Home About Articles Ask the Sheikh
Maswali na Majibu

Jibu la Swali: Uongozi wa Mtu Mmoja katika Uislamu

February 20, 2019
4923

(Mfululizo wa Majibu ya Mwanachuoni Mtukufu Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah, Amiri wa Hizb ut-Tahrir, kwa Maswali ya Wageni wa Ukurasa Wake wa Facebook "Fiqhi")

Jibu la Swali

Uongozi wa Mtu Mmoja katika Uislamu

Kwa Mohammad Hadoud

Swali:

Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Hali yako vipi sheikh wetu,

Nina swali kuhusiana na yale ambayo chama kimeyafanyia tabanni (msimamo rasmi).

Miongoni mwa misimamo ya chama ni kwamba uongozi katika Uislamu ni wa mtu mmoja, yaani Khalifa ndiye mwenye mamlaka yote mikononi mwake ndani ya dola, kwa maana; Khalifa ndiye dola.

Kwa ufafanuzi zaidi; Khalifa ana haki ndani ya dola kuwa mtawala, kadhi, na kila kitu...

Na jambo hili linaonekana kupingana na maneno yaliyotajwa katika kitabu cha Ad-Dawla (Dola ya Kiislamu) ambapo ilikuja katika ukurasa wa 129:

(Hivyo basi, Mtume (saw) alisimamisha chombo cha Dola ya Kiislamu yeye mwenyewe, na akakikamilisha katika uhai wake. Dola ilikuwa na mkuu, wasaidizi, magavana (waali), makadhi, jeshi, wakurugenzi wa idara, na baraza linalorejewa kwa ajili ya ushauri (shura). Chombo hiki katika umbile lake na mamlaka yake ni njia ambayo ni wajibu kufuatwa, na kwa ujumla imethibiti kwa mutawatir.)

Naomba ufafanuzi;

Jazakumullahu Khayran na Mwenyezi Mungu afungue kheri kupitia mikono yenu.

Jibu:

Walaikum Salaam Warahmatullahi Wabarakatuh,

1- Inaonekana mwanzoni mwa swali lako unaashiria kile kilichokuja katika kitabu cha Ash-Shakhsiya Al-Islamiyya (Shakhsiya ya Kiislamu) Sehemu ya Pili katika mada ya "Uamiri" ambapo pamekuja maelezo yafuatayo:

(...Ama huyu amiri, Sharia inalazimu awe mmoja, na haijuzu kuwa zaidi ya mmoja. Uislamu haujui uongozi wa pamoja (collective leadership), wala haujui urais wa pamoja. Hakika si vinginevyo, uongozi katika Uislamu ni wa mtu mmoja pekee (individual), hivyo ni lazima rais au amiri au kiongozi awe mmoja, na haijuzu kuwa zaidi ya mmoja. Dalili ya hilo iko wazi katika maandiko ya Hadith zilizotangulia na katika kitendo cha Mtume (saw). Hadith zote zinasema: «أحدهم» (mmoja wao), «أحدكم» (mmoja wenu). Na neno ahad ni neno la wahid (moja), nalo linaashiria idadi, yaani mmoja na si zaidi. Na hilo linafahamika kupitia ufahamu wa kinyume (mafhum al-mukhalafa). Na ufahamu wa kinyume katika idadi, sifa, kikomo, na sharti hufanyiwa kazi bila ya hitaji la andiko jingine, na hautenguliwe isipokuwa katika hali moja tu, nayo ni iwapo kutakuja andiko jingine linaloufuta... Kwa msingi huo, kauli ya Mtume (saw):

فَلْيُؤَمِّرُوا أَحَدَهُمْ "Basi wamfanye mmoja wao kuwa amiri"

إِلَّا أَمَّرُوا أَحَدَهُمْ "ila wamfanye mmoja wao kuwa amiri"

فَأَمِّرُوا أَحَدَكُمْ "basi mfanyeni mmoja wenu kuwa amiri"

Inaonesha kupitia ufahamu wa kinyume katika Hadith hizi kwamba haijuzu kufanywa amiri zaidi ya mmoja. Kutokana na hapa, uamiri ni wa mmoja, na haijuzu kuwa wa zaidi ya mmoja kabisa kwa mujibu wa maandiko ya Hadith, yawe ya kutamkwa (mantuq) au ya kufahamika (mafhum). Na hilo linaungwa mkono na kitendo cha Mtume (saw), kwani katika matukio yote aliyoweka amiri, alikuwa akiweka mmoja tu na si mwengine, na hakuwahi kuweka zaidi ya mmoja katika mahali pamoja kabisa... Kwa msingi huo, haijuzu kwa jambo moja kuwa na wakuu wawili, wala kwa mahali pamoja kuwa na wakuu wawili. Bali ni lazima mkuu awe mmoja tu, na ni haramu kuwa zaidi ya hapo. Hata hivyo, inapaswa kueleweka kuwa urais, uamiri, na uongozi katika Uislamu si utukuzaji wa kiongozi (za'ama), kwa sababu za'ama inapelekea kumfuata kiongozi huyo (kwa nafsi yake). Ama urais katika Uislamu, wenyewe unampa mkuu haki ya kusimamia mambo na mamlaka (sultan) katika jambo ambalo amepewa urais wake, na utekelezaji wa kila kilichoingia chini ya urais wake kulingana na mamlaka aliyopewa kama amiri, ndani ya mipaka ya kile alichopewa na Sharia kuhusiana na jambo alilowekwa kuwa mkuu kwalo...) Mwisho wa nukuu kutoka kitabu cha Ash-Shakhsiya Al-Islamiyya Sehemu ya Pili.

