ni kufungamana na hukumu ya kisheria) na (Asili katika vitu ni uhalali madamu haijaja dalili ya uharamu).
Natumaini kuwa katika haya kuna utoshelevu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi na Mwenye hekima zaidi.
Ndugu yenu Ata bin Khalil Abu al-Rashtah
29 Jumada al-Akhirah 1441 H Inayoambatana na 23/02/2020 M
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amlinde) kwenye Facebook
Kiungo cha jibu kutoka kwenye ukurasa wa Amir (Mungu amlinde) Web