2- Kauli hii kwamba uongozi na uamiri katika Uislamu ni wa mtu mmoja haipingani na kile kilichokuja katika kitabu cha Ad-Dawla Al-Islamiyya (Dola ya Kiislamu) kinachosema:

(Hivyo basi, Mtume (saw) alisimamisha chombo cha Dola ya Kiislamu yeye mwenyewe, na akakikamilisha katika uhai wake. Dola ilikuwa na mkuu, wasaidizi, magavana, makadhi, jeshi, wakurugenzi wa idara, na baraza linalorejewa kwa ajili ya ushauri. Chombo hiki katika umbile lake na mamlaka yake ni njia ambayo ni wajibu kufuatwa, na kwa ujumla imethibiti kwa mutawatir. Mtume (saw) alikuwa akitekeleza majukumu ya mkuu wa dola tangu alipowasili Madina hadi kufa kwake (saw), na Abubakar na Umar walikuwa wasaidizi wake, na Maswahaba waliafikiana baada yake kusimamisha mkuu wa dola atakayekuwa Khalifa wa Mtume (saw) katika urais wa dola pekee, si katika Utume wala Unabii, kwa sababu ilihitimishwa kwake (saw). Hivyo basi, Mtume (saw) alisimamisha chombo cha dola kikamilifu katika uhai wake na akaacha mfumo wa utawala na chombo cha dola vikiwa vimejulikana na kudhihiri wazi kabisa.) Mwisho.

Yaani maandiko hayo mawili hayapingani, bali yanaafikiana kikamilifu. Hii ni kwa sababu andiko la kwanza katika kitabu cha Ash-Shakhsiya Al-Islamiyya Sehemu ya Pili linazungumzia uamiri kwa ujumla katika Uislamu, iwe ni uamiri wa safari, uamiri wa kikundi, au uamiri mkuu wa Waislamu (Khilafah). Uamiri katika Uislamu ni wa mtu mmoja na si wa kikundi, yaani haijuzu kwa kikundi kuwa ndicho chenye mamlaka katika uamiri, bali mamlaka ya uamiri ni ya mtu mmoja tu ambaye ndiye anayemiliki uamuzi wa mwisho... Jambo hili, ingawa ni hukumu ya kisheria, pia ni hivyo kiuhalisia, kwani hali halisi ya mambo haiwezi kunyooka iwapo mamlaka katika uamiri na utawala yatakuwa ya kikundi, bali ni lazima yawe ya mtu mmoja, yaani uamuzi wa mwisho uishie kwa mmoja... Hali kadhalika Khilafah, ambayo ni uamiri mkuu (urais mkuu wa Waislamu), ni wa mtu mmoja, yaani mwenye mamlaka ni yule mtu anayebaiwa kuwa Khalifa, naye humiliki kupitia bai’ah mamlaka yote ya utawala, usultani, na kupitisha hukumu (tabanni) bila ubaguzi...

3- Lakini kuwekwa mamlaka kwa Khalifa haimaanishi kabisa kuwa Khalifa afanye kazi zote za utawala na usultani yeye mwenyewe. Bali maana yake ni kwamba mamlaka ni yake, na kila anayepewa mamlaka katika utawala na usultani anapata mamlaka yake kutoka kwa Khalifa kwa Khalifa kumwakilisha katika hilo. Kwa hivyo, watawala wote katika Khilafah kama wasaidizi, magavana... n.k., na wote wanaosimamia idara za mahakama, vyombo vya utawala, jeshi... n.k., na wanakuwa na mamlaka, hakika Khalifa huwawakilisha kwa niaba yake katika mamlaka hayo. Hakuna anayemiliki mamlaka yoyote asili isipokuwa awe ni mwakilishi wa Khalifa kwa njia yoyote ile...

4- Mamlaka ni jambo moja, na utekelezaji wa kazi ni jambo jingine. Mtume (saw) alikuwa akimiliki mamlaka yote ya utawala na usultani, lakini hakuwa akifanya kazi zote za utawala na usultani yeye mwenyewe, bali alikuwa akisaidiwa na wengine kama ilivyobainishwa katika kitabu cha Ad-Dawla Al-Islamiyya na vitabu vingine vya Chama. Mtume (saw) aliunda katika uhai wake chombo kamili cha dola, na kitendo chake (saw) kilionyesha kuwa chombo hiki katika umbile lake na mamlaka yake ni njia ambayo ni wajibu kufuatwa, yaani ni hukumu ya kisheria na si mbinu (uslub) inayobadilika kulingana na mazingira na hali... Kwa hivyo, kusimamisha chombo cha dola hakupingani na kuwekwa kwa mamlaka kwa Khalifa, kwa sababu Mtume (saw) huku akiwa anamiliki mamlaka yote, alisimamisha chombo cha dola na akakipa mamlaka. Kitendo cha Mtume (saw) kilikuwa dalili kubwa zaidi kwamba hakuna mgongano kati ya kuwekwa kwa mamlaka kwa Khalifa na kati ya kusimamisha chombo cha dola kilicho na mamlaka yaliyotokana na mamlaka ya Khalifa. Vyombo hivyo hufanya kazi ya kumsaidia Khalifa katika kusimamia mambo ya dola kulingana na mamlaka anayowapa Khalifa... Na hili ndilo lililokuwa katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kwani pamoja na udogo wa dola aliyoiunda Mtume (saw), kuendesha kwake kulihitaji kusimamisha chombo ambacho Mtume (saw) angekitumia kupata msaada katika kusimamisha utawala na kusimamia mambo ya watu... Sembuse ikiwa dola ni pana na kubwa sana...?!

5- Pamoja na kwamba mamlaka ni ya Khalifa, lakini amefungwa na hukumu ya kisheria. Ikiwa atatoka nje ya hukumu ya kisheria na kuwadhulumu raia au hakutekeleza vizuri sheria ya Mwenyezi Mungu, basi Mahakama ya Mazalim huangalia jambo lake, na ina mamlaka ya kumwondoa madarakani kwa mujibu wa hukumu za Sharia... Iimekuja katika Ibara ya 87 ya Muqaddimat ad-Dustur (Utangulizi wa Katiba) iliyotolewa kutoka katika dalili za kisheria yafuatayo: (Kadhi wa Mazalim ni kadhi anayewekwa ili kuondoa kila dhuluma inayotokea kutoka kwa dola dhidi ya mtu yeyote anayeishi chini ya mamlaka ya dola, iwe ni miongoni mwa raia wake au wengine, na iwe dhuluma hiyo imetoka kwa Khalifa au kwa wale walio chini yake miongoni mwa watawala na wafanyakazi.) Na ili kuhakikisha kuwa hakuna khofu isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Khalifa hamiliki mamlaka ya kumwondoa Kadhi wa Mazalim wakati anapokuwa akiangalia dhuluma iliyotokea kutoka kwa Khalifa... Imekuja katika Ibara ya 88 (...Haijuzi kumwondoa "Kadhi wa Mazalim" wakati anapokuwa akitekeleza jukumu la kuangalia dhuluma dhidi ya Khalifa...) Na imekuja katika maelezo ya ibara hiyo: (...Hiyo ni kwa sababu kubaki kwa mamlaka ya kumwondoa mkononi mwa Khalifa katika hali hii kutaathiri uamuzi wa kadhi, na hivyo kuzuia uwezo wa kadhi wa kumwondoa Khalifa au wasaidizi wake kwa mfano, na mamlaka haya ya kumwondoa yatakuwa njia ya kuelekea kwenye haramu, yaani kubaki kwake mkononi mwa Khalifa katika hali hii ni haramu.) Na Ibara ya 90 imesisitiza mamlaka ya Mahakama ya Mazalim katika kumwondoa Khalifa ikiwa anastahili hilo, ikasema katika Ibara ya 90: (Mahakama ya Mazalim ina haki ya kumwondoa mtawala yeyote au mfanyakazi katika dola, kama ambavyo ina haki ya kumwondoa Khalifa, na hilo ni iwapo kuondolewa kwa dhuluma kunahitaji uondoaji huu.) Kwa hivyo, hakuna kinga (immunity) kwa Khalifa mbele ya mahakama; akikosea anahisabiwa na akistahili kuondolewa anaondolewa.

Kwa mujibu wa hayo, Khalifa ingawa mamlaka ni yake ndani ya dola, lakini amefungwa na hukumu za kisheria mbele ya Mahakama ya Mazalim... Naye, kama tulivyobainisha hapo juu, husimamisha vyombo vya dola ili kumsaidia katika mambo ya utawala na kumsaidia katika kusimamia mambo kulingana na mamlaka anayowapa katika kazi anazowakabidhi.

Natumaini kuwa ule mgongano uliokuwa akilini mwako umeondoka na imekubainikia kuafikiana kwa maandiko mawili yaliyotajwa hapo juu. Mamlaka ni jambo moja, na vyombo vinavyomsaidia Khalifa katika kuendesha mambo ya dola na kumsaidia katika kusimamia mambo ya raia ni jambo jingine.

Ndugu yenu, Ata Bin Khalil Abu Al-Rashtah

14 Jumada al-Akhira 1440 H Sawa na 19/02/2019 M

Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amiri (Mungu amuhifadhi) kwenye Facebook

Link ya jibu kutoka ukurasa wa Amiri (Mungu amuhifadhi) kwenye Google Plus

Share Article

Share this article with your network